Wednesday, November 27, 2013

Hoja za Omar Ilyas Dhidi ya Uchambuzi wa Lwaitama

Huyu ndio Lwaitama... Sijashangaa!


Nimesoma andiko la Dr. Lwaitama. Mzee wetu na mwalimu wetu lakini pia mpambanaji wa kudumu katika mapambano ya kifikra.

Nimeangalia andiko lake katika angle mbalimbali na kugh'amua sababu ya alichokiandika, sina uhakika kama ndio msimamo wake lakini nia ya andiko lake linalolenga kuhalalisha hatua ya CHADEMA kuwasimamisha uongozi Zitto na Kitila.

Naamini andiko lake linalenga katika kitu kimoja kikubwa. Hofu ya kuwa na upinzani legevu ama kudumaa kwa nguvu za upinzani zilizokuwa zikionyesha kukua. Hofu ambayo hata mimi ninayo na inapaswa kuwepo miongoni mwa wote wapenda maendeleo ya demokrasia nchini kama mimi na ndugu yangu Zitto na pia wale waumini wa ajenda ya kuing'atua CCM madarakani hata kwa mbadala wowote.

Katika andiko la Mzee Lwaitama ameangalia kitu kimoja pekee, nacho ni ule mkakati wa mabadiliko ndani ya chama ulioandaliwa na Samson Mwigamba na kuhaririwa na Dr. Kitila Mkumbo.

Mzee Lwaitama amejaribu kufumbia macho sababu zingine zote zilizofikisha hitimisho la kuwavua nafasi zote za uongozi Zitto na Kitila. Uamuzi ambao sasa unaonyesha wazi kuwa ni batili kutokana na ukiukaji mkubwa wa katiba ya chama hicho na uchakachuaji wa taratibu zao, ingawa wahusika wameamua kukubaliana nao.

Ningeliweza kusema kuwa hiyo yawezekana ni kwa sababu yeye kama walivyo wengi wanategemea habari za siasa zetu zaidi kutoka na kile kinachoripotiwa ama kuwekwa wazi katika vyombo va habari. Yaani ametengeneza angalizo lake katika muktadha wa taarifa rasmi ya uongozi wa CHADEMA pekee. Ningeliweza kusema labda hakusikia utetezi wa kina Zitto ambao ulikuwa na ufafanuzi wa kile kilichojiri katika kikao kilichofikia maamuzi hayo magumu aliyoyasifia. Lakini hapana. Katika andiko lake pia amewatuhumu kina Zitto kutokana na utetezi wao hivyo ni wazi amesikia ama kusoma taarifa ya kina Zitto kwa umma kupitia vyombo vya habari.

Mzee Lwaitama kama ilivyo kwa uongozi wa CHADEMA na pia muasisi wa chama hicho Mzee Mtei wamekwepa kabisa kukubali ukweli kwamba, moja; uamuzi uliofikiwa ni kilele cha safari ndefu iliyoanzia mwaka 2009 mara baada ya Zitto kutaka kugombea Uenyekiti wa chama hicho na kuambulia kuambiwa na mwenye chama kuwa kama anataka uenyekiti aende akaanzishe chama chake. Pili; uamuzi uliofikiwa ulifuatia mjadala mrefu wa zaidi ya nusu ya muda wote wa kikao uliohusiana na kinachoitwa usaliti wa Zitto wa kukiumbua chama chake kwa unafiki wa suala la uwazi na umakini wa matumizi ya kodi ya wananchi wanayopata kama ruzuku. Tatu; kuwa mbali na tuhuma ya kuandaa mkakati wa kugombea uongozi kinyume na mipango rasmi ya viongozi na wenye chama, kilichotokea ni hitimisho la tuhuma na juhudi lukuki za kumtuhumu Zitto kwa usaliti wa maslahi ya chama chake na hata kumbambikia fitna ya kuhongwa na CCM na vyombo vya usalama ili kufanikisha hilo.

Mzee Lwaitama hakufanya hilo kwa kupitiwa bali kwa makusudi ya kuweza kujenga hoja yake ambao imelenga katika kuilinda CHADEMA na athari za uamuzi wao ambao umekiuka hata misingi ya katiba yao. Na hapa ndipo namuona Mzee Lwaitama amepitiliza hata ile hulka yake niliyoizoea. Kwa andiko hilo ni wazi anapambanua kuwa kwake yeye ni sawa kabisa kuvunja katiba ama kutumia vibaya misingi ya katiba ili kufanikisha mchakato wa kuonyesha kuwa CHADEMA ni mahiri zaidi ya CCM.

Lakini pia hata tukiangalia suala hili kwa msingi wa huo mkakati pekee. Hapa Mzee Lwaitama hajaitendea haki sifa yake ya uanamapinduzi. Labda ndio masuala ya ustaafu haya, spirit ya uanamapinduzi inapungua kiasi.

Unapohalalisha matumizi mabaya ya sheria ama uchakachuaji wa misingi ya katiba yako ili kufanikisha maamuzi unayo amini ni muhimu kwa usalama wa kundi lako na maslahi yake, ni dalili ya ama kutokuwa muaminifu wa siasa za misingi ama kuwa tayari kuenzi hulka ya uvunjaji misingi ndani ya kundi hilo na kwa kuwa kundi hilo ni kundi la kisiasa ina maana kuwa unarasimisha utamaduni hatari ambao utaathiri zaidi taifa letu kuliko kuliokoa kama ambavyo Mzee Lwaitama anaamini kuhusiana na utume wa CHADEMA.

Vilevile inaelekea Mzee Lwaitama ama hajasikia ama hataki kuamini kuwa ingawa Zitto ni mlengwa nambari moja wa mkakati huo lakini yeye hakuhusika kuandaa wala hata kuona hadi ulipowekwa wazi katika kikao cha kamati kuu ya chama chake. Ukiondoa ushuhuda wa Kitila kuwa Zitto hakuuona mkakati huo hapo kabla lakini hilo linajionyesha wazi hata ndani ya waraka huo ambao unasema wazi kabisa kuwa endapo Zitto ambaye ndio mlengwa mkuu akikataa kukubaliana na mkakati huo yaani kukubali kugombea uenyekiti wa chama chake katika uchaguzi unaokuja basi wengine akiwemo Kitila na Mwigamba na wengineo ndio waangaliwe kuchukua nafasi ya Zitto kufanikisha mkakati ho.

Vilevile nashindwa kukubali kuwa Mzee Lwaitama ameshindwa kung'amua kuwa kama ni suala la makundi basi hata hao waliowashughulikia Zitto na Kitila ni sehemu ya siasa za makundi ndani ya chama hicho na pia tuhuma hizo pamoja na uamuzi wa uamuzi wa kuwasimamisha uongozi na kutaka kuwanyang'anya uanachama ni sehemu ya mkakati wa upande mwingine kuhusiana na mchakato wa madaraka ya ndani ya chama hicho. Yawezekana kundi lingine ama pia wakawa na waraka wao ama wakawa wamekosa weledi wa kuweza kujenga mikakati yao kisomi kama inayojionyesha katika mkakati wa Mwigamba, lakini mkakati upo na unatekelezwa kwa rasilimali na vikao halali na haramu vya chama chao.

Lakini zaidi, Mzee Lwaitama anapohalalisha siasa za makundi za upande wa watawala wa chama na kuwataka kina Zitto kuendelea kukandamizwa na wao kujizuia kutojitetea ama kupanga mipango itakayokikomboa chama chao kutoka katika hatima inayojongea kwa chama chao na taifa lao kutokana na fikra potofu na matendo maovu ya walio madarakani ati kwa kuwa taratibu za chama chao haziruhusu hilo, hapo ni sawa na kuwaambia ndugu zetu wa Palestina kuwa wana makosa ya kupanga na kutekeleza mipango yao ya kulikomboa taifa lao kutokana na ukoloni, ukandamizaji na ubaguzi wa Waisraeli kwa kuwa wanakiuka sheria za watawala wao na waliopaswa kutokujiona wanaweza bali wafuate taratibu zilizopo.

Lakini pia katika hili ndipo ninaposema kuwa Mzee Lwaitama ameandika andiko lake kama vile ni mmoja wa wale wachambuzi wetu mahiri ambao hufanya uchambuzi wao katika masuala mbalimbali kwa kutegemea hisia zao, maslahi yao na taarifa a.k.a propaganda zinazopatika katika vyombo vya habari pekee. Kitu ambacho sitaki kukiamini kwani hakujuana na Zitto na Kitila barabarani kama alivyojuana na Mbowe, Dr. Slaa na Tundu Lissu hivyo ni wazi anajua masaibu yaliyowakumba ndugu zake hawa kwa miaka zaidi ya mitano sasa hadi kufikia kilele chake sasa.

Anajua wazi ni jinsi gani Zitto amejitahidi kunyamazia mengi na hata wakati mwingine kuudanganya umma kuwa hakuna mgawanyiko ndani ya chama chake au hata kuwa hakuna mipango ya kummaliza kisiasa na kimaisha pale yanapotokea mambo kama hayo mradi tu kulinda usalama na ustawi wa chama chake.

Mzee Lwaitama anapowakemea ndugu na wadogo zake Zitto na Kitila kwa kuthubutu kujitetea hadharani kutokana na ujahili wa kisiasa wa baadhi ya viongozi wa chama chao kitu ambacho anakiona kama kinatishia uimara usiokuwepo wa CHADEMA, ni tukio ambalo kulielewa unapaswa kujua kwa undani jinsi anavyoangalia siasa za nchi yetu na ni jinsi gani anaamini [...] ndio inaweza kututoa hapa tulipo. 

Nakubaliana na hisia za baadhi ya watu akiwemo Mzee Lwaitama ambao wanaamini kuwa CHADEMA na mapungufu yake yote ilifikia lile lengo la kuwa na upinzani utakaoweza kuipa changamoto CCM na serikali yake na hali hii ina athari katika hilo. Lakini pia kinachoendelea sasa ni zaidi ya kuendeleza nguvu hizo za upinzani mahiri. Ni mpambano wa kujenga upinzani madhubuti wenye kulenga kuandaa mbadala makini badala ya bora mbadala.

Mzee Lwaitama anaungana na wanaojaribu kujidanganya kuwa mapungufu makubwa yaliyopo CHADEMA yanapaswa kuendelea kuachwa hadi pale ushindi wa kuiondoa CCM madarakani utakapopatikana. Lakini ukiwauliza baada ya ushindi kupatikana, yaani waheshimiwa hawa wanaofanya haya sasa watakapokuwa na dola mikononi mwao, inawezekana kweli wakajirudi na kuondokana na mapungufu yao ya sasa kwa manufaa ya kuepusha athari zake kwa Watanzania na Tanzania yetu? Mimi naamini hapana. Kama ilivyo vigumu kwa CCM kujisafisha hivi sasa ndivyo itakavyokuwa vigumu CHADEMA kusafishika ikiwa madarakani. Cha ajabu yeye kama mmoja wa wanaoamini kuwa njia pekee ya CCM kujisafisha na uozo uliokigubika chama hicho ni wao kutolewa madarakani ndio pia mmoja wa wanaojidanganya kuwa CHADEMA ya sasa itaweza kubadilika itakapokuwa madarakani.


Kwa kifupi andiko la Mzee Lwaitama halijalenga kujipendekeza kwa watawala watarajiwa wa CHADEMA bali kujaribu kupunguza athari za mafanikio ya kimtizamo maslahi lakini makosa ya kisiasa ya kundi la viongozi hao katika kulidhibiti kundi la wanamadiliko ndani ya chama katika muktadha mzima wa hatma ya chama hicho na nafasi yake katika kuwabana CCM.

CHANZO:

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP