Friday, March 7, 2014

Ngeli, Lahaja na (Ma)Dai ya/la Kiswahili Kina Kwao

MASWALI

1. Jambazi amekamatwa au Jambazi limekamatwa?

2. Dawa imepakwa au Dawa lilipakwa?

3. Jino ilivunjwa au Jino lilivunjwa?

4. Makala yameandikwa au Makala iliandikwa?

5. Mada yametolewa au Mada imetolewa?

*KWA NINI? (ELEZA TAFADHALI)

MAJIBU

1. Jambazi amekamatwa au Jambazi limekamatwa? amekamatwa kama bado
kidhana unamuona ni mtu ila kama kidhana umemvusha kuwa jitu basi
limekamatwa

2. Dawa imepakwa au Dawa lilipakwa? me na li hapa si suala la ngeli ni
suala la wakati me ni uliopita sasa hivi na li ni uliopita kabisa

3. Jino ilivunjwa au Jino lilivunjwa? jino lilivunjwa ni sahihi hiyo
ni ngeli ya j/l

3. Makala yameandikwa au Makala iliandikwa? nadhani ili/imeandikwa ila
sina hakikka

4. Mada yametolewa au Mada imetolewa? nadhani imetolewa ila sina maelezo 
- Demere
 ---
Ifuatayo ni nukushi toka katika makala ya Ahmed Rajab yaliyochapishwa katika Raia Mwema la 326, Desemba 4, 2013:

Katika mhadhara huo amesema mengi Ngũgĩ yasiyo na ubishi na amempa sifa nyingi Mwalimu Julius Nyerere, sifa anazostahiki kupewa kwa jinsi alivyokifanya Kiswahili kuwa lugha ya taifa. Lakini lazima nibishane naye Ngũgĩ kwa kudai kwamba kwa Nyerere kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya taifa “Hatimaye, Kiswahili kikawa na kwao.”

Hapo kidogo Ngũgĩ ameteleza. Siku zote Kiswahili kimekuwa na kwao. Hakijatimliwa kikenda uhamishoni. Wakoloni walikuja wakakikuta kwao, wakaondoka, na wakakiacha huko huko kwao. 

Na kwao ni kule ambako wenyeji wake wanasema “vita hivi” na “vita vya” nasi wasemao “vita hii” au “vita ya”.  Ni wale wale wasemao “makala haya” na si wasemao “makala hii”. Na wasemao kwa inadi “makala hii” basi na waendelee na kusema “maradhi hii” badala ya “maradhi haya” kama kisemwavyo Kiswahili huko kwao.
Kwa vile neno “makala” liko katika ngeli ya JI/MA basi huwa “makala manana”. Na “kitabu chanana”/ “vitabu vyanana”; “nyumba nyanana”, “ndizi nyanana” na “tabia nyanana”.

Huko kuliko kwao Kiswahili humsikii mtu akisema “dhehebu”; wenye lugha yao wanajua kwamba madhehebu yanaweza kuwa mamoja kama makala yalivyo mamoja au mengi. Pia wanajua kwamba hakuna neno “dhumuni” bali ni “madhumuni”.

Huko ambako Kiswahili ni kwao wafuasi wa madhehebu ya Shi’a huitwa “Mashia” na humsikii mtu kuwaita “Washia”.  Akiwa mmoja huitwa “Shia” nasi “Mshia”.

Vivyo hivyo kwa wafuasi wa madhehebu ya Suni. Waswahili wanawaita “Masuni” na si “Wasuni”.  Kule ambako Kiswahili ni kwao mtu atauliza: “Yule ni Suni au ni Shia?” Humsikii mtu akiuliza: “Yule ni Msuni au ni Mshia?”

Mwalimu Nyerere kweli amefanya kazi kubwa ya kukinyanyua na kukisambaza Kiswahili katika taifa zima. Lakini si sahihi kamwe kusema kwamba kwa kufanya hivyo “Hatimaye, Kiswahili kikawa na kwao.” Kiswahili siku zote kimekuwa na kwao, ila katika huko kusambazwa kwake Kiswahili kimedakwa na wengine wanaokifanya kuwa ni chao. Hilo si jambo baya, la kujiweza kwa kujipa uwezo wa kuisarifu lugha nyingine ilimradi wasijaribu kutuweza. Wasikipotoshe Kiswahili chetu kwa kukisema tusivyokisema wenyewe Waswahili.  

- Sabatho 
---
Kama nimemuelewa Ahmed Rajab (nimeinukuu barua pepe yake hapo juu), makala yapo/ipo kwenye ngeli ya Ji/Ma, na kama kweli yako/iko humo kwa nini basi 'umoja' na 'wingi' wake unafanana na hivyo ku(ya/i)fanya (ya/i)onekane ipo kwenye ngeli inayotumia 'hii' na 'hizi'? 

Hata kwenye huo mfano wa (ma)dhehebu na (ma)dhumuni ambao Mwanazuoni mmoja humu aliwahi kuushikilia bango nao unaleta utata maana hata watu wa madhehebu ya Mwanazuoni huyo wanajiita Wasabato ilhali, kama kweli Ahmed yuko sahihi na kama nimemuelewa vizuri, wanastahili kuitwa Masabato? Ama kweli "Kiswahili kina kwao" na "Kiswahili kina wenyewe"! 
- Chambi
---
Pamoja na kukubali kwamba watu wanafanya makosa mengi ya Kiswahili na hasa hawafuati sheria za sarufi vizuri, nadhani ni muhimu kukubali pia kwamba lugha zote zinabadilika.  Kwa kutoa mfano mmoja tu, katika Kiingereza kutokana na msukumo wa jinsia utakuta kwamba mara nyingi watu wanatoa sentenso kama hii (hasa wanapoongea)

When a person is sick, they go to hospital. 

Badala ya when a person is sick he or she goes to hospital.  Ili kukwepa kutaja he na she wanatumia wingi ... they.

Kuna mifano mingi ya aina hiyo.

Sasa lini tunang'ang'ania sheria ifuatwe na lini tunakubali mabadiliko.

Wafaransa, kama Waswahili, wanakuwa prescriptive.  Wanajaribu kudhibiti matumizi ya lugha na kukataza matumizi mengine (sijui wanafanikiwa kiasi gani, kwa mfano Academie Francaise inajaribu kuzuia maneno ya Kiingereza

Upande mwingine Waingereza ni descriptive.  Iwapo neno au lugha fulani imeshaanza kutumika na wengi, wanaiweka kwenye kamusi n.k. 

Wengine wanasema ndiyo maana Achebe alivuma alivyovuma (licha ya kupigwa vita na wahafidhina wa lugha) wakati Ahmadou Kourouma ambaye aliafirikisha kifaransa kama Achebe alivyofirikisha kiingereza alishuhudia kupigwa marufuku kwa vitabu vyake vya kwanza kama Les soleils d'independence
- Mabala
---
Richard Mabala neno 'aliafirikisha' nalo limeshaingizwa ama? Nimelipenda! Inanikumbusha vile Kiswahili cha mtaani kilivyo 'embrace/adapt' neno 'change' na kuzua  neno 'a(li/me/ta)nichenjia'...
- BeeJay
---
Neno hili lilizaliwa leo.  Natafuta hakimiliki tehe tehe tehe
- Mabala
---
Anachokizungumza Ahmed Rajabu siyo Kiswahili bali ni lahaja ya Kiswahili aipendayo yeye. Ndiyo, zipo lahaja lakini kamwe zisiitwe Kiswahili cha wenyewe bali lahaja tu. Mimi humchukulia Ahmed kama mpotoshaji wa Kiswahili Sanifu bila yeye mwenyewe kujua, kwa kudhani tu yuko sahihi. Anatumia sauti pekee kujenga hoja kuliko mantiki. Nitamjibu hiyo makala yake.
- Matinyi
---
Hata Kiingereza kina lahaja, na walau lahaja kadhaa zinakubalika, japokuwa kile cha Malkia ndio kinaitwa kiingereza sanifu. Nadhani anachosisitiza Rajab ni kwamba usanifishaji wa Kiswahili uliambatana na uingizaji wa miundo/maumbo ambayo hayaendani na miundo/maumbo asili ya lugha husika. 

Pengine cha kufurahisha ni kwamba lahaja iliyochukuliwa na kufanywa kuwa lahaja sanifu ni ya huko huko kwa akina Rajab. Je, yeye kama mswahili mzawa hana haki ya kulalamika pale anapoona lugha yake inapotoshwa? Ukisoma kamusi za Kiswahili zilizoandaliwa na taasisi za Zanzibar au hata maandiko ya Kiswahili mengi toka visiwani utagundua namna Kiswahili chao kinavyotofautiana na hiki tunachojifunza huku. Kamusi moja niliyoiona hata jina lake lenyewe lilinishangaza: Kamusi LA Kiswahili. Huku tungetumia YA.
- Sabatho
---
Hata mimi hii makala niliipenda maana kwa sasa hususan kuna upotoshaji mkubwa unaendelea kwa minajili wa kudai hiki Kiswahili cha bara hiki cha Unguja na hata wengine kudiriki kukitukuza zaidi Kiswahili kilichonukuliwa na wakoloni wamisonari kuwa ndio sahihi zaidi kuliko kile kinachofundishwa na waliozaliwa na lugha yao. Alimradi....
- Salma
---
Kwa mujibu wa hayo makala uliyoyapenda, unatakiwa useme "mimi hayo makala niliyapenda"
- Chambi
---
Ndo upotoshaji ninausema suala hapa si makala bali ni wakati ambao tayari nishauanisha kwa kusema niliipenda na kumbuka unaweza kutumia hii/hizi!?
- Salma
---
Watu wa visiwani wanaweza kuwa na Kiswahili chao na wengine wakawa na cha kwao pia. Hata kiingereza cha Marekani, Canada, Australia, Uingereza hakifanani. Lakini hapa ninachokiona ni madhara ya kutokienzi Kiswahili, hatukitumii kujifunza maarifa mashuleni na hivyo tunakidumaza. Fikiria wewe Mwanazuoni katika fani yako laiti kama ungetumia Kiswahili wakati wote wa masomo yako leo hii ungekua na uelewa mkubwa sana wa lugha. Ungekua na misamiati mingi na si rahisi kuafanya makosa madogo madogo kama kuchanganya "R" na "L", "kuua" na "kuuwa" "kua" na "kuwa" nk. 

Sisi sote ni wahanga wa kutoenzi Kiswahili!
- Shangwe
---
Kwanza, Unguja kuna zaidi ya lahaja moja.

Pili, wataalam wa Kiswahili wa kwanza wa Baraza la Afrika Mashariki walikuwa Waswahili, siyo Wazungu.

Tatu, hakuna miundo ya Kiswahili iliyojengwa na wakoloni.

Nne, Ahmed Rajabu ana haki ya kulalamika na hata kulazimisha hoja kwamba yeye ndiye mwenye Kiswahili chenyewe lakini hiyo haiifanyi hoja yake kuwa sahihi.

Tano, kwa kutumia mfano neno "makala" ni vizuri tukakumbuka pi hili si neno la Kiswahili bali ni la Kiarabu. Limeazimwa tu.

Lakini pia, kwa kuheshimu mifano ya awali, kuwa Ahmed anasema kwa Kiswahili  "sahihi" - - siyo sanifu naamini - - ilibidi tuseme Shia na siyo Mshia. Pia Mashia na siyo Washia. Je, ni sahihi kusema "Islam" badala ya "Mwislamu" au "Maislam" badala ya "Waislamu"? Mimi kwangu haiji na wala haipo, sijui watetezi wa Kiswahili cha wenyewe mnasemaje?

Lakini pia, kwa kuheshimu maana inayobebwa na ngeli za JI/MA mjadala utakuwa mpana zaidi. Zina mantiki yake na haipingiki kirahisi. Hakuna lugha isiyokuwa na mantiki.
...
Kwamba Kiingereza nacho kina lahaja kunasaidia nini katika mjadala huu, hebu nisaidie hapo.

Pili, lahaja si hoja; zipo kwenye kila lugha ila lahaja ni lahaja tu hata kama ina historia ya kuibeba lugha fulani sanifu. Kwamba, Kiswahili Sanifu kilichomoka kutoka kwenye Kiunguja hakukifanyi Kiunguja kuwa Kiswahili sahihi bali kinabakia kuwa Kiunguja.

Hoja hii ndiyo Wakenya hujidanganya nayo kuhusiana na Kimvita ambacho kiko mbali zaidi na Kiswahili kuliko hicho ki-Ahmed Rajabu.


Kiunguja, Kimakunduchi, Kipemba, Kingazija, ni baadhi tu ya lahaja zinazozungumzwa Unguja. Sasa tuzichukue zote tuziite Kiswahili cha wenyewe? Ahmed anazunguka humu humu kwenye lahaja. Ni tatizo pia lililopo kwenye Kiarabu ambapo Mwarabu Misri anadai chake ni bora zaidi na wa Sudan anasema hivyo, lakini wote wanapoteana na cha Mauritania na cha Kuwait, n.k. na wote hawa wanatofautiana na Kiarabu Sanifu ambacho wengine hukiita cha Aljazeera na vyuo vikuu.
 ---
Matinyi

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP