Loading...

Sunday, October 13, 2013

Tumkumbuke Mwalimu,Tumuenzi Kwa Vitendo

Tumkumbuke Mwalimu, Tumuenzi Kwa Vitendo

Na Bashiru Ally

Ndugu zangu nawaasa, tumkumbuke Mwalimu,
Sifa zake na siasa, ni hazina maalumu,
Tutumie kila fursa, kutenda kama Mwalimu
Tumkumbuke Mwalimu, tumuenzi kwa vitendo.

Alikuwa ni shujaa, wa kueneza upendo
Alikuwa mjamaa, msomi na mzalendo,
Hakuwa mwenye tamaa, kifikra na vitendo,
Tumkumbuke mwalimu, tumuenzi kwa vitendo.

Alikuwa mtetetezi, wa walonyimwa uhuru,
Alipinga waziwazi, siasa za kikaburu,
Alipinga ubaguzi, udini na ubeberu,
Tumkumbuke Mwalimu, tumuenzi kwa vitendo.
  
Aliamini kwa dhati, katika kujitawala,
Rushwa aliidhibiti, kwa haki alitawala,
Dhamana hakusaliti, kwa kuitamani  hela,
Tumkumbuke Mwalimu, tumuenzi kwa vitendo.

Alikuwa muandishi, wa vitabu na makala,
Alikuwa ni mcheshi, hasa kwenye mijadala,
Alichukia uzushi, utandawizi na hila,
Tumkumbuke Mwalimu, tumuenzi kwa vitendo.

Kumbukumbu ya Mwalimu, isifanywe kwa msimu,
Liwe ni letu jukumu, kutenda kama Mwalimu,
Nia hii ikitimu, atatulipa Karimu,
Tumkumbuke Mwalimu, tumuenzi kwa vitendo.

Twakuomba Mola wetu, ibariki Tanzania,
Lilinde na Bara letu, dhidi ya maharamia,
Warehemu ndugu zetu, wote walotangulia,
Ewe Mola ibariki, Afrika na watu wake.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP