Loading...

Tuesday, April 16, 2013

Sikika: Serikali Itoe Taarifa Sahihi Kuhusu ARVs


ARVs Bandia: Serikali itoe taarifa sahihi kulinda afya za watumiaji

Tumesikitishwa kupata taarifa kwamba watu 5,358 wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU) waliokuwa kwenye matibabu wameacha kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARVs), mkoani Dodoma.

Taarifa kupitia vyombo vya habari  na taasisi mbalimbali kuhusu Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) kuacha kutumia dawa, zimekuja kipindi ambacho wananchi na wadau wa UKIMWI wakitafakari hatma ya uchunguzi wa sakata la kutengenezwa dawa bandia za ARVs. Dawa hizo aina ya TT-VIR toleo namba (batch number oc.01.85) zilisambazwa katika mikoa ya Mara, Tanga na Dar es Salaam tangu Mei, 2011.

Kuwepo kwa ARVs bandia na taarifa juu ya WAVIU kuacha kutumia dawa kunadhihirisha udhaifu uliopo ndani ya mifumo na mamlaka za serikali zilizopewa kusimamia ubora, uwepo na upatikanaji wa dawa.  Sikika inaamini, pengine kuna uhusiano wa karibu kati ya uwepo wa dawa hizo bandia nchini na WAVIU hao kuingiwa hofu na kuacha kutumia dawa.

Tunaamini hayo kwa kuzingatia ukweli kwamba suala la mgonjwa kutumia dawa kwa kiasi kikubwa linategemea imani na utayari wa mhusika. Uwepo wa dawa bandia ama zisizo na ubora unapunguza imani na hivyo kuweza kusababisha mgonjwa kuacha kuzitumia na kupelekea kuathirika zaidi.

Sakata la kuwepo kwa ARVs bandia lililochukua takribani miezi nane sasa, limekuwa na sura tofauti hususan juu ya nani anahusika moja kwa moja baada ya kiwanda kinachodaiwa kutengeneza dawa hizo Tanzania Pharmaceticals Industry (TPI) kukanusha kuhusika na utengenezaji huku Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) wakisisitiza kuwa dawa hizo zimetoka kiwandani hapo.

Sikika inathamini na kutambua juhudi za serikali za kutekeleza taratibu za kisheria ikiwemo ukaguzi na uchunguzi wa kimaabara uliofanywa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia TFDA.  Hatua nyingine iliyochukuliwa na serikali ni kukifungia kiwanda cha TPI kutokana na nyaraka zilizokutwa MSD kuonesha kuwa TPI iliiuzia MSD dawa hizo. Serikali pia iliwasimamisha kazi watendaji watatu wa MSD.

Usambazaji na matumizi ya dawa aina ya TT –VIR 30 toleo namba 0C .01.85 pia ulipigwa marufuku na serikali ilizitaka mamlaka za serikali za mitaa kupitia waganga wakuu, kukusanya dawa hizo  bandia kutoka vituo vya huduma za afya na kwa wananchi,  na kisha kuzirudisha MSD.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na MSD, takribani makopo 8,000 ya toleo hilo kati ya zaidi makopo 12,000 yaliyosambazwa yalikusanywa. Hivyo kwa hesabu rahisi, kuna takribani makopo 4,000 ambayo bado yapo kwenye mzunguko na ambayo hakuna taasisi yenye uhakika wa yalipo makopo hayo; kwenye vituo vya huduma ama kwa wananchi.

Serikali ililifikisha suala la ARVs bandia kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) kwa uchunguzi na hatua zaidi za kisheria. Lakini, pamoja na juhudi hizo za serikali, Sikika hairidhishwi na kasi ndogo ya ufuatiliaji wa tatizo hilo hususan muda mrefu unaotumika kupeleleza.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya DPP, jalada la kesi ya ARVs bandia limepokelewa na linashughulikiwa ili kupata muelekeo wa nani ahusishwe na kwa kosa gani kabla ya kuachia mamlaka husika jukumu la uchunguzi wa kina.  Kwa maelezo ya ofisi hiyo,  suala la ARVs bandia limechukua muda mrefu (zaidi ya miezi miwili), tofauti na muda wa kawaida wa siku 14 unaotumiwa na ofisi ya DPP kushughulikia kesi mbalimbali zinazofikishwa hapo, kutokana na uzito/unyeti wa suala hilo.

Wakati taratibu hizo za kitaalamu na kisheria zikiendelea, tunaishauri serikali kutoa taarifa rasmi kwa wananchi juu ya dawa bandia (makopo 4,000) ambazo hazijakusanywa. Je, ziko vituoni au zilishatumiwa na wananachi? Kama zilishatumiwa, je serikali ina taarifa zozote juu ya waliozitumia dawa hizo? Je, kuna madhara yoyote waliyopata kutokana na kuzitumia?

Kwa kutoa taarifa sahihi, serikali itasaidia kuwatoa mashaka wanaotumia ARVs na kuwajengea imani waendelee kuzitumia bila kuathiri afya zao.  Sikika inaamini kuwa kuwepo kwa dawa zenye ubora na uhakika kutaongeza imani kwa WAVIU kuendelea kuzitumia na kuimarika afya zao.

Makala hii ya Sikika imeandikwa na Aisha Hamis, Afisa Programu, Idara ya VV na UKIMWI.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP