Wednesday, July 25, 2012

MASIHA WA TANZANIA 2015 NI NANI?


Lakini licha ya kukumbatia itikadi yenye kuwarudisha wanyonge utumwani, soko la siasa limekuwa likizalisha masiha takribani kila uchaguzi mkuu. Ni uchaguzi wa mwaka 2000 pekee ndio haukua na masiha. Mwaka 1995 alikuwa Mrema, 2005 Kikwete na 2010 Slaa. Kila mara masiha hawa wamefanikiwa kununua hisia na matumaini ya wanyonge. Lakini je, masiha hawa walikuwa mfumo mbadala wenye kurejesha matumaini kwa wanyonge? Je, na sisi wanazuoni, wajibu wetu ni nini juu ya kuibuka na kushuka kwa masiha? 

Mwl. Lwaitama anasema tusipuuze umuhimu wa masiha. Wao ni alama tu, ambayo kwayo wanyonge watajiletea ukombozi. Historia inamtetea Mwl. Lwaitama. Tangu Toussaint L’Ouverture hata Kinjekitile wanyonge wameweza kupambana dhidi ya ubeberu kwa kutiwa shime na masiha.

Lakini historia hiyo hiyo, ikisaidiwa na mantiki, vinaweza kumkosoa Mwl. Lwaitama: Katika harakati za uhuru miaka ya 50 na 60 Afrika pia ilizalisha masiha. Karibu kila nchi ilikuwa na masiha. Wanyonge walikuwa nyuma yao na kupambana pamoja nao. Ukoloni ukaondoka. Je, masiha kama Kenyatta na Banda walijenga mifumo ya aina gani baada ya ukoloni? 


Hata waliojaribu kujenga mifumo mbadala kama Nyerere bado walikuwa na mapungufu makubwa kiitikadi. Ubeberu ni mradi wa kiuchumi, wao waliushambulia kisiasa. Licha ya kujaribu kujenga ujamaa kwa namna walivyoona inafaa, hawakujikita sana katika kuziondoa nchi zao katika mfumo wa kibepari wa kimataifa, wala kujenga uchumi wa kitaifa (national economy).


Hilo mosi, pili ni kwamba ipo haja ya kutofautisha mazingira yaliyowatengeneza masiha waliopambana na ubeberu katika sura ya ukoloni na hawa wa sasa wanaoibuliwa na soko holela la siasa. Ubeberu katika sura ya biashara ya utumwa na ukoloni ulikuwa ni wa moja kwa moja, na ulikuwa na mawakala wenyeji wachache. Ukatili wake ulikuwa ni dhahiri na haikuwa kazi ya masiha kuhubiri juu ya ukatili huo. Hivyo, Ilikuwa ni rahisi sana kusema: Mzungu akiondoka mambo yatakuwa sawa. Haikuwalazimu sana masiha wa wakati ule kutaja mifumo mbadala watakayoijenga ili kuleta uhuru wa kweli. 

Je, hivi sasa tukiambiwa mtu fulani [ma’ke masiha wa kitanzania huwa maarufu kuliko vyama vyao] akiingia madarakani ndio mwisho wa matatizo nasi tukubali tu bila kuhoji? Tena masiha wenyewe ni wa ‘kutengenezwa’ (‘artificial’): kupanda kwake kunategemea umoja katika mtandao uliomuunda, mtandao unaoanzia katika chama chake na kujieneza katika vyombo vyenye ushawishi katika jamii kama asasi zisizo za kiserikali, vyombo vya habari, vyuo vikuu, na hata madhehebu ya dini. Mtandao ukifarakana ndio mwisho wa umasiha! Tumeyashuhudia hayo walau katika vyama viwili. 

Sina hakika kama ‘masiha wa Mwl. Lwaitama’ atafika 2015 akiwa na umaarufu aliokuwa nao 2010. Historia ya vyama vingi Tanzania inatuonyesha kuwa umaarufu wa masiha ni katika uchaguzi mmoja tu. 

Dastan, nadhani hiki ndicho unachokihitaji: Sharti ‘tumvue nguo’ huyo masiha na kuonyesha ngozi yake halisi. Je, na sisi wanazuoni tutakuwa kama timazi [‘pendulum’] tukipanda na kushuka na masiha? Yaani, masiha akiwa mashuhuri nasi tunapanda nae na kumnadi, akishuka nasi tunashuka nae, akijisikia kuhama chama nasi tuhame nae, akifa kisiasa nasi tufe nae; kisha akiibuka mwingine nasi tuibuke nae? Halafu muda wote huo tukiwalisha matumaini wanyonge kuwa ‘huyu ndiye atakayewafikisha katika nchi ya ahadi’?

Mwandishi: Sabatho Nyamsenda

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP