Saturday, November 10, 2012

Uchakachuaji wa Hoja Muhimu ya Halima Mdee!

Ni vyema kuweka rekodi sawa kuhusu kile kilichotokea Bungeni Alhamisi hii ili, Inshallah, itakapofika Aprili 2013 tukirejee na kujiuliza kwa nini tuliruhusu kirahisi tu iwe hivi. Pamoja na madai kuwa eti ni muhimu sana watu kufikia muafaka unaojali matakwa ya pande mbili (compromise) za kisiasa (bipartisanship) ukweli ni kwamba kilichofanyika majuzi kilikuwa ni uchakachuaji wa hali ya juu sana. Yafuatayo hapo chini ni maelezo mafupi, ya kwa nini ni uchakachuaji mkuu na si muafaka, yatokanayo na alichokisema Mdadisi katika mjadala wa Wanamabadiliko mtandaoni.

Hoja ya Mdee ilifanyiwa uchakachuaji wa hali ya juu - sikiliza dakika za mwanzo za hicho kiunganishi hapo chini usikie hitimisho lake, alichofanya Tibaijuka ni kutoa hoja ya kubadili vipengele viwili  muhimu sana vya hoja hiyo hivyo kusababisha hitimisho lake lisiwe tofauti na kufanya tathmini au tafiti za uwekezaji katika ardhi ambazo tayari zimefanyika na zinaendelea kufanyika sana; kiini cha hoja kuu ni kusitisha kwanza kwa muda uwekezaji hadi tathmini ya kina ifanyike, kina Tibaijuka, Nagu na Lukuvi wakajipanga Kiserikali kuzuia sitisho na sasa nasikia hadi eneo la Oysterbay Police linaenda kwa wawekezaji, kama hilo ni kweli utaelewa kwa nini Serikali haitaki kabisa hili la la kusitisha, eti litazuia kazi nyingi ambazo zinaendelea- za kuwekezwa!

Kiunganishi chenye Hitimisho la Hoja za Mdee/Tibaijuka: http://udadisi.blogspot.com/2012/11/sikiliza-soma-hoja-ya-zitto-ya.html

Hapo alipoingilia kati Mbowe suala halikuwa kuipigia kura ya ndiyo/hapana hoja ya Mdee. Ilikuwa ni kupitisha hoja (mbadala) ya Tibaijuka ya kubadili vipengele viwili vikuu ambavyo ndivyo moyo wa hoja ya Mdee. Hivyo, kura zingepigwa bado hiyo ndiyo ya Wabunge wengi wa CCM ingepitisha hoja (badilishi) ya Tibaijuka. Kwa ufupi, Tibaijuka aliiteka (hijack) hoja ya Mdee. Inshallah tutalikumbuka hili Aprili!

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP