Saturday, May 10, 2014

Mapambano Dhidi ya Kutawaliwa Akili

DEREVA WANGU WA TEKSI[1], RICHARD WAGNER NA MAPAMBANO DHIDI YA  KUTAWALIWA AKILI[2]

Ngugi wa Thiong’o

Heshima mliyonipa leo imefungamana na kipindi muhimu katika maisha yangu. Mwaka elfu moja  mia tisa na themanini  na nne nilialikwa na Chuo Kikuu cha Auckland, New Zealand, kutoa mihadhara mine kuhusu Siasa za Lugha Katika Fasihi ya Afrika. Wakati huo nilikuwa nikiishi London, baada ya kulazimika kuishi nje ya nchi yangu kutokana na udikteta wa serikali ya Kenya. Pamoja na Wakenya wenzangu,  ambao nao walikuwa wakiishi uhamishoni, na pia watu wa mataifa mingine waliokuwa  wanatuunga mkono, nilikuwa nimeshughulika na siasa za harakati za kupinga ukandamizaji nchini Kenya.

Tulikuwa tukifanya kazi mchana na usiku ili kuwaelimisha na kuwahamasisha watu wa mataifa mengine duniani kuhusu yaliyokuwa yakitendeka Kenya –  nchi ambayo nchi  za Magharibi  zilikuwa zikiisifu kuwa ni mfano  mzuri wa demokrasia na utulivu katika bara la Afrika.

Kwa hivyo, ingawa nilikuwa nimeukubali mwaliko huo wa Auckland, miezi mitatu kabla ya kusafiri kwenda New Zealand, sikuwa nimeanza hata kuwa na fikira yoyote kuhusu mihadhara hiyo, na sikuwa nimeandika hata mstari mmoja! Sikuwa nimepata wakati wala makini ya kulifanya hilo. Nikaanza kubabaika: Nikazungumze nini? Nianzie wapi?

Miezi miwili niliyokuwa katika Chuo Kikuu hiki ndiyo iliyoniokoa! Nilikuwa nimealikwa hapa kuwa Profesa kwa muda mfupi. Mambo mchanganyiko yaliifanya ziara yangu hiyo hapa Bayreuth kuwa ni mahali muwafaka pa kupatia ilhamu. Kwani hapa kulikuwa na kazi iliyokuwa ikifanywa  kuhusu lugha za Afrika, na fasihi iliyotokana na lugha hizo: 

Kulikuwa na “Iwalewa-Haus”, iliyokuwa ikiongozwa na Ulli Beier – mtu aliyefanya kazi muhimu kuhusu Fasihi ya Afrika iliyoandikwa kwa lugha za Ulaya. Ulli Beier alikuwa ni mmojawapo wa waasisi wa vituo vya waandishi vya Mbari huko Nigeria; na pia mhariri wa jarida lililoitwa Black Orpheus.  Jarida hilo na vituo hivyo vilikuwa ni miongoni mwa asasi zilizotangulia kuchapisha maandishi  ya waandishi wa Afrika yaliyoandikwa kwa lugha za Ulaya,  katika miaka  ya Sitini ya karne iliyopita. Na asasi hizo mbili zilichangia katika kufanikiwa kwa Kongamano la Waandishi wa Kiafrika Wanaoandika kwa Kiingereza, lililofanyika Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala,  mwaka elfu moja mia tisa na sitini na mbili.    

Lakini jambo muhimu zaidi lililonitokelea hapa Bayreuth ni lile la kuwa karibu na Jumba la Masrahi laTamasha la Bayreuth - jumba alilolijenga Richard Wagner. Msije mkanielewa visivyo! Chuo Kikuu cha Bayreuth hakikunipa tiketi ya kwenda kwenye tamasha la kila mwaka katika jumba la opera. Bali niliambiwa kwamba mtu ilimbidi kununua tiketi miaka kumi kabla, au awe ameirithi kutoka kwa bibi au babu yake.

Lakini, kwa nini Wagner? Kuna nyakati chache katika maisha yangu ya uandishi ambapo ilinibidi kupata ilhamu kutokana na muziki wa kutoka Ujerumani. Baina ya mwaka elfu moja mia tisa na sitini na tano, na mwaka elfu moja mia tisa na sitini na saba, nilipokuwa Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza -  ambako ndiko  nilikoiandika riwaya yangu, A Grain of Wheat -  nilipokuwa nimekwama katika uandishi, nilikuwa nikijikwamua kwa kusikiliza sehemu ya mwanzo ya “Fifth Symphony “ ya Beethoven.

Safari moja nilimwelezea habari hii dereva wangu wa teksi huko Marekani, anayeitwa Danny Durant. Hapo hapo, nikagundua kwamba kumbe alikuwa ni mpigaji mahiri wa fidla (au vailini), na pia nikafahamu kwamba alikuwa akielewa mambo mengi kuhusu historia ya muziki. Basi tangu wakati huo, anapokuwa ananiendesha kutoka Irvine,  ambako ndiko ninakosomesha, na kunipeleka  Los Angeles, ambako ndiko ninakopandia ndege ninaposafiri, mazungumzo ya Danny Durant huwa ni kuhusu muziki kwa jumla  - lakini hasa kuhusu ubingwa wa muziki kutoka Ujerumani, na muziki wa Bach. Kwa sababu ya mapenzi yake ya muziki, Danny pia anajua habari nyingi mno kuhusu maisha ya kimuziki ya Leipzig, ingawa hajapatapo kufika huko.

Miaka mitatu iliyopita - tarehe kama ya leo – mimi niliuzuru mji wa Leipzig. Lakini si kwa sababu ya kwamba Richard Wagner alizaliwa katika mji huo, au kwamba alikuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Leipzig, bali ni kwa sababu ya Abdilatif Abdalla, mmojawapo wa washairi maarufu wa Kiswahili duniani.
Abdilatif, ambaye kwa miaka  kumi na tano alisomesha Lugha ya Kiswahili na Fasihi katika Chuo Kikuu cha Leipzig, alikuwa anastaafu. Na Chuo Kikuu hicho kiliandaa kongamano la kimataifa la siku mbili kwa heshima yake. Nilipokuwa huko Leipzig nikasikia kwamba kila Jumamosi huwa kuna aina ya tamasha kwenye Kanisa la Mtakatifu Thomas, ambako, karne kadhaa zilizopita, Johann Sebastian Bach alikuwa akiongoza kwaya. Nikayakumbuka mazungumzo ya Danny Durant kuhusu Sebastian Bach. Lakini Jumamosi hiyo walikuwa wanapiga muziki wa Vivaldi. Hata hivyo, nikasema , “Haidhuru!”  Kwa vile Danny Durant alinielezea kuhusu Kanisa hili, nikajiambia ni lazima nilizuru.

Pamoja na Abdilatif;  na kaka yake, Sheikh Abdilahi Nassir; na rafiki yetu, mchapishaji vitabu, Walter Bgoya; na Khamis Ramadhan, aliyekuwa akipiga filamu, tukaelekea Kanisani. Tulipofika, Kanisa lilikuwa limeshajaa tele, na sehemu yote ya mbele ilikuwa imeshakaliwa!

Kaka yake Abdilatif ni miongoni mwa mashekhe na viongozi maarufu wa Waislamu nchini Kenya. Alikuwa amevaa mavazi ya Kiislamu – kanzu na kofia. Tulipoingia kanisani na kutembea masafa marefu hadi sehemu ya nyuma kabisa ya Kanisa ili kutafuta nafasi ya kukaa, nilikihisi kihangaiko na wasiwasi uliokuwa umewatanda wale waliokuwa wakitutazama tulipokuwa tunaingia. Hatimaye, tukapata nafasi karibu na sehemu alipozikwa Bach.  Kidogo nilijihisi sikuwa na utulivu moyoni mwangu nilipoona kwamba kiu yangu kuhusu Bach ilisababisha fazaa na wasiwasi kanisani. Shughuli yenyewe ilipomalizika kwa salama, nilifarijika! Tukatoka nje, na kupiga picha karibu na sanamu la Johann Sebastian Bach.

Sikuuhisi msisimko kama huo kuhusu Wagner nilipokuwa hapa Bayreuth mwaka elfu moja mia tisa na themanini na nne. Lakini miaka miwili kabla, nilipokuwa bado niko Kenya, nilitaka kutumia Ride of the Valkyries, ambayo ni sehemu ya opera ya Wagner, The Ring Cycle, katika tamthilia yangu ya pili niliyoiandika kwa Kikikuyu, Maitu Njugira; yaani “Mama, Niimbie”.
Hebu fikiria: Wagner akishindana na ngoma za kiafrika, katika tamthilia ya lugha ya kiafrika, inayoigizwa na wanakijiji  nchini Kenya. Lakini, hilo halikufanyika. Kwani serikali iliizuia tamthilia hiyo kuigizwa katika mwaka elfu moja mia tisa na themanini na mbili – mwaka ambao nililazimika kuishi uhamishoni.

Kwa hivyo, mkusanyiko wa mambo haya matatu - mwaka elfu moja mia tisa na themanini na nne, Bayreuth, na Wagner – yalinikumbusha yaliyonikumba Kenya miaka michache kabla, kwa sababu ya harakati zangu na mapambano kuhusu Lugha – ambayo ndiyo iliyokuwa mada ya mihadhara yangu huko Auckland, New Zealand.

Wagner akawa ni kiungo baina ya Limuru, mahali nilikozaliwa; London, nilikokuwa uhamishoni; na New Zealand, nilikokuwa ninakwenda. Kwa hali yoyote ile iwayo, ukweli ni kwamba ni wakati nilipokuwa hapa kwenye kijiji cha St. Johannis, Mei 15, mwaka elfu moja mia tisa na themanini na nne, ndipo nilipouandika mhadhara wa kwanza, ambao baadaye ulikuwa ni sehemu ya kitabu changu maarufu cha nadharia, Decolonising the Mind.     

Katika kitabu hicho nilijishughulisha zaidi na uhusiano baina ya mkoloni na aliyetawaliwa na mkoloni – uhusiano ambao matokeo yake yalikuwa ni lugha za Ulaya kuyatawala maisha ya bara la Afrika kiuchumi, kisiasa na kitamaduni. Wakati wa mapambano dhidi ya ukoloni, Waafrika wa tabaka la kati walizitumia lugha za Ulaya kuwa ni mbinu za kuzipa uwezo lugha za Afrika katika mapambano hayo. Lakini baada ya uhuru kupatikana, tabaka hilo likafanya kinyume na hivyo: likazitumia lugha za Afrika kuzipa uwezo lugha za Ulaya.

Wakati wa mapambano dhidi ya ukoloni, Waafrika waliokuwa na elimu walikuwa ni wasasi katika msitu wa lugha za kigeni. Baada ya uhuru,  wasomi hao wakawa ni mateka na mahabusu katika gereza la lugha za Ulaya. Tunalofanya sisi wasomi wa tabaka hilo ni kuikusanya elimu na maarifa yetu na kuyafungia katika majumba ya makumbusho na makavazi ya lugha za Ulaya. Hii imekuwa ndiyo hali ya kisomi ndani na nje ya Afrika.

Katika makongamano ya taaluma za Afrika, nimepata mara kadha wa kadha kuuliza swali hili: Ni wasomi wangapi kati ya waliohudhuria, ambao wamepata kuandika angalau maandishi mamoja kwa lugha yoyote ya Afrika? Huwa hakuna hata mtu mmoja anayeinua mkono! Maana yake ni kwamba maarifa na ujuzi wetu kuhusu Afrika  huwa yanapitia kwenye kichujio cha lugha za Ulaya na misamiati yake.

Labda hoja yangu hii itaeleweka vizuri zaidi tukiliuliza swali hili kivingine: Unaweza kumpata Profesa wa Historia ya Italia, au Utamaduni wa Italia, ambaye hajui hata neno moja la Kitaliani? Au kumpata Profesa wa Utamaduni wa Ujerumani na Historia, ambaye hafahamu Kijerumani?

Mamlaka za kikoloni, kama zilivyokuwa hapo zamani, huenda zikawa haziko tena barani Afrika; lakini Ulaya inaendelea kuyatamalaki mabongo. Matokeo yake yamekuwa ni kuzikumbatia kwa nguvu kabisa lugha za Ulaya, na kuzikana lugha za Afrika: Kuukumbatia  ugeni, na kuukimbia uzawa wetu. Hii ndiyo hali ya bara la  Afrika hivi leo.

Kwa hakika, tatizo hili si tatizo la Afrika pekee  bali ni tatizo linalotokea  kila mahali palipokuwa na utawala wa kikoloni;  na pia ni tatizo la walionyimwa uwezo na nafasi katika jamii. Msingi wake umechimbwa kutokana na dhana ya kwamba lugha zinaweza kuhusiana kwa mujibu wa viwango vyake tu. Yaani twaweza kusema kuwa ni mfumo wa kilugha wa ki-Darwin , ambapo mwenye nguvu humvamia mnyonge ili apate kuendelea kuishi.

Fikira ya kwamba lugha yangu na utamaduni wangu ni bora kuliko wako, inaonyesha kama kwamba ndiyo hali iliyoko duniani, licha ya kwamba kuna huo unaoitwa utandawazi. Sina haja ya kuzungumza kwa urefu kuhusu historia ya maumivu na uchungu – kwa mfano, mauaji, au mauaji ya halaiki – ambayo yanaweza kutokea iwapo tutazitazama lugha na tamaduni kwa mtazamo huu. Hata hivyo, mahusiano baina ya watu, vikundi vya jamii, na rangi za watu, au maeneo mbalimbali ya dunia, yanaendelea kutazamwa kwa mujibu wa vyeo na daraja. Baadhi ya watu wanaamini kama kwamba lugha zao ni lugha takatifu, yaani ni lugha anazozungumza Mungu. Lakini, kwani ni lazima lugha ziwe na uhusiano unaotegemea viwango na daraja zao?

Lugha na tamaduni zinafaa zihusiane kimtandao. Mtandao unategemea mfumo wa  “Nipe, nikupe”. Sawa na mfumo wa daraja. Daraja linalotumika huwa ni la kuwavusha wa huku na kule; si la kuwavusha watu wa upande mmoja tu. Likitumiwa hivyo, halitakuwa daraja tena.

Kwa hivyo, tuendelee kujenga madaraja baina ya lugha na tamaduni mbalimbali, bila ya kujali ukubwa au udogo wao. Na hili linahitaji kuziendeleza harakati dhidi ya wanaotamalaki mabongo ya wengine. Nimepata bahati ya kuwa na mimi nimo katika harakati hizi. Na harakati hizi zinaniunganisha na juhudi za mamilioni ya watu wengine duniani wanaopigania haki za lugha, kwa msingi wa kwamba kila lugha na kila utamaduni una uwezo wa kutoa na kupokea. Mshairi wa Kiingereza, John Donne, alitunga akasema:

No man is an island,
Entire of itself,
Every man is a piece of the continent,
A very part of the main…
Any man’s death diminishes me,
Because I am involved in mankind,
And therefore never send to know for whom the bell tolls;
It tolls for thee

Twaweza kusema maneno kama hayo kuhusu lugha na tamaduni mbalimbali: Kwamba hakuna lugha au utamaduni ambao ni  kama kisiwa; zinategemeana. Kuzifanya lugha chache zikatawala na kuzidunisha lugha nyingine duniani ni kama kuichukua okestra ya Wagner ukaipunguza ala, na kuzibakisha ala chache tu za aina moja, na zenye sauti zinazofanana. Kifo cha utamaduni na lugha yoyote kinaidunisha okestra ya binadamu wote duniani.

Ikiwa heshima hii ninayopewa leo na Chuo Kikuu hiki kitukufu itasaidia kuikumbusha dunia kwamba mapambano ya kupigania lugha yanaendelea, basi naipokea kwa shukurani nyingi. Kwani uhai wa kila lugha na utamaduni duniani unaitajirisha okestra hiyo ya binadamu.

Ahsanteni sana.  


[1] Jina lake ni Danny Durant.
[2] Hotuba ya kupokea Digrii ya Heshima ya Uzamifu, Chuo Kikuu cha Bayreuth, Ujerumani, tarehe 5 Mei, 2014, iliyotolewa kwa Kiswahili. Imefasiriwa na Abdilatif Abdalla kutoka Kiingereza.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP