Thursday, April 24, 2014

Serikali Tatu zitaondoa Kero ya (Wana)jeshi?

Serikali Tatu zitaondoa Kero ya (Wana)jeshi?

Chambi Chachage

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ameibuka tena na kile ambacho gazeti maarufu la Mwananchi kinayaita "Maswali Saba ya Jaji Warioba." Kama ilivyokuwa siku alipolihutubia Bunge Maalum la Katiba, mwanasheria huyo nguli amezikonga nyoyo za watetezi wa mfumo wa Serikali Tatu, almaarufu kama S3. Safari hii alikuwa mzungumzaji wakati wa kutoa matokeo ya utafiti wa asasi isiyo ya kiserikali ya Twaweza inayoongozwa na mwanaharakati maarufu, Rakesh Rajani.

Kati ya yale aliyonukuliwa akiyasema Jaji Warioba, lililonifanya nitafakari sana alfajiri hii ni hili kuhusu wanajeshi:"Tatizo ambalo wametueleza ni kuchoshwa na kitendo cha kupiga mizinga 21 kwa Amiri Jeshi Mkuu wakiwa Dar es Salaam na wakiwa Zanzibar. Walisema kwa nidhamu ya jeshi, Amiri Jeshi Mkuu ni mmoja tu. Nadhani mngewaondolea kero hiyo na si mambo mengine." Huku kuchoshwa inasemekana kunatokana na ile hali ambayo aliwahi kuisemea hivi katika hotuba yake kwa Bunge Maalum la Katiba: "Waasisi walituachia Muungano wa Nchi Moja yenye Serkali Mbili, siyo nchi Mbili zenye Serikali Mbili."

Tukiirejea Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo Tume hiyo inayoitwa kimakosa kuwa ni Tume ya Warioba kutokana na utamaduni wa kuzipa tume majina ya wenyeviti wao pengine kutokana na ushawishi wao, tunakutana na suluhisho hili la hiyo kero ya wanajeshi katika Ibara ya 71(2): Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu..." Lakini Rasimu hiyo hiyo inatuambia katika Ibara ya  237(1) kuwa kutakuwa Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa ambalo litakuwa pia lina wajumbe hawa wawili: Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar. Hili ni Baraza ambalo, kwa mujibu wa Ibara ya 72(2)(a), litakuwa chini ya uwenyekiti wa Amiri Jeshi Mkuu huyo wa Nchi ambaye, kwa mantiki ya hoja ya jana ya Jaji Warioba, ndiye atakuwa na stahili ya kupigiwa mizinga 21 (katika eneo moja tu la nchi) hivyo kuondoa hiyo kero ya jeshi.

Swali la kujiuliza ni, je, kero hii itokanayo na kile ambacho tunaweza kukiita kuwa na nchi ndani ya nchi ama dola ndani ya dola kitakuwa kimeisha baada ya kuanzisha Serikali Tatu? Na hapa ndipo inabidi tujiulize kwa kina Rasimu ya Pili ya Katiba inamaanisha nini hasa inaposema "Nchi" na inaposema "Nchi Washirika" katika muktadha wa "Shirikisho". Ni wazi kabisa kuwa inaposema Nchi inamaanisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa pale inaposema "sheria za nchi" na kuiwekea msisitizo. Utata unakuja pale inapotoa ufafanuzi huu katika Ibara ya 254(1): "Katika Katiba hii, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo...."Nchi Washirika" maana yake ni Tanganyika na Zanzibar..."

Hapa tunaona mtanziko wa dhahiri kati ya jitihada za Rasimu kuunda/kusimika nchi moja - ya Tanzania - yenye "sheria za nchi" na hofu ya kuvunja/kuondoa nchi zingine mbili - za Tanganyika na Zanzibar - zitakazokuwa/zenye sheria za nchi husika kama 'zitakavyoruhusiwa/zilivyoruhusiwa' na Ibara za 64, 65, 66, 67 na 68. Ni jaribio tete na tata la kuridhisha kila upande/eneo.

Ni dhahiri kuwa, bila mabadiliko makubwa katika Katiba ya Zanzibar na bila ya itakayokuwa Katiba ya Tanganyika kuacha kutosimika Utaifa wa Kitanganyika, mtanziko huu wa Rasimu ya Pili ya Katiba utapelekea kuwa na nchi tatu badala ya nchi moja. Na si nchi tatu tu, bali pia wananchi wa nchi tatu. Sote tayari tunajua kumekuwa/kuna wananchi wa Zanzibar. Utangulizi wa Katiba ya Zanzibar ya 1984 toleo la 2010 unasema hivi: "NA KWA KUWA wananchi wa Zanzibar tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani." Itakuwa ni maajabu kuwa na Katiba ya (Serikali ya) Tanganyika isiyo na/ya (wana)nchi wa Tanganyika.

Maajabu hayo ndiyo ambayo mtetezi mkuu wa Serikali Tatu zilizoboreshwa (S3z), Zitto Zuberi Kabwe anataka kuyafanya. Nia yake inayoonekana kuwa njema na ya dhati kabisa ni kurasimisha nia ya Rasimu ya Pili ya Katiba ya kuwa na Nchi Moja na kufifisha kama sio kuua kabisa mtanziko wa kuwa na nchi zingine mbili za ziada ambazo zitazalishwa na S3 ambazo hazijaboreshwa. Lakini swali zito sana ambalo bado halijajibiwa na mtetezi huyo ni: Je, unaweza(je) kuwa na Serikali (kwa mantiki ya Serikali Kuu na sio Serikali za Mitaa) ya eneo (ambalo kihalisia ni nchi wala sio mtaa, kijiji, wilaya, mkoa au jimbo) bila kuwa na nchi na wananchi ambao wanahudumiwa na Serikali hiyo? Kwa lugha rahisi zaidi: Je, unaweza(je) kuwa na Serikali ya Tanganyika bila kuwa na nchi ya Tanganyika na wananchi wa Tanganyika, yaani Watanganyika?

Ukishindwa kutokuwa na Watanganyika na Wazanzibari utaweza kuwa na Watanzania? Mtanziko wa kuwa Mtanganyika na papo hapo kuwa Mtanzania tunauweza? Wataalamu wa masuala ya wasifu wanasema sisi sote tuna wasifu zaidi ya mmoja, kwa mfano mtu anaweza akawa Mpare na bado akawa Mtanganyika na vile vile akawa Mtanzania. Lakini hapa (U)Pare sio nchi, serikali, taifa, dola wala taifa-dola, tulishauvunja 'udola' wake labda umebaki 'ukabila' tu. Lakini (U)Tanzania ni nchi, ni serikali, ni taifa, ni dola na dola-taifa. Je, tutaweza kuidumisha kwa kuunda/kurejesha tena (U)Tanganyika ambayo haitataka kuwa vyote hivyo - nchi, serikali, taifa, dola, dola-taifa na hivyo kuinyonga Tanzania maskini?

Hayo yote yakitokea Tanganyika haitataka kuwa na jeshi lake kweli? Itaridhika tu na hiki ambacho Rasimu ya Pili ya Katiba inakisema katika Ibara ya 250: "Bila ya kuathiri masharti ya Sura hii, Wakuu wa Nchi Washirika wanaweza kumuagiza kiongozi yeyote wa Jeshi la Polisi au Idara ya Usalama wa Taifa kuchukua hatua yoyote ambayo ni muhimu kwa ajili ya kulinda au kuimarisha usalama wa eneo lolote la Nchi Mshirika husika"?  Wataridhika hasa ukizingatia huyo Mkuu wa 'Nchi Mshirika' wa Tanganyika ndiye atakuwa na watu/wananchi wengi zaidi na  hivyo kuwa na wanajeshi wengi zaidi kwenye Jeshi la Wananchi wa Tanzania labda itokee maajabu mengine ya kuwa na jeshi dogo?

Wanajeshi wataridhika? Wananchi je? Wa wapi? Tanganyika? 

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP