Monday, November 25, 2013

Lwaitama: CCM, CHADEMA na 'Umoja ni Ushindi'

Asante ... kwa uchambuzi wenye tafakuri tunduizi. Nitajaribu baadaye kufuata nyazo zako. Lakini kitu kimoja kiko wazi. Chadema kama taasisi imechukua uamuzi sahihi. Kaulimbiu ya CCM ya tangu Aprili 2012 ni eti "Umoja ni Ushindi" hivyo malumbano ya kutuhumiana ufisadi na ugamba yanabomoa umoja na kupunguza uwezekano wa ushindi kwa hiyo lazima kuwavumilia viongozi wandamizi walio na nguvu ndani ya CCM vile kuwavua vyeo vyao katika chama kutatufanya tushindwe kushinda katika chaguzi.

Chadema imetekeleza kaulimbiu mbadala  na kusema; hapana, viongozi wandamizi wanaocheza karata nje ya uwanja na kuandamwa na tuhuma za usaliti tutathubutu kuwavua uongozi hata kama hilo litayumbisha chama kwa muda kwa sababu ya umaarufu wao au kuwa kwao na uwezo mkubwa wa uchambuzi wa mambo hautakizua chama kama taasisi kuwavua vyeo au hata kuwafukuza uanachama. 

Mfano wa Dakta Salim Ahmed Salim ni muafaka hapa. Alipigwa vita na kutuhumiwa hata mauaji ya mwaasisi wa Zanzibar ya baada ya Mapinduzi lakini hata baada ya kuzushiwa mambo mengi ya hovyo na mwisho wa siku CCM kikashinda uchaguzi 2005 bendera yake ikipeperushwa na mgombea ambaye hakuwa na sifa za uadilifu na umahiri wa uchambuzi wa masuala ya kitaifa na kimataifa wa kulingana na wa Dakta Salim Ahmed Salim. Lakini vile yeye ni mwenye hulka ya unyenyekevu na kutojiona bora kuliko wenzake na kutotawaliwa na dhana ya kuwa bila yeye kuwa Rais basi hakuna la maana chama chake kingeweza kikafanya, aliendelea kuwa mwanachama wa CCM na mwaka 2010 alijitokeza kumpigia kampeni ya urais kipindi cha pili mgombea ambaye mtandao ulimbeba 2005.

Bila shaka mgombea wa urais wa CCM wa 2005 na 2010  alinufaika na kuchafuliwa kisiasa kwa Dakta Salim. Labda tofauti ya wale waliovuliwa uongozi na Chadema na Dakta Salim Ahmed Salim  ni wao kutokuwa na nidhamu ya kichama cha ukombozi ambayo inadai kuwa au ujiondoe kama hujaridhika na uongozi uliopo au ukibaki basi uwe tayari kuvumilia kuchafuliwa na wale wasio na uwezo wa kiakili kama wewe pale unapotaka kuwaondoa madarakani tena kwa kucheza nje ya uwanja wa mchezo wa siasa unaofuata sheria zinazotungwa na wale wale ambao kwa wakati huo ndio wenye uwingi wa kura katika vikao halali za chama husika. 

Vinginevyo wewe utakuwa unakisaidia chama tawala cha CCM kwa kuanzisha zogo kuhusu eti mapungufu ya viongozi waliopo kwa kujiaminisha kuwa wewe ni bora kuliko wao ambapo na wao wanajiona ni bora kuliko wewe. Kwani Kambona si alikuwa kiongozi mahiri na mwenye maono kuliko hata wazee wetu kama Mzee Kawawa? Lakini historia ya TANU ikiandikwa yeye ataonekana msaliti na Mzee Kawawa ataonekana shujaa, siyo? Kwani Rais Reagan na Rais George Bush ndio walikuwa wenye akili na umahiri kuliko viongozi wa Republican Party ya enzi zao au ndio walikuwa muafaka kuongoza ili kuleta umoja ndani ya chama? 

Alipokufa Dakta Mondlane ni kwa nini wasomi kama Marcelino dos Santos walimpisha Samora Machel kuongoza Frelimo kama si kutii dhana ya nidhamu ya juu ndani ya chama cha ukombozi kuzuia kuanzisha migogoro inayowasaidia watawala wa wakati huo kujinadi kama wenye utulivu na hivyo kutokuwepo na mbadala. Kwa nini hadi leo Malkia wa Uingereza ni mama Elizabeth badala ya Prince Charles? hivi kuongoza taasisi lazima aliyeonekana anafaa lazima awe mwenye akili au umahiri wa uchambuzi wa mambo kuliko wenzake?

Kuanzisha mtandao wa siri wenye lengo la kubadili uongozi wa juu wa chama cha ukombozi ni usaliti na anayeandaa mkakati huo wa siri hawezi kujinadi kama eti mwanademokrasia, yeye ni mwanamakundi ya siri siri ndani ya chama husika kama hao anaowatuhumu yeye kuwa na makundi yao yakuwadumisha kwenye uongozi. Haiwezekani kusema ni sawa kutumia mbinu za kisirisiri nje ya utaratibu uliopo halafu ukajinadi kuwa mtetezi wa demokrasia na wenzako eti wahafidhina. 

Ningewaelewa hawa waliovuliwa uongozi kama wangejenga hoja hiyo ndani ya chama chao kwa uwazi kabisa na hoja hiyo ikikosa kupata kuungwa mkono basi wangetulia na kujaribu tena na tena hadi hoja yao ipate kuungwa mkono na wajumbe wengi wa vikao husika vya chama chao. Vinginevyo wangejitoa uanachama wa chama husika. Hivyo ndivyo mwanademokrasia anavyotarajiwa kufanya. Mimi nilijitoa TANU tangu 1973 na sijarudi CCM hadi leo vile najua hoja zangu zitakuwa na uungwaji mkono finyu kwa sasa katika vyombo vya maamuzi, labda pale CCM kikiondolewa madarakani kikabaki na waumini wa kweli wa ujamaa na umajumui wa kiafrika.

  
Kama wewe ni akina Abdul Nasser anayepanga mapinduzi ya kutumia nguvu kisisiri basi sema hivyo nayo inaitaji ujipange kufanikisha hilo wakati muafaka na ukishindwa katika mipango yako kubali kushindwa na anzisha chama chako au kama Ndugu yangu Mabere Marando jiunge na chama unachokubaliana nacho zaidi ya hicho ulimo. 

Haiwezekani eti chama cha maana kiogope kuondoka kwa wanachama wafuasi wa mwanachama au kiongozi mmoja au wawili au watatu wanaojiona wao ni bora kuliko wenzao. Kwa kitendo cha Chadema kuwavua uanachama viongozi wao wanadamizi wanaokiri tena na tena kuwa walisuka mtandao wa siri wa kuwaondoa  katika chaguzi zijazo viongozi wenzao wanaowaona wao kuwa ni wahafidhina na wao ni wanademokrasia ni kitendo cha ujasiri na kujenga uhalali wa kudumu wa Chadema hata kama  kitayumba na kutorokwa  na wanachama kiasi kidogo au kikubwa kwa sasa na hata kukosa ushindi kwenye changuzi za wakati huo. 

Uchambuzi wenye kusukumwa na tafakuri tunduizi unanituma niseme heko Chadema kwa kuthubutu hata kama  chama kitashindwa katika uchaguzi wowote ujao. Kitendo hiki pekee kimeonesha njia  kwa kusema kuwa dhana ya "Umoja ni Ushindi" ni dhana bora kuacha itekelezwe na CCM ya mafisadi ambao kwao kuwa na timu ambayo ina akina Ronaldo kibao kila mmoja akikimbia  na mpira kufunga yeye badala ya kutoa pasi ni jadi ya CCM ya leo. Lengo ni labda kutafuta kumzidishia umaarufu Ronaldo mhusika binafsi na labda kwa CCM ya sasa hilo ni sawa kwa vile CCM haijioni kama chama cha ukombozi tena bali chama dume na chama tawala milele na milele. Chadema ya Freeman Mbowe, Dakta Slaa, John Mnyika, Mabere Marando, Prof Baregu na Prof Safari, kutaja wachache, ni bora iendelee kujiona kama chama cha ukombozi kuona ni sawa kukataa dhana ya ki-CCM ya "Umoja ni Ushindi" 

Uchambuzi wangu unaweka kando urafiki na udugu wa kifamilia wa karibu kati yangu na Dakta kitila Mkumbo na  mwanangu Zitto Kabwe na heshima na mapenzi yangu kwao kama wachambuzi mahiri wa mambo vinabaki pale pale. Wanaweza kuishi bila hata  kuwakwenye chama chochote kama mimi na bado wakaendelea kutetea mabadiliko Tanzania katika nafasi zao katika jamii.

2 comments:

Anonymous November 25, 2013 at 5:57 PM  

I like your analysis Dr. Your so up

Anonymous November 26, 2013 at 6:11 PM  

Mwalimu wangu wa falsafa UDSM.....umenena kwa upande huo ulioegemea

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP