Thursday, June 26, 2014

Kupasuka kwa Vyama na Hatma ya Demokrasia

Tanzania na Afrika Kusini ni nchi zenye mambo mengi yanayofanana. Nyimbo zetu za taifa hazina tofauti sana. Hali kadhalika bendera zetu. Na hata baadhi ya lugha zetu.

Vyama tawala vya nchi hizi mbili navyo vinaendelea kushika hatamu licha ya kukua kwa vyama vya upinzani toka miaka ya 1990. Hata historia ya mipasuko ya vyama nayo inafanana kiasi.

Baada ya tofauti za kimtazamo na kimbinu katika miaka ya mwanzo ya 1960, mwanasiasa machachari Zuberi Mtemvu na baadhi ya wanachama wenzake wa Tanganyika African National Union (TANU) waliunda chama cha African National Congress (ANC).  Chama chenye jina kama hilo huko Afrika Kusini, yaani ANC, nacho kilikumbwa na tofauti katika miaka ya mwisho ya 1950 na kupelekea kuundwa kwa chama cha Pan Africanist Congress (PAC) chini ya mwanasiasa mahiri, Robert Sobukwe. 

Migawanyiko, ama mipasuko, ya vyama vya kisiasa inaweza kuwa chachu ya kukuza demokrasia au ya kudidimiza harakati za ukombozi. Ni vigumu kujua ni kwa kiasi gani ANC ya kina Mtemvu ingetusaidia kwa lipi maana baada ya kumpa Mwalimu Julius Nyerere na TANU changamoto kwenye uchaguzi mkuu wa 1962 haikupata tena fursa hiyo mwaka 1965 kutokana na kuanzishwa kwa mfumo wa chama kimoja eti ili kudumisha umoja. 

Wenzetu wa Afrika Kusini wao wanajua kwa kiasi gani PAC iliwasaidia ama kutowasaidia katika harakati zao. Wapo wanaoona kuwa ilidhoofisha na kuchelewesha kupatikana kwa demokrasia kwa kuwa nchi za Afrika ziligawanyika kuhusu nani wa kumsaidia - ANC au PAC? Utata huu umegusiwa katika wasifu wa Nelson Mandela wa Long Walk to Freedom anapoelezea alivyogundua jinsi gani PAC ina mvuto Afrika na ambavyo imekuwa ikiifanyia majungu ANC alipozuru nchi yetu na nchi zingine na hivyo kuifanya kazi yake ya kutafuta ushirikiano wetu kuwa ngumu.

 Lakini ndio hao hao PAC waliosimamia, japo wengine wanadai kudakia, harakati za kupinga kulazimishwa kutembea na pasi za kibaguzi. Japo baadhi ya wanaharakati hao waliuliwa katika mauaji yanayojulikana kama Sharpville Massacre mwaka 1960, harakati zao zilikuwa chachu kubwa katika kuleta demokrasia nchini kwao.

Historia ya wenzetu kwa kiasi fulani sasa inajirudia. Mwaka 2008, kabla ya uchaguzi mkuu uliopita, wanasiasa kadhaa wa chama cha ANC walianzisha kwa makeke chama chao na kukibatiza jina la lililokuwa vuguvugu muhimu katika historia ya demokrasia ya nchi hiyo kutokana na kupitishwa kwa kwa Freedom Charter (Azimio la Uhuru) huko Kliptown mwaka 1955, yaani Congress of the People (COPE). Wapo waliotegemea kitakipa chama tawala changamoto kubwa na kukifanya kisiweze kuhodhi maamuzi ya kibunge n.k. Lakini migongano ya kiwasifu pamoja na kugombania madaraka kati ya vinara wake wakuu wawili kati ya watatu, Mbhazima Shilowa na Mosiuoa Lekota, ilichangia kukidhoofisha chama hicho.

Kuibuka kwa chama kingine cha Economic Freedom Fighters (EFF) kilichoundwa na vijana matata waliojikuta hawana jinsi ila kutoka ANC nako kumechangia kufifia kwa COPE. Chama hicho kipya kinachoongozwa na mwanasiasa maarufu, Julius Malema, hakina hata zaidi ya mwaka 1 ila kimeweza kujizolea kura zipatazo milioni 1 katika uchaguzi mkuu wa 2014. Kwa lugha ya mtaani ya vijana, kinakipumulia kooni chama kikuu cha upinzani nchini humo, Democratic Alliance (DA) kinachoongozwa na mwanasiasa  mwerevu, Helen Zille, na huenda muda wowote kikawa chama kikuu cha upinzani na hata kuchukua dola kwenye chaguzi zijazo.

Chama hicho ambacho maana ya jina lake ni 'Wapigania Uhuru wa Kiuchumi' kimevuta hisia za vijana wengi wa hali ya chini na hata ya kati. Pamoja na kiongozi wake mkuu kuonekana ni mkaidi na mkwasi, anaendelea kujizolea wafuasi wakiwamo wasomi. Profesa mmoja katika chuo kikuu maarufu huko Johannseburgh aliwahi kusikika akisema kuwa ni jambo la kushangaza, na linalostahili kuchunguzwa, kuwa wanafunzi wake wengi makini wa shahada ya uzamivu ni wanachama wa chama hicho cha 'mtata' Malema.

Ni nini kinawavuta Dali Mpofu, mwanasheria msomi, na wenzake kujiunga na chama kinachozungumza lugha ya kijamaa/kisoshalisti japo inaonekana ni dhahiri kuwa kiongozi wake mkuu ana ukwasi wa kibepari/kifisadi? Ni nafasi rahisi ya kukuza demokrasia? Je, ni fursa ya kupata sifa na madaraka makubwa ya haraka haraka?

Au ni mvuto tu wa mwanasiasa mwenye uwezo mkubwa wa kuongea na wananchi wa kawaida na ushawishi mkubwa kwa umma? Kama ni mvuto huo wa halaiki ambao wataalamu wa sayansi ya siasa wanauita upopulisti, je, una nafasi gani katika kukuza demokrasia ndani ya chama hicho na nchi yao kwa ujumla?

Hapa kwetu Tanzania tuna nini cha kujifunza kutokana na migawanyiko/mipasuko ya vyama vya kisiasa huko Afrika Kusini? Katika makala ya Kutoka 1995 Kuelekea 2015 tulirejea kidogo historia ya mtafaruku wa NCCR uliopelekea kufunguliwa kwa kesi katika mahakama kuu ili kutatua ugomvi wa madaraka katika ya kundi la Augustine Mrema na kundi la Mabere Marando. Ni vyema tukaichambua kwa kina historia hii na ya mitandao ya CCM katika muktadha wa leo ili tujielewe badala ya kuwa bendera fuata upepo.

Kwa wale wanaoamini kuwa Mwalimu Nyerere alitabiri kuwa upinzani thabiti utatoka CCM basi pengine huu ndio wakati mwafaka wa kuhakikisha chama tawala kinapasuka katikati na ikiwezekana mpasuko huo uzae CCM-Safi na CCM-Fisadi. 

Na kwa wale wanaomini kuwa vyama vya upinzani ndio mwokozi wa demokrasia basi labda wakati ndio huu wa kuleta mipasuko mikubwa katika vyama vinavyoakisi ukiritimba/urasimu wa chama tawala ili kuzalisha vyama vyenye demokrasia na uwazi zaidi.

Lakini wale wanaomini kuwa demokrasia ya kweli haitokani na siasa za vyama bali mavuguvugu ya wananchi wakati ndio huu wa kutafakari na kuchukua hatua kuhusu hatma ya demokrasia yetu.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP