Wednesday, October 29, 2014

Wako Wapi Kina Anna Calculator?


Wako Wapi kina Anna Calculator?

“Watu wananiona mimi kama mwehu, lakini nina akili zangu timamu kabisa!” – Anna wa Mtwara

Jacqueline Mgumia

Usiku wa tarehe 17 Oktoba 2014 nilikuwa Villa Park, Mtwara nikipata chakula cha jioni. Katika kuongelea burudani za mji huo mmoja wa watu tuliowakuta mezani alitutaarifu kuwa walikutana na binti aliyeitwa “Calculator” mwenye uwezo mkubwa wa hesabu aliyekuwa kivutio kikubwa. Nilishangazwa, kwani mara nyingi vivutio vya wageni ni sanaa – sikuwahi kudhani hesabu nayo ni sehemu ya sanaa. Kwa butwaa nikauliza, “sasa huyo binti ana uwezo gani”?

Mmoja wa mashuhuda akasema, “juzi tulipokuwa tunakula huyo Calculator alipita, nasi kwa shauku tukataka kupima uwezo wake, hivyo, weita akatuambia tumuulize swali lolote la hesabu atatujibu. Tukamuuliza ‘kuna tisa ngapi katika mia moja?’ Kwa wapesi kabisa akajibu kuna tisa ‘20', wakati sisi tulidhani kuna tisa 19. Calculator aliwakumbusha kwamba 99 ina tisa mbili, kwa maelezo hayo wapimaji wakaingiza mikono mifukoni mwao na kumpa fedha kidogo  kama pongezi.

Kutokana na hamu ya kutaka kumfahamu Calculator nilimuuliza mhudumu tunawezaje kumuona. Kwa haraka haraka akatujibu, “yule! hayuko vizuri. Hakai sehemu moja anazungukazunguka tu. Labda mumjaribu kesho jioni.” Jioni tuliyoambiwa haikuwa nzuri kwetu kwa kuwa tulikuwa tunaondoka kurudi Dar es Salaam kesho yake alfajiri, hivyo, tukaamua kurudi mchana kesho yake kumtafuta.

Nikamuuliza mhudumu tuliyemkuta iwapo anamfahamu Calculator, yeye mara moja aligeuka na kuelekea counter, aliporudi akatwambia, calculator haipo counter. Hakika alikuwa hamfahamu Calculator mtu bali kitu, hivyo, tukasubiri mhudumu wa pili ambaye alituvunja moyo zaidi. Alisema, “hakuna anayefahamu Calculator, anatokea wapi, anaishi wapi wala simu yake.” Pia akatueleza kuwa hotelini hapo kuna wakati anafika na wakati mwingine hafiki, kwani kuna wakati wanamfukuza iwapo anaonekana kuwasumbua wateja.

Ingawa uhalisia wa kumuona ulianza kufifia, ndani ya moyo nilishikwa na hamu ya kukutana naye labda kwa sababu nilikuwa siamini kwa nini mtu mwenye uwezo kama yeye anafanya sanaa ya hesabu hotelini, na pia kwa nini watu wamuone hana akili timamu?

Hivyo, nilipopanda bajaji kurudi nilipofikia, nikamuuliza dereva wa bajaji kama anamfahamu Calculator. Kwa bahati nzuri alikuwa anamfahamu ila akasema itakuwa vigumu kumpata kwani anazunguka sana mchana na hafahamu anakaa wapi. Tukakubaliana katika mizunguko yake iwapo atakutana naye amuombe aje hotelini kwetu na atakapomleta tutamlipa usafiri wake. Aliridhia na kutoa tahadhari kwamba anaweza asimpate kwani Calculator ana mizunguko mingi sana pia “hapendi watu wanavyomuitaita na kumshangaa.” Nikatoa salaam ampe: “mwambie sisi hatumshangai tunataka kutambua uwezo wake.”

Saa moja baadaye, dereva wa bajaji alipiga simu kwamba amempata. Nilitoka nje na kukutana na dada ambaye alijitambulisha kwa jina la Anna! Swali langu la kwanza lilikuwa jina la Calculator limetokea wapi. Alijibu, “napita huko njiani watu wananiuliza ngapi jumlisha ngapi, ama ngapi gawa kwa ngapi, nawajibu. Wao wanaangalia kwenye calculator walipoona sikosei wakaanza kuniita Calculator.”

Anna alimaliza darasa la saba mwaka 2002 ila baba yake alimwambia hakufanikiwa kuchaguliwa kuendelea na shule. Hivyo, alienda kuishi na bibi yake mzaa mama kufuatia kifo cha mama yake. Leo hii Anna ana umri wa miaka 27, anaishi na bibi yake na mama yake mdogo hapo Mtwara. Toka alipomaliza la saba hakubahatika kuendelea na masomo wala kupata kazi kutokana na ugonjwa wa kifafa unaopelekea aanguke anguke hivyo kuwafanya waajiri wengi kukataa kumpa kazi.

Baada ya kufanya maongezi naye kwa muda mrefu na kumuuliza hesabu za kujumlisha, kugawa, kuzidisha na kutoa kwa zaidi ya nusu saa nilijiridhisha kwamba Anna hakika ni Calculator. Baadhi ya maswali niliyomuuliza yalikuwa: Kuna mtu ana matofali 552. Akaamua kuwapa watu watano kila mmoja matofali 72, je, yeye atabakia na matofali mangapi? Kwa haraka, ndani ya sekunde tatu alijibu 192. Mimi kwenye calculator jibu lilikuja 190, nikamwambia kakosea, akarudia hesabu hiyo na kusema kwamba jibu ni 192, nikarejea tena kuhakiki kwenye calculator, ni kweli mimi ndiye nilikuwa nimekosea.

Baada ya hapo nikamuuliza hesabu hizi za kuzidisha na kugawanya kwa haraka haraka: (i) 920 x 5= 4600, (ii) 927 x 4 = 3708, (iii) 48 x 49 = 2352, (iv) 97 x 95 = 9 515, (v) 2300/7 = 328.571, (vi) 322/5= 64.4, (vii) 1950/6 = 325, (viii) 9580 x 250 = 2,355,000. Katika hesabu zote hizi, alikosea namba (iv) lakini alipopewa nafasi ya kusahihisha, alitoa jibu sahihi ambalo ni 9215. Kila swali aliweza kutoa jibu lake ndani ya sekunde 10, mengi akijibu ndani ya sekunde 3. Hata watu waliokuwa jirani walikuja kumsikiliza na  walistaajabu.

Hakika tulistaajabishwa na uwezo wake na hata kumfanya rafiki yangu aliyekuwa karibu, Chambi Chachage, kumuuliza alijifunza wapi hisabati. Anna alijifunza hesabu kupitia shule ya msingi, kama vijana wengi wa Kitanzania. Anakumbuka mbinu za kukumbuka urahisi wa mahesabu kupitia MAGAZIJUTO (Mabano, Gawanya, Zidisha, Jumlisha, Toa). Pia kichwani kwake kuna kumbukumbu ya table nzima ya kuzidisha. Anasema alizikariri hesabu hizo kwa ufasaha alipokuwa shule ya msingi. Anapofanya hesabu anaziona kirahisi tu kichwani japo kuna wakati kinamuuma.

Kwa uwezo huo, nilidhani Anna angefanya vizuri kwenye hesabu alipokuwa shuleni. Lakini akasema hapana, alipokuwa shule alikuwa anapata na kukosa, kwani kuna wakati alipokuwa anaumwa alishindwa kujua mbinu gani wenzake walijifunza na hivyo kukosa hesabu mpya. Anna aliendelea kujifunza hesabu alipotoka shule, kwani yeye kichwani huwa anaziona namba kwa urahisi pale anapotembea barabarani na huwa zinamvutia. Pia hujifunza namba kwa kuangalia magazeti na kujibu maswali ya watu anaokutana nao.

Kwa kuwa nafahamu kwamba tunapofika darasa la saba watu wengi tunakuwa hatufahamu trilioni na bilioni, nilimuuliza yeye namba hizo alizijuaje baada ya kuziandika kwa usahihi kwetu kwenye karatasi tuliyompa. Alisema namba nyingi anajifunza kupita matangazo ya Tigo na Voda, kwani wanatoa zawadi za mamilioni na hivyo yamemsaidia kujua bilioni 1 ina milioni elfu 1, na trilioni ina sifuri 9.

Katika kuelezea uwezo wake alisema hesabu zote ambazo ni chini ya elfu moja ziwe za kutoa, kujumlisha, kugawanya ama vipeo na vipeuo huwa hazimchukui muda kuzifanya. Anaweza kuzijibu hizo ndani ya sekunde zisizozidi tatu. Lakini hesabu zinazoanzia na maelfu kwenda juu na ambazo zina mchanganyiko wa namba nyingi huwa anazifanya kuanzia sekunde 5 mpaka 10.

Pia huwa anakosea hapa na pale hasa hesabu inapokuwa na namba zilizochanganyika sana au zinapokuwa na jibu lenye desimali baada ya kugawanya. Moja ya hesabu hizo ni 950 x 2443, alitoa jibu la 2,318, 850 ambapo alikosea namba mbili, jibu sahihi likiwa 2,320, 850. Katika maswali ya kugawanya hukosea desimali namba inapokuwa kubwa sana, kwa mfano, nilipomuuliza 9568/869 ni ngapi,  alitoa jibu la 11.011 badala ya 11.010.

Sasa Anna anakitumiaje kipaji hiki? Kwa kuwa hana kazi na watu wamekuwa wanavutiwa na uwezo wake, anafanya sanaa ya hesabu. Watu wanapomuita akiwajibu maswali magumu kwa furaha huwa wanampa fedha kidogo. Wengi wa watu hawa ni wageni, hivyo hufikia mahotelini. Lakini kwa kuwa ana ugonjwa wa kifafa amekuwa akianguka mara kadhaa mbele ya watu na hivyo wenye hoteli humfukuza kwa hofu anaweza kuangukia wateja mahali pao pa azi.

Sasa mimi nabaki kushangaa tu! Ni watu wangapi wana uwezo kama wa Ana na hawajulikani kabisa ama wamebaki kufanya sanaa ya hesabu? Je, ni nini kifanyike mtu anapokutana na kipaji kama hicho?

Najiuliza, ni sahihi kweli kumuita mtu mwehu kwa kushindwa kujua uwezo wake? Ni kweli alifeli darasa la saba au kifafa kilimfanya asiendelee na shule? Nini hatma ya kina Ana Calculator wa Tanzania?

Tunawatambuaje? Tunawasaidiaje? Tunawatumiaje?

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP