Friday, November 23, 2012

Ubaguzi 101: Mtanzania Masomoni Ujerumani

Uafrika, Uarabu na Uzungu Ujerumani

Kiula Kiula

Cologne si mbali na Dortmund, majiji yote hayo mawili yapo kwenye jimbo moja la Northrhine Westphalia, kwa hiyo litokealo Cologne ni rahisi kutokea Dortmund pia. Sina hakika sana na hilo la waarabu na waafrika kutotembea usiku ila binafsi nimeshatembea usiku mara kadhaa kwenye viunga vya Cologne. Sikatai, matukio ya kibaguzi yamewahi kuripotiwa mara kadhaa ni kweli kama lile la mwafrika kusukumizwa kwenye reli wakati treni inakuja na kwa kuwa ilikuwa karibu kabisa basi unajua kilichotokea.

Niseme tu kuwa, Cologne ni mji wa kitalii, watu wengi sana kutoka kona zote za dunia hii hufika pale kwa ajili ya kujionea mto Rhine pamoja na hadithi ya "Makufuli ya wapendanao". Pia wengine hufika ili kushangaa hekalu la Cologne "Koln Dom" ambalo ni miongoni mwa majengo makubwa kabisa ya makanisa kwa Ulaya kama siyo kubwa zaidi. Katika jiji hili pia kuna Schokoladenmuseum yaani Chocolate Museum ambayo pia huvutia watalii.  Pia ni Cologne ambapo sherehe maarufu za kila mwaka "Rosenmontag" (Jumatatu ya Mawaridi) al maarufu kama Karnival hufanyika. Kwa maana hiyo, vyombo vya usalama vinajitahidi kupambana na matukio yote yasiyofaa yenye kuharibu taswira ya Cologne ikiwemo ubaguzi.

Kwa Dortmund, siku za hatari kwa watu wasio na asili ya Ujerumani mara zote hutangazwa na vyombo vya habari na kuwatahadharisha watu kuchukua tahadhari. Mara nyingi hizi huwa ni siku zile ambazo "Neo - Nazis" huwa aidha wanaandamana au wanafanya mihadhara yao. Maandamano huwa ni hatari zaidi kwa sababu wakati hao wahafidhina wa "Neo - Nazis" wakitangaza kuandamana, wajerumani ambao kwa namna moja au nyingine waliathiriwa na sera hizo nao hujipanga kwenda kuvaana nao na mara kadhaa huwa wanapigana kweli ingawa vyombo  vya usalama vipo makini kwa asilimia 200 kuhakikisha hakuna madhara makubwa yanayotokea. Mfano, Septemba mwaka jana "Neo - Nazis" 5000 walijimwaga katika mitaa ya Dortmund, wenzao wanaowapinga nao wakajitosa mitaani kuvaana nao na wakaishia kupigana haswa, hakukuwa na vifo ila kadhaa walijeruhiwa.

Pia, maeneo ya hatari kwa Dortmund yanajulikana na hata appearance ya wale extreme "Neo - Nazis" inajulikana pia. Hii inakusaidia kuchukua tahadhari zaidi ingawa ni nadra kwao kukushambulia. Binafsi sijawahi kukumbukwa na kituko kikubwa cha ubaguzi wa rangi zaidi ya tukio la dada mmoja (mjerumani) kunisusia kiti cha treni, nilipokwenda kukaa naye yeye kwa hasira akaamua kunyanyuka. Kisa hiki kilinikera na nilikiweka kwenye makala yangu fupi "I'm Still Learning" iliyochapishwa katika jarida la "African Positive".

Kama kuna maeneo ya hatari zaidi kwa Ujerumani basi Berlin ni mojawapo hasa pande zile ambazo hapo awali zilikuwa ndani ya mipaka ya Ujerumani Mashariki. Si ajabu kujikuta upo ndani ya U - Bahn (Treni za ardhini) halafu mtu usiyemjua akaanza kukushambulia kwa matusi mazito mfululizo. Hili nimewahi kulishuhudia zaidi ya mara moja katika mara chache sana nilizotembelea Berlin. Wapo pia wanaoshuhudia kufukuzwa njiani na vibibi vya Kijerumani ambavyo huwa vinashangaa hawa watu wamefikaje huku. Jimbo la Thuringen (Katikati kabisa mwa Ujerumani) pia ni maarufu kwa vitendo vya kibaguzi na ndio sababu hata weusi kule ni wa kuhesabu. Wakati fulani tukiwa kwenye jimbo hili tulikutana na mweusi mmoja kwenye mji wa Weimar uliopo kwenye jimbo hili, alitueleza kuwa walikuwa weusi wawili tu kwenye mji mzima! Ila nilifarijika hapa kwa kukuta kahawa ya "Africafe made in Tanzania" ikiuzwa kwenye duka moja.

Nimalizie kwa kusema kuwa sehemu kubwa ya jamii ya kijerumani hujitahidi sana kuficha hisia za kibaguzi. Labda ukutane na mjerumani mahali fulani mko wawili tu hapo kuna uwezekano mkubwa sana wa kushuhudia ubaguzi ila kwenye wengi huwezi kuliona hilo. Lakini pia kama taifa wanaona aibu sana kwa mambo ambayo taifa lao limehusika nayo hasa vita vyote viwili vya dunia, mauaji ya wayahudi n.k. Hii ni sababu kubwa inayowafanya hata siku yao ya taifa ambayo ni Oktober 3 huwa hakuna maadhimisho yoyote zaidi ya kuwa ni public holiday i.e. siku ya mapumziko. Ukiwauliza kwa nini hamsherehekei wanakwambia hawana cha kusherehekea. Aibu wanayojisikia ilikwenda mbali zaidi mfano, hadi 2006 ilikuwa ni kosa au kitendo cha aibu kukutwa aidha nyumbani kwako au sehemu ambayo siyo ofisi ya umma unapeperusha bendera ya taifa la Ujerumani! Ulionekana kama "Neo -Nazis" vile. Hali ilibadilika wakati Ujerumani ilipoandaa kombe la dunia mwaka 2006 na kuanzia hapo kupeperusha bendera ya taifa lao imekuwa ni uzalendo kama ilivyo kwingineko duniani. Kwa kifupi wajerumani wengi hujivunia sana umji/jiji na hasa hasa umajimbo kuliko utaifa (Kitabu cha "These Strange German Ways and The Why of the Ways" kimelieleza hili kwa kina). Ni rahisi sana kumsikia Mjerumani akijisifu kuwa yeye ni Berliner, Dortmunder au Hamburger au pengine Bavarian kuliko kujiita Germania.

CHANZO CHA SIMULIZI:

CHANZO CHA PICHA:

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP