Loading...

Wednesday, October 2, 2013

Umajumui wa Afrika: Kurunzi la Mapambano


UMAJUMUI WA AFRIKA: KURUNZI LA MAPAMBANO YA WANYONGE

Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

Mirengo finyu
Juma lililopita niliandika makala yaliyokemea itikadi finyu za ukabila (wa makabila, maeneo na  wa ki-nchi), udini na ukaburu (wa uzawa na wa kiumri). Nilisema kuwa itikadi hizi finyu zimelenga kuwagawa wanyonge ili kwa kupitia dini zao, umri wao, jinsia zao, makabila yao au nchi zao wajione wao ni sawa na watu wanaowanyonya na kuwafukarisha. Itikadi finyu hizi huzalishwa na kuenezwa na watu wa tabaka la juu ili kukwepesha wanyonge wasiungane na kuanzisha mapambano ya kitabaka. Katika makala ya juma hili, nitaelezea itikadi pana inayopaswa kuongoza mapambano ya wanyonge wa Afrika.

Sehemu kubwa ya watu wetu ni maskini. Umaskini huo si wa asili, si wa kuzaliwa nao. Asili haikuumba matajiri na maskini. Umaskini ni zao la mfumo unaowafukarisha wengi, na kuwatajirisha wachache. Kwa hiyo kama tukiamua kusema kuwa ufukara huzalishwa na mfumo kristo basi matajiri wote waitwe wakristo na mafukara wote waitwe waislamu. Hivyo vita iwe ni maskini dhidi ya matajiri bila kujali majina yao au madhehebu yao. Kama umaskini huzalishwa na jinsia basi kila maskini aitwe mwanamke na kila tajiri aitwe mwanaume, na minyukano ya kitabaka iendelee. Hali kadhalika kama umaskini huzalishwa na Tanganyika (Muungano) basi matajiri wote waitwe Watanganyika na mafukara waitwe Wazanzibari bila kujali walikozaliwa au wanakoishi, kisha vita dhidi ya wanaowafukarisha iendelee.

Itikadi ya wanyonge
Itikadi pekee itakayowaunganisha wanyonge bila kujali dini, vyama, jinsia, rangi, umri au nchi ni itikadi ya Umajumui wa Afrika (pan-Africanism). Itikadi hii haikuzaliwa barani hapa. Ilizaliwa ughaibuni, miongoni mwa watu weusi, ambao walipelekwa katika nchi za Amerika kama watumwa. Hata baada ya kukomeshwa kwa biashara ya utumwa, weusi hawa hawakutambuliwa kama binadamu. Walibaguliwa. Walinyanyaswa. Walikandamizwa. Walinyimwa fursa za kupiga kura, kumiliki mali, kujiendeleza kielimu, n.k. Wapo waliodiriki kusema kuwa utumwa ulikuwa bora kwani watumwa walilishwa na hata kupewa matibabu walipougua ili waendelee kuzalisha. Kadri weusi hawa walivyobaguliwa, kunyanyaswa na kukandamizwa ndivyo walivyogundua udhaifu wao. Udhaifu huo ulitokana na rangi za ngozi zao – ngozi nyeusi! Hivyo rangi ya ngozi zao ikazalisha itikadi ya kupigania usawa na kupinga ubaguzi wa rangi katika nchi za Magharibi.

Umajumui ukazaa utaifa
Ni baada ya vita kuu ya pili ya dunia ndipo itikadi ya Umajumui wa Afrika ilipochukua sura mpya, sura ya kulikomboa bara la Afrika. Hii ilitokea katika kongamano la tano la kimajumui lililofanyika katika mji wa Manchester, nchini Uingereza mwaka 1945. Kati ya waliohudhuria walikuwepo pia Kwame Nkrumah na Jomo Kenyatta.  Wito ukatolewa kwa Waafrika kupigania uhuru wao toka kwa wakoloni, na kisha baada ya uhuru kupatikana kuliunganisha bara la Afrika ili kuunda dola moja lenye nguvu.

Kwa nini kuiunganisha Afrika? Kwa sababu mipaka iliyounda vinchi ambavyo leo tunavitukuza haikuwekwa na Waafrika. Iliwekwa na wakoloni kwa madhumuni ya kugawana bara letu ili wapore rasilimali zetu bila kuingiliana. Na wakoloni walipoligawa bara hili, hawakuitisha kura ya maoni kwa wenyeji ili kujua kama jamii ya Wamasai au Wajaluo wangekubali kugawanywa katika nchi mbili tofauti. Kwa hiyo wakati wa harakati za ukombozi ajenda ilikuwa uhuru na umoja.
Kama ambayo Profesa Shivji husema, ni umajumui wa Afrika (pan-Africanism) ndio uliozaa uzalendo/utaifa (nationalism). Nkrumah aliporejea Ghana hakwenda kupigania uhuru wa Ghana. Alianza kwa kupigania uhuru wa Afrika Magharibi. Lakini kwa sababu za kimkakati, ilibidi kukomboa koloni moja moja na baadae kuziunganisha nchi huru. Ndio maana hata katiba ya Ghana ilikuwa na kifungu kisemacho kuwa Ghana itakuwa tayari kusalimisha mamlaka (sovereignty) yake kwa dola huru la Muungano la Afrika. Hata Nyerere alikuwa tayari kuchelewesha uhuru wa Tanganyika ili nchi za Afrika Mashariki zipate uhuru zikiwa zimeungana.

Wanyonge walipoporwa itikadi yao                
Nimekwisha kutoa hoja ya kwamba itikadi ya umajumui wa Afrika ilikuwa ni itikadi ya kuwakomboa wanyonge. Ilikuwa ni itikadi iliyowaunganisha wanyonge ili wapambane na kuishinda mifumo yote kandamizi na ya kinyonyaji. Kati ya mwaka 1900 na 1945 itikadi hii ilikuwa ya kupinga manyanyaso na ubaguzi dhidi ya watu weusi katika nchi za Magharibi. Kati ya mwaka 1945 na 1960 itikadi hii ilichukua sura ya ukombozi, lengo likiwa ni kulikomboa bara la Afrika toka katika ukoloni, na hatimaye kuunganisha ili kujenga nchi moja. Lengo la uhuru lilitimia, la umoja limebaki kuwa ndoto.

Je, kwa nini nchi huru za kiafrika zilishindwa kuungana? Viongozi walioingia madarakani walinogewa na madaraka na hivyo kuwa na maslahi katika kutukuza vi-nchi walivyorithi kutoka kwa wakoloni. Nkrumah tayari alikuwa ameliona hili na akawaonya viongozi wenzake kuwa Afrika kama Afrika isingeungana katika miaka ile ya 1960 basi ingekuwa ngumu kuiunganisha.
Nkrumah aliwaonea huruma wanyonge wa Afrika kwani ndio wangeendelea kuwa kitoweo cha mabeberu. Wakulima na wafanyakazi wangeendelea kulipwa kiduchu, huku wakikosa huduma bora za afya, elimu na maji, ilhali mataifa ya kibeberu yakiendelea kuneemeka kwa rasilimali na malighafi kutoka Afrika. Viongozi wasingekuwa na cha kupoteza kwani waliendelea kuneemeka na kodi za wanyonge pamoja na “makombo” ya mabeberu.

Jaribio la mwisho la kuwashawishi viongozi wa Afrika kuungana mara moja lilifanyika mwaka 1965 katika mkutano wa Umoja wa nchi huru za Afrika uliofanyikia mjini Accra, nchini Ghana. Hoja ya Nkrumah ilikataliwa tena, na mwaka uliofuatia Nkrumah alipinduliwa katika mapinduzi yaliyopangwa na kusimamiwa na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA).

Kati ya watu walioongoza upinzani dhidi hoja ya Nkrumah alikuwa ni Nyerere. Nyerere alitaka Afrika iungane kwa kupitia mashirikisho ya kikanda na baadae mashirikisho hayo ndiyo yaungane kuunda dola la Afrika. Lakini Nkrumah alitaka nchi zote za Afrika kusalimisha mamlaka yao mara moja na kuunda dola moja. Kwa hiyo, Nkrumah na Nyerere walitofautiana juu ya njia za kuunda dola moja la Afrika. Lakini wote walitaka Afrika iungane.

Wapinzani wa Nkrumah walidandia hoja ya Nyerere wakijidai kuiunga mkono, lakini lengo lao likiwa kukwamisha kila jitihada za kuiunganisha Afrika. Mwaka 1997, akihutubua halaiki ya watu nchini Ghana, Nyerere alikiri kuwa pengine Nkrumah alikuwa sahihi. Ilikuwa rahisi kuiunganisha Afrika katika miaka ya 1960 kuliko ilivyo sasa. Kisha Mwalimu akasema kuwa mara baada ya Mkutano wa Accra, kuna rais mmoja aliyemfuata na kumshukuru kwa kuipinga hoja ya Nkrumah. “Yaani siamini kama narudi nchini kwangu nikiwa bado mkuu wa nchi. Nimefurahi sana”, kiongozi huyo alimtamkia Mwalimu. Na hapo ndipo Mwalimu alitoboa siri ya jeshi la watu wenye maslahi ya kukataa Afrika isiungane:

Ukichukua idadi ya nyimbo za taifa, bendera na pasi za kusafiria za nchi mbalimbali, na watu wenye stahiki ya kupigiwa mizinga 21, hapo hujazungumzia mawaziri, mawaziri wakuu na mabalozi, utapata jeshi zima la watu wenye nguvu na ushawishi walio na maslahi ya kuifanya Afrika iendelee kugawanyika. Hicho ndicho Nkrumah alichokutana nacho mwaka 1965”.

Naweza kuongezea kuwa hicho ndicho kinachoikumba nchi yetu sasa. Hata zinazoitwa kero za Muungano kwa kiasi kikubwa zinahusu mamlaka/matakwa ya wanasiasa kuliko maslahi ya moja kwa moja ya wananchi wetu.

Kwa ufupi, ajenda ya umajumui wa Afrika iliporwa toka mikononi mwa wanyonge na viongozi wa Afrika walioingia madarakani baada ya uhuru kupatikana. Katika kupigania uhuru, itikadi hii ilitumika kuwahamasisha wanyonge dhidi ya ukoloni. Mara baada ya uhuru kupatikana itikadi hii ikahamia mikononi mwa viongozi walioshika madaraka. Suala pana la ukombozi wa wanyonge likafinyangwa na kubakia kuwa kamradi kadogo ka kuziunganisha nchi za Afrika. Na hata ajenda ya kuiunganisha Afrika pia ikaondolewa mikononi mwa wanyonge na kuwa ni suala la watawala walioingia madarakani. Taratibu, wanyonge wakaanza kuisahau itikadi yao ambayo ingeongoza mapambano dhidi ya watawala wakatili, waporaji na vibaraka ndani ya nchi, na mabeberu wa nje ya nchi.

Wanyonge waidai itikadi yao
Nimalizie kwa kusema sio kila nchi za kiafrika zinapoanzisha ushirikiano, au hata zikiwa na lengo la kuungana zinakuwa zimeongozwa na itikadi ya Umajumui wa Afrika. Sasa hivi, kwa kuwa nchi za kibeberu zimeamua kushirikiana, basi zinazitaka nchi za kiafrika pia kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi. Mabeberu wanataka kuendelea kuzipora nchi hizi kwa pamoja. Kwa mfano, nchi za Umoja wa Ulaya sasa zinaingia mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi (economic partnership agreements [EPAs]) na Jumuiya za kikanda za Afrika ili kurahisisha uporaji wa rasilimali za Afrika. Jumuiya ya Afrika Mashariki pia imo. Huwezi kuiita jumuiya hii kuwa ni ya kimajumui.

Lengo la itikadi ya umajumui kama ilivyopiganiwa na Nkrumah na Nyerere halikuwa kujenga nchi moja tu. Tunajenga nchi moja ili iweje? Lengo lilikuwa ni kujenga nchi moja ili kupambana na waliotupeleka utumwani, waliopora rasilimali zetu na kuwachinja babu na bibi zetu, walioligawa bara letu na kulitawala. Biashara ya utumwa, ukoloni na hata ubaguzi wa rangi ni sura tofauti tofauti za dubwasha liitwalo ubepari. Kwa hiyo, kadiri ubepari unavyobadili sura ndivyo itikadi ya umajumui inavyotakiwa kubadili sura ili kupambana nao.

Kwa hivi sasa ubepari umechukua sura ya uliberali mambo-leo, mfumo ambao unatumiwa na mabeberu pamoja na vibaraka wao wa ndani kupora rasilimali za wanyonge kwa kisingizio cha uwekezaji na ubinafsishaji. Viwanda vyetu vimeuzwa kwa bei ya kutupa, nyumba za serikali zimeporwa, dhahabu inatolewa karibu na bure na watawala wakipewa vyandarua wanashangilia kama “mazuzu”. Ardhi pia inaporwa. Huduma za afya, elimu na maji sasa ni bidhaa: huna pesa huzipati. Wanaofeli mitihani ni watoto wa maskini katika shule za kata. Mambo haya yanatokea huku Bara, yanatokea visiwani. Yanatokea Tanzania, Kenya, Misri, na hata Afrika Kusini. Wanaoumia ni wanyonge wote bila kujali dini zao au makabila yao, jinsia zao au umri wao, maeneo yao au nchi zao. Ni itikadi ya Umajumui wa Afrika pekee ndiyo inaweza kuongoza mapambano ya wanyonge dhidi ya mabeberu na vijibwa wao wa ndani. “Wanyonge wote unganeni. Hamna cha kupoteza isipokuwa minyororo yenu!”

Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP