Tuesday, November 13, 2012

Mizengo Pinda: Tusilaumiane Kuhusu Kiswahili

IV UENDELEZAJI WA LUGHA YA KISWAHILI 


22. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Bunge, Waheshimiwa Wabunge walipokea na kujadili pamoja na mambo mengine Maazimio mbalimbali. Niruhusu nirejee Azimio lililonigusa sana kuhusu Uanzishaji wa Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili. Awali, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Chama cha Kiswahili Tanzania (CHAKITA) na Wawakilishi kutoka Uganda walianzisha wazo la kuwa na Mpango wa Kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki. Hata hivyo, Baraza hilo halikuanzishwa, badala yake ikapendekezwa kuanzisha Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili. Azimio la Kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo ya Lugha ya Kiswahili tumelipitisha katika Bunge hili. Nitumie fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri sana mliyoitoa. 

23. Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala kuhusu kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo, michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge imeonesha umuhimu wa kutumia fursa zilizopo kwa Tanzania kuwa Dira, Mfano na Kitovu cha Lugha ya Kiswahili. Aidha, Waheshimiwa Wabunge walionesha umuhimu wa kutumia Kiswahili kama nguzo imara ya Mshikamano, Amani na Utulivu miongoni mwa Watanzania. Lakini pia majadiliano yamebaini Changamoto zilizopo. 

Moja ya Changamoto hizo ni hoja ya Waheshimiwa Wabunge wengi kwamba, Nchi jirani ya Kenya inatumia fursa zilizopo za Lugha ya Kiswahili vizuri zaidi kuliko sisi. Kutokana na uzito wa hoja hiyo, ndiyo maana ninapenda nami niseme machache. 

24. Mheshimiwa Spika, Tanzania ni Mdau Mkuu wa Matumizi ya Kiswahili katika Afrika. Ziko taarifa kwamba Watanzania ndiyo walioanzisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Ghana, Chuo Kikuu cha Port Harcourt, Nigeria na Chuo Kikuu wa Sebha, Libya. Inawezekana upo ukweli pia kwamba leo hii wengi walioko katika Vyuo hivyo ni kutoka Kenya. Japo imekuwa vigumu kupata takwimu za Ajira ya Walimu wanaofundisha katika Nchi hizo kutokana na kwamba ajira iko katika Soko Huria. Hakuna Chombo maalum kinachoratibu Ajira za Walimu hao kwenye Vyuo Vikuu. Nina hakika hii ni moja ya sababu zilizofanya Wachangiaji wengi kutumia “Uzoefu” zaidi katika kujenga hoja hiyo kwamba Walimu wengi wanatoka Kenya. Wakati sasa umefika wa kuwa na Utaratibu Maalum wa upatikanaji wa Walimu wa Kiswahili wenye sifa za kufundisha Nje ya Nchi. 

25. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wameainisha mapungufu mbalimbali ambayo yanachangia katika tofauti iliyopo kati yetu na jirani zetu wa Kenya. Pamoja na mapungufu hayo, bado Tanzania imekuwa Kitovu cha Lugha ya Kiswahili Duniani. Walimu wa Kiswahili Nchini Ujerumani, Hamburg, Berlin, Colon, Leipzig na Chuo cha INALCO Ufaransa, walifundishwa na Walimu kutoka Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) Zanzibar na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwalimu wa Siku Nyingi wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha London (School of Oriental African Studies - SOAS) anatoka Tanzania, Prof. Farouk Topan ambaye ndiye alikuwa Mkuu wa Kwanza wa Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Walimu wa Kiswahili hadi sasa kule Korea, katika Chuo Kikuu cha Hankuk wanatoka Tanzania. Walimu wa Osaka, Japan walitoka Tanzania, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Zanzibar. 

26. Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, yapo mahitaji makubwa ya Lugha ya Kiswahili kwa sasa. Katika Afrika ya Mashariki peke yake, Uganda wanahitaji Walimu zaidi ya 10 kwa ajili ya Vyuo vyao Vikuu. Vilevile, wanataka Walimu katika Shule za Sekondari. Rwanda na Burundi wanahitaji Walimu na Jamhuri ya Watu wa Kongo (DRC) wanahitaji Walimu kwa ajili ya Vyuo vyao vya Lubumbashi na Kalemie. DRC wanahitaji pia Vitabu vya Kiswahili Sanifu. 

27. Mheshimiwa Spika, mahitaji ya Kiswahili yako katika Nchi nyingi. Chuo Kikuu cha Kwazulu, Natali, Afrika ya Kusini kimeanzisha masomo ya BA Kiswahili, hivyo, watahitaji Walimu. Chuo Kikuu cha Zimbabwe kinahitaji Walimu wa Kiswahili. Namibia wameomba Walimu kuanzisha Kiswahili katika Chuo chao Kikuu. Jamaica Wanahitaji Walimu wa kuanzisha masomo ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha West Indies. Baadhi ya Vyuo Vikuu vya Marekani kikiwemo Chuo Kikuu cha Lugha cha Monterey, California wanahitaji Walimu wa Kiswahili. Hapa Nchini Vyuo Vikuu zaidi ya 20 kando ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam vimeanzisha Masomo ya Kiswahili na vitahitaji Walimu wenye Shahada za Uzamili na Uzamivu katika Kiswahili. Hivyo, mahitaji ni makubwa kupita kiasi na hivyo hii ni fursa kubwa kwa Watanzania wenye sifa kujipatia ajira. 

28. Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Desemba 2005, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akifungua rasmi Bunge jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema na nanukuu: 

“Lugha ya Kiswahili imeanza kupata umaarufu Afrika na Duniani. Umoja wa Afrika umekubali Kiswahili kuwa moja ya Lugha zake Kuu. Aidha, Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu zimekubali kutumia na kuendeleza Kiswahili. Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha kuwa juhudi hizi zinaendelezwa na kuhakikisha kuwa Lugha ya Kiswahili inakua Nje ya Mipaka ya Afrika”.

Mwisho wa Kunukuu. 

29. Kwa maneno haya ya Mheshimiwa Rais, ni dhahiri kwamba, Serikali inajali umuhimu wa kuendeleza Lugha ya Kiswahili, kwa vile ina nafasi nzuri ya kupanuka na kushiriki katika ujenzi wa Jamii ya Watanzania na Jamii mpya ya Afrika ya Mashariki na hata Duniani kote. 

30. Mheshimiwa Spika, tunayo Changamoto ya kukifanya Kiswahili kiwe Lugha ya Dunia. Lakini pia tunalo jukumu la kuhakikisha kwamba Lugha ya Kiswahili inafundishwa na kutumika Mashuleni, ikiwa ni pamoja na Shule za Msingi, na kwamba inafundishwa katika Shule za Sekondari na Vyuo vya Elimu ya Juu. Aidha, tunahitaji kuhakikisha kwamba Lugha ya Kiswahili inatumika vizuri na kwa ufasaha katika Shughuli za Serikali, hapa Bungeni, katika Mahakamani na maeneo mengine kwa faida ya Wananchi wetu na Taifa kwa ujumla. Hata hivyo, pamoja na msisitizo huo, yapo maeneo ambayo tunahitaji kuyafanyia kazi zaidi. Kwa mfano: 

Moja: Bado kuna maeneo mengi yanayohusu Taaluma ya Kiswahili ambayo hayajafanyiwa utafiti wa lugha. Utafiti ndio uhai wa Taaluma na chimbuko la maarifa mapya. Ni kazi ya Wanataaluma wa Kiswahili kufanya tafiti za kina ambazo zitakifanya Kiswahili kitumiwe Kimataifa.

Pili: Vyuo Vikuu vilivyoanzishwa, pamoja na kuweza kufundisha somo la Kiswahili kwa Wanachuo wa Shahada ya Kwanza, bado havina Wahadhiri wa kutosha wa kufundisha mafunzo ya Uzamili na Uzamivu. Tunalo jukumu la Kuanzisha Programu za Shahada za Uzamili na Uzamivu zitakazokidhi mahitaji makubwa ya uhaba wa Wataalamu wa Kiswahili Ndani na Nje ya Nchi. 

Tatu: Hapa Nchini hakuna Chuo Kikuu kinachotoa mafunzo ya Ukalimani. Watu wanaohitaji stadi hii ya ukalimani wanalazimika kwenda kusomea katika Vyuo Vikuu vya Nje ya Afrika Mashariki. Mimi najiuliza, hivi hili nalo tunalikubali wakati Lugha ni yetu? Ninaamini tunao uwezo wa kutumia Vyuo Vikuu na Vyuo vingine tulivyonavyo kufanya kazi hii ya kufundisha Wakalimani. Ni vizuri Vyuo vyetu Nchini vianzishe Idara za Mafunzo ya Ukalimani ili kupunguza tatizo hilo.

Nne: Imebainika pia kwamba, hata kama kukiwepo na Wakalimani, bado hakuna Kumbi za kisasa zenye vifaa vya kusikilizia Tafsiri za Lugha mbalimbali. Kumbi nyingi tunazofanyia Mikutano tukiacha Ukumbi wa Kimataifa wa Arusha (AICC) hazina Vifaa hivyo. Changamoto tulio nayo kama Nchi na hasa Wawekezaji wa Kumbi za Mikutano ni kuhakikisha Kumbi zinazojengwa na zilizopo zinakuwa na Vifaa vya kutoa huduma ya Ukalimani. Lengo ni kutumia fursa hiyo katika kukuza Lugha yetu ya Kiswahili. 

31. Mheshimiwa Spika, mimi napata shida sana kuona Warsha yenye Wageni wasiozidi Kumi (10) na Waswahili 200 inaendeshwa kwa lugha ya Kiingereza, tena bila kujali kama Waswahili hao wanaelewa Kiingereza au la. Wanachojali ni kuwafurahisha Wageni wachache. Kwa maoni yangu hii ni kasumba isiyo na maelezo. Changamoto iliyo mbele yetu ni kuondoa kasumba hii kwa kupenda kutumia lugha yetu ya Kiswahili wakati wote. Tuondoe wasiwasi katika matumizi ya Lugha ya Kiswahili. Tumeshuhudia Kiswahili kikikuzwa na kutandazwa katika Mifumo ya Kompyuta ya Linux na Microsoft. Tumesikia pia kwamba, kama njia mojawapo ya kuboresha matumizi ya Kiswahili sanifu, tayari Wataalamu wa lugha kwa kushirikiana na Wataalamu wa Kompyuta wameweza kutengeneza Programu Maalum ya Kisahihishi cha Lugha ya Kiswahili katika Kompyuta ambayo inatumiwa kusahihisha maneno ya Kiswahili. Haya ni maendeleo makubwa yaliyofikiwa ya kukiingiza Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Duniani. 

32. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba Lugha ya Kiswahili imekua sana. Wote ni mashahidi kwamba Mashirika makubwa ya Utangazaji Duniani yanatangaza Kiswahili. Tunajua sana Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Sauti ya America, Radio ya Ujerumani Deutsche -Well na Radio France International. Wako pia Al Jazeera, Radio Vatican, Radio Japan na Radio ya Umoja wa Mataifa. Aidha ziko Nchi zenye Vituo vya Radio vinavyotangaza kwa lugha ya Kiswahili, kwa mfano, China, India, Syria, Misri, Sudan n.k. Hii pia ni ishara kwamba Kiswahili kinakua kwa kasi sana. 

33. Mheshimiwa Spika, tunaweza kuongea mengi ya nadharia kuhusu lugha yetu nzuri ya Kiswahili kwa muda mrefu. Tunatakiwa sasa tuanze kutekeleza hayo mengi kwa vitendo. Naomba kuhimiza Taasisi mbalimbali Nchini, ziweke juhudi zote katika kukuza Lugha ya Kiswahili ili iweze kutumika katika Nyanja zote za mawasiliano ikiwemo Sayansi na Teknolojia. Vilevile, natoa Rai kwa Watanzania wote wakiwemo Waheshimiwa Wabunge kujitahidi kila tunapozungumza Kiswahili kuepuka kuchanganya na maneno ya Lugha ya Kiingereza kwenye mazungumzo yetu. 

34. Baadhi yetu tunamkumbuka Mwandishi na Mshairi wa Riwaya Bwana Shaban Robert (1909 – 1962) ambaye aliandika kuhusu Lugha ya Kiswahili na kukifananisha na ladha ya Titi la Mama. Katika moja ya Mashairi yake, aliandika na nanukuu: 

“Titi la Mama litamu, hata likiwa la Mbwa, Kiswahili naazimu, sifayo iliyofumbwa, Kwa wasiokufahamu, niimbe ilivyo kubwa, Toka kama mlizamu, funika palipozibwa, Titi la Mama litamu, jingine halishi hamu. Lugha yangu ya utoto, hata sasa nimekua, Tangu ulimi mzito, sasa kusema najua, Ni sawa na manukato, moyoni mwangu na pua,Pori bahari na mto, napita nikitumia, Titi la Mama litamu, jingine halishi hamu”. 

Mwisho wa Kunukuu. 

35. Anachosema Bwana Shaaban Robert ni kuonesha thamani ya Kiswahili jinsi kilivyo na utamu wa aina yake katika matumizi. Historia ya Shaaban Robert, tunaambiwa alithubutu kulikataa kabila lake la Kiyao na kujiita Mswahili kuonesha jinsi alivyokipenda Kiswahili. Nasi tujivunie Kiswahili, tukipende, tukitumie, tukienzi na tukithamini. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumechangia katika kuendeleza Lugha ya Kiswahili. 

36. Mheshimiwa Spika, Watanzania sasa si wakati wa kulalamikiana na kulaumiana juu ya Matumizi ya Lugha ya Kiswahili, bali sasa tushirikiane kujenga Lugha yetu ya Kiswahili. Njia iko wazi, nadhani sasa kazi kwetu!

Hotuba: 

Picha:

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP