Wednesday, November 6, 2013

Nyerere na Posho

Dondoo kutoka kwenye "Maelezo ya Rais, Mwalimu Julius K. Nyerere kuhusu Huduma ya Taifa - Dar es Salaam, Jumapili, Oktoba 23, 1966"

Tuendavyo si sawa
Lakini nasema, wananchi, tuendavyo si sawa. Tutakaa tunafikiria mishahara, mishahara, ni wale wenye kipato tunaohusika, sio yule mkulima, au kabwela. Vijana waongo hawa, wanasema sisi tunafikiria baba zetu, wakulima maskini. Ungemfikiria mkulima usingezidai hizo pesa. Anatozwa nani ulipwe, kama siyo masikini? Ukitaka kufikiria masikini wanasema makomunisti. Watu tuache kufikiria habari za watu masikini tukae tunafikiria kujijazia mali, mali, mali, hivyo tunakwenda nayo wapi hiyo mali, wananchi?

Wananchi wa Tanzania, ikiwa ninyi viongozi, mtakaa mnadai binafsi mali, mali tu, basi nchi hii hajengeki, ng'o! Wananchi mnasema, kwanza tuanze na raha, ndio tujenge nchi; kwanza tupate majumba mazuri, na magari mazuri, na kitumbua chenye asali, halafu ndio kazi ianze. Lakini duniani haiwi hivyo. Duniani mnapoipokea nchi yenu masikini kama hii, mnaanza kwanza kwa kazi ya kuijenga, raha inakuja baada ya kazi. Hata tukisema wachache waanze kwa raha, sasa tunasema wengine wawe ni watumisi wa wachache? Maana haiwezekani wote waanze kwa raha hata kidogo; lazima wengine wote wabaki katika taabu.

Mbona Watanzania wengine wanashukuru
Juzi juzi nikaambiwa wafanyakazi wa bandarini, wamepitia mjini Dar es Salaam wakifurahi, kwa sababu wamepata masai mbili! (Masai ni ile noti ya shilingi mia, ina picha ya mmasai, kwa hiyo kwa mkato huitwa masai). Makuli wanafurahi wamepata masai mbili, yaani shilingi mia mbili; wanafurahi mno. Wanafurahia nini masikini wale? Hivyo shilingi mia mbili zina kumfurahisha mtu? Lakini wao zimewafurahisha. Kwa sababu, watu masikini, watu hao masikini wanapata kima cha chini kizuri pale, Sh. 330/-. Na hizo Sh. 330/- hazifikii hata nusu ya posho ya Mheshimiwa huyu anayedai haki yake. Lakini masikini hawa wanafurahi, wanapita humu wanashangilia.

Hawa wanafunzi wenu wenye elimu kubwa, wao posho tu, posho ya kufundisha darasani, karibu Sh. 800/-. Wanatuambia, tusipoziongeza tutakiona cha mtema kuni! Ndugu zangu, wenye elimu, tutaijenga nchi namna hiyo? Tutakuwa majibwa kupora na kunyang'anya tu mali ya wananchi? Nasema namna hiyo haiwezekani. Wananchi tuijenge nchi yetu.

...

Posho yao
Tukasema posho je!

...

Nataka muelewe wananchi, nataka muelewe nini wasilolitaka vijana hawa! Huyu analihudumia Taifa anapewa Sh. 790/- posho tu, na bado haijatosha; wananchi, bado haijatosha! Katika hizo Sh. 790/- anazopata hatumkati hata senti moja ya kodi, hatumkati kodi ila kama amenunua bia, maana katika kila chupa ya bia kuna kodi ya Serikali. Lakini bila hivyo Sh. 790/- za posho ya kijana wa National Service hizi haziguswi; ni posho siyo mshahara. Siyo mshahara maana siku hizi Tanzania, kwa waheshimiwa kama wale, hakuna mishahara midogo ya namna hiyo? Hakuna!

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP