Wednesday, April 16, 2014

Shivji na Sura Mbili za Usaliti wa Kitaaluma

Je, Profesa Shivji ana Sura Mbili za Usaliti wa Kitaaluma?


Ndugu Mhariri

Naandika makala haya kwa sababu moja tu nayo ni kubainisha UONGO ulioandikwa kwenye gazeti la Raia Tanzania (gazeti dada na hili) na mwandishi wa makala aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Mihangwa. Mihangwa ameandika makala mbili katika gazeti hilo kwa nyakati tofauti na yote yamebeba ujumbe wa uongo na matusi mazito juu ya kile anachodai kuwa ni ‘sura mbili za usaliti wa kitaaluma wa Profesa Shivji kuhusu Muungano’. Aidha, uongo na matusi hayo mazito vimerudiwarudiwa (neno kwa neno) na Mihangwa katika makala yake ya tarehe 5 Aprili 2014 (ukurasa wa 10) na tarehe 10 Aprili 2014 (ukurasa wa 12-13). Katika makala hayo, Mihangwa anahitimisha kwa kusema kwamba  Shivji amesaliti taaluma yake na kwa hivyo ni  "mamluki wa kujitakia". Hali hii imenishangaza na kunisononesha. Sitajikita kwenye matusi kwa sababu msingi wa mijadala yenye manufaa ni hoja na siyo matusi.

Mihangwa ametumia mtindo wa uandishi unaofanana kwa kunukuu maneno kutoka kwenye kitabu cha Shivji (2008) kiitwacho “Pan-Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika-Zanzibar”. Amenukuu sehemu ya aya mojawapo iliyomo katika kitabu hicho cha Shivji  ( angalia ukurasa wa 209 ) na kutumia nukuu hiyo kuandika uongo.

 Nukuu iliyotumiwa na Mihangwa ni hii: “Firstly, the Articles of Union, which is the constituent document of the Union, provided for three governments and that the political association envisaged was a federation…The Articles did not dissolve Tanganyika nor abrogate the constitution of Tanganyika. It was Act (No. 22 of 1964) of the Tanganyika Parliament ratifying the Articles which abrogated the constitution of Tanganyika. This was contrary to the Articles”.
Mihangwa mwenyewe ameitafsiri nukuu hiyo  kwa kiswahili kama ifuatavyo: ‘…mkataba wa Muungano ambao ni sehemu ya Hati ya Kikatiba ya Muungano inasimika serikali tatu za Muungano, na kwamba Muungano wa kisiasa uliokusudiwa ni wa Shirikisho. Mkataba wa Muungano haukufuta au kuuwa Tanganyika wala kutangua au kubatilisha Katiba ya Tanganyika. Ni sheria ya Bunge la Tanganyika lililoketi kuridhia Mkataba huo ndilo lililotangua na kubatilisha Katiba ya Tanganyika kinyume cha Mkataba wa Muungano”.

Baada ya kusoma kwa makini sehemu yenye nukuu hiyo (ukurasa wa 209), nimebaini kwamba maneno yaliyomo kwenye nukuu hiyo siyo ya Shivji mwenyewe kama Ndugu Mihangwa anavyodai katika makala yake bali ni sehemu ya muhtasari wa uchambuzi wa Shivji wa hoja kuu za waraka unaodaiwa kuandaliwa na wanasheria wa Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar, kwa ajili ya kupelekwa katika Mahakama ya Katiba. Waraka huo, kwa mujibu wa Shivji, ndilo chimbuko la mashtaka dhidi ya Mzee Jumbe mbele ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Profesa Shivji ameutumia waraka huo katika kitabu chake kwenye sehemu anayochambua zahma ya kisiasa katika kipindi cha ‘kuchafuka’ kwa hali ya siasa Zanzibar (1983-1984). 

Muhtasari wa Shivji kuhusu hoja kuu za waraka huo unaanzia ukurasa wa 208 hadi 213 na kichwa cha habari cha sehemu hiyo ni ‘Zanzibar’s case for three governments’. Tena hata kabla ya kuwasilisha muhtasari wa hoja kuu za waraka huo, Shivji anaanza kwa kusema (angalia ukurasa wa 209): ‘Although the document is over 100 printed pages, the thrust of the position taken by the authors, which was in effect Jumbe’s position, may be summarized in two major points’.  Anachosema hapa Shivji ni kwamba: ‘ Kwa kuwa waraka una zaidi ya kurasa 100, msisitizo katika msimamo wa waandishi  wa waraka huo, ambao ndiyo msimamo wa Jumbe, unaweza kugawanywa  katika hoja kuu mbili’. Shivji anaendelea kuzijadili hoja hizo mbili. Uchambuzi huo unaanzia ukurasa wa 209 hadi 213. Maneno yaliyonukuliwa na Mihangwa ndiyo hoja kuu ya kwanza ya waraka huo unaochambuliwa na Shivji. Hoja mbili za waraka uliochambuliwa na Shivji katika kitabu chake zinaakisi msimamo wa Jumbe kuhusu hati za Muungano na muundo wa Muungano. Huo siyo msimamo wa Shivji.

Iweje sasa Mihangwa augeuze msimamo wa Mzee Jumbe na wanasheria wake kuwa ndiyo MSIMAMO wa Shivji. Alichokifanya Mihangwa ni kunukuu sehemu ndogo ya kitabu cha Shivji inayojadili msimamo wa Mzee Jumbe na kudai kuwa huo ndiyo msimamo wa Shivji. Na kwa kutumia UONGO huo, aliousuka kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe, Mihangwa anamtusi Shivji kwa kumuita msaliti wa kitaaluma. Wasomaji wa Raia Tanzania amueni: kati ya Shivji na Mihangwa, nani msaliti wa kitaaluma?

Makala haya yameandikwa na Bashiru Ally na kuchapishwa katika gazeti la Raia Mwema toleo  Na. 347 la Jumatano April 16 hadi Aprili 22,2014

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP