Loading...

Wednesday, February 20, 2013

Elimu ni suala la kisiasa au kitaaluma?


Elimu ni suala la Kisiasa au Kitaaluma?

Chambi Chachage

23 Julai 2008

Siasa ni taaluma. Kama ilivyo kwa taaluma yoyote, siasa ina wataalamu wake. Lakini si kila mtaalamu wa siasa ni mwanasiasa. Na si kila mwanasiasa ni mtaalamu wa siasa.

Pengine utata huu ndio uliomfanya Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, ajaribu kumpatia elimu ya siasa kila mwanasiasa wa serikali yake. Ili kutimiza lengo hilo wanasiasa walipelekwa katika chuo cha Kivukoni kupata mafunzo ya taaluma ya siasa na itikadi.

Pamoja na jitihada hizo bado nchi yetu ilijikuta ikifanya maamuzi mengi kwa kuzingatia utashi wa kisiasa badala ya kuzingatia ushauri wa kitaaluma. Kwa mfano, mwaka 1981 Mwalimu Nyerere aliunda tume iliyoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Elimu, Jackson Makwetta. Tume hiyo iligundua kuwa wanafunzi wengi wa sekondari hawapati elimu stahiki kwa sababu lugha inayotumika kuwafundishia haileweki kwa wanafunzi walio wengi achilia mbali walimu wao.

Kutokana na utafiti huo, wataalamu hao walipendekeza kuwa wanafunzi wafundishwe kwa lugha ambayo wanaitumia katika maisha yao ya kila siku. Cha ajabu dakika ya mwisho siasa iliingilia kati. Pendekezo hilo likatupwa kapuni. Wataalamu kutoka Uingereza wakaletwa. Wakafanya utafiti. Wakagundua kilekile ambacho wataalamu wetu walikigundua. Lakini wataalamu hao wa Kiingereza wakatoa pendekezo tofauti. Wakasema tuongeze bidii katika kufundisha Kiingereza.

Naam pendekezo la wataalamu kutoka katika nchi inayozungumza ‘Kiingereza cha Malkia’ likaonekana ni la kitaaluma zaidi. Lakini kumbe lilikuwa ni pendekezo la kisiasa tu. Ndio, lilikuwa la kisiasa maana nyuma ya pazia kulikuwa na mkakati kabambe wa kutupatia msaada wa kuchapa vitabu mbalimbali vya Kiingereza na kuleta wataalamu kutoka Uingereza kuja kutufundisha Kiingereza eti ili tuweze kukitumia kufundishia. Mkakati huu wa kisiasa ulilenga kuendeleza utegemezi wetu kwa Uingereza, utegemezi ambao haujawahi kuvunjika kikamilifu toka siku tulipojitwalia uhuru wetu wa kisiasa kutoka kwa Waingereza mnamo mwaka 1961.

Hivyo, misaada ikamwaga. Vitabu vikachapishwa. Tukasoma ‘Kalulu the Hare’ na ‘Hawa the Bus Driver’. Picha za sungura mwitu aitwaye Kalulu na dereva wa basi aitwaye Hawa zikatuvutia. Lakini je elimu iliyowasilishwa na hadithi hizo ilitufikia? Au vitabu hivi vilikuwa ni zana tu ya kutufundisha Kiingereza? Je, tulikuwa tunajifunza lugha ya Kiingereza au tulikuwa tunajifunza mada halisi zinazohusu jamii yetu? Lo mpaka leo najiuliza ni nini hasa nilijifunza!

Miaka mingi imepita sasa toka tufanye uamuzi huo wa kisiasa na kuubatiza kuwa ni wa kitaaluma. Lakini taaluma ya ufundishaji inaendelea kutudhihirishia kuwa sekta yetu ya elimu bado inadorora hasa katika suala la ubora wa elimu japokuwa tumekuwa na mipango mingi ya kuiendeleza. Baadhi ya wataalamu wetu wanaendelea kutukumbusha kuhusu baadhi ya yale mapendekezo ya tume ya Makwetta. Je, tunawasikiliza? Au tunatumia majukwaa ya kisiasa kutoa matamko ambayo yanakinzana na hali halisi kama inavyoainishwa na tafiti za kitaaluma?

Lakini siasa ni nini hasa? Kwa ufupi siasa ni taaluma au shughuli inayohusiana na mamlaka. Na tunapozungumzia mamlaka tunaongelea suala zima la mgawanyo wa madaraka na rasilimali. Hapa tunajiuliza nani ana mamlaka juu ya suala fulani au rasilimali fulani, kwa nini na kwa ajili ya manufaa ya nani? Pa tunajiuliza nani anadhibiti mamlaka hayo na kwa namna gani?

Hivyo, mwanasiasa mwenye taaluma ya siasa anategemewa kuwa na uwezo wa kutumia mamlaka yake kufanya maamuzi yanayozingatia utaalamu husika. Kwa mfano, mwanasiasa ambaye hana taaluma ya ualimu anaweza kutumia utalaamu wake wa kisiasa kuupima ushauri wa watalaamu wa elimu na kuutumia ushauri huu kufanya maamuzi sahihi. Si lazima ajue kila kitu kuhusu elimu lakini taaluma yake ya kisiasa inapaswa kumuandaa kuwa na uwezo wa kutafakari, kuhoji, na kutumia taaluma zingine kwa manufaa ya jamii iliyompa mamlaka yake.

Yule mwanasiasa mahiri wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, alilitambua hilo. Pamoja na kuwa na taaluma ya ualimu bado aliona ni vyema ampeleke msaidizi wake, Joan Wicken, katika Kijiji cha Ujamaa Litowa ili ajifunze namna ya kuendesha shule ya msingi inayojitegemea. Shule hiyo ilikuwa imeanzishwa na wanakijiji wenyewe ambao baada ya kujifunza hali na mahitaji ya mazingira yao walijiundia mfumo wao wenyewe wa elimu unaokidhi hali na mahitaji yao halisi.

Baada ya Joan Wicken kutoa mrejesho wa uzoefu wake huko, Mwalimu Nyerere aliunda sera ya ‘Elimu ya Kujitegemea’. Inasemekana kuwa kwa kiasi kikubwa sera hii ilitokana na taaluma asilia ambayo Joan aliipata katika Shule ya Msingi ya Litowa. Pamoja na mapungufu yake, hii ilikuwa ni jitihada ya aina yake ya kuoanisha maamuzi ya kisiasa na maamuzi ya kitaaluma.

Je, mapendekezo ya kamati maalumu iliyoundwa hivi karibuni na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kuipitia upya sekta ye elimu yatazingatiwa na wanasiasa wetu? Waziri na Naibu Waziri wa wizara hii wameshanukuliwa wakisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo tutaanza kutumia lugha ya Kiingereza  kufundishia katika ngazi zote za elimu. Je, matamshi yao yanamaanisha kuwa wameshafanya maamuzi yao ya kisiasa hata kabla tume waliyoiunda wao wenyewe haijalifanyia utafiti wa kitaaluma suala hili? Je, utoaji wa elimu ni mchezo wa kuigiza?

Kila kitu ni siasa. Hivyo, changamoto iliyo mbele yetu ni kuhakikisha hatutenganishi maamuzi ya kisiasa na maamuzi ya kitaaluma. Yanategemeana. Tukifanya maamuzi ya kisiasa bila kuzingatia ya kitaaluma tutaishia kujiuliza ‘bora elimu au elimu bora?’ Na tukifanya maamuzi ya kitaaluma bila kuzingatia ya kisiasa tutabaki tunauliza 'sera poa lakini utekelezaji mmh?’

© Chambi Chachage

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP