Wednesday, October 24, 2012

Karibuni Tujadili Maendeleo ya Uchumi Linganishi

Japo sidhani kama mada hii itapata wanamjadala wengi kama ile mada nyingine inayogusa sana hisia za watu na inayeendelea kujadiliwa sana nchini ningependa kuwakaribisha tu. Naam nawakaribisha tujadili hoja mbalimbali ambazo zimeibuliwa na kundi ambalo linafanya kile ambacho mwanahistoria wa Afrika, Anthony Hopkins, anakitambulisha kama 'Historia Mpya ya Uchumi wa Afrika'. Hili kundi limetiwa chachu na tafiti za Daron Acemoglu, Simon Johnson na James Robinson ambao kwa kifupi watu wanapenda kuwaita AJR. Katika kundi hili wapo kina Nathan Nunn, Philip Osafo-Kwaako (ambaye anafanya tasnifu kuhusu Tanzania), Avner Grief, Jeremiah Dittmar, Sascha Becker, Guido Tabellini, Stanley Engerman na Kenneth Sokolof (ES), Tristan Reed, Marcella Alsan, Leonard Wantchekon na wengineo. Karibu wanazuoni wote hawa wana tovuti zao mtandaoni zenye machapisho yao na takwimu mbalimbali walizotumia ambazo tunaruhusiwa kuzitumia kuthibitisha walichogundua ama kuzichambua kwa ajili ya ugunduzi wetu wenyewe. Kwa ujumla tafiti zao zinalinganisha maendeleo ya kiuchumi ya muda mrefu kati ya mabara, nchi, jamii, 'makabila. na hata dini mbalimbali.

Ningependa tupitie baadhi ya hoja zao hasa ambazo zimewasilishwa katika kitabu kipya cha AJR ambacho dondoo zake zinapatikana hapa: http://whynationsfail.com/ . Kwa kuanzia, tujadili kwa nini Afrika (inaonekana) imeachwa nyuma (sana) katika maendeleo ya kiuchumi katika kipindi cha miaka 500? Je, ni kwa sababu ya 'kubadilika kwa mafanikio' ambako kina AJR wanadai kunatokana na kusimikwa, kwa wingi, kwa taasisi ambazo zinapora rasilimali badala ya taasisi ambazo zinajenga mfumo wa kulinda mali (binafsi)? Au ni kwa sababu ya kile ambacho kinafanana na madai ya ES kuwa aina za 'ukoloni mbaya sana', 'ukoloni mbaya' na 'ukoloni mzuri' zimekuwa na athari tofauti na za muda mrefu sana kati ya nchi na hata ndani ya nchi husika ambapo maeneo fulani yameendelea kuwa na uchumi mzuri ilhali maeneo mengine yameendelea kuwa uchumi mbaya. 

Kwa Tanzania, hoja yao inaweza kumaanisha baadhi ya maeneo yanaendelea kuwa na uchumi mzuri zaidi ukilinganisha na yale maeneo yaliyokuwa na mfumo mbaya sana wa manamba, uchimbaji wa madini na kadhalika wakati wa ukoloni. Na kama ni hivyo, basi, nini kifanyike kubadili tofauti hizi za kihistoria?

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP