Wednesday, March 19, 2014

Serikali Tatu na Zimwi Likujualo

Serikali Tatu na Zimwi Likujualo

Hatimaye Jaji Warioba amelihutubia Bunge Maalum la Katiba. Ule mzozo wa nani aanze kuhutubia kati yake na Rais Kikwete sasa ni historia. Kwa umahiri mkubwa Mwenyekiti huyu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba amekong’a nyoyo za wanaotaka Serikali Tatu.

Hata baadhi ya wapinzani wa zimwi hili tusilolijua sasa wamemgwaya Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi alivyopanga hoja zake na za Tume yake. Tayari wengine wameshabadili mtazamo na sasa wanaamini kuwa lile zimwi tulijualo la Serikali Mbili limetula vya kutosha. Sasa tunahitaji Zimwi mbadala.

Hakika mwanataaluma huyo aliyebobea katika sheria alijipanga vilivyo. Pengine sehemu pekee ya kupangua hoja zake ni matumizi ya maneno haya: “Tathmini ya Tume.” Ni vigumu kujua wapi maoni ya wananchi yanaishia na wapi tathmini au maoni ya Tume, ama vinara wa Tume, yanaanzia. Ni Zimwi lenye vichwa vingapi hasa raia tunalitaka?

Hapa tunaongelea wanatume ambao kwa namna fulani waliakisi tofauti za kimtazamo za wananchi. Pamoja na hayo mbinu yao ilikuwa ni hii: “Hata tulipopata matatizo ya kufikia uamuzi kwa suala lolote hatukukimbilia kupiga kura. Tulijifungia kwenye vikundi vya watu wenye mawazo kinzani na mwisho tukafikia maridhiano na muafaka. Dira yetu ilikuwa Maslahi ya Taifa. Hatukupiga kura hata mara moja kwa jambo lolote wala kuwa na mawazo mbadala. Kila Ibara iliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo ninaiwasilisha katika Bunge Maalum la Katiba, inaungwa mkono na kila mmoja wetu.”

Hayo aliyoyanena Jaji yanatukumbusha uchambuzi huu wa Profesa Shivji ambaye amekuwa mwiba mchungu kwa Tume: "Baada ya kuisoma Rasimu kwa kina, mimi nadhani kwamba masharti mengi ya Rasimu na muundo wake mzima ni matokeo ya mivutano mikali katika Tume. Bahati mbaya hatuna mwenendo wa majadiliano ya Tume wala taarifa yao rasmi, hata taarifa ya awali. Lakini usomaji wangu wa awali unaniambia kwamba Rasimu hii ni maelewano kwa maana ya compromise, na sio mapatano, au mwafaka, kwa maana ya consensus. Nijieleze kidogo. Katika maelewano au compromise, pande zinazokinzana hatimaye zinakubali kwa shingo upande ili kutokwamisha maamuzi. Pande zote zinapata kidogo na kupoteza kidogo, na kila upande huwa na mkakati wake wa kupata zaidi katika duru ya pili. Kwa hivyo, maelewano kamwe hayawezi kuwa kwa moyo safi. Maelewano au compromise, yanazaa uamuzi legelege. Mapatano au consensus, kwa upande mwingine, ni maafikiano yanayofikiwa baada ya mjadala mrefu, kila mmoja akilenga kuthibitisha hoja yake na kwa njia hii kusadikisha wenzake kwamba hoja yake ni sahihi. Baada ya kufikia uamuzi wa mwafaka, kila mmoja anatoka akiwa ameridhika na amefurahi. Katika compromise, kila mmoja anatoka amenuna. Ni wazi kwamba huwezi ukapata mwafaka fastafasta. Lazima utachukua muda.” (Ukurasa wa 7-8, “Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya: Mhadhara wa Kuaga Kigoda cha [Taaluma cha] Mwalimu [Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam]” Mwaka 2013).

Hakuna ubishi hapo kwenye hilo la msongo wa muda maana uchaguzi mkuu wa 2015 umekaribia. Jaji kwa namna fulani naye kaligusia katika hotuba pale aliposema: “Tume imekamilisha kazi yake kwa muda ulipangwa kutokana na kazi nzuri ya Sekretarieti. Wakati Wajumbe wa Tume walipokuwa wanakusanya maoni mikoani, Watumishi wa Sekretarieti waliofuatana na Wajumbe, walifanya kazi kwa muda mrefu sana, hata siku za mapumziko. Walikuwa wa kwanza kuamka na wa mwisho kwenda kulala.” Hakuna kulala hadi kieleweke, ndivyo tusemavyo mtaani na kwa kiasi kikubwa hakukuwa na kulala hadi Zimwi tusilolojua lieleweke. Kabla ya hapo ilibidi lieleweke kwa wanatume.

Hao wanatume walipoeleweshwa, ama kueleweshana, ndipo yakafikiwa ‘maelewano’ haya bila hata kupiga kura: “Hiyo haina maana kwamba kila mmoja wetu ameacha imani yake, itikadi yake na msimamo wake. Kuna mambo ambayo kila mmoja wetu amebaki na imani yake na msimamo wake. Kwa mfano, kwenye suala la Muungano tupo tunaoamini muundo unaofaa ni Serikali Moja, tupo tunaoamini Muundo wa Serikali Mbili, tupo tunaoamini Serikali Tatu na tupo tunaoamini Muungano wa Mkataba. Tunachoamini wote kwa pamoja ni umuhimu wa kuendelea kuwepo na kudumu kwa Muungano. Baada ya kuwasikiliza wananchi, dira yetu imekuwa ni maslahi ya Taifa na siyo maslahi ya makundi yetu au nafsi zetu. Nawashukuru sana wajumbe wenzangu wa Tume kwa kusimamia misingi ya kiutendaji ambayo imetuwezesha kukamilisha kazi hiyo.” Hiyo Sentensi ya mwisho ya Jaji hapo inatukumbusha tena msongo wa muda kuelekea 2015.

Hatua ambayo ilibidi ifuatie kabla ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba hawajapigana vikumbo kuhusu Zimwi tulijualo dhidi ya tusilolijua ndiyo hii ya hotuba ya takribani saa nne aliyoitoa Jaji. Ni hotuba ya kuelewesha na si ya kuwasilisha rasimu. Ya kuwaelewesha nini? Kutuelewesha ‘maoni’ ambayo Jaji anayaiita “Tathmini ya Tume.”

Hatuna budi sasa kuzirejea kwa kina sehemu ambazo hayo maneno ya “Tathmini ya Tume” yanatumika kama rungu kutuelewesha kuhusu Zimwi tusilolijua: “Tathmini ya Tume ni kwamba siyo rahisi mambo haya kutekelezwa chini ya muundo wa Serikali mbili.” Je, wananchi wangapi tuliulizwa kuhusu urahisi huo? Na kitu kutokuwa rahisi ina maana hakiwezekani? Na hizo jitihada za kuyarahisisha hayo mambo, kadri muda unavyokwenda na changamoto mpya zinavyoibuka, ambazo hotuba imezianisha katika sehemu ya 147 na 148 ndio mwisho wa safari? Zimwi la Serikali Tatu ndio mwarobaini?

Hapo kwenye sehemu ya 127 ya Hotuba kuna hitimisho hili: “Kwa hiyo, tathmini ya Tume ni kwamba Muundo wa Serikali moja hauna uhalisia.” Hitimisho hilo linatokana na uchambuzi huu: “Njia pekee ambayo ingefanya maendeleo ya Zanzibar yapewe uzito sawa na mambo ya Tanzania Bara ni kuyaweka mambo yote ya Zanzibar chini ya Serikali ya Muungano, yaani kuwa na Serikali Moja. Lakini kama nilivyosema, wakati wa kukabidhi Rasimu kwa Marais wetu, Muundo wa Serikali Moja una changamoto nzito. Waasisi waliona matokeo ya Muundo huo ni Zanzibar kumezwa na Tanganyika. Tume ilipokuwa inakusanya maoni, wananchi wengi, hasa Zanzibar, walionyesha hofu hiyo ni kubwa sana hivi sasa kuliko ilivyokuwa mwanzoni.”  Wameonaje kuwa Zimwi la Serikali Moja tusilolijua halina uhalisia ila la Serikali Tatu tusilolojua ndilo lina uhalisia?

Hapana shaka Jaji ana jibu. Linapatikana kwenye sehemu ya 133: “Tume ilitafakari kama kuna uwezekano wa kuyarudisha mambo yaliyoondolewa kwenye orodha kufuatia muafaka wa 1994, lakini tathmini ya Tume ni kwamba kufanya hivyo ni kuzua mgogoro upya kwani itaonekana mamlaka (autonomy) ya Zanzibar yanaingiliwa. Wakati Tume ilipokuwa inakusanya maoni, wananchi wengi wa Zanzibar kutoka makundi yote mawili, yaani wale waliotaka Muungano wa Serikali Mbili na wale waliotaka Muungano wa Mkataba, wote walipendekeza mambo mengi yaondolewe kwenye Orodha ya Muungano. Wale waliotaka Muungano wa Mkataba walitaka mambo yote yaondolewe kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano isipokuwa suala la ulinzi. Wale waliotaka Muundo wa Serikali mbili walitaka mambo yote ya uchumi yaondolewe kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Katika hali hiyo, kuyarudisha mambo ambayo hivi sasa yako chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hata kama siyo kikatiba, kunaweza kuleta mgogoro wa kisiasa.” Kama “msingi wa Muungano”, kama sehemu ya 175 ya hotuba inavyosema, ni Hati/Makubaliano ya Muungano (Articles of Union) ya mwaka 1964 yaliyokuwa na mambo ya Muungano 11 kwa nini ishindikane kuyapunguza kikatiba baada ya kuongezwa maradufu kinyemela? Si ndicho hicho  Wazanzibari wamekuwa wakikidai?

Hatutaitendea haki Tume tusipoona utata huo kuhusu historia tete unaojidhihirisha zaidi kwenye sehemu hii ya 157 ya Hotuba: “Kwa Ta[t]hmini ya Tume, Muundo wa Serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa. Muungano wa Serikali mbili waliotuachia waasisi siyo uliopo sasa. Umebadilishwa mara nyingi, wakati mwingine bila ya kufanya mabadiliko kwenye Katiba. Waasisi walituachia Muungano wa Nchi Moja yenye Serikali Mbili, na siyo Nchi Mbili zenye Serikali Mbili. Muundo wa Serikali Mbili unaweza kubaki tu kama orodha ya mambo ya muungano haitapunguzwa bali itaongezwa. La sivyo, Serikali ya Muungano itabaki na rasilimali na mambo ya Tanzania Bara tu. Katika hali hiyo, pande zote mbili zitaendelea kulalamika. Kwa upande, mmoja Zanzibar itaendelea kulalamika kwamba Tanzania Bara imevaa koti la Muungano kwa faida yake, na kwa upande mwingine, Tanzania Bara itaendelea kulalamika kwamba mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara na rasilimali zake ndizo zimekuwa Muungano.” Hivi kweli hata wanatume waliokuwa viongozi wa juu wa  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wakati wa kuongeza mambo ya Muungano hawakumbuka nia hasa ya/za kufanya hivyo?

Haiwezekani tukachakachua historia kirahisi namna hii na kusahau (kusema) kuwa Serikali Mbili ilikuwa pia ni muundo tu wa mpito kuelekea kwenye Serikali nyingi chini ya Shirikisho laAfrika Mashariki. Hotuba ya Jaji imejikita kwenye mpito wa kuelekea kwenye Serikali Moja ambao, kwa mujibu wa “Tathmini ya Tume”, hauna uhalisia. Na kama kweli hauna uhalisia basi ina maana tumebakiwa na mwisho mmoja tu ambao Muungano wa Serikali Mbili unaulenga, yaani Umoja wa Afrika (Mashariki). Na tukisema huo nao hauna uhalisia basi hakuna mwisho mwingine zaidi ya kuvunjika kwa Muungano. Lakini hotuba ya Jaji inajaribu kutabiri, ama kutuambia inajua, hautavunjika.

Haijalishi nani amevunja Katiba, kinachohitajika ni kuchukua hatua kuilinda. Lakini hotuba ya Jaji inaendeleza utamaduni wa kulalamika kuhusu upande mmoja wa Muungano kuivunj kana kwamba Katiba mpya itakuwa na kinga ya kujaribiwa kuvunjwa. Heri angetueleza, kwa kutumia taaluma yake ya Sheria, kuhusu namna ya kukabiliana na uvunjaji huo wa Katiba aliyoapa kuilinda. Na mashabiki wa mbadala wangeenda mbali zaidi na mibadala kwa  kutuonyesha namna ambavyo Mahakama ya Katiba, ambayo tayari inaruhusiwa kuundwa kwa mujibu wa Katiba ya sasa japo hatujawahi – labda kwa sababu ya woga – kujaribu kuisimika, inaweza kutatua migogoro ya Muungano. Hata mwasisi mmojawapo alishaacha kulimung'unyia maneno hilo suala: Halafu tukizitazama takwimu alizowasilisha Jaji zinaonesha kuwa Wazanzibari wengi wanataka Muungano wa Mkataba: “Mchanganuo wa takwimu hizi unaonyesha kuwa wananchi waliotoa maoni kuhusu muundo wa Muungano kwa upande wa Tanzania Bara, 13% walipendelea Serikali Moja, 24% walipendekeza Serikali Mbili na 61% walipendekeza Serikali Tatu. Kwa upande wa Zanzibar, 34% walipendekeza Serikali mbili na 60% walipendekeza Muungano wa Mkataba, na 0.1% (watu 25) walipendekeza Serikali Moja.” Ina maana ‘Muungano wa Mkataba’ ni sawa sawa kabisa na wa Serikali Tatu? Kama si sawa kwa 100% hii haina maana tunalinganisha machungwa na matofaa?

Haishangazi tupo tunaosema waasisi hawana majibu ya matatizo ya Muungano tuliyo nayo leo. Inabidi tukabiliane na kero mpya wenyewe na ikibidi tutafute mbadala. Lakini tusiache mbachao kwa msala upitao kisa umetuambia, ama kututabiria, kuwa kuifufua Tanganyikani kuiua na kuizika Tanzania. Nchi yetu bado changa. Mtoto akililia wembe?

Halahala mti na macho. Kwa hakika hotuba hii inatukumbusha methali na misemo ya wahenga wetu walioona mbali. Ndio wao waliosema Zimwi likujualo halikuli likakwisha.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP