Saturday, November 24, 2012

Tupigie Kura (Referendum) Lugha ya Kufundishia?

UFUATAO NI UCHAMBUZI  MFUPI WA MFUATILIAJI WA KARIBU WA UKUSANYAJI WA MAONI YA WANANCHI WA TANZANIA KUHUSU KATIBA MPYA

Suala la lugha ya kufundishia linaibuliwa sana katika maoni. Kwa usikivu wangu ninahisi watu wengi wanapendelea Kiswahili kitumike hata vyuoni. Lakini wako wanaopendelea Kiingereza.

Kinachodhihirika kwangu ni mgawanyiko ulioko unaotokana zaidi na matabaka. Wale wanaotumai kuwa watoto wao watafanya kazi majuu au kwa vibaraka wa nje wanatetea sana hoja ya Kiingereza. Wale wanaohitaji kuwa huduma ziwafikie kwa lugha nyepesi na wapate ufahamu wa nini kinaendelea katika maisha yao wanapendelea zaidi Kiswahili kitumike. Na kuna wale bado ulimbukeni umewasakama kwa kuona ustaarabu ni kunena Kiingereza au kurashia maneno mawili matatu ili nao waonekane wamo.

Suala linalozungumzwa sambamba na hili ambalo linatofautiana ni lile la lugha ya taifa. Hapa ndipo hoja za kukitukuza Kiswahili au kudumisha utaifa zinapoangushwa. Suala la lugha mama halinogi vyema (si vema jamani) kwa baadhi ya wazalendo ambao wana lugha zao mama ambazo si Kiswahili na kamwe hatusemi Kiswahili kitawale lugha nyingine na kwa namna hii basi kama vile tunavyodhani Wakenya au Waganda wanaunganishwa na lugha ya kigeni, yaani Kiingereza, basi sisi tujivunie kuwa kuna  lugha ya Kiafrika inayotuwepesishia mawasiliano.

1 comments:

M. M. Mwanakijiji November 24, 2012 at 5:03 AM  

Kuna hoja tatu ambazo zipo katika hili na naamini mara nyingi zimekuwa zikichanganywa na kuchanganya. Kuna suala la lugha ya kufundishia (academic language), kuna lugha ya mawasiliano ya kimataifa (international language) na lugha ya mawasiliano ya sisi kwa sisi.

Wanaopendekeza kutumia lugha ya Kiswahili wanasikika kana kwamba wanataka lugha moja tu IWE - kwenye mambo hayo matatu. Yaani, Kiswahili kiwe cha kufundishia, na hivyo kiwe cha mawasiliano ya kimataifa na mawasiliano ya sisi kwa sisi. Katika hili wanaposema "wanatukuza" Kiswahili ni kana kwamba hawataki mtu ajifunze lugha nyingine ya kigeni (katika hili ni Kiingereza).

Naamini, hakuna mtu anayetukuza lugha ya Kiswahili ambaye anataka watu wasijifunze lugha ya Kiingereza. Tatizo ambalo watu wanajaribu kulishughulikia (la uzungumzaji fasaha wa Kiingereza) halihusiani kabisa na suala la kufundishia. Kama watoto wetu wanapomaliza shule ya msingi na sekondari wanazungumza Kiingereza vizuri na kuandika vizuri suala la lugha ya kutumia chuo kikuu halipo. Linakuwepo tu kwa sababu watoto wetu wanapofika chuo kikuu bado wanaonekana wana shida sana ya Kiingereza na hivyo watu wanataka kuondoka na shida hii kwa kuikwepa - tufundishe kwa Kiswahili tu.

lakini hilo linadhania kuwa hicho Kiswahili nacho kinaeleweka kwa ufasaha wa kutosha. Ukweli ni kuwa hat lugha ya Kiswahili kwa baadhi ya watu ni shida sana. Sasa tuwafundishe kwa lugha zao za asili?

Lakini jambo jingine linalotokana na hayo matatu hapo juu ni kuwa Watanzania wanaotaka kutumia Kiswahili kuanzia msingi hadi chuo kikuu wanashindwa kutuambia ni wapi mtu atajifunza lugha nyingine ya kimataifa kwa ajili ya maendeleo yake ya kikazi na mawasiliano ya kimataifa? Kama lugha ya Kiingereza itakuwa ni optional na itaendelea kufundishwa kwa namna ile ile kama sasa mtu huyo aliyefundishwa kwa Kiswahili toka msingi hadi chuo kikuu ataandika makala zake za kimataifa kwa Kiswahili au ndio itabidi atafute mkalimani au ajifunze Kiingereza baadaye (ukubwani?)

Sote tunajua tunachohitaji kukifanya - kutilia mkazo lugha ya Kiingereza kuanzia walimu wake na mazoezi yake kwa vitendo. Sasa hivi "English Medium" imekuwa ni bahati nasibu ya kutoza fedha ghali kwa shule kwa sababu mtoto akitoka huko ung'eng'e umemkaa vizuri? Kwanini kwenye shule za Kata Kiingereza hakifundishwi vizuri? Kwanini kwenye shule za serikali (msingi na sekondari) Kiingereza inaonekana ni shida? Inawezekana vipi kufundisha Kiingereza vizuri kwenye shule ambayo ina mwalimu mmoja tu?

Tusikwepe tatizo; tuna tatizo la msingi kwenye mfumo wetu wa elimu na hatuwezi kulikimbia kwa kuamua kutilia mkazo Kiswahili na kuondokana na Kiingereza. Tutakuwa kama mbuni mchangani.

Kujifunza Kiingereza siyo suala la anasa ni suala la lazima katika ulimwenggu wa leo. Wafaransa wanajifunza Kiingereza (hata kama hawapendi); Wajerumani wanajifunza Kiingereza, Wachina, Wakorea, n.k Si kwa sababu lugha zao hazitoshelezi - wanapanua uwezo wa wao kuwasiliana duniani. Lugha ya Kiingereza ndio lingua franca ya dunia.

Hatuna ujanja ni lazima tujifunze na kujifunza vizuri. Wazee wetu wengine waliosoma darasa la nne la Mkoloni bado wanazungumza Kiingereza vizuri tu sisi leo tunashindwa nini kukiboresha?

JIBU: Ni kushindwa kwa utawala ulioko madarakani - ni jambo gani wameweza kufanya vizuri tukajivunia kuwa limefanywa vizuri?

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP