Friday, October 19, 2012

Uislamu,Ukristo,Upagani na Dai la 'Mfumo Kristo'

Japokuwa nchi yetu ya Tanzania inaongozwa na Rais na Makamu wa Rais walio waislamu na ina Katiba ambayo siyo ya kidini bado kuna madai kuwa tupo chini ya 'Mfumo Kristo'. Ukiichambua kwa mapana dhana ya 'Mfumo Kristo' utaona inamaanisha 'Mfumo wa Kimagharibi' kwa kuwa kwa kiasi kikubwa taasisi, elimu, taratibu na sheria zetu zinatokana na 'Ustaarabu wa Kimagharibi' (Western Civilization) ambao unasemekana ni zao la 'Ustaarabu wa Kikristo' (Christian Civilization) ulioletwa 'kwanza' kwetu na wamishionari na wakoloni waliotoka katika 'nchi za kikristo na kimagharibi'. 

Ndio maana kama hivyo ndivyo watoa madai wanavyoamini basi kushambulia watu au/na vitu ambavyo hatuoni uhusiano wa moja kwa moja na madai yao mengine, ni sehemu ya kupambana na huo wauitao 'Mfumo Kristo'. Hoja hii haipingani na hoja jadidi ya Mwanasosholojia wa Dini kuwa nchi yetu iko katika ombwe la itikadi/dira ya kitaifa na matatizo ya ajira na ujira hasa kwa vijana hivyo kufanya iwe kazi rahisi kuwafanya waone tatizo ni huo 'Mfumo Kristo' ambao wanauona ndio, kihistoria, umewanyima elimu na ajira. 

Kwa mfano, mjomba wangu ambaye ni muislamu anadai kuwa tunakosea tunapomsifu Mwalimu Nyerere kwa kuchukua shule za wamishonari/makanisa na hivyo eti kuwasaidia waislamu wasome. Kwa mujibu wa tafsiri yake ya historia ya Tanzania, moja ya sababu ya waislamu kuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru ni ili waweze kujenga shule zao wenyewe zitakazotoa elimu bila kulazimika kufuata misingi ya wakoloni na wamishionari ambao walikuwa ni wakristo. Hivyo kwa tafsiri yake, Nyerere alichofanya baada ya uhuru ni kuwazuia waislamu wasiweze kujenga shule zao na hivyo kuwafanya, kwa ujumla, waendelee kuwa nyuma kuliko wakristo. Inawezekana kabisa kuna ukweli katika hilo.

Ni vigumu kuelewa hoja hizo bila kuvua lensi za Kikristo na kuutafiti kwa kina ukweli wake. Tunapaswa kuelewa watoa madai wanamaanisha nini hasa wanaposema kuwa tatizo ni 'Mfumo Kristo' kujikita katika nyanja ya maisha na taasisi zetu. Inabidi tuwaelewe na tujielewe kwa undani kwanza. Na kama alivyosema mpagani fulani, kudhani kutofikiria dini ni kutokuwa na udini ni sawa sawa tu na kudhani kutofikiria rangi (color blindness) ni kutokuwa na ubaguzi wa rangi. Hivyo, tunapaswa kujiuliza, je, kweli tumesimika mfumo ambao kwa kudhani haufikirii dini (religion blindness) unawaacha nyuma waumini wa dini fulani? Kwa mantiki hii, inawezekana kabisa kuwa yale maneno ya Nyerere, aliyoyarejea mwaka 1995 kuhusu Tanzania kutokuwa na dini, kuhusu yeye binafsi kutofikiria suala la dini wakati wa kuteua viongozi ni sehemu ya upofu wa dini unaopelekea watu wa dini fulani wasahaulike kwa kuwa hawaonekani kuwa wapo.


[Kwenye hotuba hii Nyerere anaongelea udini kuanzia dakika ya 10 na sekunde 21]

2 comments:

Anonymous October 23, 2012 at 8:58 AM  

Suala sio kukataa kwamba hakuna "mfumo Kristo" sio la hekima. Cha muhimu ni kutafiti ina maana gani, ilianza wapi na ina maanisha nini kwa watu tofauti. Hapo hapo kuna suala la kihistoria nchi za kimaghraibi zinajiona na kwa upande fulani ni zao la tamaduni za kikristo. Sio mimi nasema hilo msome Max Weber ujionee mwenyewe na sikiliza hotuba za viongozi wengi wa magharibi. Kwa hio kukataa hilo ni kukataa historia. Kwangu mimi ni suala la haki za wananchi ndio kitu cha msingi. Kumbuka utamaduni wa kiislamu umechukua mengi kwa Wakristo na Wakristo walisaidia kwenye mambo mengi ya kiutawala na kisayansi kwa waislamu kwa mfano kule Spain, Syria na Turkey.

Anonymous December 15, 2013 at 12:13 AM  

Max weber nae kafiri huyo mfumo huo huo

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP