Monday, November 19, 2012

Buriani Mwenyekiti wa Tume ya Makweta

"Ulale Panapostahili Mzee Makweta, labda sasa watu watasoma Ripoti ya Makweta ya 1982 iliyopendekeza kutumia Lugha ya Kiswahili kama  Lugha ya Kufundishia masomo yote  tangu elimu ya wali hadi Chuo Kikuu huku Kiingereza kikifundishwa vizuri kama somo kwenye Taasisi ya Lugha za Kigeni (Institute of Foreign Languages) na matawi yake nchi nzima...Ripoti ilipuuzwa na leo tunavuna matunda ya ukaidi huu dhidi ya kazi nzuri ya utafiti wa miaka miwili uliyoisimamia vizuri. Mimi nitakukumbuka pia kwa sura yangu kufananishwa na  ya kwako!!!Ulale Panapostahili Mzee Makweta!! Nabubujikwa na machozi nikiona jinsi mfumo wa elimu wa enzi zako  ulivyovurugwa na wanasisa wenye kutojali matokeo ya kutowekeza vyakutosha katika elimu  na kung'ang'ania  sera ya lugha ya kufundishia  ya kimamluki inayofuatwa sasa ya kudhani eti elimu ni kujua Kiingereza tu basi....matokeo  ambayo kati ya viashiria vyake ni wahitimu mbumbumbu mzungu wa reli wa mambo yote ya kisayansi wenye imani potovu za kishirikina kama zilivyojitokeza  katika  matukio ya Mbagala  yaliyozaa kuchomwa moto  makanisa...Mfumo  wa  elimu unaozidi kuwagawa Watanzania kitabaka, kikanda, kikabila,  na kidini. Mungu atunusuru na matokeo mengine hasi mbele ya safari...Kifo chako kizindue Watanzania zaidi na zaidi wenye dhamira ya kuthubutu kupigania utekelezaji wa Ripoti ya Makweta katika mazingira ya sasa kwa kuunda Tume ya Makweta ya miaka hii. Ulale Panapostahili Mzee Makweta" - Mwalimu Lwaitama

"[Mwalimu] Lwaitama na Wote Mlioguswa na Msiba huu mkubwa!!! 

Kwetu sisi, Wapigania Ukombozi na wapenda Mabadiliko, na Maendeleo tumepata PIGO KUBWA kuondokewa na mtetezi wa Elimu ya Ukombozi kupitia katika Lugha ya Kiswahili. 

Kama ulivyosema kwa usahihi, Mwalimu Nyerere alipounda tume hiyo chini ya Ndg. Jackson Makweta, alitarajia kuwa matokeo ya utafiti wa tume hiyo, yatainufaisha Tanzania na kuiletea mabadiliko. Hakuna kitu kilichomsononesha Waziri Makweta, kama kudharauliwa kwa matokeo ya utafiti wake huo (kulikofanywa kwa makusudi na mtu aliyepewa dhamana ya kuupitia na kutoa ushauri wa kitaalamu).

 Katika makala aliyoiandika mwishoni mwa mwaka jana ili kuiwasilisha katika Mkutano ulioandaliwa na HakiElimu na Shule Kuu ya Elimu hapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Ulifanyika katika Ukumbi wa Mihadhara Yombo), Mzee Makweta alisema maneno ya uchungu kabisa kuhusiana na mwenendo wa Elimu Tanzania na jinsi ambavyo mawazo yake yalipuuzwa na kusababisha mporomoko huu wote. Hakuweza kuwepo kuiwasilisha mwenyewe, lakini makala ilitumwa kwa waandaaji na kutolewa hadharani....

Katika makala hiyo naomba sasa ninukuu mistari michache aliyoiandika kwa uchungu mwishoni mwa makala hiyo:

"...sasa ninakubaliana na Karl Max aliyesema kuwa "utumiaji nguvu, ni mkunga wa kila jamii iliyo na mimba ambapo ni lazima mtoto azaliwe... [katika hali hiyo] nguvu hiyo ni ile ya kiuchumi....  inafikia wakati uamuzi mgumu ni lazima ufanyike katika maisha ya mjamzito ambaye muda wa kujifungua umefika, na yeye hajifungui, kinachofuata ni upasuaji, ili kuokoa maisha ama yake na mtoto au yake mwenyewe....Wakati kama huu, umefika kwa Tanzania sasa, ikiwa tunataka kuwa na maendeleo ya kweli ....."  Mwisho wa kunukuu.

Kwa mkosi mkubwa, mawazo ya Ndg. Makweta kuhusu elimu YALIPINGWA NA PROFESA MMOJA WA ELIMU  ambaye KWA SABABU ZA UBINAFSI NA ZA KUPATA PESA, alionesha kuwa kungelikuwa na matokeo tofauti ikiwa mawazo ya Mzee  Makweta yangelifuatwa. BAADAYE PROFESA HUYO ALIITWA MSALITI WA UMMA WA WATANZANIA - jambo ambalo hajaweza kukanusha hadi leo. Huu ulikuwa mkosi. Na katika makala hiyo, Mzee Makweta anaandika kwa kusononeka kuwa hakuona ni kwa nini utafiti wake ulipingwa bila kuonesha mawazo mbadala wa maendeleo ya elimu Tanzania.

Wanaojua kisa hiki, wanaelewa ninachokiandika.

Mungu amlaze Mzee Makweta mahali pa raha ya kiroho. Ajue kuwa bado kuna baadhi ya watu - na labda ni wengi, ambao wanayaenzi, kuyaheshimu na kuyapigania mawazo yake kuhusu elimu ya ukombozi"

- Dakta Mutembei

CHANZO CHA KUMBUKIZI:

CHANZO CHA PICHA:

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP