Wednesday, August 20, 2014

Taifa Stars Nayo Inahitaji Kocha Kijana?

Taifa Stars Nayo Inahitaji Kocha Kijana?

Kwa mara nyingine tena timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeshindwa kufuzu kusonga mbele katika mashindano ya kimataifa ya kandanda. Imetolewa na timu ya Taifa ya Msumbiji, Black Mambas. Visingizio vinaendelea kutolewa kuhusu kipigo hicho.

Licha ya kuishirikisha ‘kamati ya ufundi’, timu yetu imebwagwa. Pamoja na kuwepo kwa posho za kutosha kuulipa msafara wa viongozi wa michezo walioongozana na timu yetu, ‘tumepigwa bao’. Japo tuna kocha mwenye uzoefu wa siku nyingi, tumeambulia kichapo.

Pengine sasa ni wakati mwafaka wa kuwa na kocha kijana wa kuwanoa vijana wenzake. Labda wataelewana zaidi. Si vijana ndio wana mawazo na maono mapya? Kama asilimia kubwa ya wachezaji ni vijana kwa nini kocha awe mzee ilhali vijana wapo wamejaa tele?

Hata huko kwenye ligi za kimataifa makocha vijana si ndio wanazidi kuja juu – kina Pep Guardiola? Na hata miondoko yao inafananafanana, yaani, imekaa kiujanaujana kuanzia kwenye mavazi, maneno na mbinu?  Si nasi tuanze basi ‘ujanaishaji’ wa kocha wa Stars?

Au tunasubiri tupate kwanza Rais Kijana Ikulu mwaka 2015 ndio atuletee Kocha Kijana? Kama matokeo ya timu yetu ya taifa ya mpira ni kielelezo cha utendaji wetu kama taifa, si tuanze na Kocha Kijana tuone utendaji wake utakavyousonda kidole wa Rais Kijana?

Makala mbalimbali kuhusu ujio wa makocha wapya wa mpira walio vijana, yanadai wao wako tayari kuthubutu. Ni vigumu kwao kufanya maamuzi ya kihafidhina hata inapobidi kufanya hivyo ili walau kupunguza uwezekano wa kushindwa. Wanataka ‘makubwa’.

Diego Simeone, kocha wa Atletico Madrid, ni mmoja wao. Katika mechi ya fainali ya kombe la vilabu mabingwa wa Ulaya alitaka sana kutwaa kombe. Aliyekuwa mfungaji wake mahiri, Diego Costa, hakuwa fiti. Ila alimpanga tu. Wakapoteza nafasi ya pekee.

Yupo pia Andre Villas-Boas (AVB) katika kundi hilo la makocha. Pamoja na umahiri wake vijana wenzake waliokuwa wanaichezea timu aliyokuwa anaifundisha waliacha kumsikiliza ‘dogo’ mwenzao. Hivyo, ujana wake sio uliompa uhalali kuwa kocha wao.

Obama ni rais mwenye mvuto wa pekee kwa baadhi ya ‘marais vijana’ kama Maurinho alivyo kwa baadhi ya hao ‘makocha vijana’. Lakini kuvaa na kuongea kama Obama na Maurinho hakumfanyi mtu kuwa rais au kocha mzuri. Wao wana uzoefu wao wenyewe .

Uthubutu wa ujana una umuhimu wake. Ila unahitaji uzoefu. Uzee ulipoanza kumuingia kiongozi wa zamani wa Ethiopia – aliyewaongoza vijana wenzake waliovaa kaptula na kufuga afro kuingia madarakani kimapinduzi katika barabara za Addis – aliliona hilo.

Baada ya uzoefu huo, hayati Zenawi alisema hivi: “Tofauti kubwa kati yangu – Meles wa sasa – na Meles wa miaka 35 iliyopita ni kuwa nikiwa kijana nilikuwa na ujasiri na uthubutu wa kuzifikia mbingu kwa kishindo. Meles wa sasa hana tena ujasiri na uthubutu huo…Kwa nini? Kwa nini hofu ya Mungu imeingizwa kwa Meles? Nadhani kwa kiasi fulani ni kwa sababu ya uzoefu wa kushindwa na kufanikiwa, uzoefu wa maisha wenyewe ambao unamfanya mtu awe na hekima na wakati huo huo kupungukiwa na ujasiri na uthubutu. Kama tutaweza kuunganisha hekima itokanayo na umri/uzee pamoja na ujasiri na uthubutu wa ujana basi tunaweza kuondokana na uwendawazimu wa kurudia kile kile [ambacho tumekuwa tunakirudiarudia Afrika na kutegemea matokeo tofauti]”

Taifa Stars itaendelea tu kuwa kichwa cha mwendawazimu alichokiongelea Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, kama tutaendelea tu kurudia kile kile (ushirikina, ubadhirifu na uzembe ) na kutegemea matokeo tofauti (kucheza Kombe la Dunia, Kombe la Afrika na Kombe la Mabara). Haitajalisha kama tuna Kocha Kijana au Kocha Mzee. 

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP