Tuesday, February 11, 2014

BUNGE LA KATIBA: MWANZO MBAYA MWISHO MWEMA?

BUNGE LA KATIBA TANZANIA 2014: MWANZO MBAYA MWISHO MWEMA?

Bunge la Katiba limekwishatangazwa. Vikao vyake karibu vitaanza. Kama vikao hivyo vitafanyika Dodoma kama ilivyoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari, itabidi ifanywe juhudi ya ziada ya kuwapatia makazi nadhifu na lishe bora zaidi ya watu 1500 kwa siku 70 au zaidi. Watu hao zaidi  ya 1500 ni pamoja na wajumbe kama 600 wa Bunge, wengi wao wakiwa ni wanasiasa wa vyama mbalimbali, na wapambe wao (kama vile wasaidizi wa mawaziri, madreva, watumishi wa Bunge, wafuasi na wenzi wa wabunge, n.k.). Kama vikao vingefanyika Dar es Salaam hapangekuwa na tatizo la makazi, na huenda gharama zingepungua kidogo. Bila shaka mabilioni mengi ya shilingi, ambayo yangeweza kujenga barabara, hospitali, shule na viwanda, yatatumika.  Baadhi ya watu wanaopenda utani wanasema hizo ndizo “gharama za demokrasia.”  Watani wengine wanadhani ni “gharama za ufisadi.” Yawezekana kuna ukweli katika kauli zote mbili, ila ukweli kamili utadhihirishwa na matokeo ya kongamano hilo ― yaani ni aina gani ya Katiba, na kwa mantiki hiyo, ni aina gani ya Taifa, litazaliwa kutokana na kongamano hilo la gharama kubwa.  La msingi kwa sasa ni kwamba, vyovyote viwavyo, gharama zote za kongamano zitalipwa na mlipa kodi, hususan mkulima na mfanyakazi wa Tanzania.

Baada ya majina ya wabunge kutangazwa, ruwaza fulani imeanza kujitokeza. Yawezekana ruwaza hiyo imepangwa au haikupangwa. Kwanza, kuna juhudi ya kuhusisha vikundi vingi vya kijamii katika mchakato huu – walemavu, wakulima, wafanyakazi, wavuvi, wafugaji, vikundi vya kidini, asasi za kijamii, n.k. Hii ni kwa mujibu wa sheria ya machakato wa Katiba, na ni jambo zuri. Pili, kitakwimu kuna uwiano mzuri kiasi wa kijinsia (baadaye, katika makala nyingine, nitaeleza upungufu wa aina hiyo ya uwiano). Dosari za dhahiri pia zipo; hapa nitataja tatu: kwanza kuna utamalaki wa wanasiasa (wa vyama) dhidi ya makundi mengine ya kijamii. Kwa mahesabu ya haraka nimepata idadi ya wanasiasa 399 yaani takriban asilimia 66 katika Bunge hilo. Hii ni hatari na ni mwanzo mbaya, maana wanasiasa, kama kundi, kwa hulka na maslahi hawatofautiana sana katika masuala ya kikatiba. Wote nia yao ni kutawala, na ikiwezekana kutawala milele.  Sauti za wanasiasa binafsi wachache wa kimaendeleo wenye kujali zaidi maslahi ya nchi na Umma huenda zikagubikwa na zile za umati wa wanasiasa “wa kawaida” wenye kusaka maslahi binafsi au ya vyama vyao. Huu ni mwanzo mbaya.

Dosari ya pili niliyoibaini ni uwiano mbaya wa uwakilishi.  Mathalan, wakulima, ambao ni kama 70% ya Watazania, wanawakilishwa na wajumbe 20 tu kama wafanyakazi. Chama cha Mapinduzi, chenye wanachama kama milioni 5, kinawakilishwa na wajumbe zaidi ya 250 (kwa makisio yangu). Zanzibar yenye watu milioni moja imewakilishwa na theluthi moja ya wajumbe. Hili labda ni suala la kisheria na lina nia nzuri ya kuwapa sauti zaidi Wazanzibari na kujenga muamana kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano (muamana ambao rasimu ya Katiba itakayojadiliwa inautengua kwa kupendekeza serikali tatu).
Dosari ya tatu ni kukosekana kwa uwakilishi wa makundi kadha muhimu ya kijamii. Mathalan kundi la mabepari (wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa) halina uwakilishi rasmi (kutoka “Chambers of Commerce” na kwingineko). Je, tuchukulie kuwa kwa kuwa wanasiasa wengi pia ni mabepari, basi kundi hilo limewakilishwa?

Kundi la watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama (polisi, wanajeshi, wanausalama, jeshi la kujenga taifa, jeshi la kujenga uchumi) vilevile halikuwakilishwa. Ingawa Katiba ya sasa inawazuia watu hao kushiriki katika siasa, lakini Bunge la kutunga Katiba kwa hulka yake linapaswa kuwa jumuishi – halipaswi kuwa Bunge la kisiasa kwa maana ya kawaida ya Kikatiba, maana hili ni Bunge la mwafaka wa Kitaifa. Kuliacha nje kundi hilo kubwa na muhimu ni dosari ambayo gharama yake hatimaye iaweza kuwa ghali.

Kundi jingine muhimu ambalo halikuwakilishwa ni lile la waumini wa dini nyinginezo nje ya zile za Ukristo na Uislamu. Hawa ni pamoja na wafuasi wa dini mbalimbali za Kihindi/Kiasia, na wanajadi, yaani waumini wa dini ya asili. Hapa lazima nikiri kuwa sina hakika kamili, maana data niliyo nayo ni majina tu ya wawakilishi 10 wa dini. Ingawa majina hayo yanaonekana kuwa ya Wakristo na Waislamu, lakini sina uthibitisho kamili. Je baadhi yao wanaweza kuwa Wahindu, Mabudha au Wanajadi? Je, makundi hayo hayakuhama-sishwa ili yapendekeze majina ya wawakilishi wao kwa Rais? Sina jibu kwa hilo, ila naona uwezekano wa kuwapo ubaguzi wa kidini katika jambo hili, hasa tunapokumbuka kuwa wanajadi, kwa makisio yangu, hawapungui watu milioni tano.  Huu nao ni mwanzo mbaya.
Mchakato wa kuwapata wabunge 201 “wa nyongeza” ulielekeza mapendekezo yapelekwe kwa ma-Rais wa Muungano na wa Zanzibar, ambao wangeteua wawakilishi kutokana na mapendepekezo hayo. Hili limefanyika. Dosari za mchakato huo zimekwishajadiliwa na wachambuzi wengi katika vyombo vya habari na sitazirudia hapa.

Je, tuhitimishe kuwa huu ni mwanzo mbaya wenye kubashiri mwisho mwema? Au ni mwanzo mbaya utakaokuwa na mwisho mbaya? Jibu bado ni kitendawili. Je kuna uwezekano wa kurekebisha hali kabla ya kikao cha kwanza cha Bunge hili tarehe 18 Februari? Kwa baadhi ya dosari uwezekano upo kama pakiwa na utashi wa kisiasa. 

[M.M.Mulokozi, 9/2/2014]

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP