Monday, June 11, 2012

MWAPACHU, HYDEN, MARX NA U-SASA-ISHAJIBALOZI MWAPACHU: UDSM ACHANENI NA UMAKSI

Na Sabatho Nyamsenda 

Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, iliandaa Kongamano kwa ajili ya kutabaruku kazi za mwanazuoni Goran Hyden. Kongamano hilo lilifanyika jana (jumamosi, 9/6/2012) katika Hoteli ya Serena (zamani Moven Pick)! Kazi zake nyingi zilijadiliwa ikiwemo ile ya “Beyond Ujamaa in Tanzania: Underdevelopment and an Uncaptured Peasantry”. Goran mwenyewe pia alikuwepo. Mijadala ikaanza. Kama kawaida, wanazuoni wengi walioalikwa (naweza sema zaidi ya 99%) ni wale ‘waliozaliwa mara ya pili’ kitaaluma. Pia walikuwepo baadhi ya watumishi wenye nyadhifa za juu serikalini: Gavana wa BOT, Prof Ndulu; Katibu Mkuu mstatafu wa EAC, Balozi Mwapachu, mabalozi n.k. 

Mjadala ukaanza. Kazi za Goran zikachambuliwa. Zikalinganishwa na kipindi chetu cha sasa… Lakini, ooo. Kwa bahati mbaya washiriki wengi hawakuwa na hamasa ya mjadala wa tafakuri. Wengi waliishia kukubaliana na Goran, kwamba mkulima mdogo (peasant) haja-sasaishwa [najaribu kuunda kitenzi cha usasa, yaani modernization]. Wakamuuliza Goran: ‘Sasa tutafanyaje, ili kubadili peasant awe farmer?’ 

Goran akatoa jibu: Serikali ya Mwalimu ilifanya makosa: ilitumia njia laini sana ili kumbadili mkulima [natumia mkulima kumaanisha peasant] na ndiyo maana haikufanikiwa. Kwa nini haikufanikiwa? Mosi, mkulima mwenyewe aliendelea kugoma. Hii ni kwa sababu aliendelea kukumbatia tabia za kijadi na hivyo kumfanya kuishi katika uduni wa maendeleo uliojikita katika uchumi wa kufadhiliana (economy of affection). 

Pili, serikali yenyewe iliendelea kutumia mbinu za ushawishi ikiwemo kuwapatia zawadi wakulima. Zawadi hizo ni kama huduma za bure za elimu, afya, maji n.k. Hii iliendelea kuwafanya wabweteke na hivyo kutokuwa na ari ya kuongeza uzalishaji. Tatu, mwongozo wa 1971 uliwapa nguvu kubwa wafanyakazi. Waliongezewa stahiki zao na kupewa likizo n.k. Mafao hayo yalitumwa kwa ndugu zao huko mashambani na muda wa likizo pia ulitumika kutembelea ndugu, kuhudumia wagonjwa, n.k. Haya yote yaliendeleza uchumi wa kufadhiliana na kudidimiza uzalishaji – viwandani na mashambani. 

Goran akatoa mfano wa serikali iliyowahi kuitawala Tanzania [wakati huo Tanganyika] na kufanikiwa, japo sio sana, kumbadili mkulima. Ni serikali ya kikoloni. Tunaweza kujifunza toka kwao. Akaenda mbali zaidi: Kamwe hakutakuwa na maendelea iwapo mkulima huyu hatabadilishwa! Sharti abadilishwe ndipo nchi itaweza kupiga hatua. Ujio wa wakulima wakubwa usipingwe. Ni mbinu njema ya kisasa ya kuongeza tija katika uzalishaji na kutoa mfano kwa wakulima wadogo kujifunza.

Ebo!? Nilishangaa na kujiuliza, iweje mwanausasa huyu atoe mawazo ya aina hiyo nasi tukayakumbatia pasi na kuyahoji? Mimi na wenzangu wawili (Eluka Kibona na Richard Mbunda, wanafunzi wa shahada ya uzamivu) tukapiga moyo konde na kuomba kuchangia. Kwanza, tulihoji uhalali wa nadharia ya usasa na wanausasa wenyewe katika kuleta maendeleo. Hii ni nadharia ya kibwenyenye inayowagawa watu katika makundi mawili: sisi wanausasa, tumestaarabika na kuendelea; na ‘wao’ wasIostaarabika wanaojididimiza kimaendeleo. Sharti tuwabadili. Ndivyo nchi za Kibeberu zilivyoitazama, na zinavyoitazama, Afrika! Waliowapeleka Waafrika utumwani ama wakoloni walihalalisha biashara hiyo haramu kama mbinu ya kumstaarabisha na kumuendeleza Mwafrika. Katu hawasemi jinsi ubeberu (katika sura zake za utumwa, ukoloni na sasa uliberali mamboleo) ulivyoidumaza, na unavyoendelea kuididimiza Afrika! 

Na sisi, ‘wasomi tuliostaarabika na kuishi maisha ya kisasa’, tunakaa hotelini (baada ya mfadhili kutoa pesa) na kujadili jinsi ya kumbadili peasant awe farmer? Tena tunasema eti wakoloni walifanikiwa kidogo? Tuna tofauti gani na mabeberu? Je, tuna uhalali gani wa kufanya hivyo? Na hivi ndivyo mkakati wa ‘Kilimo Kwanza’ ulivyoundwa. Matajiri kadhaa wakakaa na Mkuu wa nchi hotelini, halafu kesho yake tukasikia kaulimbiu: ‘Enyi wakulima msiostaarabika, sasa ni zama za Kilimo Kwanza. Achaneni na jembe la mkono, nunueni Power Tiller’. Ni mkulima gani mdogo aliyealikwa ili kuunda mkakati huo?

Swali likarushwa kwa Profesa mmoja mtaalam wa sera za umma: Je, hukutufundisha darasani kwamba sera bora ni ile inayoanzia chini (bottom) na kwenda juu (up)? Kama hivyo ndivyo, kwa nini basi tusiende kwa huyo mkulima ili kujifunza badala kumuelimisha? Je, sisi tunajua mahitaji yake kuliko yeye mwenyewe? 

Na hapo ndipo nikakumbuka kisa cha yule msomi mwenye ma-digrii mengi ya kilimo/ufugaji aliyetumwa na serikali kwenda kuwastaarabisha wamasaai. Kisa hiki kipo katika riwaya ya Chachage iitwayo Almasi za Bandia [Na kinatoka kwenye makala ya Andreas Fuglesang kuhusu The Myth of People's Ignorance]. Basi mtaalam na msaidizi wake walitembea umbali mrefu kwa siku kadhaa pasi na kuona makazi yoyote. Wakiwa wamekaribia kukata tamaa, kwa mbali wakaona manyatta. Wakakimbia kuifuata. Njiani kulikuwa na mto mkubwa, hivyo ikawalazimu kuogelea ili kuweza kuuvuka. Wakafanya hivyo. Hatimaye wakaifikia ile manyatta na kukuwakuta wenyeji. Mtaalamu hakutaka kupoteza muda. Akaanza kuwaelimisha wamasaai. Akazungumzia juu ya ufugaji wao wa kuhamahama na jinsi unavyowadidimiza kiuchumi na kuharibu mazingira. Akawafundisha mbinu za kisasa na faida zake. Akawataka wabadilike! Baada ya kumaliza, mzee mmoja akamuuliza swali: Kijana kwa nini ulipovuka mto uliogelea badala ya kutumia daraja ambalo sisi wenyeji tunalitumia? Msomi akapigwa na butwaa: ebo, kwani ninyi mna daraja? Mbona sikuliona wakati nakuja? Mzee akamjibu, iwapo hujui kama tuna daraja ama la umewezaje kujua matatizo yetu hata kufikia hatua ya kuja kutubadilisha? 

Tukazidi kuuchambua mkakati wa Kilimo Kwanza. Huu ni mfano mzuri wa nadharia ya usasa. Na unasifiwa kweli na nchi za Magharibi. Mkakati unazungumzia juu ya mapinduzi ya kijani. Je, mapinduzi hayo yataletwa na nani? Mkulima dagaa ama papa? Jibu linafahamika: Waasisi wa mkakati huo ni wakulima wakubwa na mashabiki wao. Wanatetea ujio wa wakulima wakubwa kwa misingi iliyoainishwa na Goran hapo awali. Lakini swali la kujiuliza ni: ‘Je, dagaa na papa wanaweza kukaa pamoja kwa amani?’ Mbona tangu kuanzishwa kwa mkakati huu kuna malalamiko mengi ya uporaji wa ardhi? Na uporaji huo unazidi kuongezeka kila kukicha. 

Papa kummeza dagaa si suala geni hapa nchini. Katika sekta ya madini, ujio wa makampuni makubwa ya uchimbaji ulitetewa kwa misingi hiyo hiyo: wana teknolojia ya kisasa, wataongeza uzalishaji, watatoa ajira, watalipa kodi, wataongeza fedha za kigeni na hivyo kukuza pato la taifa. Nini kilitokea kama si uporaji? Ulianza uporaji wa ardhi na machimbo kwa wachimbaji wadogo na wakulima wadogo. Katika mgodi wa Bulyanhulu, baada ya kampuni ya Sutton Resources (baadaye ilinunuliwa na Barrick Gold) kusaini mkataba na serikali, kilichofuatia ni kuwafukuza wachimbaji wadogo wapatao 200,000 kikatili (inasadikika kuwa watu 54 walifukiwa wakiwa hai). Wachimbaji wadogo waliambiwa kuwa uchimbaji wao si halali na hivyo kutimuliwa bila kulipwa fidia. Japo mkataba ulisainiwa wakati wa Mwinyi lakini utimuaji ulifanyika wakati wa Mkapa. Haya yote yalifanyika kana kwamba serikali ya Mkapa ilisahau kuwa wachimbaji wadogo ndio waliovumbua dhababu katika mgodi huo. Zaidi ya hapo, Rais Mwinyi mwenyewe alikuwa amekwisha kuwaahidi wachimbaji wadogo kuwa hakuna kampuni itakayowatimua katika machimbo hayo. Hata katika kampeni zake za urais, mwaka 1995, Mkapa pia aliahidi hivyo hivyo. Je, nini kilichotokea? Walitimuliwa.

Watanzania walioajiriwa na Kampuni ya Barriki katika Mgodi wa Bulyanhulu ni 2,447. Unapowanyang’anya ajira watu laki mbili na kuajiri elfu mbili unatengeneza ajira au unapora ajira? Zaidi ya hapo, isipokuwa kampuni moja (Resolute), makampuni yote ya madini yana misamaha ya kodi. Sheria (hata hii mpya) inayaruhusu makampuni kuhamisha faida yote inayochumwa nchini. Kirejeshwacho nchini ni takwimu tu; fedha zote huwekwa ama kuwekezwa nje. Ndiyo maana, wakati madini huchangia asilimia 40 ya mauzo ya nje, mchango wake katika pato la taifa ni pungufu ya asilimia tatu. Teknolojia? Hoja hii pia haina mashiko. Tumeshuhudia tulivyoachiwa mashimo huko Buhemba na utiririshaji wa sumu katika vyanzo vya maji huko Tarime. Ni teknolojia gani ya kisasa inayoleta madhara makubwa katika mazingira na uhai wa binadamu kuliko hata ilivyokuwa kwa wachimbaji wadogo? 

Baada ya kuona uporaji ulioanza kufanyika dhidi ya wachimbaji wadogo katika sekta ya madini, Chachage aliwahi kuandika kuwa ‘Mnyonge Atarithi Ardhi lakini si Haki za Uchimbaji wa Madini’ (‘The Meek Shall Inherit the Earth but Not the Mining Rights'). Hii ilikuwa ni mwaka 1995. Pengine wakati huo, mnyonge aliweza kurithi ardhi. Sio sasa! Baada ya uporaji katika madini, sasa sehemu kubwa ya mtaji wa Makampuni makubwa inaelekezwa katika kilimo. Kilichotokea kwa wachimbaji wadogo ndicho kinachofuatia kwa wakulima wadogo. 

Kinachofanywa na makampuni makubwa ni uporaji wa rasilimali za watanzania! Uporaji huu si mgeni katika historia ya ubepari. Ni njia ya kulimbikiza mtaji. Karl Marx aliita njia hiyo, ulimbikizaji wa awali (Primitive Accumulation). Ni ulimbikizaji unaotumia mbinu za kikatili za uporaji na uharamia. Hiyo, ilikuwa ni katika hatua za mwanzo za ubepari. Marx alidhani kuwa ubepari ukiendelea hutumia mbinu za ‘kisasa’ za ulimbikizaji. Sasa ni karne ya tano tangu ubepari uanze; na ni karne ya pili tangu uingie katika hatua (ya mwisho?) ya ubeberu. Bado, wafuasi wa Marx kama David Harvey wanaifufua dhana ile ile ya ulimbikizaji wa awali na kuipa jina jipya la ulimbikizaji wa kiporaji (Accumulation by Dispossession) ili kuelezea uporaji unaofanyika katika zama hizi za uliberali mamboleo.

Mwisho tukahoji: Kama watu tunaowasifu kuwa ‘waliostaarabika’ na kutumia mbinu za ‘kisasa’ bado wanatumia mbinu za awali na za kikatili zisizo na hata chembe ya ‘ustaarabu’ (primitive/ barbaric) kwa nini tusifikirie kwanza ‘kuwastaarabisha’ na kuwabadili wao kabla ya huyo mkulima, ambaye anapaswa kuiga mfano wao?

Hapo moto ukawaka: Balozi Mwapachu akaomba kipaza sauti. ‘Vijana sharti mbadili mtazamo na kwenda na wakati !’ alionya. Akasema kuwa tatizo la vijana wetu ni kwamba bado tunatumia nadharia zilizopitwa na wakati ambazo hazina nafasi katika ulimwengu wa sasa. Kuna uporaji wa ardhi?, aliuliza, Wapi? Akasisitiza kuwa hakuna uporaji wa ardhi uliowahi kufanyika hapa nchini, hata chembe moja. Akatutaka twende Kilombero tuone jinsi makampuni makubwa yanavyoleta faida na kubadili maisha ya watu. ‘Hizi falsafa za Kimaksi zinawapotosha vijana’, aliunguruma kisha akawageukia wahadhiri na kuwauliza: ‘Bado mnafundisha Umaksi? Bado mnawalazimisha vijana kujibu mitihani kwa kutumia nadharia za Kimaksi na wasipofanya hivyo mnawafelisha?’. Akatugeukia na kuhitimisha: ‘Vijana, ulimwengu unabadilika. Sharti na ninyi mbadilike’. Alipomaliza nikamrushia bango la utani: ‘So you want us to be captured too?’ Vikafuatia vicheko. Laiti Balozi Mwapachu angejua kuwa Umaksi ulizikwa hapa chuoni tangu miaka ya 80! Laiti angelijua kuwa wahadhiri wote waliomzunguka ni ama ‘wamezaliwa mara ya pili’ kitaaluma na kuachana na ukale wa Maksi labda asingewauliza.

Katika vipindi vilivyofuatia, hakuna aliyemjibu Balozi Mwapachu. Ni yeye aliyekuwa akiongoza mjadala na kuwataka washiriki kutozungumza zaidi ya dakika moja huku akiainisha maeneo ya kuzungumzia. Watu hawakuchangia, mjadala ukapoteza hamasa! Siku ikaisha.

Na Sabatho Nyamsenda,
Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


MAONI YA MSOMAJI

Ahsante sana Sabatho kwa kutushirikisha suala hili na kwa uchambuzi.

Naam huo ndiyo mtafaruku wa kifikra tulioufikia katika nchi yetu. Nadharia za utu zinadharauliwa na kupuuzwa, na mara nyingi hazina watetezi (hongereni kwa kusimama).

Yalinikuta mwaka juzi nadhani kwenye kongamano la mwaka la watafiti lililoandaliwa na REPOA kwenye kahoteli kamoja kazuri jijini karibu na ufukwe mzuri (sijui Whitesands au Giraffe pale - zinanichanganya). 

Makuwadi wa usasa ni wakali sana na hawana simile. Hawachelewi kujimwaga kwenye fallacies na mijitusi. Kosa langu niliwaambia kuwa KILIMO KWANZA sio pro poor, sio user friendly, hakimhusu mkulima bali mfanyabiashara (baraza la wafanyabiashara tanzania nadhani ndiyo wenye kilimokwanza).  Niliwaambia kisa mkasa cha Kijiji cha Olarash huko Monduli ambako wanafuga ng'ombe kwa wingi na wanayo samaki hadi ziada lkn pia udongo wao ni phosphetic, lakini walilazimishwa kusign vocha za mbolea (wasioyohitaji) ili mama/sijui baba mwenye tenda ya kuuza pembejeo auze tu. 

Huko huko Monduli kisa mkasa cha kijiji kinaitwa Barabarani nadhani, walipelekewa mbegu bora za mahindi ilhali walihitaji mpunga maana ndiyo kilimo chao (lakini mama alishanunua za mahindi-lazima wachukue) USASA HUU. Niliwaambia kumsasarize mkulima wa Tanzania hakuhitaji pembejeo tu jamani mbona hamuongelei zaidi masoko? Nikatoa mfano wa mananasi yanayooza Chalinze, na mahindi yanayonyeshewa na kuoza huko Rukwa. Nikasema jamani tatizo la mkulima 'mshamba' wa Tanzania huyu sio uzalishaji  tu- mbona maeneo mengine anazalisha hadi ziada (ofkozi hata matumbo yetu na hata tumeota manyama uzembe ni kwa kula chakula kilichozalishwa na huyu mkulima mshamba wa Tanzania). 

Nimepita Chato juzi, nimekuta PAWATILA zimebwagwa hapo nje mbele ya ofisi ya Halmashauri-kisa haziuziki, hazihitajiki- ila ndo zishauzwa hizo au sio? Ndiyo usasa wa kilimo kwanza, afu sabatho unaleta zako zipi, eti botomu apu, tutauza lini? Hata Mkapa kasema majuzi- pawatilaz za kilimo kwanza ni upuuz sehemu kubwa ya nchi.

Hata hivyo naungana na Mwapachu kwamba hakuna uporaji wa ardhi nchini maana hajaporwa yeye, ndiyo usasa wenyewe.

Msomaji: Adam Lingson
----

* Picha kwa Hisani ya TheHabari & Mjengwablog
* Makala kutoka kwenye Mtandao wa Wanazuoni

3 comments:

John Mwaipopo June 14, 2012 at 8:42 PM  

nimeipenda hii ila nilivutiwa zaidi na jinsi ulivyokuwa ukujaribu kukiboresha kiswahili kiwe cha "kisasa". nadhani maneno mengine siyo lazima yakawa ya kisasa zaidi kwa sababu yana namna nyingine ya kupeleka ujumbe ule ule. kwa mfano isingefaa "mkulima hajafanywa wa kisasa"

John Mwaipopo June 14, 2012 at 8:42 PM  

nimeipenda hii ila nilivutiwa zaidi na jinsi ulivyokuwa ukujaribu kukiboresha kiswahili kiwe cha "kisasa". nadhani maneno mengine siyo lazima yakawa ya kisasa zaidi kwa sababu yana namna nyingine ya kupeleka ujumbe ule ule. kwa mfano isingefaa "mkulima hajafanywa wa kisasa"

Unknown June 15, 2012 at 12:05 AM  

Labda wadau tunasoma na kutafakari kwa makini sana yanayosemwa na hawa watetezi wa "usasa" kama alivyoita Sabatho Nyamsenda. Lakini kumbuka kwamba watetezi na mfumo wa usasa hususan unavyoletwa na mashirika ya maendeleo yana mantiki yake yenyewe. Ninacho maanisha, kama alivyodai Fergusson kwenye "The Anti-Politics Machine" kwamba kama hakuna tatizo litatengenezwa na kama hakuna "mshamba" nawe pia ataundwa ili biashara ya maendeleo iendelee. Misaada ni biashara kubwa na ili iweze kuhalilishwa haina budi akatengenezwa mshamba na tatizo. Sio kama matitizo hayapo lakini darubini haielekezwi kwa wakulima wenyewe, masuala ya utawala, miundo mbinu na udhalimu wa masoko ya kimataifa. Jambo la rahisi ni kuelekeza kidole kwenye tamaduni na desturi za Kiafrika. Kumbukeni kwa nchi za maghrabi kuzungumzia Afrika ni kuzungumzia suala la utamaduni. Ni ajabu historia inavyojirudia yenyewe kuanzaia Goran na sasa KILIMO KWANZA. Asante kwa madini adhimu haya.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP