Thursday, September 13, 2012

UZITO WA WITO WA ZITTO DHIDI YA VIZITO

 TANGAZO LA COCACOLA NA WITO WA ZITTO DHIDI YA VIZITO

Na Sabatho Nyamsenda

Zitto Kabwe ameandika makala yaliyochapishwa katika gazeti la Raia Mwema (toleo na. 259, Septemba 12 – 18, 2012), yenye kichwa Taifa la mafukara milioni 30 na mabilionea 30. Ni makala yaliyoandikwa kwa uhodari mkubwa wa lugha, yenye hoja jadidi na yaliyonakishiwa kwa takwimu stahiki. Lakini pia, ni makala ambayo yatamwacha msomaji akidai zaidi: “Mbona hakwenda mbali?” Pengine mwandishi kutokana na ‘ubize’ wake hakuwa na muda wa kutosha wa kutoa uchambuzi wa kina, ama hana uelewa wa kina juu ya mfumo anaopambana nao ama alikwepa kwa makusudi. Anajua mwenyewe. Lakini kwa vyoyote vile, haya ni makala yanayohitaji kupewa uzito stahiki. Mimi nimeandika mapitio haya ikiwa ni sehemu ya kutabaruku kazi hii muhimu ya ndg. Zitto.

Mijini hakuna mafukara?
Zitto anatutaka tuwe makini: hatuna budi kutofautisha umaskini na ufukara. Umaskini, anasema, ni ‘hali ya kukosa’ huduma/mahitaji ya msingi lakini ufukara ni ‘hali ya kukoseshwa’ huduma hizo. Na maskini wako mijini, mafukara vijijini. Zitto anaamini kuwa mjini kuna fursa [barabara, viwanda, umeme, n.k.] hivyo hakuna ufukara. Vijijini hakuna fursa, pamesahaulika. Mbaya zaidi, watu wa mijini [wakiwemo maskini] huwanyonya wale wa vijijini kwa kuwapunja bei za mazao yao na kufaidi huduma na miundombinu yote ya msingi. 

Ili kuepusha ubishi wa kidhana, ambao nadhani unaweza kupindisha mjadala, nitatumia neno fukara badala ya maskini kwa maana iliyokusudiwa na Zitto. Zitto anatuaminisha kuwa mjini hakuna mafukara: ‘Maskini wa mijini sio mafukara’. Kwamba wao huongezewa, badala ya kunyang’anywa, fursa kutokana na miundombinu na huduma. Lakini sehemu kubwa ya wakazi wa mijini ni wachuuzi, machinga, mama ntilie, wapiga debe, wabeba zege n.k. Hawa wamekimbia vijijini ama kutokana na ukosefu wa huduma na miundo-mbinu ama kutokana na kuporwa ardhi na kazi zao [mathalani, wakulima na wachimbaji wadogo] ili kupisha wawekezaji wakubwa. Wajapo mijini pia hufukarishwa. Ni mara ngapi tumeshuhudia makundi hayo niliyoyataja hapo juu wakifukuzwa ‘kama mbwa’ ili kusafisha jiji? Wamefukarishwa vijijini, wanafukarishwa mijini pia. 

Huduma na miundombinu ijengwayo mijini sio kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watu wa tabaka la chini, ambao ndio wengi mijini. Na kwa kweli, kila eneo [haijalishi ni la mjini au kijijini] linapowekewa huduma thabiti za afya, elimu, umeme, maji na barabara, walio mafukara huporwa maeneo hayo ama kwa hila ama mabavu na kusukumwa mbali zaidi ili wakaishi maeneo yasiyo na huduma hizo. Fukara hana haki ya mahitaji ya msingi!

Wala mafukara wa mijini hawana kauli juu ya bei za vyakula [vizalishwavyo na mafukara wenzao wa vijijini] na mahitaji mengine ya msingi. Bei hizi hupanda kila uchao na mafukara hawa wa mijini wapigapo kelele huambiwa hazipandishwi na watu bali ‘soko’. Hivyo, wenye serikali hawana chochote cha kufanya kwani soko lina akili ya kujiendesha lenyewe na ni dhambi kuliingilia. Idadi ya milo na aina ya vyakula walavyo mafukara wa mijini, mabanda waishimo, kazi wafanyazo, n.k. haziwezi kuwatofautisha na wenzao wa vijijini. Wote ni mafukara, wote wamefukarishwa na hawana budi kubomoa chanzo cha ufukara wao. Hakuna anayefaidi kuliko mwenzake hapa! Lakini je, chanzo cha ufukara ni nini hasa?

Kiini cha ufukara nini?
Zitto anadai, ‘Ufisadi unasababisha ufukara’. Hilo halina shaka. Lakini msomaji makini atagundua kuwa Zitto anataja vyanzo kadhaa vya ufukara vikiwemo sera na mikakati, watawala wetu na hata wakazi wa mijini. Tuzungumzie hicho chanzo kikuu – ufisadi. Zitto ametoa mifano kadhaa ya ufisadi ulioibuliwa nchini mwetu. Yote inafahamika kwani ndio wimbo kwenye vyombo vya habari. Kwa ufupi, anasisitiza kuwa chanzo ni uporaji ulioharamishwa kisheria ambayo ndiyo maana iliyokusudiwa ya ufisadi. Na uporaji huo hutajirisha kikundi cha watu wachache tu na kufukarisha mamilioni ya Watanzania. Kwa maana nyingine, sheria zikibadilishwa na kuhalalisha uporaji huo, msamiati wa ufisadi utakuwa umepoteza maana. Je, ufukara utakwisha?
Na mifano ipo mingi juu ya sera na sheria mbalimbali zitungwazo ili kuhalalisha uporaji. Nchi yetu ilipofanya mageuzi ya uchumi, sera mpya zilitungwa na kupigiwa msumari wa sheria. Hivyo, mambo yote yaliyokuwa yameharamishwa wakati wa utaifishaji, yakahalalishwa wakati wa ubinafsisaji, likiwemo suala la viongozi kujilimbikizia mali.
Pengine ipo pia haja ya kuzungumzia uporaji uliohalalishwa kisheria ambao ndio chanzo halisi cha ufukara. Na uporaji ndio umekuwa mbinu kuu ya kujipatia mtaji katika historia nzima ya mfumo wa kibepari. Mwandishi hajautaja, seuzi kuujadili, ubepari/ubeberu wala sura yake ya sasa, uliberali mambo-leo, katika makala yake. Sababu anaijua mwenyewe. Msomaji atabaki akijiuliza: Je, ni kuogopa kuonekana 'mjamaa' na hivyo kupunguza mashabiki? Au ni kuepusha balaa la watu kuanza kuhoji itikadi za vyama, kikiwemo chake? Au ni kukwepa kwa makusudi kufungua watu kuwa hata mishahara na marupurupu ya wabunge [mbali ya 'posho za kukaa kitako' kama anavyoziita] ni sehemu ya uporaji uliohalalishwa kisheria?

Pamwe na ufinyu huo wa dhana ya ufisadi na mfumo unaozalisha ufisadi, makala ya Zitto yaweza kuwa na ladha ya muarobaini kwa waliojibatiza ‘umalaika’ [wengi wakiwa wa chama chake] katika vita dhidi ya ‘mashetani’, yaani mafisadi. Ufisadi ni sehemu ya mfumo, hivyo, kama asemavyo Zitto, ‘ni lazima kuondoka kwenye hali ya kwamba; ushujaa ni kutaja tu fulani na fulani ni fisadi’. Hivyo mpambanaji halisi wa ufisadi sharti apambane na mfumo unaozalisha mafisadi. 

Nani alaumiwe?
Makala haya yanatupa lawama kwa watawala wetu kwa kuwatelekeza mafukara wa vijijini na kukumbatia sera zinazozalisha ufukara. Yanahukumu kakundi ka watu wachache kanakotajirika kwa kufukarisha mamilioni. Wote hawa ni wa ndani ya nchi. Sijui kwa nini mwandishi ameamua kutumia mrengo huo wa ‘ndani ya nchi’ na kuacha kabisa kujadili mfumo wa kibepari wa kimataifa (ubeberu) ambao ndio kiini hasa. Kila aina ya ufisadi unaotajwa na mwandishi unahusika moja kwa moja na makampuni ya kimataifa na mtaji toka nje. Hivyo, ipo haja ya kwenda katika mizizi kwani watawala wetu na ‘mabilionea’ anaowataja mwandishi ni mawakala tu wa ndani wa mabeberu. Ndio maana mwaka 2010 rais wetu, baada ya kulalamikiwa sana juu ya uwingi wa safari za Marekani alipasua jipu: kwamba alipochaguliwa tu mara ya kwanza (2005), safari yake ya kwanza alikwenda Marekani lengo likiwa ni ‘kuomba baraka za wakubwa’, nao baada ya kumsaili wakamwambia: ‘Yes. You are a good man’. Sina hakika kama walitaja good man ama good boy!

Na hao 'mabilionea' wa Zitto, je? Wao ni mawakala tu wa mtaji wa  kimataifa. Kampuni ya Coca Cola ni mfano thabiti juu ya makampuni za kibeberu zilivyojitandaza na kuinyonya Afrika huku watawala wa Kiafrika wakishangalia. Na kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere, mwezi Mei 1989, akizungumza na vibepari uchwara vya Bongo [ambao Zitto anawaita 'mabilionea']:

Kwa Coca-Cola kwa sababu Marekani wao wana nguvu sana kwa Coca-Cola, Marekani sasa anataka wote tuwe wanywa Coca-cola.
Ndugu Mengi, mkipenda msipende mtatuuzia tu Coca-Cola basi kwa Coca-Cola inauzwa tu… Kwa hiyo tunajivunia ule ugonjwa… tunajivunia ule ugonjwa wala hatuuonei haya.. unaparedi silaha za wakubwa, unaparedi madege ya wakubwa, unaparedi macoca-cola ya wakubwa na unajivunia tu, unasema sisi tumeendelea. Ukimwambia umeendelea kwa nini, anakwambia ’njoo uone mabarabara yetu’[1]

Ndio maana, wakati mafukara wakilalamika juu ya ugumu wa maisha, watawala wanawashangaa na kuhoji ‘mbona huko nje tunasifiwa?’

Tafakuri iendelee
Lakini nani atayasoma makala haya? Nani atayatafakari? Nani atayazingatia? Zitto anahofia kuhusu maisha ya sasa na ya baadae. Wengi wetu tumesinzia. Ndio maana Coca Cola katika tangazo lao jipya, ambalo linachezwa sana redioni na kwenye televisheni, wanaisifu sana Afrika: ‘Kuna sababu bilioni moja za kuipenda Afrika’, tangazo linasema, ‘Wakati ulimwengu unahofia kuhusu maisha ya baadae… Waafrika bilioni moja wanafurahia Coca Cola’! Ndiyo. Coca Cola wako sahihi kabisa, tumesinzia! Sijui kama watatoa tangazo la namna hiyo kuisifia Bolivia ambayo, pamoja na kutaifisha makampuni ya kibepari katika sekta kuu za uchumi, imewaamuru Cocacola kufunga virago vyao ifikapo Desemba 2012. Wabolivia wameapa kujenga nchi mpya na mfumo mpya unaozingatia utu na usawa badala ya vitu na tamaa ya kujilimbikizia. 
Natoa wito kuwa makala ya Zitto yasomwe, yajadiliwe na yawe chachu kwa wale waliochoshwa na jinsi mambo yanavyoenda na hivyo kudai mbadala. Naamini, baada ya kuyasoma makala hayo, nchi nzima itakaa chini kujitafakari juu ya tulipotoka, tulipo na twendako. Hata chama cha Zitto, naamini kitayatumia makala haya kujenga msingi wake wa kiitikadi, msingi ambao utakifanya kuwa chama hasa cha wanyonge badala ya chama cha wajasiria-siasa wanaobwabwaja maneno ili wachaguliwe katika – nikiazima kirai cha mwandishi – ‘nafasi za ulaji’. Zitto pia achukulie ukosoaji unaofanywa katika andiko lake kama msingi wa kujiimarisha zaidi, kulikana tabaka lake kinadharia na kivitendo na kujitanabahisha na makabwela [ambalo ndio chimbuko lake] ili arejee kuwa Zitto Kabwe badala ya Kizito wa Makabwela!  

[1] Imenukuliwa toka Shivji, I.G., 2004, “Reforming Local Government or Localizing Government Reform”, in Mpangala, G.P. et al (eds), The Commemorations of Mwalimu Julius K. Nyerere’s 79th and 80th Birth Dates. Dar es Salaam: MNF.

CHANZO CHA MAKALA: 

VYANZO VYA PICHA:
g

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP