Wednesday, September 10, 2014

Katiba Mpya: ‘Ukikimbia Nchale, Ukisimama Nkuki’?

Katiba Mpya: ‘Ukikimbia Nchale, Ukisimama Nkuki’?

Kitanzi kilichokuwa kimeufunga mchakato wa kutunga Katiba Mpya kinaonekana kimefunguliwa. Hii ni baada ya kile kinachoonekana kuwa ni maridhiano kati ya Rais Kikwete na kinachojulikana kama Kituo cha Demokrasia Tanzania (TDC). Maamuzi hayo yanaonekana yatapelekea Katiba Mpya ipatikane baada ya uchaguzi mkuu wa 2015.

Huu unaonekana kuwa ni ushindi mkubwa kwa unaojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Pia inaonekana ni ushindi kwa wanaharakati wanaopinga namna ambavyo Bunge Maalum la Katiba (BMK) limekuwa likiendeshwa kimburuzo chini ya Mwenyekiti Sitta na jinsi ambavyo Rasimu ya Katiba Mpya iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba (TMK) iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Warioba imekuwa ikichakachuliwa.

Swali la kujiuliza ni: Je, maelewano haya ya wanasiasa kule kwenye Ikulu ndogo mjini Dodoma na yale ya pale Ikulu kubwa jijini Dar es Salaam yana tofauti gani? Kama chanzo kimojawapo kikuu cha kuvurugika kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya, kama baadhi ya wachambuzi walivyosisitiza toka awali, ni kumwachia Rais awe na madaraka makubwa katika uteuzi wa TMK na BMT pamoja na kwenye kutiririsha mwelekeo wa mjadala wa kitaifa, nini kitabadilika sasa? Maamuzi ya mchakato wa Katiba Mpya ambayo inatakiwa kutenganisha miingiliano na madaraka ya mihimili mikuu mitatu ya dola – Bunge, Mahakama na Serikali – yanapofanyika Ikulu tutegemee nini kipya?

Rais ajaye 2015 ndiye atakuwa hana uchu wa kuhodhi madaraka hayo makubwa ya kusimamia mchakato wa kutunga Katiba Mpya? Nini kitamzuia? Mabadiliko mapya ya Sheria ya Kutunga Katiba? Nani atayapitisha mabadiliko hayo? Bunge hili hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) linaloendeshwa na Spika Makinda ambalo lina wabunge wengi kutoka chama tawala ambacho kimechangia kwa kiasi kikubwa kuteka nyara mchakato kutoka kwa wananchi? Au baada ya uchaguzi Bunge litakuwa tofauti?

Uchaguzi Mkuu huo wa 2015 bila Katiba Mpya utaendeshwa na Tume ya Uchaguzi iliyoboreshwa na kuwa huru (zaidi) kwa sababu wanasiasa kutoka vyama vya upinzani wamekutana Ikulu na kukubaliana na Rais aondokaye kuwa iwe hivyo? Rais huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala ambacho kinataka kushinda tena ndiye atahakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki? Ama marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi katika Katiba ya sasa ya mwaka 1977 ndiyo yatakuwa mwarobaini?

Chama tawala kina makundi/mitandao ya marais watarajiwa ambao wengi wao wanataka kushinda mwakani. Wao na wapambe wao (wakiwamo wabunge wanaowaunga mkono) wana nguvu/madaraka na maslahi gani katika hili la kuboresha Katiba ya sasa? Kama moja ya sababu zilizopelekea vyama vya upinzani kudai Katiba Mpya, hasa baada ya uchaguzi tete wa 2010, ni vipengele vyake vinavyohusu Uchaguzi Mkuu, je, wagombea kutoka chama tawala wanataka mabadiliko hayo yatakayowarahisishia kazi wapinzani?

Mtanziko wa Katiba bado upo japo kitanzi kimelegezwa kwa muda. Kupata Katiba mpya kabla ya Uchaguzi wa 2015 ni jambo ambalo sasa linaanza kukubalika kuwa si kwamba ni gumu tu bali haliwezekani. Lakini hii haimaanishi tutapata tu Katiba Mpya baada ya Uchaguzi wa 2015 hasa kama michakato ya kisheria ya maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Tume ya Uchaguzi itakuwa inafanywa na taasisi zilizojaa wajumbe au wabunge wa chama tawala ambao maslahi yao makubwa ni kushinda ubunge au urais.

Jenerali Ulimwengu alienda mbele zaidi na kuhitimisha hivi: “Ni dhahiri, na ushahidi upo, kwamba chama-tawala hakikutaka tangu mwanzo, hakitaki sasa na wala hakitataka kamwe kuandika Katiba mpya. Kisa? Chama hicho na wakubwa wake wanaona Katiba iliyopo sasa inawafaa wao na maslahi yao. Si maslahi ya nchi, bali maslahi ya wakuu walio madarakani leo.” Hitimisho lake, japo haliutendei haki uwezekano wa mtu au  kitu chochote kile kubadilika, linatukumbusha kuwa ni hatari sana kuwaachia wanasiasa, hasa walio watawala au wanaotaka kuwa watawala wetu, wawe na madaraka makubwa katika kuendesha mchakato wa kupata Katiba ya Wananchi. Hilo ni kosa kubwa tulilolifanya.

Lakini tunajua kosa kubwa zaidi ni kurudia kosa. Tumeshaona zaidi ya mara moja sasa jinsi ambavyo mikutano ya sharbati/juisi Ikulu inavyoleta maridhiano/maelewano ya kisiasa yanayopelekea mchakato wa kutunga Katiba Mpya ufuate mielekeo ya wanasiasa. Sasa jukumu ni letu kuhakikisha kuwa tunatumia fursa hii ya mtanziko huu wa Bunge la Katiba kurudisha mchakato huo kwa wananchi – kwenye Bunge la Wananchi la Katiba.


Ndiyo. Tumegota. Ila hapo tulipojifikisha sio mwisho wa ‘safari ya matumaini.’ Japo tukisimamisha mchakato huu ‘ni shida’ na tukiendelea nao pia ‘ni shida,” mtanziko huo kwa kiasi fulani umetusaidia wananchi kukifanya kile kile ambacho mwanazuoni huyo wa Ukatiba amekuwa akisisitiza miaka nenda rudi kuwa ndiyo msingi mkuu wa utungaji wa Katiba ya kidemokrasia: Majadiliano Mapana ya Kikatiba ya Kitaifa. Hakika kama tunachohitaji ni Katiba tu iliyoandikwa vizuri tunaweza hata kuwakodisha wanasheria waliobobea watuandikie kama washauri wataalamu. Lakini hicho sicho tunachohitaji.

Tunachohitaji ni mchakato wa kina wa kitaifa wa kujenga mwafaka kati ya wananchi. Huo mwafaka wetu sisi wananchi wenyewe ni moyo wa nchi. Utakuwa na uhalali kwetu na utakutambulisha kwetu. Tutauona wetu. Tutauhisi wetu. Tutalinda chetu. Tutatetea chetu. Mwafaka huo kati ya mwananchi na mwananchi ndiyo Katiba ya Wananchi. 

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP