Tuesday, March 25, 2014

Mtanziko wa Wanamuungano, Mkanganyiko wa Wanazuoni na Mpasuko wa Wanasiasa

Wananchi na Mtanziko wa Wanamuungano, Mkanganyiko wa Wanazuoni na Mpasuko wa Wanasiasa 

Mjadala mkali unaoendelea nchini kuhusu muundo wa Muungano unazidi kuzalisha mitanziko, mikanganyiko na mipasuko. Sasa ni vigumu kwa mwanamuungano, mwanazuoni na mwanasiasa kutenganisha misimamo itokanayo na matokeo ya kiimani, kitafiti na kiitikidi. Hali hii tata inatukumbusha kile mwasisi mmojawapo wa Muungano alichokiita 'Mtanziko wa Mmajumui wa Afrika'.

Mwasisi huyo alikuwa akimaanisha kuwa muumini wa Umoja wa Afrika ana mtanziko utokanao na hitaji la kujenga Muungano wa bara lake na hitaji la kujenga nchi yake. Hivyo, kuwa na uwiano thabiti kati ya mahitaji hayo mawili ambayo si mara zote yanaendana ni changamoto kubwa. Sasa hali hii inajidhihirisha miongoni mwa tulio waumini wa Muungano wa Tanzania ambao pia ni watetezi wa uhuru (zaidi) wa Zanzibar ndani ya Muungano.

Mwanamuungano, ikiwa ni pamoja na baadhi ya makamishna wa Tume Maalum ya Mabadiliko ya Katiba, anajua fika kuwa bila uhuru zaidi wa Zanzibar ndani ya Muungano umoja huo utakufa tu. Lakini pia wanajua kuwa kuutafuta uhuru huo eti kwa kuifufua - ama kuihuisha - Tanganyika kutaiua Tanzania. Kanuni ya Muungano wetu ndivyo ilivyo, kuwa na Tanganyika kubwa yenye Serikali yake ni kuifanya iwe kubwa kuliko hata Tanzania achilia mbali Zanzibar ambayo itaelemewa na ukaka huo mkubwa kuliko hata ilivyo sasa ambapo kuna malalamiko wa 'Tanganyika kulivaa koti la Muungano'. Tanganyika ikirudi itabidi ilivae kabisa koti lote la Muungano hivyo kupelekea Zanzibar kujitoa ama itabidi ilivue kabisa koti hilo na hivyo kusababisha pia Muungano uvunjike. 

Mwanazuoni, ikiwa ni pamoja na walio wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, anajua fika kuwa kuna tatizo kubwa katika uhalali wa kisayansi wa takwimu zilizowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuwekewa msisitizo na Jaji Warioba katika hotuba yake ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa Bunge Maalum. Ni vigumu kwa Wanazuoni hawa kupinga hoja za Rais Kikwete dhidi ya takwimu hizo wakati wa hotuba yake ya kuzindua Bunge hilo licha ya ukiukaji wake wa uhuru wa Vyombo Vikuu vya kuandaa Katiba Mpya. Dakta Kitila Mkumbo amelielezea kwa weledi hili la mkanganyiko wa takwimu za Tume kama ifuatavyo:

Tatizo kubwa kuhusu maoni ya wananchi katika ripoti ya Tume ya Warioba ni ukweli kwamba washiriki hawakupatikana kwa njia ya kinasibu (random sampling). Hawa ni watu waliojitolea kwenda kutoa maoni kwa hiari yao na kwa sababu zao na hawakuchaguliwa kama inavyofanyika katika tafiti za kimaoni (opinion polls). Njia hii ya kupata washiriki katika lugha ya kitafiti inaitwa ‘convenience sampling’. Hii ndio njia ya kupata washiriki ambayo inadharaulika kuliko zote katika utafiti takwimu na matokeo yatokanayo na njia hii huwa hayakubaliki kisayansi, na hakuna jarida la kitafiti makini linaloweza kukubali kuchapisha matokeo yatokanayo na maoni ya washiriki waliopatikana kwa njia hii. Ndio kusema, kisayansi, maoni ya wananchi katika ripoti ya Tume ya Warioba ni kiashiria tu (indicative) na hayawezi kutiliwa manani katika kufikia uamuzi wa maana na mkubwa.  Tungekuwa makini katika mchakato huu, tungeitisha kura ya maoni ya wananchi wote kuhusu Muungano kabla ya kuandika Katiba. Aidha, kama Tume ya Warioba ilihitaji kutumia matokeo ya utafiti takwimu katika kujenga hoja yake wangefanya utafiti wa kisayansi katika utaratibu wa ‘opinion poll’. Takwimu zilizopo katika ripoti ya Tume kwa sasa hazina uhalali wa kisayansi katika ulimwengu wa utafiti wa kitakwimu (Mkumbo: http://www.wavuti.com/2014/03/mkumbo-uhalali-wa-kitafiti-wa-maoni-ya.html)

Mwanasiasa, ikiwa ni pamoja  Mwanazuoni Dakta Mkumbo mwenyewe, anajua fika kuwa itikadi zimeingilia sana misimamo mingi. Hii ni hatari sana maana kuna wanasiasa na wafuasi wao wameamua kufumbia macho hoja nzito kuhusu uhai na hatma ya Muungano na mustakabali wa Tanzania ndani ya Serikali Tatu kwa kuwa tu wanakichukia chama tawala na madhila yake. Chuki yetu kwa CCM ambayo inaendelea kutumia ubabe ili hoja ya Serikali Mbili ipite isitufanye tukakanganyikiwa na kuacha kuichambua kwa undani hii hoja tete tunayoletewa kwenye 'sahani ya fedha' kama mbadala japo haijathibitishwa popote kuwa inaweza kufanya kazi katika nchi yenye historia, taasisi na wasifu wa kipekee kama yetu. Wapo wanaodiriki kusema eti tusonge mbele tu na kutotumia rejea za chambuzi jadidi kama uchambuzi huu hapa chini wa Jaji Warioba kisa aliutoa kabla hajawa Mwenyekiti wa Tume:

Sasa hivi kiini ni ugomvi wa madaraka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hivi ukileta serikali tatu, ugomvi huu hautakuwapo? Ukileta Serikali ya Tanganyika yenyewe haitadai madaraka? Mwisho wataomba madaraka hadi Serikali ya Muungano isiwe na chochote. Hivi Serikali ya Tanganyika kwa mfano ikawapo, ikataka iwe na wimbo wake wa Taifa, bendera yake, nembo yake, kisha inadai ifanye biashara ya nje, unafikiri tutakuwa tumefika wapi? Ni kwamba tutakuwa tunaondoa Muungano na kurudisha Tanganyika na Zanzibar. Lakini kama wananchi wanataka hivyo, sawa (Warioba: http://www.raiamwema.co.tz/jaji-warioba-tusidanganyane-kutaka-serikali-tatu-ni-kuvunja-muungano#sthash.XMjhRYCx.gd9YFh5E.dpuf)

Maoni ya wananchi, wakiwamo wasomi/wanazuoni wetu, lazima yachambuliwe kwa namna zote - kisiasa, kihistoria na kadhalika - ili tuweze kufanya kile ambacho Rais amekisisitiza kuwa ni uamuzi utokanao na kuwa na taarifa (informed decision). Ndiyo, wananchi tunapaswa kufanya maamuzi baada ya kusoma au walau kusikia chambuzi ambazo wanazuoni/wasomi (hasa) waliosomeshwa kwa kodi zetu walizifanya kutokana na taaluma zao za sheria, sayansi ya siasa na zinginezo. Kwenye hili hata Mwanazuoni mahiri Dakta Mkumbo anaruhusu itikadi zake za kisiasa zimfanye asitumie kipimo kile kile alichokitumia kuupinga uhalali wa takwimu za Tume kudai kuwa hoja yao ya Serikali Mbili ina mashiko; na kudai kuwa eti uzoefu na uzalendo na hata ukada wa Jaji Warioba, Dakta Salim Ahmed Salim na Joseph Butiku, waliokuwa kwenye Tume, ni kielelezo kuwa msimamo wa sasa wa Serikali Mbili sio ule ule wa CCM ya Mwalimu Nyerere ilhali sote tunajua kuna misingi na misimamo mingi mizuri ya enzi za mkuu wao huyo wa zamani wa kazi imevunjwa licha ya kuwepo kwa wazee wetu hao toka atutoke:

Ndio kusema msingi mkubwa wa mapendekezo ya muundo wa serikali tatu katika ripoti ya Tume ya Warioba unapaswa kutokana na uzito wa sababu ambazo wananchi walizitoa kuhusu kwa nini wanataka muundo wa serikali tatu na sio wa serikali mbili uliozoeleka. Hivi ndiyo uhalali wa utafiti hoja (qualitative research) unavyojengwa. Utafiti hoja hauangalii idadi ya watu bali uzito wa hoja husika. Kwa maoni ya Tume, ambayo nami nakubaliana nayo, ili tuendelee na muundo wa serikali mbili itahitajika kufanyika ukarabati mkubwa sana. Serikali ya CCM ilifanya makosa makubwa kuiruhusu Zanzibar kufanya mabadiliko makubwa sana katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ambayo kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya Muungano, wanadhani kwamba, kwa marekebisho haya ya Katiba ya Zanzibar, ilikuwa ni tangazo la Zanzibar kujitoa katika Muungano. Hili lilikuwa ni kosa kubwa la kisiasa, kiutawala na kisheria. Sasa hatuwezi kula keki na hapo hapo tuendelee kuwa nayo. Wataalamu wa mambo ya Muungano wanaeleza kwamba huwezi tena kuendelea na muundo wa serikali mbili bila kuifanyia ukarabati mkubwa Katiba ya Zanzibar, jambo ambalo linaonekana haliwezekani kwa sasa (Mkumbo: http://www.wavuti.com/2014/03/mkumbo-uhalali-wa-kitafiti-wa-maoni-ya.html)

Maadam tumeamua kujificha kwenye kichaka cha madai kuwa 'haya ndiyo maoni ya wananchi' kana kwamba sisi wengine wote tunaopinga Serikali Tatu sio wananchi na ni wafuasi wa CCM basi tuwe tayari kukusanya maoni hayo yote nchini kisayansi na ikibidi hili la Muungano tulifanyie referendamu yake yenyewe, yaani wote tulipigie kura. Na kama kweli tumedhamiria kutafuta uzito hasa wa hoja ambao hauzingatii wingi wa watu basi tutulie na tutafakari kwa kina kuhusu miaka 50 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mjenga nchi ni mwananchi. Nchi hii ni yetu sote. Wananchi tusikubali kabisa mtanziko wa wanamuungano, mkanganyiko wa wanazuoni na mpasuko wa wanasiasa utupe Katiba itakayovunja nchi yetu changa kipenzi kisa 'kipya kinyemi ingawa kidonda'.

Mungu ibariki Tanzania. 
Dumisha Uhuru na Umoja.
Wake kwa Waume na Watoto
Mungu ibariki Tanzania na Watu wake.

Sunday, March 23, 2014

Uhalali wa Hotuba na Uzito wa Hoja ya Rais

Uhalali wa Hotuba na Uzito wa Hoja ya Rais 

Ni jambo la muhimu kutenganisha haya masuala mawili. Mosi, uhalali wa hotuba ya Rais Kikwete ya kuzindua Bunge Maalum la Katiba. Pili, uzito wa hoja yake kuhusu Muundo wa Muungano.

Kuhusu uhalali, wa kisheria, kidemokrasia na kimadaraka, hakika Rais alivuka mipaka. Hilo halina ubishi. Cha ajabu ni kuwa miongoni mwa wanaolalamikia hili ni wale wale ambao toka mwanzoni kabisa  tuliwaambia msimwachie Rais akahodhi mchakato huu hasa kwenye uteuzi. Wapo waliobisha na kusema eti sisi tunaleta upinzani tu badala ya ushirikiano ili tusonge mbele kuleta mabadiliko. Bahati nzuri matamshi na maandishi yao yapo mitandaoni - kwenye facebook, twitter, blog, makundi ya google na yahoo kama Wanazuoni, Wanabidii na Wanamabadiliko - kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo vitakavyohoji tulifikaje hapa tulipo.

Rais alichokifanya ni kuutumia mwanya huo mpana waliuotoa wanamaridhiano hao, wakiwamo ambao sasa wapo kwenye kile wanachokiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kutoa hotuba yenye hoja yenye uzito (weight) utakawaolemea wajumbe hasa wale wa chama tawala ambacho yeye anakiongoza kama Mwenyekiti, yaani CCM, na ambao ni wengi zaidi japo mahesabu aliyofanyiwa Rais yanayonyesha bado kutakuwa na kazi ya kuwashawishi wapinzani wa muundo mmojawapo ili kupata theluthi mbili inayohitajika kupitisha Rasimu ya Katiba Mpya. Zaidi ya hilo aliongozana na viongozi wakuu wa zamani wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akiwamo Amani Abeid Karume, mtoto wa Mwasisi mmojawapo wa Muungano, na hata Mama Maria Nyerere, mjane wa mwasisi mwingine wa Muungano, ili kuwatumia ipasavyo kisiasa kuipa msisitizo (insistence), ukubali (legitimacy), mamlaka (authority) na nguvu (power) hoja yake kuu siku hiyo. 

Hiki ndicho kitu wachambuzi wa sayansi ya siasa wanachokiita Onyesho la Madaraka (Display of Power) na wachambuzi wa utamaduni wa siasa wanakiita Siasa za Maonyesho (Politics of Performance). Wajumbe walimpa Mwenyekiti wa Baraza Maalum la Katiba, Samwel Sitta madaraka makubwa kisheria ya kumwalika mgeni rasmi tena katika mazingira hayo na hata walipoambiwa atakuja na ugeni wote huo hawakugoma. Walidhani atatoa hotuba huru ambayo haitaegemea upande wowote. Sasa wanalalamika.

Huyu ndiye Mwenyekiti ambaye alipita kwa kishindo kwenye uchaguzi huu eti kwa kuwa alionekana ndiye angalau angalau hatakuwa na upendeleo kwa upande wowote na kuongoza kwa kasi na viwango (speed and standard). Lakini, kama tulivyoona, ndiye Mwenyekiti Sitta aliyekuwa akimwongezea maneno Rais Kikwete wakati anahutubia hilo Bunge Maalum, tena maneno ambayo yanaonesha kabisa wapi wote wameegemea - kwenye mtazamo wa chama chao na Serikali ambayo Mwenyekiti Sitta bado ni Waziri wa Baraza lake la Mawaziri chini ya Rais Kikwete. Kwa kiasi kikubwa mgongano huu wa madaraka waliufumbia macho. 

Cha ajabu hata viongozi mahiri miongoni mwa wanajumbe wanaharakati na UKAWA n waliokuwa na vigezo vya kutosha hawakugombea Uenyekiti. Wala yale madai yao ya muda mrefu ya kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri asitoke katika chama chochote cha kisiasa hawakuweza walau kutuonyesha, hata kama ni kwa mfano, yanawezekanaje walipokuwa wanamchagua Mwenyekiti wa Bunge Maalum. Wagombea wakuu walitoka vyama vya kisiasa na hatimaye Mwenyekiti na Makamu wake wote wakatoka kwenye chama tawala na tena Sitta akiwa ni yule yule aliyepitishwa bila kupingwa na chama chake kilichokwishatoa msimamo wake kuhusu Muundo wa serikali katika Muungano. Uchaguzi huo umedhihirisha kuwa kura ya turufu wanayo CCM-Zanzibar ambao CCM-Bara wakifanikiwa kukubaliana nao ni rahisi 'kura kutosha'.

Tupo tunaopinga uhalali wa Rais kutoa hotuba vile lakini hatupingi uzito wa hoja yake kuhusu Muungano. Ni hoja nzito iliyojikita katika historia na uelewa wa misingi ya Muungano ambayo hata Jaji Warioba anaifahamu fika ila, kama mwanasheria mmoja alivyohisi, inaonekana kwa ajili ya kutafuta  maridhiano (compromise) badala ya mapatano (consensus) ameamua kuyaweka kapuni, tukubali yaishe. Huyu ni Warioba aliyenukuliwa akisema haya baada ya uchambuzi wa kisheria ambao kwa kiasi kikubwa ulitokana na kijitabu chake cha Tanzania: Hatma ya Muungano:

  Sasa hivi kiini ni ugomvi wa madaraka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hivi ukileta serikali tatu, ugomvi huu hautakuwapo? Ukileta Serikali ya Tanganyika yenyewe haitadai madaraka? Mwisho wataomba madaraka hadi Serikali ya Muungano isiwe na chochote. Hivi Serikali ya Tanganyika kwa mfano ikawapo, ikataka iwe na wimbo wake wa Taifa, bendera yake, nembo yake, kisha inadai ifanye biashara ya nje, unafikiri tutakuwa tumefika wapi? Ni kwamba tutakuwa tunaondoa Muungano na kurudisha Tanganyika na Zanzibar. Lakini kama wananchi wanataka hivyo, sawa (Warioba: http://www.raiamwema.co.tz/jaji-warioba-tusidanganyane-kutaka-serikali-tatu-ni-kuvunja-muungano#sthash.XMjhRYCx.gd9YFh5E.dpuf)

Ni wananchi gani hao waliosema wanataka mpaka Warioba ikabidi sasa aseme "sawa" tu kuwa tuwe na muundo wa Muungano ambao chambuzi mbali mbali kisheria na kikatiba zake zilionyesha haufanyi kazi? Ni hoja zipi hizo ambazo zilimfanya Warioba na wanatume wenzake waseme "sawa" japo wanakiri kuwa wamebaki na hii misimamo yao ambayo hakuiwasilisha kama uchambuzi,  tathmini na ripoti mbadala ya wanatume ambao hawakukubaliana? Alichofanya ni kutuambia kuwa wanachoamini wanatume "wote pamoja ni umuhimu wa kuendelea kuwepo na kudumu kwa Muungano" lakini kuhusu namna ya kuufanya Muungano huo wa miaka 50 uendelee kweli inaonekana Warioba anakiri kuwa: 

Hiyo haina maana kwamba kila mmoja wetu ameacha imani yake, itikadi yake na msimamo wake. Kuna mambo ambayo kila mmoja wetu amebaki na imani yake na msimamo wake. Kwa mfano, kwenye suala la Muungano tupo tunaoamini muundo unaofaa ni Serikali Moja, tupo tunaoamini Muundo wa Serikali Mbili, tupo tunaoamini Serikali Tatu na tupo tunaoamini Muungano wa Mkataba (Warioba: http://www.wavuti.com/2014/03/hotuba-ya-rasimu-ya-katiba-mpya.html)

Sasa kuna wanamaridhiano wanaoona kuwa njia iliyobaki ni kusonga mbele kwa kuacha mabaya ya hotuba ya Warioba na ya Rais Kikwete, kuchukua mazuri ya hotuba hizo na kisha kuboresha rasimu ya pili ya Katiba. Tatizo la kujaribu kuuma na kupuliza, kumfurahisha huyu na yule, hata pale misingi ama nguzo muhimu ya ujenzi na ubomoaji wa wa nchi, dola  na taifa-dola (nation-state) ni kuja na miundo isiyotekelezeka na isiyozingatia kuwa unaweza kurithishwa dola na mkoloni bila kuwa hasa na taifa hivyo hitaji kujenga taifa-dola. Matatizo ya Muungano, kama chambuzi za Warioba tulizozirejea zinavyoonesha, yanatokana na kugombania madaraka. Hivyo, huwezi kutafuta njia ya katikati ya kuunda Nchi (Country) Moja, Dola (State) Moja na Serikali (Governments) Tatu.

Tukitaka kuelewa tatizo hili tuangalie historia ya mchakato wetu wa kugatua madaraka, yaani kupeleka madaraka katika ngazi za chini. Serikali Kuu imekuwa ikihodhi madaraka hayo huku Serikali za Mitaa zikiyadai miaka nenda rudi. Kinachozifanya Serikali hizi za mitaa zisiyapate madaraka haya kwa uwiano stahili ni kutokana na kutokuwa na nguvu za kiuchumi na kisiasa ukilinganisha na Serikali Kuu. Sasa unapotaka kuunda mfumo mbadala usio wa Dola Shirikisho (Federal State) ila ni wa Dola Moja (Unitary State) ambao nao una Serikali Tatu, kiuhalisia ni kuwa unaunda Serikali Moja yenye Serikali za Mitaa Mbili (Local Governments). Lakini tofauti kubwa hapa ni kuwa hizo Serikali za Mitaa sio za Mikoa, Wilaya wala Majimbo - ni za nchi mbili: Tanganyika na Zanzibar. Na si hivyo tu, hizo Serikali Mbili ndizo zenye nchi na dola ilhali hiyo Serikali Moja ni Serikali Hewa tu, isiyo na 'nchi/eneo'.

Hatari ya muundo huu unaolenga kuridhisha makundi mawili makuu katika mjadala - lile linalodai Serikali Tatu na lile linalodai Serikali Mbili - ni kuwa bado limekaa katika mfumo ule ule ambao utaoifanya Serikali ya Jamhuri ya Muungano iwe "Tegemezi na Egemezi" katika Serikali Tatu kama hotuba ya Rais ilivyosisitiza au iwe 'Kandamizi na Onevu' kama hotuba ya Warioba inavyoonekana kuelezea hali ilivyo katika Serikali Mbili za sasa. La pili litatokea kama na pale ambapo muundo huo mbadala utafanikiwa kweli kuweka mambo mengi mazito ya Muungano chini ya Serikali Kuu ya Muungano ili kuipa nguvu na kuweza kweli kupunguza nguvu za hizo Serikali za Tanganyika na Zanzibar ambazo ndizo hasa zitakazokuwa na nchi pamoja na rasilimali na watu wake. Ila kufanya hivyo ni sawa sawa na kuunda Serikali Moja ambayo itaifanya Tanganyika iwe Kaka Mkubwa aliye mbabe zaidi ya hata ilivyo sasa ambapo Zanzibar inaiona imevaa 'Koti la Muungano'.

Kinara wa muundo huu mbadala anatuambia kuwa eti tunaweza kuwa kama Afrika Kusini. Lakini Afrika Kusini baada ya kupata uhuru/demokrasia mwaka 1994 haikufanya kile ambacho sisi tulikifanya mwaka 1964. Wao wangekuwa na hali tete na tata kama yetu kama nao wangeungana na nchi ndogo ya Lesotho ambayo kijiografia ipo ndani yao au Swaziland ambayo iko mkabala nayo ama Namibia ambayo ilikuwa ikiitawala enzi za Mfumo wa Ubaguzi (Apartheid). Majimbo (Provinces) ya sasa Afrika Kusini -  Eastern Cape, Free State, Gaueteng, KwaZulu-Natal, Limpopo, Mpumalanga, Northen Cape, North-West na Western - kutokana na wingi na mengi yao kutoakisi moja kwa moja tawala zilizokuwepo kabla ya ukoloni na ubaguzi hayana utaifa (nationalism) wa pamoja wa baadhi yao dhidi ya utaifa mmoja wa Afrika Kusini kama ambavyo Zanzibar imekuwa nao na wazalendo wa Kizanzibari (Zanzibari Nationalists) wamekuwa wakiupigania kwa pamoja licha ya kuwepo pia kwa ule wa (U)Pemba dhidi ya Unguja.

Hata yale Majimbo-Nchi (Bantustan) yaliyoundwa Afrika Kusini enzi za Ubaguzi wa Rangi - Transkei, Bophuthatswana, Venda, Ciskei, KwaZulu, Lebowa na QwaQwa - hayakufanikiwa kujenga utaifa endelevu japo kwa kiasi fulani yaliundwa kwa kufuatilia jiografia ya himaya/falme/uchifu ambazo zilikuwepo kabla ya uvamizi wa Makaburu na Waingereza huko Afrika Kusini.  Ukitumia mifano hiyo Tanzania ni sawa na kulinganisha madai ya U(Zanzibar) na ya Usukuma, Uchagga, Unyamwezi, Uhehe, (U)Buhaya ambayo kwa kiasi kikubwa tuliyamaliza baada ya kufuta uchifu mara baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

Afrika Kusini inajiendesha kama Dola Moja kwa namna ambavyo tungeweza kujiendesha kama tungekubali kujivunjavunja katika majimbo makubwa (provinces) kadhaa yatakayoleta uwiano mpana wa madaraka kama ilivyo kwenye Dola Shirikishi zenye majimbo (states) nyingi, ndogo kwa kubwa, kama Marekani. Lakini hilo ni sawa na kuivunja nchi iwe katika kanda kadhaa na kama tulivyoona tayari kumeanza kuwa na siasa za ukanda Tanzania Bara zitokonazo kwa kiasi kikubwa na ushindani wa vyama vikuu vya kisiasa Tanzania Bara - CCM na CHADEMA - na kwa upande wa Zanzibar, (hasa) kabla ya mwafaka na Serikali ya Umoja,  zitokanazo na (uliokuwa) ushindani mkali kati ya CUF na CCM. 

Huku kudhani tutakuwa kama Afrika Kusini kwa kuwa na nchi mbili ambazo zitajiendesha kana kwamba sio nchi bali sehemu tu za utawala (units of governance) ni kuziambia zikubali kuwa na hadhi ndogo ya Serikali za Mitaa chini ya Mamlaka Kuu (Central Authority). Ni Kusadikika (Utopia). Jaribio la utekelezaji wake utaiweka Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mweka katika hali mbaya sana ambaye atakuwa hana nguvu kulinganisha na watendaji wakuu wa washirika wa Muungano - Kiongozi Mkuu wa Tanganyika na Zanzibar hata kama hutaiwata Marais. Na kama mwasisi mmoja wa Muungano alivyosisitiza, "huwezi kumtikisa Rais wa nchi bila kuitikisa Nchi yenyewe." Mtikiso huo utakuwa na athari kiasi gani ukiwa na nchi hewa?

Kutafuta maelewano kusitufanye tusisahau kanuni za kujenga na kubomoa nchi. Pamoja na utata wa uhalali wa hotuba ya Rais na utete wa hoja zake, kwenye hilo la Muundo wa Muungano alichokisema kina uzito. Asiyesikia la mkuu huvunjika guu.

Uwiano wa Utanganyika, Uzanzibari na Utanzania

UMOJA WA WANAOTAKA TANGANYIKA:
Ni umoja wenye mashaka. Ndani yake wapo wanaotaka Tanganyika ndani ya Muungano wa Kishirikisho wa Serikali Tatu. Lakini pia wapo ambao hawaitaki Zanzibar, eti imewachosha.


Wote wakishapata wanachokitaka - yaani Tanganyika, umoja wao utavunjika. Wasioitaka Zanzibar watadai Muungano uvunjike. Wanaotaka Muungano watajikuta na Tanganyika tu.

Lakini hiyo Tanganyika ina uhakika gani itakuwa na umoja? Falme na Uchifu wa zamani ukitaka nchi zao itakuwaje? Au mikoa/kanda kutaka kujitenga au kujiunga na nchi jirani?

Tanzania ni nchi tuliyoijenga kwa taabu sana. Ujenzi wa miaka 50 unaweza kubomolewa kwa siku 50 tu. Nchi hujengwa na wenye moyo na umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

MADARAKA NA MUUNDO WA MUUNGANO:
Hili suala naliangalia kwa macho ya uchambuzi wa kimadaraka (power analysis) zaidi na sio kwa mapenzi tu ya kutaka tu kitu kiwe au kwa uchambuzi wa kimuundo (structural analysis) tu. Tatizo lilipo kimadaraka ni kuwa kwa kiasi kikubwa Zanzibar/Wazanzibari hawataki uwiano tenge wa madaraka ambao unatokana na Serikali ya Muungano kuwa na mambo mengi ya Muungano maana kwao ni sawa na Tanganyika kuvaa koti la Muungano.

Tanganyika/Watanganyika, kama ambavyo nimesema awali, kwa sasa wana umoja wa mashaka maana hivi leo kinachowaunganisha ni kutaka Tanganyika: Humo wamo wanaotaka Serikali Tatu ili Tanganyika iwepo tu, sio kwa sababu wanataka Muungano; pia wapo wanaotaka Muungano wa Serikali Tatu kwa sababu wanadhani ni suluhisho la kero za Muungano na humo humo wanaotaka hivyo kwa sababu wanaona wanaibeba Zanzibar na imekuwa mzigo; lakini pia wanaotaka Tanganyika bila Muungano, hivyo kupata Tanganyika kwao ni hatua ya kwanza kuelekea kuvunja Muungano. Pia kuna hili kundi jipya ambalo linadhani eti inawezekana kuwa na Serikali Tatu bila kuwa na mfumo wa kishirikisho kana kwamba wenzao wanaotaka Tanganyika wanaitaka iwe tu kama Serikali za Mitaa ambazo mpaka leo zinalalamika kuwa Serikali Kuu haigatui/haipeleki madaraka ngazi za chini.
  
Hili ni suala la mgawanyo wa madaraka (power) zaidi kuliko muundo (structure). La watu zaidi ya taasisi. Ndiyo.

KUUNGANISHA SERIKALI, NCHI NA DOLA-NCHI:
Rais kaelezea vizuri kabisa kwa nini hatuwezi kuwa na Serikali 3 kwa maana hasa ya Serikali Kuu (Central Government). Hii dhana ya Nchi Moja, Dola Moja na Serikali Tatu ingeweza kufanya kazi tu kama maana ya Serikali Tatu hapa ni Serikali za Mitaa Mbili (Local Goverments) na Serikali Kuu Moja jambo, ambalo nalo haliwezekani kwa sababu Zanzibar haiwezi kukubali kuwa na Serikali hiyo yenye hadhi ndogo kiasi hicho. 

Mchakato wa ugatuzi wa madaraka i.e. kupeleka madaraka katika ngazi za chini umeshindwa kwa sababu kwa kawaida Serikali Kuu haitaki/haikubali kuziachia Serikali za chini madaraka. Lakini katika hizi Serikali Tatu zinazopiganiwa sasa ukweli, kama Rais alivyouelezea vizuri sana, ni kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa haina nguvu/madaraka ukilinganisha na Serikali za Washirika hasa huyo Mshirika mnayemdai ambaye atakuwa ni zaidi ya Kaka Mkubwa, si kwa Zanzibar tu ila hata kwa Tanzania pia, yaani Tanganyika. Uchambuzi wa madaraka (power analysis) ni muhimu sana katika suala badala ya kuleta dhana za kidhahania na matamanio ilhali hazifanyi kazi nje ya makaratasi. Serikali kwa Maana ya Serikali Kuu hujiendesha ikiwa na nchi na dola.

Kanuni za kuunda Dola Moja (Unitary State) ziko wazi kama ambavyo kuunda Dola Shirikisho (Federal State) zilivyo. Ukiwa na nchi moja kubwa inaungana na nchi ndogo Dola Shirikishi na Dola Moja zinawezekana tu kwa kuipa nafasi ya upendeleo nchi ndogo. Hali inakuwa tofauti unapokuwa na nchi nyingi, ndogo na kubwa, zinazoungana ambapo mgawanyo wa madaraka na rasilimali unakuwa na uwiano mpana (stretched). Hapo unaweza kuamua kuwa na Dola Shirikishi la nchi kadhaa au Dola Moja inayoamua kujiendesha kwa majimbo kadhaa. Hili la pili linawezekana kama Tanzania Bara itakubali kujivunjavunja na kuwa na majimbo makubwa kama manne yatayoungana na Zanzibar (kama Wazanzibari watakubali) na hivyo kutokuwa na Kaka Mkubwa anayeitwa Tanganyika. Hatari yake ni kuwa hayo Majimbo 5 yenye uwiano mpana wa madaraka ya kisiasa na kiuchumi yanaweza yakavunja nchi kama utaifa wa Tanzania hiyo hautaweza kujengwa na badala yake watu wakawa wanajenga utaifa wa hayo majimbo yao. Lile la kwanza litawezekana wenzetu wa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudani Kusini wakikubali tuungane. Ila naona ni kama vile tuna haraka sana na kusahau kuwa Serikali Mbili ni mpito tu wa kuelekea kwenye Umoja Mkubwa.

Tusifanyie mzaha suala la kupangua nchi, dola, na dola-nchi iliyojengwa - inahitaji uhakika sio majaribio tu.
 WARIOBA (1994):
Kama Zanzibar ikikubaliwa kuwa na madaraka zaidi katika mambo kama uraia, ulinzi na usalama, mambo ya nje na uhusiano wa mataifa, viwanda, biashara, hali ya hatari, posta na simu, kodi na mabenki, Tanganyika nayo itapewa madaraka hayo hayo … Matokeo yake Serikali za Tanganyika na Zanzibar zitakuwa na nguvu sana na Serikali ya Muungano itakuwa dhaifu kabisa. Mambo yanayobaki yatafanya Muungano uwe dhaifu kuliko Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ilivyokuwa. (Warioba (1994: 17) Tanzania: Hatima ya Muungano)


WARIOBA (2011): 
Wakati wote kwa mwananchi wa kawaida, kumekuwa hakuna matatizo ya Muungano. Matatizo yanatoka kwenye midomo ya viongozi.

Shughuli za wananchi wa kawaida haziangalii orodha ya mambo ya Muungano, bali haki yao kama raia. Wanajiona ni raia katika shughuli zao za kibiashara au nyingine. Mwananchi wa kawaida anaona anayo haki ya kufanya biashara mahali popote. Wananchi wamezoa hivyo. Msiwafikishe mahali wakajiona kuwa kwenda Zanzibar au kuja Bara inabidi wafuate taratibu za kwenda Kenya au Uganda.

Tunayo matatizo ya madaraka, kwamba unazo Serikali mbili kwa hiyo yale yaliyomo kwenye orodha ya Muungano ni kuonyesha Serikali hii ina madaraka gani. Wanagombania madaraka.

Kama suala ni mafuta au mengine tuzungumze. Inategemea mnavyokubaliana, tusije kuongeza au kupunguza kwenye orodha mambo ambayo yatakuja kuwatenganisha wananchi. Kama kwa mfano, kuna watu wanafikiri kuimarisha Muungano ni kuwa na serikali tatu, unaimarishaje?

Sasa hivi kiini ni ugomvi wa madaraka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hivi ukileta serikali tatu, ugomvi huu hautakuwapo? Ukileta Serikali ya Tanganyika yenyewe haitadai madaraka? Mwisho wataomba madaraka hadi Serikali ya Muungano isiwe na chochote.

Hivi Serikali ya Tanganyika kwa mfano ikawapo, ikataka iwe na wimbo wake wa Taifa, bendera yake, nembo yake, kisha inadai ifanye biashara ya nje, unafikiri tutakuwa tumefika wapi?

Ni kwamba tutakuwa tunaondoa Muungano na kurudisha Tanganyika na Zanzibar. Lakini kama wananchi wanataka hivyo, sawa.
Lakini tukivunja Muungano madhara yake ni makubwa sana kwa pande zote mbili. Mimi naamini wale wanaotaka serikali tatu wanajua nia yao ni kuvunja Muungano na huu ndio ukweli. Ukianzisha serikali tatu, maana yake unavunja Muungano.


WARIOBA (2014): 
Hiyo haina maana kwamba kila mmoja wetu ameacha imani yake, itikadi yake na msimamo wake. Kuna mambo ambayo kila mmoja wetu amebaki na imani yake na msimamo wake. Kwa mfano, kwenye suala la Muungano tupo tunaoamini muundo unaofaa ni Serikali Moja, tupo tunaoamini Muundo wa Serikali Mbili, tupo tunaoamini Serikali Tatu na tupo tunaoamini Muungano wa Mkataba.

Friday, March 21, 2014

Kweli Ndiyo Maana!

Tupo tuliosema msimwachie Rais auhodhi mchakato huu. Wapo waliobisha ila leo wanalalamika. Hayo ndiyo matokeo ya kumwachia madaraka makubwa ya kuteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Baraza Maalum la Katiba. Yamepelekea pia kupata Wenyeviti kutoka Chama Tawala. Na kupata Mwenyekiti aliyekuwa anamwongezea maneno Rais wakati anahutubia leo. Kazi kubwa kwa wanaodai Serikali 3 sasa ni kuwashawishi wajumbe wapatao 80 ambao kwa mujibu wa hesabu alizochambuliwa Rais ndio wanahitajika kupata hiyo theluthi mbili ya kura kuipitisha. Na kwa Chama Tawala kazi rahisi ni kuwashawishi (kuwatisha?) wajumbe wapatao 16 ambao kama hesabu alizozisema Rais ziko sawa ndio wanahitajika kupitisha Serikali 2. Pia hapo tujiulize hizo hesabu alipigiwa lini - je, kabla au baada ya kuwachagua wale wajumbe 201 wasio wabunge?

"Ndiyo maana, wachache wetu tulipendekeza tuwe na Bunge Maalum la kuchaguliwa na wananchi moja kwa moja. Lakini watawala wetu, pamoja na watawala watarajiwa na wengi wa wanaharakati, katika busara zao na kwa maslahi yao, hawakutilia maanani pendekezo letu. Tumepoteza nafasi ya kipekee ya kihistoria ya kuwa na Bunge Maalum la kuchaguliwa, jambo ambalo limetufikisha hapa tuliko" - Profesa Issa Shivji: Dhana na Maana ya Bunge Maalum la Katiba

JK & JKN

"Natambua kuwepo kwa rai ya kutaka Mwalimu Nyerere asitumiwe katika mjadala huu. Nionavyo mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume katika jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo kujadili na kukubaliana kuwa mfumo wa Serikali mbili ndiyo bora kwa nchi yetu. Iweje leo tunapozungumzia kuubadili, mawazo yao yawe hayafai kutumika au hata kuzungumzwa. Hivi hasa mawazo ya nani pekee ndiyo bora zaidi kutumika? Tutakuwa hatuutendei haki mjadala huu na sisi wenyewe tunaoshiriki katika mchakato huu. Rai yangu kwenu ni kuwa mzitazame hoja zote kwa marefu na mapana yake ili mpime kama zipo sababu za kuubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa Serikali tatu. Na, kama zipo mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye mashiko. (you must make an informed decision)" - JK 

Utanganyika

UTANGANYIKA

"Vijana wa Tanganyika hawana haja ya kumbembeleza ye yote wala chombo cho chote kuhusu utaifa wao; wanalijua Taifa lao. Si jingine ni Tanganyika. Tanzania ife, izikwe, ioze. Hatuitaki."

Mimi nawaheshimu kwa dhati kabisa vijana waliotoa kauli hii. Nawaheshimu kwa sababu wana akili, wana ukweli, wana ujasiri. Wana akili za kutosha kutambua kuwa ukifufua Tanganyika, Tanzania itakufa; wana ukweli unaowazuia kutumia hila za maneno matupu kama "ndani ya Muungano," kudanganya watu wadhanie kuwa unaweza ukawa na serikali ya Tanganyika, na bado Tanzania ikabaki; na wana ujasiri wa kutosha kutamka wazi wazi kwamba wanachokitaka ni kufa, na kuzikwa, na kuoza kwa Tanzania. Watu wa namna hiyo unaweza kuhitalifiana nao, lakini lazima uwaheshimu, kwa sababu ya akili zao, na ukweli wao, na ujasiri wao.

Najua sababu nyingi na matatizo mengo yaliyowafanya baadhi ya vijana na watu wazima wengine wafikie msimamo huu wa kudai Utanganyika. Lakini Tanganyika haitasaidia chochote. Hizi jitihada za kututoa kwenye haja ya kutazama kwa makini sababu halisi za matatizo ya nchi yetu, ili tuseme sababu za matatizo yetu ni Tanzania, na dawa yake ni Tanganyika, ni jitihada za kunywesha watu kasumba. Na wako Wazalendo tele wenye akili, ukweli, na ujasiri, ambao watakataa wazi wazi kunyweshwa kasumba hiyo.

Sababu zile zile zitakazoua Tanzania zitaua Tanganyika. Tanzania haiwezi kwenda na wakati, Tanganyika isiende na wakati huo huo pia. Vijana wanatambua la kwanza, na hiyo ni hatua kubwa ya kuelewa; kosa lao ni kutotambua la pili pia. Lakini hawa ni vijana. Watu wazima hawana sababu ya kutoona yote mawili; kwamba Tanzania ikifa, na Tanganyika itakufa, kwa sababu zile zile. Kinachonishangaza zaidi ni kwamba hata lile la kwanza, ambalo vijana wanaliona wazi wazi, watu wazima, wakiwamo Viongozi, wao hawalioni; au wanaliona lakini hawana ukweli na ujasiri wa vijana hawa kukiri hivyo.

* * * * * * *

SERIKALI YA TANZANIA         ni Serikali ya Muungano
BUNGE la TANZANIA            ni Bunge la Muungano
CHAMA CHA MAPINDUZI        ni Chama cha Muungano

Vyombo vitatu hivi vikishirikiana kuiua na kuizika Tanzania, adui wa Tanzania atafanya kazi gani? Swali hili nilikuwa nikiliuliza kuhusu viongozi wa Urusi. Watu hawa wanafanya mambo ambayo ni dhahiri kwamba yatavunja nchi yao. CIA ya Marekani wanaiachia kazi gani?

Nasi twaiga Warusi
Hata katika maasi,
Tuivunje vunje Dola,
Turudie makabila?


Julius K. Nyerere (1993: 39-41). Tanzania! Tanzania!: Dar es Salaam, Tanzania: Tanzania Publishing House (TPH)

Wednesday, March 19, 2014

Serikali Tatu na Zimwi Likujualo

Serikali Tatu na Zimwi Likujualo

Hatimaye Jaji Warioba amelihutubia Bunge Maalum la Katiba. Ule mzozo wa nani aanze kuhutubia kati yake na Rais Kikwete sasa ni historia. Kwa umahiri mkubwa Mwenyekiti huyu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba amekong’a nyoyo za wanaotaka Serikali Tatu.

Hata baadhi ya wapinzani wa zimwi hili tusilolijua sasa wamemgwaya Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi alivyopanga hoja zake na za Tume yake. Tayari wengine wameshabadili mtazamo na sasa wanaamini kuwa lile zimwi tulijualo la Serikali Mbili limetula vya kutosha. Sasa tunahitaji Zimwi mbadala.

Hakika mwanataaluma huyo aliyebobea katika sheria alijipanga vilivyo. Pengine sehemu pekee ya kupangua hoja zake ni matumizi ya maneno haya: “Tathmini ya Tume.” Ni vigumu kujua wapi maoni ya wananchi yanaishia na wapi tathmini au maoni ya Tume, ama vinara wa Tume, yanaanzia. Ni Zimwi lenye vichwa vingapi hasa raia tunalitaka?

Hapa tunaongelea wanatume ambao kwa namna fulani waliakisi tofauti za kimtazamo za wananchi. Pamoja na hayo mbinu yao ilikuwa ni hii: “Hata tulipopata matatizo ya kufikia uamuzi kwa suala lolote hatukukimbilia kupiga kura. Tulijifungia kwenye vikundi vya watu wenye mawazo kinzani na mwisho tukafikia maridhiano na muafaka. Dira yetu ilikuwa Maslahi ya Taifa. Hatukupiga kura hata mara moja kwa jambo lolote wala kuwa na mawazo mbadala. Kila Ibara iliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo ninaiwasilisha katika Bunge Maalum la Katiba, inaungwa mkono na kila mmoja wetu.”

Hayo aliyoyanena Jaji yanatukumbusha uchambuzi huu wa Profesa Shivji ambaye amekuwa mwiba mchungu kwa Tume: "Baada ya kuisoma Rasimu kwa kina, mimi nadhani kwamba masharti mengi ya Rasimu na muundo wake mzima ni matokeo ya mivutano mikali katika Tume. Bahati mbaya hatuna mwenendo wa majadiliano ya Tume wala taarifa yao rasmi, hata taarifa ya awali. Lakini usomaji wangu wa awali unaniambia kwamba Rasimu hii ni maelewano kwa maana ya compromise, na sio mapatano, au mwafaka, kwa maana ya consensus. Nijieleze kidogo. Katika maelewano au compromise, pande zinazokinzana hatimaye zinakubali kwa shingo upande ili kutokwamisha maamuzi. Pande zote zinapata kidogo na kupoteza kidogo, na kila upande huwa na mkakati wake wa kupata zaidi katika duru ya pili. Kwa hivyo, maelewano kamwe hayawezi kuwa kwa moyo safi. Maelewano au compromise, yanazaa uamuzi legelege. Mapatano au consensus, kwa upande mwingine, ni maafikiano yanayofikiwa baada ya mjadala mrefu, kila mmoja akilenga kuthibitisha hoja yake na kwa njia hii kusadikisha wenzake kwamba hoja yake ni sahihi. Baada ya kufikia uamuzi wa mwafaka, kila mmoja anatoka akiwa ameridhika na amefurahi. Katika compromise, kila mmoja anatoka amenuna. Ni wazi kwamba huwezi ukapata mwafaka fastafasta. Lazima utachukua muda.” (Ukurasa wa 7-8, “Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya: Mhadhara wa Kuaga Kigoda cha [Taaluma cha] Mwalimu [Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam]” Mwaka 2013).

Hakuna ubishi hapo kwenye hilo la msongo wa muda maana uchaguzi mkuu wa 2015 umekaribia. Jaji kwa namna fulani naye kaligusia katika hotuba pale aliposema: “Tume imekamilisha kazi yake kwa muda ulipangwa kutokana na kazi nzuri ya Sekretarieti. Wakati Wajumbe wa Tume walipokuwa wanakusanya maoni mikoani, Watumishi wa Sekretarieti waliofuatana na Wajumbe, walifanya kazi kwa muda mrefu sana, hata siku za mapumziko. Walikuwa wa kwanza kuamka na wa mwisho kwenda kulala.” Hakuna kulala hadi kieleweke, ndivyo tusemavyo mtaani na kwa kiasi kikubwa hakukuwa na kulala hadi Zimwi tusilolojua lieleweke. Kabla ya hapo ilibidi lieleweke kwa wanatume.

Hao wanatume walipoeleweshwa, ama kueleweshana, ndipo yakafikiwa ‘maelewano’ haya bila hata kupiga kura: “Hiyo haina maana kwamba kila mmoja wetu ameacha imani yake, itikadi yake na msimamo wake. Kuna mambo ambayo kila mmoja wetu amebaki na imani yake na msimamo wake. Kwa mfano, kwenye suala la Muungano tupo tunaoamini muundo unaofaa ni Serikali Moja, tupo tunaoamini Muundo wa Serikali Mbili, tupo tunaoamini Serikali Tatu na tupo tunaoamini Muungano wa Mkataba. Tunachoamini wote kwa pamoja ni umuhimu wa kuendelea kuwepo na kudumu kwa Muungano. Baada ya kuwasikiliza wananchi, dira yetu imekuwa ni maslahi ya Taifa na siyo maslahi ya makundi yetu au nafsi zetu. Nawashukuru sana wajumbe wenzangu wa Tume kwa kusimamia misingi ya kiutendaji ambayo imetuwezesha kukamilisha kazi hiyo.” Hiyo Sentensi ya mwisho ya Jaji hapo inatukumbusha tena msongo wa muda kuelekea 2015.

Hatua ambayo ilibidi ifuatie kabla ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba hawajapigana vikumbo kuhusu Zimwi tulijualo dhidi ya tusilolijua ndiyo hii ya hotuba ya takribani saa nne aliyoitoa Jaji. Ni hotuba ya kuelewesha na si ya kuwasilisha rasimu. Ya kuwaelewesha nini? Kutuelewesha ‘maoni’ ambayo Jaji anayaiita “Tathmini ya Tume.”

Hatuna budi sasa kuzirejea kwa kina sehemu ambazo hayo maneno ya “Tathmini ya Tume” yanatumika kama rungu kutuelewesha kuhusu Zimwi tusilolijua: “Tathmini ya Tume ni kwamba siyo rahisi mambo haya kutekelezwa chini ya muundo wa Serikali mbili.” Je, wananchi wangapi tuliulizwa kuhusu urahisi huo? Na kitu kutokuwa rahisi ina maana hakiwezekani? Na hizo jitihada za kuyarahisisha hayo mambo, kadri muda unavyokwenda na changamoto mpya zinavyoibuka, ambazo hotuba imezianisha katika sehemu ya 147 na 148 ndio mwisho wa safari? Zimwi la Serikali Tatu ndio mwarobaini?

Hapo kwenye sehemu ya 127 ya Hotuba kuna hitimisho hili: “Kwa hiyo, tathmini ya Tume ni kwamba Muundo wa Serikali moja hauna uhalisia.” Hitimisho hilo linatokana na uchambuzi huu: “Njia pekee ambayo ingefanya maendeleo ya Zanzibar yapewe uzito sawa na mambo ya Tanzania Bara ni kuyaweka mambo yote ya Zanzibar chini ya Serikali ya Muungano, yaani kuwa na Serikali Moja. Lakini kama nilivyosema, wakati wa kukabidhi Rasimu kwa Marais wetu, Muundo wa Serikali Moja una changamoto nzito. Waasisi waliona matokeo ya Muundo huo ni Zanzibar kumezwa na Tanganyika. Tume ilipokuwa inakusanya maoni, wananchi wengi, hasa Zanzibar, walionyesha hofu hiyo ni kubwa sana hivi sasa kuliko ilivyokuwa mwanzoni.”  Wameonaje kuwa Zimwi la Serikali Moja tusilolijua halina uhalisia ila la Serikali Tatu tusilolojua ndilo lina uhalisia?

Hapana shaka Jaji ana jibu. Linapatikana kwenye sehemu ya 133: “Tume ilitafakari kama kuna uwezekano wa kuyarudisha mambo yaliyoondolewa kwenye orodha kufuatia muafaka wa 1994, lakini tathmini ya Tume ni kwamba kufanya hivyo ni kuzua mgogoro upya kwani itaonekana mamlaka (autonomy) ya Zanzibar yanaingiliwa. Wakati Tume ilipokuwa inakusanya maoni, wananchi wengi wa Zanzibar kutoka makundi yote mawili, yaani wale waliotaka Muungano wa Serikali Mbili na wale waliotaka Muungano wa Mkataba, wote walipendekeza mambo mengi yaondolewe kwenye Orodha ya Muungano. Wale waliotaka Muungano wa Mkataba walitaka mambo yote yaondolewe kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano isipokuwa suala la ulinzi. Wale waliotaka Muundo wa Serikali mbili walitaka mambo yote ya uchumi yaondolewe kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Katika hali hiyo, kuyarudisha mambo ambayo hivi sasa yako chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hata kama siyo kikatiba, kunaweza kuleta mgogoro wa kisiasa.” Kama “msingi wa Muungano”, kama sehemu ya 175 ya hotuba inavyosema, ni Hati/Makubaliano ya Muungano (Articles of Union) ya mwaka 1964 yaliyokuwa na mambo ya Muungano 11 kwa nini ishindikane kuyapunguza kikatiba baada ya kuongezwa maradufu kinyemela? Si ndicho hicho  Wazanzibari wamekuwa wakikidai?

Hatutaitendea haki Tume tusipoona utata huo kuhusu historia tete unaojidhihirisha zaidi kwenye sehemu hii ya 157 ya Hotuba: “Kwa Ta[t]hmini ya Tume, Muundo wa Serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa. Muungano wa Serikali mbili waliotuachia waasisi siyo uliopo sasa. Umebadilishwa mara nyingi, wakati mwingine bila ya kufanya mabadiliko kwenye Katiba. Waasisi walituachia Muungano wa Nchi Moja yenye Serikali Mbili, na siyo Nchi Mbili zenye Serikali Mbili. Muundo wa Serikali Mbili unaweza kubaki tu kama orodha ya mambo ya muungano haitapunguzwa bali itaongezwa. La sivyo, Serikali ya Muungano itabaki na rasilimali na mambo ya Tanzania Bara tu. Katika hali hiyo, pande zote mbili zitaendelea kulalamika. Kwa upande, mmoja Zanzibar itaendelea kulalamika kwamba Tanzania Bara imevaa koti la Muungano kwa faida yake, na kwa upande mwingine, Tanzania Bara itaendelea kulalamika kwamba mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara na rasilimali zake ndizo zimekuwa Muungano.” Hivi kweli hata wanatume waliokuwa viongozi wa juu wa  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wakati wa kuongeza mambo ya Muungano hawakumbuka nia hasa ya/za kufanya hivyo?

Haiwezekani tukachakachua historia kirahisi namna hii na kusahau (kusema) kuwa Serikali Mbili ilikuwa pia ni muundo tu wa mpito kuelekea kwenye Serikali nyingi chini ya Shirikisho laAfrika Mashariki. Hotuba ya Jaji imejikita kwenye mpito wa kuelekea kwenye Serikali Moja ambao, kwa mujibu wa “Tathmini ya Tume”, hauna uhalisia. Na kama kweli hauna uhalisia basi ina maana tumebakiwa na mwisho mmoja tu ambao Muungano wa Serikali Mbili unaulenga, yaani Umoja wa Afrika (Mashariki). Na tukisema huo nao hauna uhalisia basi hakuna mwisho mwingine zaidi ya kuvunjika kwa Muungano. Lakini hotuba ya Jaji inajaribu kutabiri, ama kutuambia inajua, hautavunjika.

Haijalishi nani amevunja Katiba, kinachohitajika ni kuchukua hatua kuilinda. Lakini hotuba ya Jaji inaendeleza utamaduni wa kulalamika kuhusu upande mmoja wa Muungano kuivunj kana kwamba Katiba mpya itakuwa na kinga ya kujaribiwa kuvunjwa. Heri angetueleza, kwa kutumia taaluma yake ya Sheria, kuhusu namna ya kukabiliana na uvunjaji huo wa Katiba aliyoapa kuilinda. Na mashabiki wa mbadala wangeenda mbali zaidi na mibadala kwa  kutuonyesha namna ambavyo Mahakama ya Katiba, ambayo tayari inaruhusiwa kuundwa kwa mujibu wa Katiba ya sasa japo hatujawahi – labda kwa sababu ya woga – kujaribu kuisimika, inaweza kutatua migogoro ya Muungano. Hata mwasisi mmojawapo alishaacha kulimung'unyia maneno hilo suala: Halafu tukizitazama takwimu alizowasilisha Jaji zinaonesha kuwa Wazanzibari wengi wanataka Muungano wa Mkataba: “Mchanganuo wa takwimu hizi unaonyesha kuwa wananchi waliotoa maoni kuhusu muundo wa Muungano kwa upande wa Tanzania Bara, 13% walipendelea Serikali Moja, 24% walipendekeza Serikali Mbili na 61% walipendekeza Serikali Tatu. Kwa upande wa Zanzibar, 34% walipendekeza Serikali mbili na 60% walipendekeza Muungano wa Mkataba, na 0.1% (watu 25) walipendekeza Serikali Moja.” Ina maana ‘Muungano wa Mkataba’ ni sawa sawa kabisa na wa Serikali Tatu? Kama si sawa kwa 100% hii haina maana tunalinganisha machungwa na matofaa?

Haishangazi tupo tunaosema waasisi hawana majibu ya matatizo ya Muungano tuliyo nayo leo. Inabidi tukabiliane na kero mpya wenyewe na ikibidi tutafute mbadala. Lakini tusiache mbachao kwa msala upitao kisa umetuambia, ama kututabiria, kuwa kuifufua Tanganyikani kuiua na kuizika Tanzania. Nchi yetu bado changa. Mtoto akililia wembe?

Halahala mti na macho. Kwa hakika hotuba hii inatukumbusha methali na misemo ya wahenga wetu walioona mbali. Ndio wao waliosema Zimwi likujualo halikuli likakwisha.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP