Thursday, February 27, 2014

Workshop on Art&Social Change with Billy Kahora

What is the role of the artist/writer as an agent of social change? How can poets and writers animate youth voice? How can the creative community in Dar and beyond work together to strengthen creative expression? These are just a few of the questions we'll explore in a day-long dialogue/workshop with guest Billy Kahora, editor of KWANI? in Nairobi, Kenya.   

We'll introduce ourselves, hear from Billy, have large and small group discussions, explore the idea of a literary digital map of Dar & beyond, and talk about the most current projects / initiatives strengthening & building a community of creative expression in Dar es Salaam and Tanzania as a whole.   

We hope you can join us for this exciting day!  RSVP by March 6, 2014 -- limited spaces available! Invite is also being sent via email, please check and respond as soon as possible.  

 Asanteni. 

Wednesday, February 26, 2014

Mwalimu Nyerere: Serikali Nne/Four Governments

"Labda ni vizuri kukumbuka kwamba shabaha ya baadhi yetu ilikuwa ni kuziunganisha nchi za Afrika Mashariki ziwe Nchi Moja. Na wakati Zanzibar na Tanganyika zinaungana, Kenya, Uganda na Tanganyika zilikuwa katika mazungumzo ya kutafuta uwezekano wa kuungana. Kama jambo hilo lingetokea, nina hakika kabisa kwamba mfumo wa nchi mpya ambayo ingezaliwa ungekuwa ni wa Shirikisho: ama Shirikisho la Nchi Tatu zenye Serikali Nne, au Shirikisho la Nchi Nne zenye Serikali Tano. Kwa kweli hata kesho Nchi za Afrika Mashariki zikiamua kuungana, na Tanzania ikawa ni mshiriki, naamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye Serikali mbili - ya Zanzibar na ya Tanganyika - kuliko Tanzania yenye Serikali mbili, ya Tanzania na Zanzibar. Wapendao Utanganyika watakuwa wazalendo zaidi, badala ya kuwa wasaliti, wakiazimia Afrika ya Mashariki iliyoungana kuwa Nchi Moja, kuliko Tanzania iliyotengana ikawa nchi mbili" - Julius K. Nyerere's (1995: 16-17) Uongozi Wetu Na Hatima ya Tanzania.
"Perhaps we should remember that the ultimate aim for some of us was to unite the countries of East Africa into One Country. And when Tanganyika and Zanzibar united, Kenya, Uganda and Tanganyika were still discussing the possibility of uniting together. If they had succeeded, I am quite sure that the new country thus created would have been a Federation; either a Federation of Three Countries with Four Governments, or Five Countries with Five Governments. In fact, if tomorrow the East African countries, including Tanzania, decided to unite, I believe it would be easier to incorporate a Tanzania with Two Governments - one of Tanganyika and another of Zanzibar - than a Tanzania with Two Governments, one of Zanzibar and another of Tanzania. Advocates of Tanganyika would be greater patriots, rather than traitors, if they called for a united East Africa with One Country, instead of a Tanzania which had been divided and had become two countries" - Julius K. Nyerere's (1995: 35-36) Our Leadership and the Destiny of Tanzania.

Tuesday, February 25, 2014

Mtanziko wa Tanzania

  Serikali 1 = Kuimeza Zanzibar
 Serikali 2 = Kuendeleza Kero
    Serikali 3 = Kuvunja Muungano
    Serikali 4 = Kuunganisha Afrika

Nyerere: Tanzania! Tanzania!

Niliuliza mwanzoni:
Sera hii ni ya nani?
Serikali kuwa tatu
Hapa Tanzania kwetu?

...

Ye yote mwenye akili
Asiyekuwa jahili,
Sera hii anajua
Itavunja Tanzania.

Wanajua wanavunja,
Na kusema kwa ujanja
Tanganyika kujitenga
Si kuvunja, ni kujenga.

Ati "ndani ya Muungano",
Tudhanie ni maneno
Ya uwezo wa hirizi
Kukinga maangamizi.

Misingi mkishavunja,
Msidhani kwa ujanja
Nyumba mtashikilia,
Ikose kuwafukia.

Kwanza fikiri gharama
Zitobebwa na kauma:
Hizi serikali mbili
Sasa twaona thakili,
Sembuse zikiwa tatu?
Wataweza watu wetu?

...

Nakiri Wazanzibari
Katiba waliathiri,
Nilidhani kazi yetu
Ni kuwabana wenzetu,
Viongozi wa Zanziba,
Waiheshimu Katiba.

Lakini ni Serikali
Ambayo haikujali,
Na kitendo kama hicho
Ikakifumbia jicho,
Na kuanza kufokea
Wale waloikemea.

Wala kuvunja Katiba
Kuvunja Nchi si tiba.

Hivi wakifanikiwa
Na nchi wakaigawa,
Kumbe hawataandika
Katiba ya Tanganyika?

Wataacha utawala
Uwe shaghalabaghala?
Na kama ikiandikwa,
Katu haitakiukwa?

Endapo itatukia
Nayo ikavunjwa pia,
Tanganyika itengane,
Wapate nchi nyingine?

Wanaovunja sharia
Na Katiba Tanzania
Dawa ni kuwashitaki
Waadhibiwe kwa haki:
Nchi yetu kuigawa
Ni uhaini, si dawa.

...

Tanzania yetu ina
Watu aina aina:
Inao hao Wapemba
Watachomewa majumba,
Sera hii ikipita
Bila ya kupigwa vita.

Lakini ina Wahaya,
Na Wasumbwa na Wakwaya,
Ina Waha na Wamwera,
Na Wakwavi, na Wakara.

Ina Anna ina Juma,
Ina Asha ina Toma,
Kadhaka ina Pateli,
Na wengine mbali mbali.

Uhasama ukipamba
Mkafukuza Wapemba,
Anojua ni Manani
Mbele kuna mwisho gani.

Hivi mnavyofikiri,
Wenzetu Wazanzibari
Walitokea mwezini
Kuja hapo visiwani?

Visiwani humo humo
Wamakonde, Wazaramo,
Wanyamwezi na Wamwera;
Na mbari nyingi za Bara.

Walotoka Arabuni
Waliondoka zamani,
Walobaki ni wenzetu,
Raia wa Nchi yetu.

Mzaramo wa Unguja
Akizuiliwa kuja
Kuishi Darisalama,
Nambieni Msukuma
Mgogo au Mngoni
Aruhusiwe kwa nini.

Na Mchagga watamwacha?
Na Muha na kina Chacha?

Mwajuma wa Zanzibari
Mkimwona ni hatari,
Hivi Juma wa Pangani
Ana uhalali gani?

Na Shabani wa Kigoma?
Na Fatuma wa Musoma?

Na vita vya uhasama
Vitapamba nchi nzima:
Hawa fukuza hawa
Kwa udini na uzawa,
Yalo Yugoslavia
Yatufike Tanzania.

Chuki hizi msidhani
Hazina udini ndani,
Maana behewa hili
Lina watu wa kila hali.

Wamo na maaskofu,
Na mashehe watukufu:
Na wasomi wa sharia,
na wachumi wetu pia,
Kila mtu ana lwake,
Anazo sababu zake.

...

Hizi pilika pilika
Za kutenga Tanganyika
Ni kutafuta nafasi
Za kupata Uraisi

...

Tanganyika mnadhani
Ina mvutano gani
Wenye nguvu kuzidia
Umoja wa Tanzania?

Wa Pwani na wa Unguja
Mkiona si wamoja,
Mtawaona wa Mtwara
Ni wamoja na wa Mara?

Wa Pemba mkiwatenga
Na ndugu zao wa Tanga,
Mtaacha wa Tabora
Wadumu na wa Kagera?

Wafipa wa Sumbawanga,
Na Wasegeju wa Tanga,
Wawatenge Waunguja,
Wao wabaki wamoja?

Hivi Waha wa Kigoma
Na Wakurya wa Musoma
Na Wazaramo wa Pwani
Watabaki majirani?

Msidhani Tanzania
Si sawa na Somalia,
Ati mtaitabanga,
Msihiliki kwa janga.

...

Kikao mchanganyiko
Cha Dodoma huko huko,
Kimesema wazi wazi
Kuwambia Viongozi:

"Serikali kuwa mbili
Si sera ya Serikali,
Bali ni sera ya Chama
Kile kilichowatuma.

Basi kairudisheni
Kwa wenyewe vikaoni,
Wapate kuijadili,
Kibidi waibadili."

Mimi kwa upande wangu
Nawanasihi wenzangu,
Sera wakiibadili,
Tafadhali, tafadhali:
Chama na kilete hoja
Serikali iwe moja

...

Nasi twaiga Warusi
Hata katika maasi,
Tuivunje vunje Dola,
Turudie makabila?

...

Mbegu mbaya imepandwa,
Lakini hatujashindwa,
Tunaweza kuing'oa,
Na nchi kuikoa.

Akipendezwa Jalia,
Itadumu Tanzania,
Amina! tena Amina!
Amina tena na tena!

Julius K. Nyerere, 16.11.1993 (TPH)

Not Too Little - A Children Book by Demere Kitunga

Mchiki is not too little to do many nice things. How about your child? Now available at Soma for 3000/=

Friday, February 21, 2014

Ndiyo Maana


"Ndiyo maana, wachache wetu tulipendekeza tuwe na Bunge Maalum la kuchaguliwa na wananchi moja kwa moja. Lakini watawala wetu, pamoja na watawala watarajiwa na wengi wa wanaharakati, katika busara zao na kwa maslahi yao, hawakutilia maanani pendekezo letu. Tumepoteza nafasi ya kipekee ya kihistoria ya kuwa na Bunge Maalum la kuchaguliwa, jambo ambalo limetufikisha hapa tuliko" - Profesa Issa Shivji: Dhana na Maana ya Bunge Maalum la Katiba

Thursday, February 20, 2014

PROFILING TANZANIA'S SCHOLARS IN THE DIASPORA - 30

Full Name

Selected Text

Linked Profile

PROFILING TANZANIA'S SCHOLARS IN THE DIASPORA - 29

Full Name

Selected Text

Linked Profile

The Tanzanian-born British Ghanaian Architect

Full Name

Selected Text

Linked Profile

The Tanzanian-born Caribbean Political Theorist

Full Name

Selected Text

Linked Profile

TOVUTI YA "CHECHE ZA AFRIKA MPYA" YAZINDULIWA


Cheche za Afrika Mpya ni medani ya ugonganishi wa mawazo na tafakuri ya maendeleo na mustakabali wa bara la Afrika.

Yeyote anayetatanishwa na fikra na matarajio ya wavujajasho wa bara letu ashiriki katika milumbi bila hofu kwa nidhamu ya kimapinduzi.

Tuesday, February 18, 2014

Launching Bookstop Sanaa in Dar: 22 February 2014


Bookstop Sanaa: Visual Art Library & Creative Learning Hub

Sunday, February 16, 2014

Haroub Othman: Yes, in My Lifetime

For erxcepts visit:

To buy visit:

PROFESA MULOKOZI: MAPITIO YA RASIMU YA KATIBA

MAPITIO YA RASIMU YA KATIBA

Wakati vikao vya Bunge la Katiba vinakaribia kuanza kule Dodoma, ni muhimu kwa Watanzania wenye kujali mustakabali wa nchi hii kuendelea kutoa mawazo juu ya Rasimu ya Pili ya Katiba na mchakato mzima wa kutunga Katiba mpya ili kupanua na kukomaza mjadala ndani na nje ya Bunge hilo.

Rajua (Maono) na Mtazamo wa Rasimu ya Pili ya Katiba
Katiba ya Kidemokrasia au Kitaifa hupaswa kuwakilisha maono ya Umma au Taifa kwa jumla kuhusu masuala muhimu ya Uhuru na Utambulisho wao, mfumo wa utawala wanaoutaka, uhusiano kati ya watawala na watawaliwa, majukumu ya watawala na mipaka ya mamlaka yao, haki na majukumu ya raia, na aina ya mfumo wa kijamii-kiuchumi wanaoutaka. 

Mgogoro mkubwa ulimo ndani ya Rasimu hii unahusu mgongano kati ya rajua ya “kumwezesha mnyonge” (aliyoishadidia Mwenyekiti wa Tume ya Kuandika Katiba) na mwelekeo wa Katiba wa kujenga uchumi huria wa kibepari na demokrasia ya wachache dhidi ya (au kwa niaba ya?) wengi. Mgogoro huu umeibuliwa na ukweli kuwa hakukuwa na Mwafaka wa Kitaifa kuhusu aina ya jamii tunayotaka kuijenga kabla ya kujitosa katika kuandaa Katiba ya kutekeleza azma hiyo. Maana, baada ya yote, Katiba ni chombo tu cha kutekeleza azma ya jamii nzima au ya makundi fulani yenye nguvu ndani ya jamii. Hivyo swali kuu la kujiuliza ni, je, Katiba yetu inanuwia kutekeleza azma ya kina nani katika jamii yetu?

Kwa upande wa mfumo wa uchumi, ambao hatimaye ndio msingi wa Katiba yoyote ile, tungeweza kukubaliana kuwa tujenge mfumo mmojawapo kati ya hii ifuatayo:

-       Ubepari huria
-       Ujamaa wa kisoshalisti
-       Ubepari wa kitaifa/kizalendo
-       Uchumi-mchanganyiko (usoshalisti + ubepari pamoja kwa viwango mbalimbali).

Kwa kadiri nilivyoielewa Rasimu ya 2 ya Katiba, naona inatuelekeza zaidi kwenye Ubepari huria, lakini wenye uliberali ndani yake, ingawa baadhi ya vifungu vyake vinagongana na azma hiyo.  Hili linashiria jambo moja: kwamba, ingawa hapakuwa na mwafaka wa kitaifa, lakini palikuwa na mwafaka wa kitabaka wa tabaka tawala nchini kuhusu aina ya jamii na utawala wanayoitaka. Katika muktadha huo, ni muhimu kujiuliza ni ubepari wa aina gani unaojengwa – ule wa kitaifa-kizalendo, au ule wa kikuwadi-kibarakala (compradorial). Mapitio haya yanafanywa kwa kuzingatia muktadha huo. Nje ya muktadha huo hapahitajiki mapendekezo bali Katiba mpya kabisa yenye mchakato na mwekeo tofauti.

MAPITIO YA KATIBA YENYEWE

Utangulizi wa Rasimu ya Pili ya Katiba unaeleza rajua na baadhi ya azma muhimu za Taifa zinazozingatiwa katika Katiba hii:

-       …Kwa kuwa sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayoheshimu na kuzingatia misingi ya utu, uhuru, haki, usawa, udugu, amani, umoja na mshikamano katika nyanja zote za maisha yetu;
     …na kwa kuwa , tunaamini kuwa misingi hiyo inaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye…
-       kujenga Taifa huru na linalojitegema…
-          kujenga umoja na mshikamano utakaowezesha kutimiza malengo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kimazingira na kulinda urithi kwa ujumla;

Tunaweza kuchukulia kuwa azma hizi ni vielelezo vya rajua ya Katiba (si ya Taifa) kuhusu aina ya nchi inayotakiwa kujengwa. “Kuheshimu misingi ya utu na haki…” na “Kujenga Taifa huru linalojitegemea” ni mambo yanayohusu takriban nyanja zote muhimu za maisha – hasa uchumi, utamaduni, elimu, sayansi, siasa na ulinzi na usalama. Je, ni mfumo gani wa uchumi na utawala utatuwezesha kuyatimiza?

Tukianza na suala la kujenga Taifa huru linalojitegemea, vifungu vya Katiba vinavyohusu suala hili vinasema Utawala utahakikisha kuwa: 
Ibara ya 10 (3) (c):


 (c) kiuchumi, Serikali inachukua hatua zinazofaa ili -
(i) kuwaletea wananchi maisha bora kwa kuondoa umaskini;
(ii) kuhakikisha kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kuwa utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine;
(iii) kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na wavuvi….


Maelezo haya yanatupeleka kwenye mfumo ulio kinyume na ubepari, kama si mfumo mchanganyiko wa uchumi. Mathalan, katika mfumo wa ubepari, haiwezekani “kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine” maana mfumo mzima umejengwa kwenye msingi wa unyonyaji wa mwajiri kwa mwajiriwa.  Je, Katiba hii inatupeleka kwenye Ujamaa? Ibara zinazofuata zinakanusha dhana hii:
Ibara ya 10 (3)(c)(xi):

“kuhamasisha uwekezaji wa pamoja baina ya raia na wasio raia katika miundombinu ya uchumi, uvunaji wa rasilimali na maliasili za Taifa;” Katiba inaona kuwa hii ni njia muhimu ya kuelekea kwenye uchumi wa kujitegemea. Maoni yangu ni kuwa njia hii inaweza kufanikisha kujenga tabaka la mawakala wenyeji wa mabepari wa kigeni. Ili kujenga Taifa huru linalojitegemea kikwelikweli katika uwanja wa uchumi, ningeshauri kifungu hiki kipanuliwe kwa kuzingatia maudhui yafuatayo:

-       kuhamasisha uwekezaji wa Watanzania katika mihimili mikuu ya uchumi,  miundombinu ya uchumi, na uvunaji wa rasilimali na maliasili za Taifa. Uwekezaji huo unaweza kufanywa na raia binafsi, au kupitia katika vikundi vyao vya uzalishaji, vijiji, vyama vya ushirika au serikali za mitaa na serikali kuu kupitia mashirika ya Umma kama NDC, TPDC, TANESCO, n.k., Pale ambapo uwezo na rasilimali za ndani hazitoshi, dola itahamasisha uwekezaji wa pamoja baina ya raia na wasio raia, na baina ya serikali ya Tanzania na mashirika yake  na serikali au makampuni ya kigeni, katika maeneo muhimu ya kiuchumi, hasa viwanda vikubwa, kilimo, nishati na uvunaji wa rasilimali….

Hapa tunaangalia maudhui zaidi. Maelezo yanaweza kuwekwa katika lugha ya kisheria baadaye. Maana ya pendekezo hili ni kwamba tukubali kujenga uchumi mchanganyiko ukiwamo uwekezaji wa dola, vyama vya ushirika, vikundi vya wazalishaji, na watu binafsi.  Tukubali ukweli kwamba hakuna bepari wa kigeni atakayetujengea uchumi unaojitegemea; kazi hii inabidi ifanywe na sisi wenyewe; kwa kuwa mabepari binafsi wenyeji ni wachache na dhaifu, dola haina budi kuingilia kati.

Suala la kujenga “umoja na mshikamano” linaambatana na mambo mengi, kama vile utamaduni na utambulisho (pamoja na kuwa na lugha moja na mfumo amali – value system - wa kitaifa), na hasa kutambua na kulinda haki za raia, na kuwa na mfumo wa uwakilishi unaowapa sauti wanyonge.

Katika Rasmu ya sasa, kuna juhudi ya kutoa haki kwa raia (ibara ya 27 na nyingine kadha), lakini katika suala la uwakilishi kuna matatizo makubwa. Rasimu imeainisha makundi kadha ya “wanyonge” wakiwamo wanawake, walemavu, wavuvi na wafugaji (Ibara ya 10 (3)). Makundi mengine makuu ya wanyonge imeyaacha. Makundi hayo ni: vijana, watu wasio na ajira, na wafanyakazi wa ujira. Kadhalika, haki za wazee (Ibara ya 48) hazijapewa uzito unaostahiki, hususani kuhusiana na haki ya kulipwa pensheni inayostahili, na kuwakilishwa Bungeni. Je hawa watawakilishwa pia Bungeni? Watawakilishwa na nani?

Hebu tuvipitie vipengele vyenye utata:

Suala la Utamaduni na TEHAMA
Utamaduni umezungumziwa kwa mtazamo wa kijadi kwa kuuhusisha na mila, desturi, lugha, mambo ya kale, n.k. Kuna haja ya kupanua wigo na kuongeza mkazo katika suala la Utamaduni kama roho na utambulisho wa Taifa, ambao inabidi ulindwe na kuenziwa kwa kila hali, huku ukiendelezwa na kubadilishwa kulingana na mahitaji ya sasa. Hivyo maelezo kuhusu utamaduni katika Ibara ya 10 yarekebishwe kwa kuongezewa madhui yafuatayo:

-       Kujenga Taifa linalojivunia utambulisho wake, lenye utamaduni imara unaokwenda na wakati, lenye kujali historia na mashujaa wake, kuthamini vitabu na usomaji, na kuhimiza, kuendeleza na kutumia TEHAMA katika elimu na maisha ya kila siku.
Kulinda Haki za Raia

Ibara ya 10 inaeleza vizuri kuhusu hatua zitakazochukuliwa na serikali kulinda haki za raia, zikiwamo za kiuchumi, kisiasa na kitamaduni. Haki ambazo hazijapewa uzito wa kutosha ni:

-   haki za wafanyakazi wa ujira, ikiwamo haki ya kulipwa ujira wa haki kwa kazi wanazofanya, na haki ya kugoma ili kudai malipo ya haki;
-   Ibara 27(1) inatoa haki ya uhuru kwa kila mtu. Pia haki ya kutonyang’anywa uhuru bila ya kufuata sheria. Hata hivyo, ibara za 39 na 40 zinanatoa mwanya kwa mtu kuwekwa kizuizini bila kupitia katika mfumo wa kimahakama. Hii ni sheria ya kale ya kikoloni, na ni hatari; inafaa ielezwe wazi kuwa hakuna mtu au mamlaka yenye madaraka ya kumweka mtu kizuizini (kwa muda unaozidi saa 48) isipokuwa mahakama.

Haki ya Uwakilishi
Hapa napo kuna utata. Katiba inabainisha namna makundi mawili ya Walemavu na Wanawake yatakavyowakilishwa Bungeni, lakini haibainishi namna makundi mengine ya “wanyonge” yatakavyowakilishwa.

Ibara ya 10(3) ( c) (iii): kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na wavuvi…
inaibua maswali mengi. Haifafanui “mazingira bora” ni yapi na watu hao watawakilishwa wapi au katika chombo kipi, na watawakilishwa na nani.
Aidha, uwakilishi wa wanawake na walemavu una utata:

  • Wanawake: Watakuwa asilimia 50 ya wabunge wa Bunge la Muungano [Ibara ya 113 (3)]. Likitazamwa kijuujuu hili ni pendekezo zuri kwa kuwa linaweka “uwakilisha sawa” baina ya wanawake na wanaume. Hata hivyo, pendekezo hili linapochambuliwa linaibua masuala mapya. Kimsingi mantiki ya pendekezo hili ni kwamba mgongano au mtafaruku mkuu katika nchi hii ni wa kijinsia kati ya wanaume na wanawake, na hii ndiyo njia ya kuutatua.  Dhana hii inachukulia kwamba wanawake wote, bila kujali hali, tabaka, imani, n.k. wana hali sawa, maslahi na mawanio sawa, na wanaume vivyo hivyo. Hivyo mwanamke yeyote anayeingia Bungeni anawakilisha wanawake, na mwanamume yeyote anayeingia Bungeni anawakilisha wanaume. Mtazamo huu si sahihi na unakanushwa na uzoevu wetu wa miaka 50 ya uwakilishi wa wanawake Bungeni. Kwanza unaficha tofauti za kitabaka na kijamii miongoni mwa makundi hayo mawili ya kijinsi. Hapa mwanamke au mwanamume mnyonge wa kijijini au mtaani anaweza asiwakilishwe.  Kuna uwezekano wa kundi dogo la wanaume na wanawake wenye uwezo, elimu na hali nzuri kushirikiana kushika madaraka kwa maslahi ya kundi lao (kama livyo sasa ambapo wakubwa wanakwenda Bungeni na wake/waume zao) dhidi ya wanawake na wanaume wanyonge. Hili haliepukiki iwapo wabunge hao wa kike na kiume watadhaminiwa na vyama vya siasa (vinavyomilikiwa na kutawaliwa na wanaume) na vyenye itikadi na maslahi ya tabaka tawala. Iwapo kifungu hiki cha uwakilishi wa kijinsia kitabakia, itabidi yaongezwe maelezo kuwa wawakilishi hao wa wanawake si lazima wadhaminiwe na Chama cha siasa; wanaweza kudhaminiwa na asasi huru za wanawake (bahati mbaya hili la uwakilishi wa asasi huru za kijamii Bungeni – kama ilivyo katika baadhi ya nchi za kimaendeleo – halijaingizwa katika Katiba), au kusimama wakiwa wagombea binafsi (wanaojidhamini au wanaodhaminiwa na asasi mahsusi za utetezi wa wanawake). Bila kufanya hivyo tutaishia kuwa na wabunge wanawake wa “mrengo wa kiume” Bungeni. Huu utakuwa ni uwakilishi wa kitakwimu, hautakuwa uwakilishi wa kweli.
  • Aidha, pendekezo la uwakilisha sawa wa kijinsia halitafanikiwa iwapo Katiba itabakiza kifungu kinachowazuia wanyonge (wakiwamo wale wasio na elimu ya kidato cha IV au wasiojua Kiingereza) kugombea Ubunge (Ibara ya 125 (1) (a) na (b) inatamka: 
-       125(1) Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika Ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo:
(a) ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja wakati wa kugombea;
(b) anajua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kiingereza na ana elimu isiyopungua kidato cha nne;
(c) ni mwanachama aliyependekezwa na chama cha siasa au mgombea huru;


-       Kifungu hicho kinawanyima kijanja asilimia kama 70% ya wananchi wote haki ya kugombea Ubunge, na kuwapa haki hiyo wasomi wachache wasiozidi 30%. Huu si ukiritimba wa kisiasa tu, bali ni ukaburu wa kisiasa, na unapingana na Ibara ya 7 (g) ya Katiba hii hii ambayo inasema mamlaka ya nchi itahakikisha kwamba:

-       “ kunakuwepo fursa na haki zilizo sawa kwa wananchi wote, wanawake na wanaume, bila ya kujali rangi, kabila, nasaba, itikadi, dini au hali ya mtu”

Ibara ya 35(2) inasema: 

…Kila mtu ana haki na fursa sawa kushika nafasi yoyote  y a  kazi, uongozi au shughuli yoyote  iliyo chini ya mamlaka ya nchi. …

na Ibara ya 25(3-4)inaongeza:

(3) Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake….
(5) Kwa madhumuni ya masharti ya Ibara hii, neno “kubagua” maana yake ni kutimiza utashi, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia utaifa wao, kabila, mahali walipotokea, maoni yao ya kisiasa, rangi, dini, jinsi, ulemavu au hali yao katika jamii kwa namna ambayo watu wa aina fulani wanafanywa au kuhesabiwa kuwa dhaifu au duni na kuwekewa vikwazo au masharti ya vipingamizi ambapo watu wa aina nyingine wanatendewa tofauti au wanapewa fursa au faida iliyoko nje ya masharti au sifa za lazima.


Napendekeza Ibara 125(1) irekebishwe kama ifuatavyo:

125(1) Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika Ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo:
(a) ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja wakati wa kugombea;
(b) anajua kuongea, kusoma na kuandika Kiswahili;

(c) ni mwanachama aliyependekezwa na chama cha siasa au kikundi cha kijamii, au ni mgombea huru;


“Kikundi cha kijamii” hapa ni vyama vya watu wenye hali na maslahi maalumu, kama vile wafanyakazi, wakulima, wanawake, wazee, vijana, wasanii, waumini, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara, n.k. Uwakilishi wa vikundi hivyo unatakiwa uwe huru – usidhibitiwe na vyama au Rais. Hivyo wawakilishi wa makundi hayo wasiteuliwe na Rais (angalia Ibara ya113(b)), au vyama vya siasa, bali wachaguliwe moja kwa moja kwa kupigiwa kura na wanachama wa makundi hayo, na wasilazimishwe kudhaminiwa na vyama vya siasa. Ni wazi kuwa hili ni pendekezo jipya lenye mtazamo tofauti na ule wa Katiba, ambayo mtazamo wake unajikita katika ubunge wa kupitia vyama vya siasa au watu binafsi tu.

Uzoevu wetu wa sasa wa uteuzi wa Wabunge wa Bunge la Katiba uliofanywa na Rais umeonesha kuwa wawakilishi wa vikundi wanaoteuliwa kwa utaratibu huo huenda wakamwakilisha Rais na Chama chake badala ya kuwakilisha vikundi vinavyohusika.

Uongozi, Utawala Bora na Uwajibikaji

Miongoni mwa mambo yanayoweza kuvuruga umoja na mshikamano wa kitaifa unaopendekezwa na Katiba ni udhaifu au ubovu wa uongozi. Suala hili rasimu ya Katiba imelizungumzia sana, na hata imeweka masharti na miiko ya uongozi (Sura ya 3 ya Katiba). Hata hivyo, ili kuwa na uongozi bora, haitoshi tu kuweka maadili na miiko ndani ya Katiba, bali inatakiwa pia kuwa na mifumo ya udhibiti na usimamizi wa viongozi walioko madarakani.  Miongoni mwa mifumo hiyo ni:

·      Uwazi katika utendaji wa serikali na vyombo vyake;
·      Udhibiti wa madaraka ya viongozi kwa njia ya Bunge, mahakama n.k.
·      Uhuru wa vyombo vya habari
·      Bunge huru lisilodhibitiwa na chama kimoja na lenye wabunge wengi wasiotoka katika vyama vya siasa
·      Uwezekano wa kiongozi, akiwamo Rais, kushitakiwa na hata kuvuliwa madaraka pindi anapovunja maadili
·      Vyombo imara vya kudhibiti ufisadi.
Katiba hii inatoa mwanya wa kuwadhibiti viongozi, lakini wakati huo huo inaufinya mwanya huo kuhusiana na Rais kwa kuruhusu Bunge pekee kumshitaki, na kuzuia watu wengine kumshtaki kwa makosa ya jinai aliyofanya akiwa madarakani au kabla au baadaye:

Ibara ya 87:

87(1) Wakati Rais akiwa madarakani, hatashitakiwa wala mtu yeyote hataendesha mashtaka ya aina yoyote dhidi yake mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai….
(3) Isipokuwa kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na kuondolewa madarakani na Bunge, haitakuwa halali kwa mtu kumshtaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au la madai dhidi ya mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo alilofanya wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya Rais.


Ibara hii ni mbaya na iondolewe; itasaidia kulinda ufisadi. Katika kipindi cha miaka 50 tangu tupate uhuru, Watanzania tumeona aina mbalimbali za Marais, wengine waadilifu, wengine wezi na mafisadi.  Kama Rais ni mwizi, fisadi, mbakaji, muuaji au mhalifu wa kivita, hakuna sababu ya kumlinda kikatiba; ashitakiwe na kupata adhabu yake. Kutoa uwezo wa kumshitaki Rais kwa Bunge tu ni njia tu ya kumlinda, hasa iwapo Bunge limejaa wabunge wa chama chake.

Ibara ya 40 (3) inasema:

Raia wa Jamhuri ya Muungano hatapelekwa katika nchi ya nje yoyote kujibu mashtaka au kufanyiwa mahojiano ya aina yoyote kinyume cha ridhaa yake, isipokuwa kwa mujibu wa sheria za nchi na mikataba ya kimataifa na wajibu wa nchi katika uhusiano wa kimataifa….

Ingawa kijuujuu kifungu hiki kinaonekana kuwalinda “raia”, lakini  kwa hakika kinawalinda viongozi. Na bila shaka kifungu hiki kinamhusu Rais pia.  Sasa kama mtu huyo hawezi kushtakiwa hapa nchini, na hawezi kushtakiwa nje ya nchi (ICC Uholanzi?), atashtakiwa wapi?  (Hivi sasa Marais wa Afrika wanafanya kampeni ya kuzuia wenzao wasipelekwe The Hague katika mahakama ya ICC kushtakiwa kwa makosa ya mauaji ya halaiki wanayotuhumiwa kuyatenda).
Pendekezo: Ibara ya  87 irekebishwe kama ifuatavyo:

87(1) Wakati Rais akiwa madarakani, hatashitakiwa wala mtu yeyote hataendesha mashtaka ya aina yoyote dhidi yake mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai isipokuwa Bunge tu. Hata hivyo, itakuwa ni halali kwa mtu kumshtaki au kufungua mahakamani shauri la jinai au la madai dhidi ya mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya mtu huyo kuacha madaraka hayo kutokana na jambo alilofanya kabla, wakati au baada ya kushika Urais.
- Rais au kiongozi au raia yeyote wa Tanzania anayetuhumiwa kutenda makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu au ufisadi ulikothiri anaweza kupelekwa kujibu mashtaka nje ya nchi kwa mujibu wa sheria za Kimataifa.


MUHTASARI WA MAPENDEKEZO/ MAPENDEKEZO MADOGOMADOGO

-        Ibara ya 19: kuh.mali ya umma, ongeza kifungu:

-        …kiongozi wa umma hatajimilikisha au kujiuzia au kuuziwa mali ya umma kama vile ardhi, nyumba, gari au mitambo wakati wa uongozi au baada ya kutoka katika nafasi yake ya uongozi;…

- Ibara ya 24(5): rekebisha suala la ubaguzi wa aina yoyote katika hali na fursa, ikiwa ni pamoja na kipingamizi cha kielimu kwa wagombea wa Ubunge [pia 34(1)]; hivyo ibara itaoana na(35)(2):  “Kila mtu ana haki na fursa sawa kushika nafasi yoyote  ya  kazi, uongozi au shughuli yoyote iliyo chini ya mamlaka ya nchi.

- Ibara ya 36 (1): Haki za wafanyakazi: Ongeza  haki ya kugoma ili kudai maslahi bora baada ya njia nyinginezo kushindwa.

- Ibara ya 40 (1): Kuna haki ya kuweka watu kizuizini? Ni mamlaka yapi yamepewa haki hiyo?
- Ibara ya 40 (1): Mazingira si suala la mtu binafsi tu; serikali inawajibikaje? (k.m. miundo mbinu ya maji taka; kutunza misitu, mito na maziwa, kuwekeza katika nishati mbadala, kuzuia uchafuzi unaotokana na kelele, n.k.)?

- Ibara ya 42(1): Inatoa haki ya elimu bora ya msingi bila malipo. Elimu ya msingi hapa ieleweke kuwa ni hadi Kidato cha IV.

- Ibara ya 43 (1): Haki za mtoto – si kupewa jina la uraia tu, bali pia kulinda utamaduni na utambulisho wake.

- Ibara ya 44: Haki na wajibu wa vijana si kushiriki katika maendeleo tu, bali pia katika ulinzi wa Taifa lao.

-Ibara ya 47 (1): Haki za wanawake: ongeza “haki ya kumiliki na kurithi mali”

- Ibara ya 59:  Ifafanue vizuri haki za mtu huyo mwenye asili ya Tanzania

- Ibara za 60-69: Hizi zinahusu muundo wa shirikisho la serikali tatu. Rasimu imejaribu kutekeleza matakwa ya makundi-tawala yenye maslahi katika muundo wa aina hiyo, lakini katika kufanya hivyo imelegeza muungano hadi kuufanya ukaribie kupoteza maana. Muundo unaopendekezwa unaelekea zaidi kwenye ushirikiano kuliko muungano. Unaweza kuwa na maana tu iwapo utakuwa ni hatua ya awali ya kwenda kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki. Vinginevyo, huenda ukatupeleka kwenye utengano. Muundo wa serikali mbili ulikuwa unalinda vizuri utambulisho wa Zanzibar; utambulisho wa Tanzania Bara haukuhitaji kulindwa kwa kuwa haukutishiwa na Zanzibar au Muungano. Kilichoikwamisha Zanzibar hata ikashindwa kuendeleza watu wake vizuri zaidi si muungano tu, bali pia siasa na sera zake za ndani zilizodhibitiwa na kikundi kidogo cha wateuliwe kilichozifuja rasilimali zilizokuwapo kwa jina la “mapinduzi.”

-       Ibara ya 60 (1):  Kinahitajika kifungu kinachozibana serikali za Zanzibar na Tanganyika zisikiuke Katiba hii katika Katiba zao na utendaji wao.

 Ielezwe kuwa Katiba hii ndiyo Katiba Mama; Katiba za Tanganyika na Zanzibar sharti zikubaliane na masharti ya Katiba hii; chochote kilicho nje kitakuwa batili.

-       72(1)(j) na (k): Kutoa msamaha kwa wafungwa na kuidhinisha adhabu ya kifo yanaweza kuwa majukumu ya Marais wa Tanganyika na Zanzibar badala ya kuwa ya Rais wa Muungano, ila kama wahusika wamekata rufaa kwa Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho.

-       Ibara ya 79(d): Umri wa mtu kuruhusiwa kugombea Urais ushushwe hadi miaka 35.

-       Ibara ya 79(e): “Shahada ya chuo cha elimu ya juu” ni ipi? Haiko wazi. Hoja muhimu ingekuwa ni kwamba awe na elimu ya kutosha ya darasani au inayolingana nayo.

-       Ibara ya 88(5): Tume ya kumchunguza Rais isiwe na wajumbe walioteuliwa naye katika nyadhifa walizo nazo (k.m. Jaji Mkuu wa Jamhuri anateuliwa na nani?)

-       Ibara ya 103: Masharti ya mawaziri kuhudhuria vikao vya Bunge yamebana mno; wao ndio wawakilishi wa serikali Bungeni, hivyo ni bora wahesabiwe kuwa Wabunge kwa mujibu wa nyadhifa zao, kama alivyo Mwanasheria Mkuu, na wahudhurie vikao vya Bunge wakati wote bila haki ya kupiga kura. Bunge haliwezi kusimamia serikali ambayo haiko Bungeni kupokea maagizo na mapendekezo ya Bunge hilo.

-Dhana ya “Waziri Mwandamizi” haina tofauti na ya Waziri Mkuu isipokuwa labda katika maslahi.

- Ibara ya 113 (2):  Wabunge wa kuwakilisha walemavu au kikundi chochote cha watu wasiteuliwe na Rais, bali wachaguliwe na walemavu wenyewe (au wanakikundi wanaohusika) kupitia vyama au vikundi vyao, na wasipitie vyama vya siasa (wanaweza kuhesabiwa kuwa wabunge binafasi kwa mujibu wa Katiba hii). Kanuni hii hii itumike kwa makundi mengine: vijana, wanawake, makundi ya kiimani, wafugaji, wafanyakazi, wakulima wadogo wadodo, wafanyabiashara, n.k.

- Ibara ya 113 (3-4): majimbo 75 ya uchaguzi yataainishwa vipi? Kama ni kimikoa, kuna haja ya kuweka utaratibu wa uundaji wa mikoa ili kuzuia ufisadi wa kisiasa kutumika katika uundaji huo kwa lengo la kuwezesha chama fulani au watu fulani kuingia au kubakia katika madaraka.

- Ibara ya 113 (3): kuweka nafasi za wabunge 2 – mwanamke na mwanamume kunatoa picha kwamba mgawanyiko au mtafaruku mkubwa nchini ni kati ya wanawake na wanaume, hivyo wanahitaji uwakilishi sawa. Je hivyo ndivyo ilivyo? Huu ni uwakilishi wa kitakwimu usioendana na uhalisi. Uzoevu wetu unaonesha kuwa wanasiasa wanawake na wanaume Bungeni mara nyingi huwakilisha kundi au tabaka lilelile, mawazo yaleyale na maslahi yaleyale. Kuwa na wanawake wengi Bungeni hakuna maana kuwa wanawake wanyonge (ambao ndio wengi) watawakilishwa. Aidha, iwapo katika miaka 50 ya uhuru aghalabu tumekuwa na wabunge wengi zaidi wa kiume (pengine hadi 70%), kuna ubaya gani kuwa na wabunge wanawake wengi zaidi ya wanaume iwapo watawakilisha vizuri maslahi na matakwa ya wapiga kura? Aidha, uteuzi wa wagombea ubunge ndani ya vyama vya siasa vinavyodhibitiwa na wanaume utahakikishajie kuwa wanateuliwa wagombea ambao ni wawakilishi wa kweli wa maslahi ya wanawake ni si ya wanaume waliowapitisha?

- Ibara ya 117: Ongeza kipengele kuwa “sheria inayotungwa na Bunge la Muungano na ambayo haikiuki masharti ya Katiba hii itakuwa na nguvu katika pande zote mbili za Muungano.”

Ibara ya 121(1-2):  Haiko wazi; kwa nini Bunge lisitunge sheria kuhusu mambo hayo yaliyotajwa  iwapo linaona inahitajika? Kwa nini kibali cha Rais kitangulie wakati hatimaye Rais atahitajika kutia sahihi?

Ibara ya 125(1): Sifa za kuchaguliwa kuwa Mbunge zirekebishwe kama ifuatavyo:

-Kipengele cha elimu ya Kidato cha IV kiondolewe, maana kinawanyima haki ya kuchaguliwa takriban 70% ya Watanzania.

- Kipengele cha kujua Kiingereza pia kondolewe kwa sababu kinawabagua Watanzania walio wengi, wakiwamo wenye digrii (iwapo watapewa mtihani nina hakika wengi wao hawatapita)

-Kipengele ( c) pia kirekebishwe; watu wengine huwa wanafungwa kwa sababu za kisiasa za kutetea wanyonge; hivyo kufungwa isiwe sababu ya kumnyima mtu haki ya kugombea. Kipengele hicho kinaweza kutumiwa vibaya na wanasiasa (hasa chama kilichoko madarakani) kuwanyamazisha wapinzani wao kwa kuwazulia kesi za kufungwa.

- Ibara ya 128(1): sababu za mtu kukoma kuwa Mbunge zirekebishwe ili zisitumiwe vibaya: k.m. (d) “kizuizi gerezani” huweza kufanywa makusudi ili kumuondoa mtu Bungeni; (g) kuondoka katika chama cha siasa isiwe sababu ya kuacha Ubunge, bali mbunge huyo aendelee na ubunge akiwa Mbunge binafsi asiye na chama, maana alichaguliwa na wananchi wa jimbo lake, si wanachama wa Chama chake tu. Hii itaimarisha uhuru wa mawazo na kujieleza ndani ya vyama na Bungeni.

-       Ibara ya 135(1): Umri wa kuwa Spika uteremshwe hadi miaka 35.

-       Ibara ya 136: Fafanua majina ya wagombea wa Uspika yatapatikanaje?

-       Ibara ya 158: Jaji Mkuu achaguliwe na Jopo la Majaji kutoka pande mbili za Muungano; asiteuliwe.

-       Ibara ya 169: Sioni sababu ya msingi kwa nini majaji wa Mahakama ya Rufaa wawe “raia wa kuzaliwa” wakati kazi waifanyayo ni ya kitaaluma/kiweledi zaidi.

-       Ibara ya 193(1)(d): Tume Huru ya Uchaguzi isiwe na madaraka ya kugawa majimbo ya uchaguzi; majimbo yaainishwe kikatiba. Mathalan, kila mkoa ungeweza kuwa jimbo moja, na mikoa  isibadilishwe ovyoovyo bali itajwe kikatiba.

-       Ibara ya 195(1): Mkurugenzi wa Uchaguzi asiteuliwe na Rais, bali aainishwe na kuteuliwa na Tume Huru ya Uchaguzi au chombo kinginecho.

-       Ibara ya 200 (1): Mwenyekiti wa Tume ya Maadili asiteuliwe na Rais. Vinginevyo itaingiliwa kinyume cha Ibara ya 206(1).

-       Ibara ya 209: Tume ya Haki za Binadamu isiteuliwe na Rais bali iainishwe Kikatiba.

-       Ibara ya 225(1): Matumizi maalumu na ya dharura yafafanuliwe – maelezo yanaacha mwanya wa kutumiwa vibaya.

-       Ibara ya 237(1): Rais hawezi kuwa Mwenyekiti wa Baraza ambalo yeye si mjumbe; aorodheshwe miongoni mwa wajumbe.

-       Ibara ya 250(1): Viongozi wa nchi washirika wakiwa na mamlaka juu ya viongozi wa Polisi na Usalama walio chini ya Muungano utendaji utakuwaje? Naona kuna utata. Labda inahitajika Polisi ya Tanganyika/Zanzibar nje ya ile ya Shirikisho.

Ibara ya 231(c): Ugharimiaji wa serikali na shughuli za Muungano unahitaji ufafanuzi zaidi. Mathalan, kila Mshirika atachangia kiasi gani (fomula gani itatumika? K.m. asilimia fulani ya GDP?). Hatimaye itakuwa lazima kuwa na kodi maalumu na tozo za Shirikisho (Federal Tax). Hivyo kila mwananchi atalazimika kulipa kodi mbili (kama ilivyo Marekani).


Lugha na Uwasilishaji

Tume imejitahidi kuandika Kiswahili kizuri na sanifu. Kuna makosa madogomadogo ya matumizi, tahjia na sarufi ambayo yanaweza kurekebishwa baada ya wabunge kukubaliana kuhusu maudhui. Mifano:

·      Disemba => Desemba
·      kuwepo, kuwemo, n.k. => kuwapo, kuwamo…
·      kuelekeza kwa lengo => kuelekeza kwenye lengo
·      Mahali pengi rasimu inatumia istilahi “rushwa” na “ubadhirifu” badala ya “ufisadi” ambayo ni istilahi jumuishi. Kuna sababu yoyote?
·      taasisi => asasi
·      “sekretariati” => lingeweza kuwa “Seketaria” ili kupunguza ukakasi.
·      mwanamme => mwanamume.

Pendekezo hapa ni kwamba baada ya Bunge kukubaliana kuhusu maudhui, wanasheria na wataalamu wa lugha wakae pamoja na kuuhariri mswada wa Katiba bila kupotosha au kubadilisha maudhui yaliyokubaliwa.

M.M. Mulokozi (Profesa Mstaafu), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Februari 2014

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP