Sunday, September 21, 2014

Wazanzibari sio Waskochi

 Wazanzibari sio Waskochi


Matokeo ya kura za maoni huko Uskochi yameacha gumzo barani Afrika. Kuanzia Abuja hadi Arusha Waafrika tunajiuliza kuna nini cha kujifunza. Hapo Mji Mkongwe, Zanzibar hiyo ndiyo habari ya mjini.

Rafiki yangu mwenye uzalendo wa Kizanzibari amenishtusha kwa kunitumia ujumbe usemao “naona umefurahi…haya furahia” baada ya kumtumia taarifa kuhusu matokeo hayo na kuuliza kiutani: “Vipi Zanzibar/Unguja/Pemba/Tumbatu?” Kutokana na sababu za kihistoria – historia binafsi na ya jumla – naipenda sana Uskochi. Nimefurahi wamepitia mchakato huu muhimu ambao inasemekana, pamoja na kushindwa katika kura, utawaletea  mabadiliko mengi yatakayoongeza uhuru wao ndani ya Muungano.

Fundisho nililolipata ni kuwa japo Wazanzibari sio Waskochi hata wao wana haki ya kupiga kura kama wenzao na watakapopata fursa hiyo tusishangae maamuzi yao kisa baadhi yao/yetu tumekuwa tukiwasemea kuwa wanataka hiki au kile. Pia yamenipa moyo kuwa sio jambo la kushangaza kupinga muundo (dhaifu) wa Serikali Tatu kati ya eneo moja kubwa na eneo moja dogo ilhali nasimamia hoja yangu kuwa ‘Zanzibar ni Zaidi ya Nchi’. Haishangazi kwani Muungano wetu bado unuweza kuongeza uhuru zaidi kwa Zanzibar.

Wapo wanaoshangazwa na Waskochi kupiga kura ya kukataa kujitenga na Uingereza. Hapa tunaongelea sehemu ambayo imekuwa na historia ndefu ya uzalendo wa Kiskochi toka enzi za William Wallace, yule shujaa wao maarufu ambaye Mel Gibson alimuigiza katika filamu yake ya Braveheart, yaani, ‘Moyojasiri’.

Filamu hiyo inaanza na maneno mazito ya Mskochi dhidi ya Muingereza ambayo kwa tafsiri ya haraka haraka yanasomeka hivi kwa Kiswahili: “Nitakueleza habari za William Wallace. Wanahistoria wa Kiingereza watasema nadanganya. Lakini historia huandikwa na wale wanaowanyonga mashujaa”. Naam, ndivyo ilivyokuwa, Wallace alinyongwa baada ya kuongoza mapambano ya Uskochi dhidi ya Uingereza.

Kwa zaidi ya miaka 700 mpambanaji huyo amekuwa kielelezo thabiti cha uzalendo wa Kiskochi. Lakini uzalendo huo umeshindwa kupata kura za kutosha za kuuvunja Muungano wao na Uingereza. Kwa nini?

Profesa mmoja wa Kinaijeria  anasisitiza kuwa japo Uingereza haikuwatisha wapiga kura kwa mtutu wa bunduki, ilitumia vitisho vya kiuchumi. Anadai mabenki na taasisi za kifedha zilitishia kujitoa Uskochi.

Pia anasema Waskochi walitahadharishwa kuwa nchi yao mpya itabidi ilipe sehemu ya deni la taifa na itakumbana na visiki kwenye suala la sarafu yao. Hili, anahitimisha, liliwatisha sana wale wapiga kura wanaokuwa hawana hakika hadi dakika ya mwisho na ambao kwa kawaida ndio wanaobadili matokeo.

 Huyo mwanazuoni ni miongoni mwa wale ambao wanahoji kama uchaguzi huo wa kutojitenga ulikuwa ni utashi tu wa Waskochi walio wengi zaidi. Lakini katika maamuzi ya masuala ya kutengana hofu huwa ina sehemu yake. Kiongozi mkuu wa Uskochi wakati wa upigaji kura huo, Alex Salmond, ameamua kujiuzulu ila amekubali matokeo hayo japo amesisitiza kuwa “kampeni inaendelea na njozi yao haitakufa kamwe”.

Ugumu wa maamuzi hayo ya Waskochi unathibitishwa na idadi ya kura. Asilimia 55 dhidi ya 45 ni ishara kuwa wamegawanyika takribani katikati katika suala hili. Hivyo, ni vigumu na labda haiwezekani kufanya uamuzi ambao utawapendeza Waskochi wote sasa. Hata kura za Sudani ya Kusini hazikufikia asilimia 100!

Zanzibar je? Itakuwaje Wazanzibari nao wakipata fursa ya kupiga kura? Wataamua kujitenga na Tanzania?

Jibu wanalo Wazanzibari wenyewe. Ili tulipate hilo jawabu lazima wapate kwanza hiyo fursa. Kile ambacho kimekuwa kinaendelea ni ‘mwamba ngoma ngozi huvutia kwake’. Anayewamba ngoma ya kujitenga atakuambia Wazanzibari wengi hawataki Muungano. Na anayewamba ngoma ya kutojitenga atakuambia Wazanzibari wengi wanataka Muungano. Hata tafiti zikikubaliana tafsiri zinatofautiana.

Ile taasisi iliyokuwa inaheshimika sana katika tafiti za kitakwimu, REDET, iliwahi kufanya tafiti mwaka 2003 & 2004 na kugundua kuwa ni asilimia 1.6 tu ndiyo walikuwa hawaupendi Muungano na hakukuwa na tofauti kubwa kati ya Wazanzibari na Watanzania Bara kuhusu hilo. Tofauti za msingi zilikuwa kwenye muundo wa Muungano. Hizo ndizo zinazoendelea kuleta mgongano katika mchakato wa katiba mpya.

Ugunduzi mwingine muhimu wa tafiti hizo, kwa mujibu wa uhakiki wa baadhi ya Wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni kuwa asilimia ya walioweza kutaja angalau faida moja ya Muungano kwa ujumla/wastani haikuzidi 50 nchini Tanzania. Kwa upande wa Zanzibar, wengi wao – asilimia 52 – walitoka mkoa wa Mjini Magharibi na Tanzania Bara walitoka mikoa ya Pwani  – Tanga (78), Pwani (64), Mtwara (64) na Lindi (62) – hivyo, kupelekea wahakiki hao kuhitimisha kuwa hii “inaashiria kwamba ni katika ile mikoa yenye maingiliano makubwa zaidi ya kijamii na kiuchumi baina ya watu wa pande mbili za Muungano ndio wanaofahamu zaidi faida za Muungano.”  Hivi hawa wakipiga kura watashinda kweli?

Demokrasia ni kama upanga ukatao kuwili. Inaweza kuleta kile kiitwacho udikteta wa walio wengi’ ambapo hata asilimia 55 inatosha kuamua nchi iendelee na kile ambacho asilimia 45 ya wenzao haikitaki. Hebu tazama picha za baadhi ya Waskochi kutoka kwenye hiyo asilimia 45 wanavyotokwa na machozi kwa kushindwa kujitenga. Je, kwao matokeo ya referenda’ ndio  maridhiano’. Piga picha ni jinsi gani kura kama hiyo ikipigwa Zanzibar na ikatokea walio wengi kutoka Mjini Magharibi wakasema hawataki kujitenga ila wenzao wa mikoa mingine walio wengi zaidi wakasema tujitenge – ndio itakuwa mwafaka’?

Cha kuzingatia ni kuwa na mfumo unaoridhiwa na wananchi wa kufanya maamuzi magumu ambayo hata kama matokeo yake hayatawapendeza wote angalau mchakato wa kufikia uamuzi huo utawapendeza wengi kama sio wote. Ni dhahiri kuwa tumegawanyika kwenye suala la muundo wa Muungano. Hakuna takwimu za taasisi au tume yoyote zinazopinga ukweli huo. Na mgawanyiko huu unachochea mgawanyiko kuhusu uwepo wa Muungano. Kwa hali ilivyo sasa hakuna upande wowote wa Muungano ambao haujagawanyika.

Ombeni Sefue amekaririwa akisema hivi kuhusu suala hilo: “Hutapata maridhiano hayo ndani ya Bunge Maalumu na hutapata maridhiano ukienda kwa wananchi.” Ni kweli. Hatuwezi kupata ‘maridhiano hayo’ kokote sasa. Tunachoweza kupata ni maridhiano ya namna ya kuridhiana. Kilichobaki ni kuamua namna ya kukipigia kura kile ambacho kitawaacha wengi tu hawajaridhika japo wengine wengi tu wameridhika.

Tuamue sasa. Kama kweli tunataka kuamua kuvunja na kuunda nchi upya tuitishe kura ya maoni huko Zanzibar. Wazanzibari wapate fursa ya kuamua kujitenga au kubaki katika Muungano wa Tanzania.

Baada ya hapo, kama wameamua kubaki, tupige kura kuamua muundo wa Muungano. Tukimaliza ndiyo tutengeneze katiba mpya. Hakika (z)itakuwa katiba mpya maana hata nchi (z)itakuwa (z)imezaliwa upya.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP