Monday, September 1, 2014

Lionel Cliffe na Mgongano wa Maslahi Tanzania

Lionel Cliffe na Mgongano wa Maslahi Tanzania

Yapata mwaka mmoja toka tumpoteze yule mchambuzi mahiri, Lionel Cliffe. Uchambuzi wake wa migongano ya maslahi Tanzania bado unahitajika leo. Hebu tuurejee kwa kina.

Katika uchambuzi huo, Cliffe anaanza kwa kusisitiza kuwa mabunge mengi katika nchi za Jumuiya ya Madola yalimzuia Mbunge kulipigia kura au kuliongelea suala ambalo ana maslahi binafsi nalo. Lakini baada ya uhuru baadhi ya mabunge yaliamua kuondoa zuio hilo linaloaibisha. Inaonekana alikuwa anamaanisha kuwaaibisha waheshimiwa.

Wabunge wa Tanzania, mwanazuoni huyo anaendelea kusisitiza, hawakuwahi kuzuiwa kiasi hicho ama ‘kivile’. Kanuni za Kudumu za Bunge zilikuwa zimewazuia tu kuongelea masuala ambayo wana maslahi binafsi ya kifedha bila kuweka wazi aina na ukubwa wa maslahi hayo. Rekodi alizozipitia mtafiti huyo zinaonyesha kuwa katika kipindi hicho inaonekana hakukuwa na maslahi yaliyowekwa wazi wala mgongano wa tafsiri ya kanuni.

Hata baada ya Azimio la Arusha kuleta mwongozo wa viongozi na sheria iliyowalazimu wabunge kuorodhesha maslahi yao ya kifedha kwa Spika, bado utekelezaji wake ulikuwa ni mgumu. Japo sheria hii pia iliwahusu wake za wabunge, mtafiti huyo anasisitiza kuwa haikuwagusa ndugu wote, hivyo, baadhi ya wabunge walitumia kipindi cha mpito kusajili maslahi yao binafsi kwa ndugu zao au kuanzisha makampuni ya muamana (trusts/waqfs) kwa manufaa ya watoto wao. Pamoja na hayo, sheria ilizuia sana migongano ya maslahi.

Jambo moja ambalo uchambuzi huu wa kihistoria unatukumbusha ni kuwa mgongano wa maslahi binafsi wa kifedha unaweza kuwa na uhusiano wa karibu sana na (unaoonekana kuwa ni) mgongano wa maslahi binafsi usio wa kifedha. Unaweza usipate hata senti moja lakini ndugu, mfanyakazi au hata rafiki yako akapata kitita cha pesa. Pia wote mnaweza msifaidike kiuchumi ila kwa namna moja au nyingine mkanufaika kijamii n.k. Mtaji wa kijamii (social capital) nao ni faida tu kama ulivyo mtaji wa kifedha (financial capital).

Mheshimiwa mbunge huwezi kujipatia umaarufu mkubwa wa kisiasa (political capital), unaoweza hata kukufanya uwe Rais 2015, kwa kulivalia njuga sakata la ufuaji wa umeme wa dharura bila kuwa wazi kuwa wewe na ndugu zako mna kampuni binafsi ya uzalishaji wa umeme. Ndiyo, mbunge huwezi kulisemea hilo bila kueleza kuwa wewe au wasaidizi wako wananufaika kwa namna fulani na malipo yatokanayo na kesi lukuki za sakata hilo.

Suala hili haliwahusu wabunge wetu tu. Linatuhusu sote tulio/tutakaokuwa katika nafasi za kufanya maamuzi yanayogusa umma japo pia yanagusa maslahi yetu binafsi ama ya watu walio karibu nasi. Anahusika yule jaji pale wa shindano lile anayejuana na mshiriki au mmiliki wa kikundi cha washiriki wale. Yule mjumbe wa bodi ya kuamua vitabu gani vitumike ilhali rafikiye anamiliki kampuni ya uchapishaji anahusika. Huyu, huyo na yule.

Nani anayenufaika au kutonufaika na mgongano wa maslahi? Ni mimi. Ni wewe. Ni sisi. Jukumu la kuyaweka wazi maslahi binafsi, yawe ya kifedha au yasiwe ya kifedha, ni la nani? Ni lako. Ni langu. Ni letu. Maslahi ya nchi ni ya nani? Ni yangu. Ni yako. Ni yetu.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP