Sunday, March 23, 2014

Uhalali wa Hotuba na Uzito wa Hoja ya Rais

Uhalali wa Hotuba na Uzito wa Hoja ya Rais 

Ni jambo la muhimu kutenganisha haya masuala mawili. Mosi, uhalali wa hotuba ya Rais Kikwete ya kuzindua Bunge Maalum la Katiba. Pili, uzito wa hoja yake kuhusu Muundo wa Muungano.

Kuhusu uhalali, wa kisheria, kidemokrasia na kimadaraka, hakika Rais alivuka mipaka. Hilo halina ubishi. Cha ajabu ni kuwa miongoni mwa wanaolalamikia hili ni wale wale ambao toka mwanzoni kabisa  tuliwaambia msimwachie Rais akahodhi mchakato huu hasa kwenye uteuzi. Wapo waliobisha na kusema eti sisi tunaleta upinzani tu badala ya ushirikiano ili tusonge mbele kuleta mabadiliko. Bahati nzuri matamshi na maandishi yao yapo mitandaoni - kwenye facebook, twitter, blog, makundi ya google na yahoo kama Wanazuoni, Wanabidii na Wanamabadiliko - kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo vitakavyohoji tulifikaje hapa tulipo.

Rais alichokifanya ni kuutumia mwanya huo mpana waliuotoa wanamaridhiano hao, wakiwamo ambao sasa wapo kwenye kile wanachokiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kutoa hotuba yenye hoja yenye uzito (weight) utakawaolemea wajumbe hasa wale wa chama tawala ambacho yeye anakiongoza kama Mwenyekiti, yaani CCM, na ambao ni wengi zaidi japo mahesabu aliyofanyiwa Rais yanayonyesha bado kutakuwa na kazi ya kuwashawishi wapinzani wa muundo mmojawapo ili kupata theluthi mbili inayohitajika kupitisha Rasimu ya Katiba Mpya. Zaidi ya hilo aliongozana na viongozi wakuu wa zamani wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akiwamo Amani Abeid Karume, mtoto wa Mwasisi mmojawapo wa Muungano, na hata Mama Maria Nyerere, mjane wa mwasisi mwingine wa Muungano, ili kuwatumia ipasavyo kisiasa kuipa msisitizo (insistence), ukubali (legitimacy), mamlaka (authority) na nguvu (power) hoja yake kuu siku hiyo. 

Hiki ndicho kitu wachambuzi wa sayansi ya siasa wanachokiita Onyesho la Madaraka (Display of Power) na wachambuzi wa utamaduni wa siasa wanakiita Siasa za Maonyesho (Politics of Performance). Wajumbe walimpa Mwenyekiti wa Baraza Maalum la Katiba, Samwel Sitta madaraka makubwa kisheria ya kumwalika mgeni rasmi tena katika mazingira hayo na hata walipoambiwa atakuja na ugeni wote huo hawakugoma. Walidhani atatoa hotuba huru ambayo haitaegemea upande wowote. Sasa wanalalamika.

Huyu ndiye Mwenyekiti ambaye alipita kwa kishindo kwenye uchaguzi huu eti kwa kuwa alionekana ndiye angalau angalau hatakuwa na upendeleo kwa upande wowote na kuongoza kwa kasi na viwango (speed and standard). Lakini, kama tulivyoona, ndiye Mwenyekiti Sitta aliyekuwa akimwongezea maneno Rais Kikwete wakati anahutubia hilo Bunge Maalum, tena maneno ambayo yanaonesha kabisa wapi wote wameegemea - kwenye mtazamo wa chama chao na Serikali ambayo Mwenyekiti Sitta bado ni Waziri wa Baraza lake la Mawaziri chini ya Rais Kikwete. Kwa kiasi kikubwa mgongano huu wa madaraka waliufumbia macho. 

Cha ajabu hata viongozi mahiri miongoni mwa wanajumbe wanaharakati na UKAWA n waliokuwa na vigezo vya kutosha hawakugombea Uenyekiti. Wala yale madai yao ya muda mrefu ya kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri asitoke katika chama chochote cha kisiasa hawakuweza walau kutuonyesha, hata kama ni kwa mfano, yanawezekanaje walipokuwa wanamchagua Mwenyekiti wa Bunge Maalum. Wagombea wakuu walitoka vyama vya kisiasa na hatimaye Mwenyekiti na Makamu wake wote wakatoka kwenye chama tawala na tena Sitta akiwa ni yule yule aliyepitishwa bila kupingwa na chama chake kilichokwishatoa msimamo wake kuhusu Muundo wa serikali katika Muungano. Uchaguzi huo umedhihirisha kuwa kura ya turufu wanayo CCM-Zanzibar ambao CCM-Bara wakifanikiwa kukubaliana nao ni rahisi 'kura kutosha'.

Tupo tunaopinga uhalali wa Rais kutoa hotuba vile lakini hatupingi uzito wa hoja yake kuhusu Muungano. Ni hoja nzito iliyojikita katika historia na uelewa wa misingi ya Muungano ambayo hata Jaji Warioba anaifahamu fika ila, kama mwanasheria mmoja alivyohisi, inaonekana kwa ajili ya kutafuta  maridhiano (compromise) badala ya mapatano (consensus) ameamua kuyaweka kapuni, tukubali yaishe. Huyu ni Warioba aliyenukuliwa akisema haya baada ya uchambuzi wa kisheria ambao kwa kiasi kikubwa ulitokana na kijitabu chake cha Tanzania: Hatma ya Muungano:

  Sasa hivi kiini ni ugomvi wa madaraka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hivi ukileta serikali tatu, ugomvi huu hautakuwapo? Ukileta Serikali ya Tanganyika yenyewe haitadai madaraka? Mwisho wataomba madaraka hadi Serikali ya Muungano isiwe na chochote. Hivi Serikali ya Tanganyika kwa mfano ikawapo, ikataka iwe na wimbo wake wa Taifa, bendera yake, nembo yake, kisha inadai ifanye biashara ya nje, unafikiri tutakuwa tumefika wapi? Ni kwamba tutakuwa tunaondoa Muungano na kurudisha Tanganyika na Zanzibar. Lakini kama wananchi wanataka hivyo, sawa (Warioba: http://www.raiamwema.co.tz/jaji-warioba-tusidanganyane-kutaka-serikali-tatu-ni-kuvunja-muungano#sthash.XMjhRYCx.gd9YFh5E.dpuf)

Ni wananchi gani hao waliosema wanataka mpaka Warioba ikabidi sasa aseme "sawa" tu kuwa tuwe na muundo wa Muungano ambao chambuzi mbali mbali kisheria na kikatiba zake zilionyesha haufanyi kazi? Ni hoja zipi hizo ambazo zilimfanya Warioba na wanatume wenzake waseme "sawa" japo wanakiri kuwa wamebaki na hii misimamo yao ambayo hakuiwasilisha kama uchambuzi,  tathmini na ripoti mbadala ya wanatume ambao hawakukubaliana? Alichofanya ni kutuambia kuwa wanachoamini wanatume "wote pamoja ni umuhimu wa kuendelea kuwepo na kudumu kwa Muungano" lakini kuhusu namna ya kuufanya Muungano huo wa miaka 50 uendelee kweli inaonekana Warioba anakiri kuwa: 

Hiyo haina maana kwamba kila mmoja wetu ameacha imani yake, itikadi yake na msimamo wake. Kuna mambo ambayo kila mmoja wetu amebaki na imani yake na msimamo wake. Kwa mfano, kwenye suala la Muungano tupo tunaoamini muundo unaofaa ni Serikali Moja, tupo tunaoamini Muundo wa Serikali Mbili, tupo tunaoamini Serikali Tatu na tupo tunaoamini Muungano wa Mkataba (Warioba: http://www.wavuti.com/2014/03/hotuba-ya-rasimu-ya-katiba-mpya.html)

Sasa kuna wanamaridhiano wanaoona kuwa njia iliyobaki ni kusonga mbele kwa kuacha mabaya ya hotuba ya Warioba na ya Rais Kikwete, kuchukua mazuri ya hotuba hizo na kisha kuboresha rasimu ya pili ya Katiba. Tatizo la kujaribu kuuma na kupuliza, kumfurahisha huyu na yule, hata pale misingi ama nguzo muhimu ya ujenzi na ubomoaji wa wa nchi, dola  na taifa-dola (nation-state) ni kuja na miundo isiyotekelezeka na isiyozingatia kuwa unaweza kurithishwa dola na mkoloni bila kuwa hasa na taifa hivyo hitaji kujenga taifa-dola. Matatizo ya Muungano, kama chambuzi za Warioba tulizozirejea zinavyoonesha, yanatokana na kugombania madaraka. Hivyo, huwezi kutafuta njia ya katikati ya kuunda Nchi (Country) Moja, Dola (State) Moja na Serikali (Governments) Tatu.

Tukitaka kuelewa tatizo hili tuangalie historia ya mchakato wetu wa kugatua madaraka, yaani kupeleka madaraka katika ngazi za chini. Serikali Kuu imekuwa ikihodhi madaraka hayo huku Serikali za Mitaa zikiyadai miaka nenda rudi. Kinachozifanya Serikali hizi za mitaa zisiyapate madaraka haya kwa uwiano stahili ni kutokana na kutokuwa na nguvu za kiuchumi na kisiasa ukilinganisha na Serikali Kuu. Sasa unapotaka kuunda mfumo mbadala usio wa Dola Shirikisho (Federal State) ila ni wa Dola Moja (Unitary State) ambao nao una Serikali Tatu, kiuhalisia ni kuwa unaunda Serikali Moja yenye Serikali za Mitaa Mbili (Local Governments). Lakini tofauti kubwa hapa ni kuwa hizo Serikali za Mitaa sio za Mikoa, Wilaya wala Majimbo - ni za nchi mbili: Tanganyika na Zanzibar. Na si hivyo tu, hizo Serikali Mbili ndizo zenye nchi na dola ilhali hiyo Serikali Moja ni Serikali Hewa tu, isiyo na 'nchi/eneo'.

Hatari ya muundo huu unaolenga kuridhisha makundi mawili makuu katika mjadala - lile linalodai Serikali Tatu na lile linalodai Serikali Mbili - ni kuwa bado limekaa katika mfumo ule ule ambao utaoifanya Serikali ya Jamhuri ya Muungano iwe "Tegemezi na Egemezi" katika Serikali Tatu kama hotuba ya Rais ilivyosisitiza au iwe 'Kandamizi na Onevu' kama hotuba ya Warioba inavyoonekana kuelezea hali ilivyo katika Serikali Mbili za sasa. La pili litatokea kama na pale ambapo muundo huo mbadala utafanikiwa kweli kuweka mambo mengi mazito ya Muungano chini ya Serikali Kuu ya Muungano ili kuipa nguvu na kuweza kweli kupunguza nguvu za hizo Serikali za Tanganyika na Zanzibar ambazo ndizo hasa zitakazokuwa na nchi pamoja na rasilimali na watu wake. Ila kufanya hivyo ni sawa sawa na kuunda Serikali Moja ambayo itaifanya Tanganyika iwe Kaka Mkubwa aliye mbabe zaidi ya hata ilivyo sasa ambapo Zanzibar inaiona imevaa 'Koti la Muungano'.

Kinara wa muundo huu mbadala anatuambia kuwa eti tunaweza kuwa kama Afrika Kusini. Lakini Afrika Kusini baada ya kupata uhuru/demokrasia mwaka 1994 haikufanya kile ambacho sisi tulikifanya mwaka 1964. Wao wangekuwa na hali tete na tata kama yetu kama nao wangeungana na nchi ndogo ya Lesotho ambayo kijiografia ipo ndani yao au Swaziland ambayo iko mkabala nayo ama Namibia ambayo ilikuwa ikiitawala enzi za Mfumo wa Ubaguzi (Apartheid). Majimbo (Provinces) ya sasa Afrika Kusini -  Eastern Cape, Free State, Gaueteng, KwaZulu-Natal, Limpopo, Mpumalanga, Northen Cape, North-West na Western - kutokana na wingi na mengi yao kutoakisi moja kwa moja tawala zilizokuwepo kabla ya ukoloni na ubaguzi hayana utaifa (nationalism) wa pamoja wa baadhi yao dhidi ya utaifa mmoja wa Afrika Kusini kama ambavyo Zanzibar imekuwa nao na wazalendo wa Kizanzibari (Zanzibari Nationalists) wamekuwa wakiupigania kwa pamoja licha ya kuwepo pia kwa ule wa (U)Pemba dhidi ya Unguja.

Hata yale Majimbo-Nchi (Bantustan) yaliyoundwa Afrika Kusini enzi za Ubaguzi wa Rangi - Transkei, Bophuthatswana, Venda, Ciskei, KwaZulu, Lebowa na QwaQwa - hayakufanikiwa kujenga utaifa endelevu japo kwa kiasi fulani yaliundwa kwa kufuatilia jiografia ya himaya/falme/uchifu ambazo zilikuwepo kabla ya uvamizi wa Makaburu na Waingereza huko Afrika Kusini.  Ukitumia mifano hiyo Tanzania ni sawa na kulinganisha madai ya U(Zanzibar) na ya Usukuma, Uchagga, Unyamwezi, Uhehe, (U)Buhaya ambayo kwa kiasi kikubwa tuliyamaliza baada ya kufuta uchifu mara baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

Afrika Kusini inajiendesha kama Dola Moja kwa namna ambavyo tungeweza kujiendesha kama tungekubali kujivunjavunja katika majimbo makubwa (provinces) kadhaa yatakayoleta uwiano mpana wa madaraka kama ilivyo kwenye Dola Shirikishi zenye majimbo (states) nyingi, ndogo kwa kubwa, kama Marekani. Lakini hilo ni sawa na kuivunja nchi iwe katika kanda kadhaa na kama tulivyoona tayari kumeanza kuwa na siasa za ukanda Tanzania Bara zitokonazo kwa kiasi kikubwa na ushindani wa vyama vikuu vya kisiasa Tanzania Bara - CCM na CHADEMA - na kwa upande wa Zanzibar, (hasa) kabla ya mwafaka na Serikali ya Umoja,  zitokanazo na (uliokuwa) ushindani mkali kati ya CUF na CCM. 

Huku kudhani tutakuwa kama Afrika Kusini kwa kuwa na nchi mbili ambazo zitajiendesha kana kwamba sio nchi bali sehemu tu za utawala (units of governance) ni kuziambia zikubali kuwa na hadhi ndogo ya Serikali za Mitaa chini ya Mamlaka Kuu (Central Authority). Ni Kusadikika (Utopia). Jaribio la utekelezaji wake utaiweka Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mweka katika hali mbaya sana ambaye atakuwa hana nguvu kulinganisha na watendaji wakuu wa washirika wa Muungano - Kiongozi Mkuu wa Tanganyika na Zanzibar hata kama hutaiwata Marais. Na kama mwasisi mmoja wa Muungano alivyosisitiza, "huwezi kumtikisa Rais wa nchi bila kuitikisa Nchi yenyewe." Mtikiso huo utakuwa na athari kiasi gani ukiwa na nchi hewa?

Kutafuta maelewano kusitufanye tusisahau kanuni za kujenga na kubomoa nchi. Pamoja na utata wa uhalali wa hotuba ya Rais na utete wa hoja zake, kwenye hilo la Muundo wa Muungano alichokisema kina uzito. Asiyesikia la mkuu huvunjika guu.

1 comments:

Anonymous March 24, 2014 at 1:17 AM  

Chambi, uchambuzi wako ni mzuri na unalenga kuhusia ili Tanzania iendelee kuweo. Ila naomba kutofautiana nawe kwa kusema kuwa umeliangalia hili kwa 'lens' isiyoakisi ukweli halisi hapa nyumbani. Kimsingi, kinadharia uliyosema yana ukweli kama scenario yetu ni kuelekea kwenye serikali ya tatu. Lakini tuangalia na scenario nyingine pia, hasa hali halisi ambayo tayari imekwisha fanywa na partner mmoja wa Muungano-yaani Zanzibar. Hii tukiacha unafiki, na ile kawaida yetu ya kufikiria ki-Africa africa (samahani kwa kutumia mfano huu) na kuweka ukweli na uhalisia pembeni ni kuwa tunachosema sasa ni cha muda tu, kwani hicho tunachokililia tunajiandaa kukizika. Na ndipo narudi kwenye hoja yako ya kuona kuwa kama kuchepukia kwenye either serikali tatu ni 'athari' mbaya wakati ubaya uko tayari. Zanzibar wamekuwa wakidai 'sovereignty' mara kwa mara na pengine nyie wataalam wetu wa sayansi ya siasa mnakuwa kama hamlioni hili. Na kwa kuwa dunia inabadilika kwa kasi, mimi wazo langu ni kuwa kama ulivyogusia uzito au hata uhalali wa hoja (na hata number ya waliosema hili au lile) sio hoja, tuwe critical kidogo. Kwa nini tusisimame na kurudi kwa wananchi, na iandaliwe maswali mfano; unataka muungano na jibu liwe ndiyo au siyo; na ikiwa ndiyo waulizwe wapendekeze aina wanayotaka (japo hii inaweza kuwa ngumu ukichukulia uelewa wa watu wetu kwa ujumla). Hilo litatusaidia, vinginevyo tunaahirisha tatizo tu, as bara kwa uzoefu wangu na utafiti mdogo ambao nimekua naufanya watu hawana shida sana na hili suala, tatizo ng'ambo ya pili.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP