Tuesday, November 26, 2013

Mjadala wa Sakata la CHADEMA Unaendelea

DASTAN:
Mwanafalsafa Osho  katika moja ya vitabu vyake nilivyosoma ameandika kuhusu chuki dhidi ya watu wenye uwezo mkubwa kiakili. Yeye alieleza kuwa uwezo mkubwa kiakili humfanya kila anayemzunguka yule mwenye nao kuonekana `mdogo` na mwenye kufifia. Hali hii huleta chuki kwa baadhi na ufuasi kwa wengine. Waliokaribiana nae kiakili au (wanaodhani hivyo) hujenga chuki na kuona tishio. Waliozidiwa sana kiakili huamua kuwa wafuasi. 

Nadhani changamoto ni kwa yule mwenye uwezo mkubwa kiakili kuwaonyesha aliowazidi(waliokaribiana nae) kuwa wanaweza kujifunza kwake na hata kumwamini. Kutowafanya wamuone tishio bali rafiki na tumaini. Kwa nini asitumie uwezo wake mkubwa kufanya hili? 

Lakini kufanya hivyo kunahitaji subira kubwa kama makala hii inavyoonyesha. Tatizo ni kuwa hakuna aliyeliainisha hili kama kizingiti. 

SABATHO:

Mwl. Lwaitama,

Sharti nikiri kwamba nakubaliana na uchambuzi wako, kwa kiasi kikubwa, nakubaliana nao. Na kwa kweli, sikutegemea uchambuzi huo toka kwako ukizingatia mapenzi ya dhati uliyonayo kwa Zitto, ambaye mara kwa mara umekuwa ukimwita “mwanangu” humu mtandaoni. Lakini umetuonyesha kuwa inapokuja suala la nidhamu/mshikamano katika Chama, upo tayari kumtosa hata mwanao.

Nimelipitia andiko la Chambi. Pale mwanzoni nilijiuliza, kwa nini ametumia nukuu ya Kitila? Maneno hayo yaliyoandikwa na mwanasaikolojia hayakuzingatia muktadha wa mjadala, na hata mifano aliyotumia ni ya kubumba, ambayo haileti mantiki katika suala la SAS au ZZK. Eti SAS alikataliwa kwa sababu alikuwa na uwezo mkubwa? Hoja mufilisi isiyozingatia historia ya siasa za Kizanzibari na minyukano iangaliayo rangi na visasi. Kwa hiyo kila mwanasiasa anayekataliwa katika chama chake ni kwa sababu ana ‘akili kubwa’? Saikolojia bila historia itaishia kutoa uchambuzi butu, unaojenga woga kwa wanajamii ili wawatetemekee watu waliojibatiza wenyewe kuwa wana uwezo/akili kubwa, na hivyo ni wao pekee na hivyo wanastahili kutawala. Tazama andiko hili toka kwa mwanasaikolojia aliyenukuliwa.

Pili, uwezo wa mtu, na hasa kiakili unapimwaje? Katika vita, akili nyingi hupimwaje? Katika siasa akili je? Darasani je? Tutampataje mwenye akili nyingi ili atuongoze, iwapo ndiye mwenye haki hiyo? Kwa kuangalia kiwango cha ufaulu wake darasani? Sina hakika kama akina MM na M1 wana rekodi yoyote ya ubora kitaaluma! Kwa kuangalia kiwango cha juu ya uchambuzi na fikra? Ningemlazimisha Shivji au Jenerali Ulimwengu agombee urais. Kwa kuangalia mafanikio ya mbinu za kisiasa, bila kujali kama ni haramu? Basi, ni Rostam Aziz ndiye angestahili kuongoza, kwani ndiye aliyekuwa “brain” ya mtandao uliomweka JK madarakani. Kwa vyovyote vile, kushindwa kwa mbinu za “wanamapinduzi” [sic!] wa CDM, kunaonyesha wazi kuwa kisiasa, wana uwezo/akili ndogo.


Niitaka kuongezea hayo tu juu ya uchambuzi wa wako Mwl. Lwaitama, na andiko la Chambi. Kama alivyokiri mwandishi mwenyewe, ana mgongano wa kimaslahi. Labda ndio maana ameanza na nukuu ya Dk. Kitila.

CHAMBI:

Mwalimu Sabatho, nukuu ya Kitila inapaswa kusomwa sanjara na hoja kuu ya mada i.e. wito kwenu wachambuzi kufanya uchambuzi wa kina/yakinifu, kwa mfano, kumchambua Kitila na misimamo yake kihistoria, hiyo ni nukuu ya Machi 2013, Kitila yupo kwenye nyaraka 2 za siri, kwa NINI????

SABATHO:

Sawa sawa Cde Chambi. Nimekuelewa sasa.

Naamini wachambuzi wasio na ushabiki na makundi-kinzani wala migongano ya maslahi wataitikia wito wako adhimu. Ukifuatilia maoni yangu katika maandiko (na mijadala ya ana kwa ana, unakumbuka pale Hill Park?), utagundua kuwa nimepoteza sifa kwa mizania uliyotumia.

Tuendelee kutafakari.

LWAITAMA:


Mwl. Sabatho,
Ninakubaliana na hoja zako mia kwa mia lakini naona umenionea kwa kusema eti "Lakini umetuonyesha kuwa inapokuja suala la nidhamu/mshikamano katika chama, upo tayari kumtosa mwanao." Mimi si mwanachama wa Chadema na sijawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha kisiasa zaidi ya TANU. Ila mimi ninatetea hoja kuwa CCM inabidi kuondolewa madarakani haraka iwezekanavyo kwa vile kuendelea kuwepo madarakani kunadumaza kukua kwa  demokrasia ya kiliberali, kitu ambacho ni hatua muhimu katika kutayarisha umma kufanya mapinduzi ya kitabaka huko mbele ya safari.  Kitendo cha mwanasiasa yeyote kinachodhoofisha vyama vya upinzani vyenye nafasi ya kukiondoa CCM madarakani kama Chadema ni kitendo cha kukwaza kukua  kwa demokrasia ya ushindani kiasi fulani ya vyama hivi vya kisiasa vinavyotetea ubepari. Uchambuzi wangu haujaongozwa na eti Zitto ni mwanangu na Kitila ni rafiki wa karibu. Undugu na urafiki kwangu utabaki milele  lakini hautanifunga katika kutoa uchambuzi wa masuala yanayogusa mustakabali wa nchi. Tuendelee kutafakari na nakaribisha hoja za kunikosoa.
SALIM:

Mwalimu Lwaitama,

Mfano wako wa SAS na ZZK una mushkel kidogo. Japo wote wamechafuliwa na wapinzani wao lakini kuna matukio na mazingira tofauti aliyoyakabili SAS na anayoyakabli ZZK. SAS alichafuliwa kama sehemu ya kampeni ya wagombea urais kwa tiketi ya CCM na alifika mpaka fainali. SAS hakuzuiliwa kugombea wala hakupata kufukuzwa kwenye chama chake baada ya kuonekana tishio. ZZK alionyesha nia ya kugombea uenyekiti wa Chadema na pia alishasema ana nia ya kugombea urais kupitia tiketi ya Chadema. Kugombea nafasi ya uenyikiti wa chama alizuiliwa kwa nguvu ya baba mkwe wa mpinzani wake ambaye inadaiwa ni mwenye chama na hakutaka mwengine ashike uongozi wa juu wa hicho chama anachomiliki isipokuwa mkwewe tu!

Mmoja aligombea na akashindwa kwenye kura, mwengine alikataliwa kwa nguvu za wenye chama asigombee na ili asiendelee kugombea akaundiwa zengwe na kufukuzwa chama (siyo kuvuliwa uongozi tu, press conference ya jana ilikuwa inazungumzia kufukuzwa tu). Hakuna shaka wapinzani wa ZZK pia wamenufaika
kwa kuchafuliwa na hatimaye kufukuzwa uanachama kwa ZZK, hakuna kipya kwa wapinzani wa SAS kunufaika kwa kuchafuliwa kwake.

SAS ameendelea kuwa mwanachama mtiifu wa CCM kwa sababu hakupata kufukuzwa kwenye chama chake kama ambavyo anafanyiwa ZZK. Hivyo sidhani kuna sababu yoyote ya kuwalinganisha wanasiasa hawa wawili kwa matukio na mazingira yasiyofanana kwa lolote lile zaidi ya kuchafuliwa ambayo ni mchezo wa kawaida sana kwenye siasa.

CHANZO: 

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP