MAPAMBANO
HALISI NI KUVUA MAGAMBA NA MAGWANDA YA UBEPARI
Sabatho
Nyamsenda
Taifa linapoparaganyika na nchi
inapopitia katika kipindi kigumu, watu huibuka na majibu ya aina mbalimbali. Siku
hizi kila jambo ni la kuombewa. Uchumi ukidorora, amani ikitoweka, watu waking’olewa
kucha, ujambazi (uliohalalishwa na ulioharamishwa) ukiongezeka, utasikia wito ukitolewa kuwa
tunahitaji kuliombea taifa letu. Na wengine wanaenda mbali na kusema katiba imtaje Mungu ili taifa letu lipone na lineemeke, ili tuwe kama Marekani.
Ubeberu na uporaji wa taifa hilo katili, lililojengwa kwa kuua wenyeji wa nchi
hiyo (Native Americans), linalotajirika kwa kupora, kwa kuvamia na kuua unaitwa
neema ya Mungu! Hata mambo ambayo utatuzi wake ni wa kisayansi, na ambayo
Muumba alitukabidhi mamlaka kamili ya kuyatatua,
tunayaweka kwenye maombi.
Miongoni mwa watu wanaoamini tiba za
kisayansi badala ya maombi ni Mwalimu Azaveli Lwaitama. Lwaitama ni msomi wa
umma. Sio umma wa wawekezaji na vijibwa vyao, bali umma wa wanyonge wanaoporwa
na kunyanyaswa na mfumo dhalimu wa ubeberu. Yeye alishaukataa ukahaba wa
kitaaluma (academic prostitution),
ambao humfanya msomi auze maarifa yake sokoni na kusaidia kuwarudisha watu wake
utumwani. Yeye ni mpambanaji, akipambana na wanyonge, ili kuibomoa mifumo
kandamizi na ya kinyonyaji.
Mapambano ya Mwl. Lwaitama yamelenga
kumng’oa wakala nambari wani wa ubeberu nchini (CCM na serikali zake). Na njia
rahisi ya kufanya hivyo ni kuunga mkono harakati za chama pendwa, na
kuwaaminisha wanyonge juu ya ujio wa masiha, atakayewarejesha katika nchi ya
ahadi, ile iliyokuwa inajengwa na Mwl. Nyerere. Hivyo Lwaitama ni kati ya
marafiki wa karibu wa Chadema na masiha wa uchaguzi wa 2010 kupitia Chama
hicho, Dk. Wilbrod Slaa.
Hivyo jabali hili la mapambano nalo
hujikuta likiimba, ukivua gamba tu kisha ukavaa gwanda mambo yote shwari.
Lakini gamba la CCM liko nje nje. Ngome yake inazidi kubomoka, sio kutokana na
jitihada za wapinzani, bali ni kutokana na chama chenyewe kusaliti itikadi
yake. CCM inastahili adhabu hiyo – ya kung’oka madarakani na hata kusambaratika
kabisa. Yumkini ‘adui’ mkubwa ni yule ‘aliyeficha gamba katika gwanda’.
Nimetaja ‘adui’ na hapa ningependa
kuibua mjadala. Mwalimu wangu huyu anafahamu vema kabisa kuwa adui wa wanyonge
ni mfumo kandamizi na nyonyaji wa ubepari, ambao kwa sasa umechukua sura ya
uliberali mamboleo. Watapambana vipi naye? Kwa itikadi ipi? Nani wa kuongoza
mapambano hayo? Mapambano yachukue sura gani? Kwa tathmini fupi, kama
tutajifunza kutokana na historia ya bara letu, hususan kuhusu vyama vya siasa,
enjioo, chaguzi na uibukaji wa masiha, vyote hivi vimekuwa vikitumika
kuustawisha mfumo wa ubepari na kutoa matumaini bandia kwa wanyonge.
Wafaidika wakubwa kwa hapa nchini ni
kijitabaka chetu cha vibwanyenye uchwara. Na kama ilivyo sifa yetu ya kitabaka,
tuna uwezo wa kuvaa sura mbili kwa wakati mmoja: sura ya wanyonge (ili tuwape
matumaini hewa) na sura ya mabepari (ambalo ndio tamanio letu kuu, ili tuishi
maisha ya raha na starehe). Mambo yakitubana sana huwa tunawatelekeza wanyonge
na kuhama upande. Na baadae tuonapo fursa ya kutupandisha ngazi ipo kwao
tunarudi na kuwalisha matumaini bandia. Kwa vyovyote vile, tuhamapo upande
nafasi yetu ya uwakala wa ubepari hubaki pale pale. Ndio maana hatuna nia
thabiti ya kujiunga na wanyonge na kupambana nao kwa dhati ili kuleta ukombozi
wa kweli.
Vita vinavyoendelea hapa nchini, vya kurushiana
mabomu na kung’oana kucha na meno, na kurushiana mipasho majukwaani, ni vita
vya mabepari uchwara. Ni vita vya kunyang’anyana fursa za kuwa watumishi wa
ubepari. Sio vita vya kugombea nafasi ya kuongoza mapambano ya kuung’oa
ubepari. Ukibanwa upande mmoja unahamia upande mwingine. Unaweza kutoka Chadema
ukahamia CCM na kupewa Ukuu wa Wilaya, unaweza kuacha ujamaa na kuwa bepari
(kama ilivyofanya CCM) ili utajirike, ukiamua utabaki Chadema na kupiga domo
ili uwe mbunge, unaweza kutoka serikalini na kuanzisha enjioo, n.k. n.k. Cha
msingi ni kwamba, popote utakapokuwa, nafasi yako ya kulamba makombo ya
mabeberu itakuwa salama.
Katika yote hayo, wananchi wengi
wameendelea kuwa watazamaji na/au mashabiki. Sana sana, wanazidi kukata tamaa
na kuamua kutopiga kura. Ndio maana pamoja na mabilioni ya fedha kumwagwa ili
kutoa elimu ya uraia, wanaojitokeza kupiga kura wanakuwa ni pungufu ya asilimia
hamsini ya wapiga kura wote waliojiandikisha.
Kama vile haitoshi, vyama vyetu
vinaanzisha vikundi vya kujilinda. Kujilinda dhidi ya nani? Polisi, mgambo na
Green Guards. Je, polisi wanaorusha mabomu na kufyatua risasi ni wa vyeo vipi?
Wa vyeo vya chini. Na, mgambo na Green Guards je? Ni watoto wa makapuku,
wanaopewa vijisenti kidogo ili wawarushie risasi makapuku wenzao walioenda
kupewa matumaini bandia na masiha-sesere. Sasa kila chama kitakuwa na colour
guard/brigade yake. Watakaokatana mapanga na kuuana katika mikutano ya hadhara
ni watoto wa makabwela ilhali watoto wa mabwana wakubwa wenye vyama wakifurahia
viyoyozi katika shule za kimataifa, ndani na nje ya nchi. Wanamlinda nani?
Dhidi ya nini? Hata wao hawajui vema ila wameambiwa wa kijani amkate panga wa
nyekundu, n.k.
Vita
vya kuung’oa mfumo huchukua sura ya mapambano ya kutafuta itikadi sahihi kama
ilivyokuwa ndani ya Urusi wakati wa kuung’oa utawala wa Tsar. Lengo si kumng’oa
Tsar, alitamka Lenin, bali kuing’oa mifumo yote kandamizi na ya kinyonyaji
ambayo ndiyo iliyomstawisha Tsar. Ma-bolsheviki (chama cha Lenin) hawakupikika
chungu kimoja na Ma-mensheviki au Ma-Socialist Revolutionaries, japo
wote walikuwa na itikadi ya kijamaa. Ushindani wao ulikuwa ni wa kiitikadi na
mfumo mbadala unaotaka kujengwa baada ya kungo’ka kwa Tsar.
Lakini nani wa kuyafafanua haya kama si
Mwalimu Lwaitama? Nani atakayewakumbusha wanyonge kuwa:
Mapambano yanaendelea,
Mapambano si lelemama,
Ile ngoma ya Pwani,
Iloleta uhuru wa Tanganyika.
Pasi ubepari kungo’ka.
Mapambano ni kuvua gamba,
La ubepari na ubeberu,
Gamba ukishauvua,
Gwanda usiuvalishe,
Ili ngozi yake halisi ijionyeshe.
Mapambano ni ya kitabaka,
Wanyonywao dhidi ya wanyonyao,
Pamwe na vijibwa vyao.
Silaha ya mnyonge sio nguvu yake,
Nguvu ni mali ya bepari,
Ainunuayo kwa bei chee au bure,
Na kuiuza aghali atajirike,
Silaha ya wanyonge ni umoja wao,
Umoja wa kitabaka,
Sio ubia na vibaraka.
Vua gamba usivae gwanda,
Gamba ni ubarakala usojificha
Gwanda ni uwakala ulojificha!