Saturday, April 19, 2014

Profesa Lipumba Amebadili Msimamo?

"Mapendekezo ya mfumo wa serikali tatu katika muungano wa nchi mbili ambapo moja ni kubwa sana kuliko nyingine na ambayo ndiyo itakayogharamia serikali ya Muungano itaathiri utaratibu mzuri wa bajeti wa kukusanya mapato kutoka vyanzo vyote na kuyagawa kwa matumizi kufuatana na vipaumbele. Vipaumbele vya Serikali ya Muungano vitakuwa mambo ya Muungano bila kujali sana vipaumbele vya mambo ya Tanganyika. Kuna tatizo la msingi la Muungano wa nchi mbili, moja ikiwa ndogo sana ukilinganisha na ya pili. Sehemu kubwa ya gharama ya Muungano inabidi ibebwe na vyanzo vya mapato ya nchi kubwa. Tume ya Jaji Warioba haikufanya uchambuzi wa kina na kubaini kuwa mfumo wa serikali ndiyo msingi wa mantiki ya kuingiza sehemu kubwa ya vyanzo vya mapato ya serikali ya Tanganyika kuwa jambo la Muungano. Msingi huu ukiondolewa, utaratibu wa kugharamia serikali ya Muungano unahitaji kufikiriwa kwa makini la sivyo serikali ya Muungano itakuwa haina vyanzo vya mapato vya uhakika. Ukizingatia mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa na Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano haina vyanzo vya mapato ya kodi kwa sababu haitasimamia sekta za uzalishaji. Rasimu ya Katiba haizungumzii taasisi yeyote ya kukusanya kodi. Kodi ni chanzo cha mapato ya serikali lakini pia ni sera ya uchumi yenye athari katika sekta za uzalishaji. Kwa kuwa serikali ya Muungano haisimamii sekta za uzalishaji hakuna mantiki na tija ya serikali hiyo kusimamia sera za kodi. Rasimu ya Katiba haiko wazi kuhusu maana ya ushuru wa bidhaa lakini inaelekea wanamaanisha excise duty na siyo kodi ya bidhaa (taxes on goods). Inaelekea Tume imekadiria gharama za mambo ya Muungano kwa hivi sasa siyo zaidi ya shilingi trilioni 1. Tukitazama bajeti ya 2011/12 kasma za baadhi ya mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa katika Rasimu ya Katiba yalitumia shilingi trilioni 1.56 wakati mapato ya excise duty ni shilingi bilioni 413.2 sawa na asilimia 26.5 ya matumizi. Ni wazi ushuru wa bidhaa kwa tafsiri ya excise duty hauwezi kugharamia serikali ya Muungano. Ni vyema mapato ya kugharamia serikali ya Muungano yakachangiwa na mapato ya serikali mbili. Katiba itamke wazi serikali za washirika zitachangia sehemu ya mapato yao yote kwenye serikali ya Muungano. Kuzuia migongano ni vyema tukafikia mwafaka wa asilimia ngapi ya  mapato ya serikali yaende kwenye shughuli za Muungano. Kwa mfano, Katiba inaweza kutamka kuwa kiasi kisichopungua asilimia 20 ya mapato yote ya Serikali za Nchi Washirika yatawasilishwa katika mfuko wa Serikali ya Muungano kwa kadri mapato hayo yanavyokusanywa. Mamlaka ya kukusanya mapato inaweza kuwa ya Muungano na ikakusanya mapato na kuyawasilisha kwa Serikali za Nchi Washirika na Serikali ya Muungano kwa uwiano uliokubaliwa. Katiba itamke kuwa Bunge la Muungano litatunga sheria ya kuweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa sehemu yake ya mapato yanayokusanywa na Serikali za Nchi Washirika yanawasilishwa kwenye mfuko wa Serikali ya Muungano. Asilimia ngapi itakidhi mahitaji ya Muungano ni suala linalohitaji utafiti na uchambuzi wa kina" - Profesa Lipumba http://www.checheafrika.org/changamoto-ya-mfumo-wa-serikali-tatu-kugharamia-serikali-ya-muungano/#comment-32

"Kwa kuhitimisha, Prof. Lipumba anasema kwamba Tume ya Jaji Warioba haikuyafikiria kwa makini masuala haya; majawabu ya juujuu hayafai. Anapendekeza, kwa uelewa wangu wa hitimisho lake, kwamba sera za uchumi, uzalishaji, fedha, na maendeleo na vyombo vya ukusanyaji kodi, viwekwe mikononi mwa serikali ya muungano, yawe mambo ya muungano; kwa hivyo, orodha ya muungano iongezeke. Tunajua sote, pamoja na Lipumba, kwamba hili haliwezi kukubalika na washirika, pamoja na Tanzania Bara. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba rasimu ya Tume ILIVYO haitekelezeki. HITIMISHO langu, kutokana na hoja za Profesa Lipumba, ni:1) Ama mambo mengi muhimu – sera za uchumi, fedha, maendeleo, uzalishaji, na vyombo vya ukusanyaji wa kodi – yawekwe katika orodha ya muungano, ambayo haitakubalika; au 2) Turudi kwenye mfumo wa serikali mbili lakini uliyobuniwa upya kutokana na hali halisi na historia yetu; au3) Tupitishe Rasimu kama ilivyo tukijua kwamba mwisho wa siku haitadumu na kuna uwezekano mkubwa wa muungano kuvunjika, tena, labda, sio kwa amani. Kwa hivyo, kwa maana na mantiki hayo, hakuna tofauti kati ya wale wanaotaka muungano wa mkataba na wale wanaoshabikia muungano wa serikali tatu ilivyopendekzwa na Tume; zote mbili ni njia kuelekea kwenye kuvunja muungano. Siamini kwamba, msomi maakini kama Prof. Lipumba, hatambui uwezekano huu, au kama, huu. Lakini, kama tunavyofahamu, KISIASA, Lipumba ni mshabiki wa rasimu ya Tume ya serikali tatu. Swali langu linalonikera: inawezekanaje, kuwa na misimamo hii miwili, ya KISOMI na ya KISIASA, ambayo yanapingana moja kwa moja, katika mtu mmoja huyohuyo?! Bila shaka, Lipumba amevaa kofia mbili, ya msomi na mwenyekiti wa CUF. Lakini, kichwa ni kilekile …" - Profesa Shivji, http://www.checheafrika.org/changamoto-ya-mfumo-wa-serikali-tatu-kugharamia-serikali-ya-muungano/#comment-32

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP