Wasomi Wanapowagombania Wakulima
Dastan Kweka:
Niliposoma
mfululizo wa hii
makala katika gazeti la Raia Mwema (katika awamu mbili), niliifurahia na
kukereka. Niliifurahia kwa sababu inagusa jambo ambalo ni la msingi sana na
lenye athari kubwa kwa watu masikini wa nchi hii. Na ililichambua kwa kina kwa kutazama
historia na mifumo iliyochagiza mabadiliko kwa karne kadhaa. Jambo hilo ni
mustakabali wa wakulima wadogo. Hata hivyo, kwa kiasi nilikereka pia hasa
kutokana na namna vipengele kadhaa vilivyojikita katika fikra zilezile za
kukosoa bila kuangalia mienendo mipya, kujifunza na kupendekeza mbadala.
Siku
chache baada ya kusoma Makala ya ndugu Sabatho Nyamsenda, nilisoma pia makala
ya Paul Sarawati (zote katika gazeti la Raia Mwema). Makala ya Ndugu Sarawati
ilikua na kichwa, Wakulima Kilimanjaro wageukia kilimo cha parachichi, na iliandikwa
kwa namna ya kumsifu muwekezaji mkubwa aliyeko sanya Juu (Wilaya ya Siha) na
namna aalivyowawezesha wakulima wadogo kugeukia kilimo cha parachichi na kupata
faida. Sikufurahishwa na makala hii hasa kutokana na kuwa nimeishi na kukulia
Kilimanjaro na nimekuwa nikifuatilia mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea
katika maisha ya wakulima wadogo mkoani humo na nafasi ya wawekezaji wakubwa
katika mabadiliko hayo. Hivyo niliamua kuandika kidogo kuhusu suala hilo katika
blogu yangu (Unaweza kufuata link hiyo na kusoma jibu langu fupi kwa
makala hiyo). Hata hivyo sikumtumia mwandishi husika.
Sasa
nitaenda moja kwa moja kwenye baadhi ya mambo ambayo yamejitokeza katika makala
hii ya Ndugu Sabatho na ambayo nina mtazamo kinzani dhidi yake.
Kuhusu
Kurasimisha Umiliki wa Rasilimali (Hasa Ardhi)
Kuhusu
hili mwandishi anaandika, “Hapa tunapaswa kujifunza kwamba wale
wanaopigia debe urasimishaji wa rasilimali za wanyonge (mfano: kutoa hati za
ardhi kwa wakulima) huwa la lengo la kurahisisha uporaji wa ardhi hiyo.”
Mimi
nafanya kazi katika taasisi ambayo mojawapo ya miradi yake ni kuwawezesha
wakulima kurasimisha umiliki wa ardhi wanayolima kwa lengo la kuikinga dhidi ya
uporaji, kupata fidia stahili ikiwa inatwaliwa au kuwawezesha kutumia kupata
mikopo ya kujiinua, pale inapobidi. Ingawa fikra za kina Hernando De Soto
zilitawaliwa na haja ya kuwawezesha wakulima wadogo ‘kuchuma faida za uliberali
mamboleo’, mapungufu yamekuwa makubwa hasa ya uporaji wa ardhi baada ya
wakulima kuchukua mikopo na kushindwa kulipa (kama mwandishi alivyotoa mfano wa
India). Hata hivyo, sisi katika NGO ninayofanyia, kwa kujifunza kutokana na
mapungufu hayo, tunawawezesha wakulima kupata hatimiliki na kisha kuwahimiza
kuanzisha SACCOS na VICOBA na kuendelea kujiinua wenyewe badala ya kuchukua
risk kubwa kwa kukopa kwenye taasisi kubwa za fedha ambazo nyingi zina riba
kubwa na siyo rafiki kwa mkulima mdogo. Kimsingi, faida za hatimiliki kwa
wakulima wadogo ni zaidi ya hoja ya mikopo (hasa kutoka katika taasisi kubwa za
fedha) na mara zote tunawaelimisha wakulima wadogo tunaofanya nao kazi kuhusu
hili suala. Kwa mantiki hii, hilo tangazo la mwandishi kwa wakulima wadogo kuwa
“wale wanaopigia debe urasimishaji wa rasilimali za wanyonge (mfano: kutoa
hati za ardhi kwa wakulima) huwa la lengo la kurahisisha uporaji wa ardhi hiyo” ni
upotoshaji na lina mapungufu makubwa hasa kwa vile ni jumuishi, lina mtazamo
finyu na hasi kuhusu urasimishaji wa umiliki wa ardhi na linakosa kujadili
mifano chanya (best practices) ya utekelezaji wa wazo hilo.
Nafasi
ya NGOs katika Kuwaunganisha Wanyonge
Katika
hili mwandishi anaandika;
“Kazi
ya wanyonge kuungana isiachwe mikononi mwa mabwanyenye-uchwara kupitia vyama
vya siasa au asasi zisizo za kiserikali (NGOs). Hawa wote, katika nafasi zao,
ni watumishi wa mabepari wa kimataifa. Hata kama hapa na pale huonekana kuwa na
ugomvi, ugomvi huo huwa haulengi katika kuubomoa ubepari. Wote hawa
wanapigania nafasi ya kuwa mawakala wema wa mfumo wa kibepari. Ndio
maana, hapa nchini, hakuna chama cha siasa chenye nia ya dhati ya kuleta mfumo
mbadala, na harakati zao zinalenga kuepusha mapambano ya kitabaka katika jamii.”
Katika
muda mfupi niliofanya kazi katika NGOs na uzoefu kwenye taasisi nyingine
(zikiwemo za tafiti za kilimo), hakuna mahali ambapo pametawaliwa na mijadala
inayohusu wanyonge na namna ya kuwasaidia (au kuwawezesha kujisaidia) kuliko
kwenye NGOs. Tatizo kubwa ni kuwa wigo wa mijadala hiyo unadunishwa na namna
NGOs zinapata fedha (funding system) ambayo pia hutegemea sana malengo ya
wanaoitoa. Tunapoona maandamano ya wanaharakati Davos, Copenhagen na kadhalika,
dhidi ya mikutano ya wakubwa na ajenda zao, lengo ni kuwa mawakala wema wa
mfumo wa kibepari? Nafikiri, badala ya kurejea ukosoaji jumuishi wa kiwango
hiki, ni vema kujikita katika mawazo mbadala ya namna gani ya kutatua matatizo
ya kimfumo katika NGOs ili taasisi hizi ziweze kuchangia vyema katika kuung’oa
mfumo kandamizi. Mchango wa taasisi hizi (hasa zile zenye kufanya kazi
sawasawa) katika kupigania haki za kiraia (Civil rights), kupigania
uwajibishwaji wa makampuni makubwa kama Monsanto, Shell, BP na kadhalika ni
mkubwa.
Kiitikadi,
NGOs ni sehemu ya uliberali-mamboleo na kimsingi kwa kiasi pia zimechangia
kunawiri kwa mfumo. Lakini kama siyo jukumu letu kama wasomi kufikiri namna ya
kuzibadili kiitikadi, mbadala wake ni upi? Tayari tumeshaona nyingi zikipigwa
vita na dola kwa sababu ya misimamo yake na hasa kwa kupinga ukandamizaji na
dhuluma. Tayari kuna maungio.
Lugha
ya Mwandishi
Mimi
ni mfuasi wa sera za Kisoshalisti (siyo ujamaa kama tunavyoujua). Hata hivyo,
sina hakika ni kwa kiasi gani uandishi wa kebehi kwa wadau wengine unasaidia
katika kuwabadilisha au kuwafanya waungane na wale wanaoonekana wanaendesha ‘harakati
safi’ za kubomoa mfumo. Mfano mimi ninayetumia muda wangu mwingi vijijini
nikijadiliana na kupanga mikakati na wakulima wadogo namna ya kuwajibisha
makampuni makubwa ya madini yanayovuna utajiri katika ardhi yao bila kurejesha
hata chembe, naweza kuwaita walioko vyuo vikuu wakifundisha (kama mwandishi wa
hii makala), kuwa ni ‘watu wenye anasa ya kubwata bila kutenda’ - (Armchair
advisors). Ndivyo vita vya maneno vinavyotumika. Kumbe kwa kiasi
kikubwa wadau hawa wanategemeana. Kuna haja ya kuwa na mjadala mpana wa namna
ambavyo lugha hizi na ‘kebehi za kisomi’ zinavyojenga kuta badala ya madaraja
katika kufikia malengo mbalimbali, siyo tu ya kubomoa mfumo kandamizi wa
kibepari.
Sabatho Nyamsenda:
Kwanza nikupatie pole kwa kukereka na lugha ya mwandishi.
Yumkini ndilo lililokuwa lengo lake: kuwakera mabwanyenye na vijibwa vyao. Sasa
wewe kama ulivyosema, sio bwanyenye. Lakini sina hakika kama sio mtumishi wao.
Lugha ya mwandishi huwakera pia hata wasomi wenzake katika vyuo vikuu (soma http://www.raiamwema.co.tz/wasomi-kaeni-kando-wanyonge-shikeni-hatamu na
hapa pia http://www.raiamwema.co.tz/elimu-yetu-izalishe-wasomi-wa-umma-si-makahaba-wa-kitaaluma).
Huwakera wanasiasa, huwakera mawakala wengine wa ubepari, n.k. Kwa ufupi, wote
hukereka na hawapendezwi na lugha ya mwandishi. Sio lengo la mwandishi hata
kidogo kukufurahisha wewe, kwani hajioni kama mtumishi wako.
Tazama ilipo tofauti yako na mwandishi:
WEWE na NGO yako mnajiona kama wakombozi wa wanyonge.
Mmewaona kuwa hawajiwezi, mbumbumbu, na hivyo mmejibatiza wajibu wa
“kuwawezesha” na “kuwasaidia”.
Ngoja nisijeonekana nakubandikia maneno mdomoni. Hivyo
nitakunukuu:
“Katika muda mfupi niliofanya kazi katika NGOs na uzoefu
kwenye taasisi nyingine (zikiwemo za tafiti za kilimo), hakuna mahali ambapo
pametawaliwa na mijadala inayohusu wanyonge
na namna ya kuwasaidia (au kuwawezesha kujisaidia) kuliko kwenye
NGOs”.
Sasa, hapo ndipo unapotofautiana na mwandishi. Na nikiri
kabisa kuwa una haki ya kukereka.
Yeye mwandishi hata alipohudhuria kongamano husika,
alijishusha, akajinyenyekeza na kusema kuwa amekwenda “kujifunza”. Eti
anawaambia wanyonge kuwa wao ndio chanzo cha maarifa! Ujumbe wa mwandishi ni
kwamba wanyonge watajikomboa wenyewe. Kwa bahati nzuri, kauli-mbiu ya MVIWATA
ni “Mkombozi wa Mkulima ni Mkulima mwenyewe”. Mrengo huo wa wanyonge kujikomboa
wenyewe unatumika sana katika mapambano ya nchi za Amerika ya Kusini.
Mwandishi huwaambia wanyonge kuwa kutokana na historia ya
mapambano yao ni kosa kubwa sana kukasimisha mamlaka ya kujikomboa kwa “wasomi”
kama yeye, wanasiasa, wana-ma-NGO kama wewe, kwani mwisho wa siku huishia
kuwauza kwa mabepari.
Lakini huwakumbusha pia kuwa kabla ya majilio ya vyama vya
siasa, vyuo vikuu na NGOs wanyonge wenyewe walikuwa wakipambana. Mapambano
yalianza tangu siku ya kwanza pale wanyonge walipokutana na mkono wa damu wa
ubepari kupitia biashara ya utumwa.
Nadhani hiyo inafafanua walau jambo moja katika majibu yako.
Mengine yatafuata, kukiwa na haja ya kufanya hivyo.
CHANZO: