Tuesday, March 25, 2014

Mtanziko wa Wanamuungano, Mkanganyiko wa Wanazuoni na Mpasuko wa Wanasiasa

Wananchi na Mtanziko wa Wanamuungano, Mkanganyiko wa Wanazuoni na Mpasuko wa Wanasiasa 

Mjadala mkali unaoendelea nchini kuhusu muundo wa Muungano unazidi kuzalisha mitanziko, mikanganyiko na mipasuko. Sasa ni vigumu kwa mwanamuungano, mwanazuoni na mwanasiasa kutenganisha misimamo itokanayo na matokeo ya kiimani, kitafiti na kiitikidi. Hali hii tata inatukumbusha kile mwasisi mmojawapo wa Muungano alichokiita 'Mtanziko wa Mmajumui wa Afrika'.

Mwasisi huyo alikuwa akimaanisha kuwa muumini wa Umoja wa Afrika ana mtanziko utokanao na hitaji la kujenga Muungano wa bara lake na hitaji la kujenga nchi yake. Hivyo, kuwa na uwiano thabiti kati ya mahitaji hayo mawili ambayo si mara zote yanaendana ni changamoto kubwa. Sasa hali hii inajidhihirisha miongoni mwa tulio waumini wa Muungano wa Tanzania ambao pia ni watetezi wa uhuru (zaidi) wa Zanzibar ndani ya Muungano.

Mwanamuungano, ikiwa ni pamoja na baadhi ya makamishna wa Tume Maalum ya Mabadiliko ya Katiba, anajua fika kuwa bila uhuru zaidi wa Zanzibar ndani ya Muungano umoja huo utakufa tu. Lakini pia wanajua kuwa kuutafuta uhuru huo eti kwa kuifufua - ama kuihuisha - Tanganyika kutaiua Tanzania. Kanuni ya Muungano wetu ndivyo ilivyo, kuwa na Tanganyika kubwa yenye Serikali yake ni kuifanya iwe kubwa kuliko hata Tanzania achilia mbali Zanzibar ambayo itaelemewa na ukaka huo mkubwa kuliko hata ilivyo sasa ambapo kuna malalamiko wa 'Tanganyika kulivaa koti la Muungano'. Tanganyika ikirudi itabidi ilivae kabisa koti lote la Muungano hivyo kupelekea Zanzibar kujitoa ama itabidi ilivue kabisa koti hilo na hivyo kusababisha pia Muungano uvunjike. 

Mwanazuoni, ikiwa ni pamoja na walio wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, anajua fika kuwa kuna tatizo kubwa katika uhalali wa kisayansi wa takwimu zilizowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuwekewa msisitizo na Jaji Warioba katika hotuba yake ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa Bunge Maalum. Ni vigumu kwa Wanazuoni hawa kupinga hoja za Rais Kikwete dhidi ya takwimu hizo wakati wa hotuba yake ya kuzindua Bunge hilo licha ya ukiukaji wake wa uhuru wa Vyombo Vikuu vya kuandaa Katiba Mpya. Dakta Kitila Mkumbo amelielezea kwa weledi hili la mkanganyiko wa takwimu za Tume kama ifuatavyo:

Tatizo kubwa kuhusu maoni ya wananchi katika ripoti ya Tume ya Warioba ni ukweli kwamba washiriki hawakupatikana kwa njia ya kinasibu (random sampling). Hawa ni watu waliojitolea kwenda kutoa maoni kwa hiari yao na kwa sababu zao na hawakuchaguliwa kama inavyofanyika katika tafiti za kimaoni (opinion polls). Njia hii ya kupata washiriki katika lugha ya kitafiti inaitwa ‘convenience sampling’. Hii ndio njia ya kupata washiriki ambayo inadharaulika kuliko zote katika utafiti takwimu na matokeo yatokanayo na njia hii huwa hayakubaliki kisayansi, na hakuna jarida la kitafiti makini linaloweza kukubali kuchapisha matokeo yatokanayo na maoni ya washiriki waliopatikana kwa njia hii. Ndio kusema, kisayansi, maoni ya wananchi katika ripoti ya Tume ya Warioba ni kiashiria tu (indicative) na hayawezi kutiliwa manani katika kufikia uamuzi wa maana na mkubwa.  Tungekuwa makini katika mchakato huu, tungeitisha kura ya maoni ya wananchi wote kuhusu Muungano kabla ya kuandika Katiba. Aidha, kama Tume ya Warioba ilihitaji kutumia matokeo ya utafiti takwimu katika kujenga hoja yake wangefanya utafiti wa kisayansi katika utaratibu wa ‘opinion poll’. Takwimu zilizopo katika ripoti ya Tume kwa sasa hazina uhalali wa kisayansi katika ulimwengu wa utafiti wa kitakwimu (Mkumbo: http://www.wavuti.com/2014/03/mkumbo-uhalali-wa-kitafiti-wa-maoni-ya.html)

Mwanasiasa, ikiwa ni pamoja  Mwanazuoni Dakta Mkumbo mwenyewe, anajua fika kuwa itikadi zimeingilia sana misimamo mingi. Hii ni hatari sana maana kuna wanasiasa na wafuasi wao wameamua kufumbia macho hoja nzito kuhusu uhai na hatma ya Muungano na mustakabali wa Tanzania ndani ya Serikali Tatu kwa kuwa tu wanakichukia chama tawala na madhila yake. Chuki yetu kwa CCM ambayo inaendelea kutumia ubabe ili hoja ya Serikali Mbili ipite isitufanye tukakanganyikiwa na kuacha kuichambua kwa undani hii hoja tete tunayoletewa kwenye 'sahani ya fedha' kama mbadala japo haijathibitishwa popote kuwa inaweza kufanya kazi katika nchi yenye historia, taasisi na wasifu wa kipekee kama yetu. Wapo wanaodiriki kusema eti tusonge mbele tu na kutotumia rejea za chambuzi jadidi kama uchambuzi huu hapa chini wa Jaji Warioba kisa aliutoa kabla hajawa Mwenyekiti wa Tume:

Sasa hivi kiini ni ugomvi wa madaraka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hivi ukileta serikali tatu, ugomvi huu hautakuwapo? Ukileta Serikali ya Tanganyika yenyewe haitadai madaraka? Mwisho wataomba madaraka hadi Serikali ya Muungano isiwe na chochote. Hivi Serikali ya Tanganyika kwa mfano ikawapo, ikataka iwe na wimbo wake wa Taifa, bendera yake, nembo yake, kisha inadai ifanye biashara ya nje, unafikiri tutakuwa tumefika wapi? Ni kwamba tutakuwa tunaondoa Muungano na kurudisha Tanganyika na Zanzibar. Lakini kama wananchi wanataka hivyo, sawa (Warioba: http://www.raiamwema.co.tz/jaji-warioba-tusidanganyane-kutaka-serikali-tatu-ni-kuvunja-muungano#sthash.XMjhRYCx.gd9YFh5E.dpuf)

Maoni ya wananchi, wakiwamo wasomi/wanazuoni wetu, lazima yachambuliwe kwa namna zote - kisiasa, kihistoria na kadhalika - ili tuweze kufanya kile ambacho Rais amekisisitiza kuwa ni uamuzi utokanao na kuwa na taarifa (informed decision). Ndiyo, wananchi tunapaswa kufanya maamuzi baada ya kusoma au walau kusikia chambuzi ambazo wanazuoni/wasomi (hasa) waliosomeshwa kwa kodi zetu walizifanya kutokana na taaluma zao za sheria, sayansi ya siasa na zinginezo. Kwenye hili hata Mwanazuoni mahiri Dakta Mkumbo anaruhusu itikadi zake za kisiasa zimfanye asitumie kipimo kile kile alichokitumia kuupinga uhalali wa takwimu za Tume kudai kuwa hoja yao ya Serikali Mbili ina mashiko; na kudai kuwa eti uzoefu na uzalendo na hata ukada wa Jaji Warioba, Dakta Salim Ahmed Salim na Joseph Butiku, waliokuwa kwenye Tume, ni kielelezo kuwa msimamo wa sasa wa Serikali Mbili sio ule ule wa CCM ya Mwalimu Nyerere ilhali sote tunajua kuna misingi na misimamo mingi mizuri ya enzi za mkuu wao huyo wa zamani wa kazi imevunjwa licha ya kuwepo kwa wazee wetu hao toka atutoke:

Ndio kusema msingi mkubwa wa mapendekezo ya muundo wa serikali tatu katika ripoti ya Tume ya Warioba unapaswa kutokana na uzito wa sababu ambazo wananchi walizitoa kuhusu kwa nini wanataka muundo wa serikali tatu na sio wa serikali mbili uliozoeleka. Hivi ndiyo uhalali wa utafiti hoja (qualitative research) unavyojengwa. Utafiti hoja hauangalii idadi ya watu bali uzito wa hoja husika. Kwa maoni ya Tume, ambayo nami nakubaliana nayo, ili tuendelee na muundo wa serikali mbili itahitajika kufanyika ukarabati mkubwa sana. Serikali ya CCM ilifanya makosa makubwa kuiruhusu Zanzibar kufanya mabadiliko makubwa sana katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ambayo kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya Muungano, wanadhani kwamba, kwa marekebisho haya ya Katiba ya Zanzibar, ilikuwa ni tangazo la Zanzibar kujitoa katika Muungano. Hili lilikuwa ni kosa kubwa la kisiasa, kiutawala na kisheria. Sasa hatuwezi kula keki na hapo hapo tuendelee kuwa nayo. Wataalamu wa mambo ya Muungano wanaeleza kwamba huwezi tena kuendelea na muundo wa serikali mbili bila kuifanyia ukarabati mkubwa Katiba ya Zanzibar, jambo ambalo linaonekana haliwezekani kwa sasa (Mkumbo: http://www.wavuti.com/2014/03/mkumbo-uhalali-wa-kitafiti-wa-maoni-ya.html)

Maadam tumeamua kujificha kwenye kichaka cha madai kuwa 'haya ndiyo maoni ya wananchi' kana kwamba sisi wengine wote tunaopinga Serikali Tatu sio wananchi na ni wafuasi wa CCM basi tuwe tayari kukusanya maoni hayo yote nchini kisayansi na ikibidi hili la Muungano tulifanyie referendamu yake yenyewe, yaani wote tulipigie kura. Na kama kweli tumedhamiria kutafuta uzito hasa wa hoja ambao hauzingatii wingi wa watu basi tutulie na tutafakari kwa kina kuhusu miaka 50 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mjenga nchi ni mwananchi. Nchi hii ni yetu sote. Wananchi tusikubali kabisa mtanziko wa wanamuungano, mkanganyiko wa wanazuoni na mpasuko wa wanasiasa utupe Katiba itakayovunja nchi yetu changa kipenzi kisa 'kipya kinyemi ingawa kidonda'.

Mungu ibariki Tanzania. 
Dumisha Uhuru na Umoja.
Wake kwa Waume na Watoto
Mungu ibariki Tanzania na Watu wake.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP