Sunday, July 22, 2012

NA HAYA YA JKT TUTAYARUDISHA PIA?

"Afande Chacha alimsogelea [Sifuni], na sasa alikuwa akisema kwa sauti ya chini, "Sasa hizi taabu ulizozipata siku zote hizi za nini. Mimi nilikwambia siku nyingi kwamba ningeongea na Afande Kongoro awe anakupa kazi rahisi, lakini wewe umeendelea kuringa. Unaona sasa?" Baada ya kutopata jibu, aliendelea, "Nafasi yako ya mwisho, sivyo nitahakikisha kwamba unapohama wiki ijayo utapelekwa Kambi la Nachingwea kwenye nyoka wengi ukafe huko! Unasikia?" Sasa alikuwa amemsogelea, akijaribu kumshika, lakini kabla hajafanya hivyo, yule msichana alipiga ukelele mkali uliopasua anga na kusikika mbali...Pale ndani kulikuwa na mayai yamevunjika, matrei yametawanyika kama vile yametupwa. Afande Chacha alikuwa amesimama, kamnyooshea kidole cha kumkemea Sifuni, huku akiwa amejawa na hasira. "Unaona hasara unayolitia taifa hili? Unaona?" alipayuka kwa nguvu. Kisha aliwageukia maafande wenzake waliokuwa wamefika na kusema kwa sauti ya hasira, "Nimemkuta huyu msichana hapa akimeza mayai kama kenge! Nilipoingia alitaka kukimbia, badala yake akaangusha matrei ya mayai!" "Mwongo! Mwongo huyu!" yule msichana alipiga kelele huku akilia kwa nguvu. "Alitaka kuni..." (Chachage Seithy L. Chachage, Makuwadi wa Soko Huria, ukurasa wa 74 - 75)

"Nilikuwa mhudumu Officer’s Mess, mpishi na msafishaji. Huyo jamaa alikuwa ni mgeni kutoka Makao Makuu ya JKT Dar es Salaam. Kwa kweli sikutaka kufanya kazi pale Mess lakini tulichaguliwa special na Matron, mimi kwa vile niijua kupika vyakula mbalimbali hasa za kizungu. Lakini uzuri wa hiyo kazi ni kuwa uanambulia mabaki ya vyakula (leftovers), na mara nyingine kulikuwa hakuna. Basi huyo Afande alikaa kambini wiki kadhaa. Katika kumhudumia tukawa tunaongea na mimi nikawa namheshimu kama kaka vile. Wala sikusikia mapenzi yoyote kwake. Basi jioni fulani, kanialika chumbani kwake kunywa soda na biskuti na kwa Maongezi zaidi. Sasa kama ulienda jeshi unajua njaa kali unayokuwa nayo. Nikaenda, kanikaribisha vizuri, nilipewa soda na tukawa tunaongea. Basi nikaona mwenzangu anabadilika ghafla! Mara ananikumbatia kwa nguvu, na kunibusu na mengine. Nikajaribu kuaga lakini jamaa hakuniachia. Baada ya ku-plead naye aniachie, kaniachia. Kaomba msamaha na kaniomba niendelee kukaa nimalize hizo soda alizoninulia. Kama mjinga nikamwamini, nikakaa nakunywa hizo soda. Tukaendelea na Maongezi, kukaa kidogo huyo kanirukia, najaribu kusimama huyo, kanivuta na kuniangusha kitandani! Mimi saa hizo nikawa naogopa kabisa nia yake!Kaniambia eti, “ukipiga makelele najua nitasema nini! Nyamaza! Huna sababu ya kunikatalia!” LOH! Kanizaba kibao! Nikamwuliza kwa nini anaifanyia hivyo, na mimi nilikuwa namwona kama kaka yangu!Hapo sasa ikaniingia. Nabakwa! Loh!" Nilimpiga mangumi na mateke lakini..." (Chemi Che-Mponda,  http://swahilitime.blogspot.com/2011/08/marudio-miaka-baada-ya-tukio-kaniomba.html )

2 comments:

Chambi Chachage July 22, 2012 at 11:03 AM  

Asante Chambi,

Mimi hii hali ya jeshi imetukumba thru Dada yangu kabisa mtoto wa Ba Mkubwa,alipokuwa jeshini alipelekwa kuhudumia kwa mazingira kama ya hii story ya polisi officers Mess Story...akatendewa hayo aliyotendewa tena na Kiongozi wa Jeshi anayeheshimika sana sana katika jamii yetu na ambaye amewahi shika madaraka ya juu kabisa katika ngazi za jeshi na kitaasisi,leo hii Dada ni marehemu ila kila nikikukumbuka huwa inaniuma sana maana alipewa mimba na kiongozi huyo.in return mchumba wake ambaye alikuwa anamsubiri kumuoa huku akisoma chuo kikuu fulani hapa mjini akabadili mawazo....

Jeshini kwetu kuna unyama na unyanyasaji wa ajabu sana wakitumia vivuli vya utii wa kila amri upewayo na mkubwa

- ALEXAsante Chambi,
Hiyo ni ishu ambayo hata mimi nimekuwa natafakari juu ya hilo baada ya kusikia stori nyingi za unyanyasaji kijinsia ya wanafunzi wangu wakienda JKT. Riwaya ya Kajubi 'Mpenzi' ilikuwa na mfano mwingine tena. Iwapo hakuna hatua za makusudi kabisa, JKT ni mahali pazuri sana kwa wengine kunyanyasa kijinsia with impunity.

- RICHARD

Chemi Che-Mponda July 28, 2012 at 12:57 PM  

Huo unyanyasaji ungelalamika kwa nani? Kama huyo Afande alivyoniambia, "Piga Kelele najua nitasema nini!" Wasichana walinyanyawa na wengi walipata mimba za maafande. Yaani acha tu!

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP