Loading...

Friday, August 16, 2013

Kuvua Magamba na Magwanda ya Upebari

MAPAMBANO HALISI NI KUVUA MAGAMBA NA MAGWANDA YA UBEPARI

Sabatho Nyamsenda

Taifa linapoparaganyika na nchi inapopitia katika kipindi kigumu, watu huibuka na majibu ya aina mbalimbali. Siku hizi kila jambo ni la kuombewa. Uchumi ukidorora, amani ikitoweka, watu waking’olewa kucha, ujambazi (uliohalalishwa na ulioharamishwa) ukiongezeka, utasikia wito ukitolewa kuwa tunahitaji kuliombea taifa letu. Na wengine wanaenda mbali na kusema katiba imtaje Mungu ili taifa letu lipone na lineemeke, ili tuwe kama Marekani. Ubeberu na uporaji wa taifa hilo katili, lililojengwa kwa kuua wenyeji wa nchi hiyo (Native Americans), linalotajirika kwa kupora, kwa kuvamia na kuua unaitwa neema ya Mungu! Hata mambo ambayo utatuzi wake ni wa kisayansi, na ambayo Muumba alitukabidhi mamlaka kamili ya kuyatatua, tunayaweka kwenye maombi.

Miongoni mwa watu wanaoamini tiba za kisayansi badala ya maombi ni Mwalimu Azaveli Lwaitama. Lwaitama ni msomi wa umma. Sio umma wa wawekezaji na vijibwa vyao, bali umma wa wanyonge wanaoporwa na kunyanyaswa na mfumo dhalimu wa ubeberu. Yeye alishaukataa ukahaba wa kitaaluma (academic prostitution), ambao humfanya msomi auze maarifa yake sokoni na kusaidia kuwarudisha watu wake utumwani. Yeye ni mpambanaji, akipambana na wanyonge, ili kuibomoa mifumo kandamizi na ya kinyonyaji.

Mapambano ya Mwl. Lwaitama yamelenga kumng’oa wakala nambari wani wa ubeberu nchini (CCM na serikali zake). Na njia rahisi ya kufanya hivyo ni kuunga mkono harakati za chama pendwa, na kuwaaminisha wanyonge juu ya ujio wa masiha, atakayewarejesha katika nchi ya ahadi, ile iliyokuwa inajengwa na Mwl. Nyerere. Hivyo Lwaitama ni kati ya marafiki wa karibu wa Chadema na masiha wa uchaguzi wa 2010 kupitia Chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa.

Hivyo jabali hili la mapambano nalo hujikuta likiimba, ukivua gamba tu kisha ukavaa gwanda mambo yote shwari. Lakini gamba la CCM liko nje nje. Ngome yake inazidi kubomoka, sio kutokana na jitihada za wapinzani, bali ni kutokana na chama chenyewe kusaliti itikadi yake. CCM inastahili adhabu hiyo – ya kung’oka madarakani na hata kusambaratika kabisa. Yumkini ‘adui’ mkubwa ni yule ‘aliyeficha gamba katika gwanda’.

Nimetaja ‘adui’ na hapa ningependa kuibua mjadala. Mwalimu wangu huyu anafahamu vema kabisa kuwa adui wa wanyonge ni mfumo kandamizi na nyonyaji wa ubepari, ambao kwa sasa umechukua sura ya uliberali mamboleo. Watapambana vipi naye? Kwa itikadi ipi? Nani wa kuongoza mapambano hayo? Mapambano yachukue sura gani? Kwa tathmini fupi, kama tutajifunza kutokana na historia ya bara letu, hususan kuhusu vyama vya siasa, enjioo, chaguzi na uibukaji wa masiha, vyote hivi vimekuwa vikitumika kuustawisha mfumo wa ubepari na kutoa matumaini bandia kwa wanyonge.

Wafaidika wakubwa kwa hapa nchini ni kijitabaka chetu cha vibwanyenye uchwara. Na kama ilivyo sifa yetu ya kitabaka, tuna uwezo wa kuvaa sura mbili kwa wakati mmoja: sura ya wanyonge (ili tuwape matumaini hewa) na sura ya mabepari (ambalo ndio tamanio letu kuu, ili tuishi maisha ya raha na starehe). Mambo yakitubana sana huwa tunawatelekeza wanyonge na kuhama upande. Na baadae tuonapo fursa ya kutupandisha ngazi ipo kwao tunarudi na kuwalisha matumaini bandia. Kwa vyovyote vile, tuhamapo upande nafasi yetu ya uwakala wa ubepari hubaki pale pale. Ndio maana hatuna nia thabiti ya kujiunga na wanyonge na kupambana nao kwa dhati ili kuleta ukombozi wa kweli.

Vita vinavyoendelea hapa nchini, vya kurushiana mabomu na kung’oana kucha na meno, na kurushiana mipasho majukwaani, ni vita vya mabepari uchwara. Ni vita vya kunyang’anyana fursa za kuwa watumishi wa ubepari. Sio vita vya kugombea nafasi ya kuongoza mapambano ya kuung’oa ubepari. Ukibanwa upande mmoja unahamia upande mwingine. Unaweza kutoka Chadema ukahamia CCM na kupewa Ukuu wa Wilaya, unaweza kuacha ujamaa na kuwa bepari (kama ilivyofanya CCM) ili utajirike, ukiamua utabaki Chadema na kupiga domo ili uwe mbunge, unaweza kutoka serikalini na kuanzisha enjioo, n.k. n.k. Cha msingi ni kwamba, popote utakapokuwa, nafasi yako ya kulamba makombo ya mabeberu itakuwa salama.

Katika yote hayo, wananchi wengi wameendelea kuwa watazamaji na/au mashabiki. Sana sana, wanazidi kukata tamaa na kuamua kutopiga kura. Ndio maana pamoja na mabilioni ya fedha kumwagwa ili kutoa elimu ya uraia, wanaojitokeza kupiga kura wanakuwa ni pungufu ya asilimia hamsini ya wapiga kura wote waliojiandikisha.

Kama vile haitoshi, vyama vyetu vinaanzisha vikundi vya kujilinda. Kujilinda dhidi ya nani? Polisi, mgambo na Green Guards. Je, polisi wanaorusha mabomu na kufyatua risasi ni wa vyeo vipi? Wa vyeo vya chini. Na, mgambo na Green Guards je? Ni watoto wa makapuku, wanaopewa vijisenti kidogo ili wawarushie risasi makapuku wenzao walioenda kupewa matumaini bandia na masiha-sesere. Sasa kila chama kitakuwa na colour guard/brigade yake. Watakaokatana mapanga na kuuana katika mikutano ya hadhara ni watoto wa makabwela ilhali watoto wa mabwana wakubwa wenye vyama wakifurahia viyoyozi katika shule za kimataifa, ndani na nje ya nchi. Wanamlinda nani? Dhidi ya nini? Hata wao hawajui vema ila wameambiwa wa kijani amkate panga wa nyekundu, n.k.

Vita vya kuung’oa mfumo huchukua sura ya mapambano ya kutafuta itikadi sahihi kama ilivyokuwa ndani ya Urusi wakati wa kuung’oa utawala wa Tsar. Lengo si kumng’oa Tsar, alitamka Lenin, bali kuing’oa mifumo yote kandamizi na ya kinyonyaji ambayo ndiyo iliyomstawisha Tsar. Ma-bolsheviki (chama cha Lenin) hawakupikika chungu kimoja na Ma-mensheviki au Ma-Socialist Revolutionaries, japo wote walikuwa na itikadi ya kijamaa. Ushindani wao ulikuwa ni wa kiitikadi na mfumo mbadala unaotaka kujengwa baada ya kungo’ka kwa Tsar.

Lakini nani wa kuyafafanua haya kama si Mwalimu Lwaitama? Nani atakayewakumbusha wanyonge kuwa:

Mapambano yanaendelea,
Mapambano si lelemama,
Ile ngoma ya Pwani,
Iloleta uhuru wa Tanganyika.
Pasi ubepari kungo’ka.

Mapambano ni kuvua gamba,
La ubepari na ubeberu,
Gamba ukishauvua,
Gwanda usiuvalishe,
Ili ngozi yake halisi ijionyeshe.

Mapambano ni ya kitabaka,
Wanyonywao dhidi ya wanyonyao,
Pamwe na vijibwa vyao.

Silaha ya mnyonge sio nguvu yake,
Nguvu ni mali ya bepari,
Ainunuayo kwa bei chee au bure,
Na kuiuza aghali atajirike,

Silaha ya wanyonge ni umoja wao,
Umoja wa kitabaka,
Sio ubia na vibaraka.

Vua gamba usivae gwanda,
Gamba ni ubarakala usojificha
Gwanda ni uwakala ulojificha!

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP