Tuesday, December 23, 2014

Hotuba ya Rais na Hatma ya Fedha za Umma

Hotuba ya Rais na Hatma ya Udhibiti wa Fedha za Serikali

Chambi Chachage

Kwa nini Rais aliagiza Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) kuhusu akaunti ya Escrow ya Tegeta isambazwe kwa umma? Hili ni swali lililozua utata hasa ukizingatia hilo halijawahi kufanyika kabla. Jibu limepatikana katika Hotuba yake ya jana kwa Taifa kupitia Wazee wa Dar es Salaam.

Ni dhahiri kuwa Rais aliamua kuwa atatumia Hotuba hiyo kutafanya uchambuzi wake (mwenyewe) kuhusu taarifa hiyo ya CAG. Kwa kuwa yeye ni kiongozi wa Serikali basi ni rahisi kuhitimisha kuwa huo hasa ndio uchambuzi wa Serikali. Swali ni: Je, una tofauti gani na uchambuzi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambao kimsingi ndiyo ulitumika kuja na maazimio nane ya Bunge kuhusu akaunti hiyo?

Wachambuzi, wakiwamo wabunge waliobobea katika kuifuatilia Escrow, wameshaanza kuchambua tofauti hizo. Mmojawapo ni David Kafulila ambaye ameainisha masuala saba ambayo yanasigana. Sehemu ya kwanza ya suala la nne inasema hivi: “Hoja kwamba kutaifisha mitambo ya IPTL kutakimbiza wawekezaji ina mapungufu kwa sababu kwa mujibu wa ripoti ya CAG, PAP alifanya utapeli wa kughushi katika umiliki wa IPTL hivyo sio mwekezaji mwadilifu hivyo kutaifisha haiwezi kutisha wawekezaji.”

Mwenyekiti wa PAC anaonekana kuendelea kutekeleza ushauri aliopewa kuhusu “Unyenyekevu (kuwa na kiasi )” kwa kuandika maneno yafuatayo katika ukurasa wake wa mitandao ya jamii: Nimemsikiliza Mhe Rais. Ninachoweza kusema ni kwamba maazimio yale hayakuwa ya Zitto Kabwe, PAC, CAG au PCCB. Yalikuwa ni maamuzi ya Bunge zima. Bunge la vyama vyote kikiwamo chama cha Rais Kikwete yaani CCM. Sisi kama Bunge tulitoa maazimio yale kwa maridhiano, uzalendo na bila kutaka kumuonea mtu yeyote. Suala hili sasa naliacha kwa wananchi. Bunge limefanya kazi yake na Serikali ambayo ndiyo tulikuwa tunasubiri maamuzi yake imeamua hivyo. Wananchi wataamua wenyewe.”

Lakini siku moja kabla Mwenyekiti huyo alisema maneno hayo mazito kwenye Mtandao wa Wazi wa Wanazuoni: “Wanazuoni  CAG kasema bila kuzungusha kuwa PAP kagushi nyaraka, kakwepa kodi, hana umiliki halali wa IPTL. Kitu ambacho CAG hakusema ni hatua gani zichukuliwe na hiyo sio kazi yake. Hiyo ni kazi ya PAC. Someni hadidu [za] rejea zote muone ni kwa nini CAG hakujibu hadidu [za] rejea 2 za mwisho. Hizo ndizo PAC ilijibu. Na hiyo ndio kazi ya PAC miaka yote.”

Hadidu hizo zinasomeka hivi kwenye ukurasa wa 50 wa Taarifa ya CAG:  “xii. Kutoa mapendekezo ya njia sahihi za kisheria zinazoweza kutumika kwa ajili ya kulinda serikali isipate hasara zaidi katika utekelezaji wa mkataba wa uzalishaji umeme kati ya TANESCO na IPTL chini ya wamiliki wapya wa IPTL yaani PAP,  xiii. Kutoa mapendekezo juu ya hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya wahusika kulingana na matokeo ya ukaguzi maalum. (Rejea Kielelezo 1).”

Mwenyekiti wa PAC pia aliurejea hivi kwa msisitizo zaidi mgawanyo huo wa majukumu kwenye mjadala huo wa Wanazuoni mtandaoni: “Taarifa ya CAG iligawiwa kwa wabunge siku moja kabla. Taarifa ya PAC iliweka taarifa hiyo kama kiambatisho namba 1 na iligawiwa. Bunge halijadili taarifa ya CAG bali taarifa ya PAC. Huu ndio utaratibu miaka yote. Mwaka 2012 mawaziri 8 waliondolewa kwa taarifa ya PAC na POAC iliyotokana na taarifa ya CAG. Hakuna aliyesema taarifa ya CAG ibandikwe kwenye magazeti.”

Swali zito la kujiuliza ni: Kama hii ndiyo kazi ya PAC miaka yote, kwa nini mwaka huu (itakikane) ifanywe tofauti? Nini hatma ya udhibiti na uhakiki wa fedha za umma/serikali baada ya ‘tofauti’ hiyo? Kwa nini kuna tafsiri tofauti kuhusu Taarifa hiyo ya CAG?

Uzito wa swali hilo na maswali hayo ya nyongeza unaonekana zaidi pale tunaposoma maneno haya aliyoyaandika Mwenyekiti wa PAC kwenye ukurasa wake wa mtandaoni siku tatu baada ya agizo la Rais kuhusu usambazaji wa taarifa ya CAG: “Sasa kuna juhudi kubwa za kutetea waliotajwa na Taarifa ya Kamati ya PAC. Magazeti, haswa ya Serikali yamekuwa yakiandika habari zenye mwelekeo wa kutetea. Ikulu imeagiza Taarifa ya CAG ichapwe kwenye magazeti, jambo ambalo halijapata kutokea huko nyuma kwani sio mara ya kwanza PAC kutumia Taarifa ya CAG kuwajibishana. Makala zinaandikwa kumshawishi Rais asitekeleze maamuzi ya Bunge. Nasaha za ‘know where to stop’ na ‘kuwa mnyenyekevu’ zinanivuta na kunishawishi kutosema lolote. Hekima inataka kumwachia Mkuu wa Nchi kuamua kwa namna itakavyompendeza. Tumwache aamue. Unyenyekevu unataka hivyo. Wenye ushawishi tofauti walikuwa na nafasi Bungeni. Walishindwa ndani ya Baraza la Taifa. Unyenyekevu ni kwa walioshindwa pia.”

Kwenye majibu yake ya juzi (na ya awali) dhidi ya Mwanazuoni mmoja anayedai kwa hamasa na kusisitiza kwa vielelezo mbalimbali kuwa PAC imepotosha/imedanganya (wa)Bunge na (wana)Nchi kuhusu masuala kadhaa na muhimu yaliyomo katika Taarifa ya CAG, kuna sehemu Mwenyekiti wa PAC alienda mbele zaidi na kusema hivi kuhusu migongano na vipaumbele vya kitafsiri: “Wanazuoni - sarakasi za CAG na taarifa ya Tegeta Escrow ipo siku umma utajua yote.... Tumeambiwa Rais anaongea kesho. Tusubiri atasema na kuamua nini. Kutokana na atakavyosema, sisi kama PAC nasi tutasema yetu ambayo hayakuwa kwenye taarifa au yamo hayajaeleweka au kuwekewa maanani.”

Mkanganyiko wa tasfiri/matumizi ya Taarifa ya CAG katika sakata la Escrow unatokana kwa kiasi kikubwa na jinsi uchunguzi huo ulivyoagizwa na zaidi ya chombo kimoja, kila kimoja kikiwa na mahitaji yake. Katika kipengele cha 1.1 cha “Utangulizi” wa Taarifa hiyo kinatuelezea “Chimbuko la Ukaguzi” ambapo tunaona kuwa: “Ukaguzi huu umetokana na barua…ya tarehe 10 Juni 2014 kutoka kwa Mh. Waziri Mkuu. Kabla ya barua hii, ukaguzi huu ulikwishaombwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kupitia barua…ya tarehe 12 Machi 2014 na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia barua … ya tarehe 20 Machi 2014. Barua ya Mh. Waziri Mkuu imefanya rejea katika maombi yaliyotangulia kutoka kwa Katibu wa Bunge na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini. Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi iliwasiliana na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini na Katibu wa Bunge kupitia barua…ya tarehe 17 Aprili, 2014 ili kukubaliana juu ya hadidu za rejea zitakazoongoza ukaguzi huu. Hadidu za rejea husika ziliridhiwa na taasisi hizo mbili kupitia barua…ya tarehe 5 Mei 2014 kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini na barua …ya tarehe 03/05/2014 kutoka kwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Kwa maana nyingine, Bunge liliagiza na Serikali nayo iliagiza uchunguzi huo maalum. Bunge lilipoipata Taarifa utaratibu tuliojulishwa hapo juu na Mwenyekiti wa PAC kuwa ni wa “miaka yote” ukaanza kama tulivyoushuhudia kwenye mjadala mkali wa tarehe 28 na 29 Novemba 2014 Bungeni. Serikali ilipoipata Taarifa ya awali, kama tulivyojulishwa katika Hotuba ya Rais, kabla ya safari yake ya matibabu Marekani aliikabidhi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) ianze kuifanyia kazi. Lakini pia tumeona Raisi akiitumia kutoa hotuba na maamuzi ya Serikali.

Hali hii inaashiria nini hasa ukizingatia kwa kiasi kikubwa tafsiri ya Serikali iliyopelekea kuamua ilichoamua kupitia Hotuba ya Rais inaonekana ni tofauti na tafsiri ya Bunge iliyopelekea kupendekeza ilichopendekeza? Na hii ni Serikali hiyo hiyo ambayo Waziri wake, Stephen Wassira, alisema (kana kwamba anawatahadharisha wanachama wenzake watakaotaka kupinga) yale maazimio nane ndiyo msimamo wa chama tawala – yaani chenye Serikali – wakati anachangia hitimisho la mjadala wa Escrow Bungeni usiku ule. Je, Rais na Serikali yake imepata kikohozi na kuwa kigeugeu? Au Rais ameona sasa Taarifa ya CAG inatumiwa vibaya na hivyo kuamua kuweka tafsiri/rekodi sawa kwa wananchi/umma?

Huyu ni Rais aliyesifiwa hivi katika ukurasa wa mtandaoni wa Mwenyekiti wa PAC: “Ni Kiongozi pekee wa Tanzania aliyeruhusu taasisi za Uwajibikaji kufanya kazi zake na hata yeye kujikuta akichukua hatua kulingana na maamuzi ya taasisi hizo. Kabla yake, hakuna Rais wa Tanzania aliyetoa nafasi kwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya kazi zake kwa uwazi na umahiri. Hatua yake ya kujadili kwa uwazi taarifa ya CAG ya mwaka unaoishia Juni 30, 2006 kwa kuwaita Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, [kisha] Makatibu Wakuu, Ma RAS na Ma DED ilijenga msingi mkubwa wa taarifa zinazofuata za CAG. Mwaka 2012 alifukuza kazi mawaziri 6 na manaibu mawaziri 2 kufuatia Taarifa za Kamati za Bunge za Mahesabu zilizotokana na Taarifa ya CAG. Haikupata kutokea katika historia ya nchi yetu Rais kufanya hivyo.”

Baada ya kuisoma kwa kina ripoti ya CAG, kuwasikiliza ‘mwanzo mwisho’ Rais katika hotuba yake na Mwenyekiti wa PAC katika mawasilisho yake Bungeni pamoja na mjadala wote ule, ninachokiona ni ‘mbaraka katikati ya laana.’ Mkanganyiko huu wa tafsiri na matumizi ya ripoti ya CAG japo ni laana pale unapochelewesha uchukuliwaji wa hatua kwa wale walioshiriki katika ufisadi, ni mbaraka pale unapotusaidia kuweka sawa mipaka na madaraka ya kutumia Taarifa ya CAG. Inapaswa kutumiwa kutenda haki na kutetea ukweli, hivyo, haipaswi kabisa watu wachache au mtu mmoja – Serikalini au Bungeni – awe na nguvu na madaraka makubwa (kupita kiasi) ya kitafsiri na kimaamuzi.

Wakati tunachambua Tuwaonao katika Ripoti ya CAG kuhusu ESCROW wadadisi tulisema hivi: “Ndio maana kwenye sayansi ya siasa ni vigumu kujibu swali la ‘Serikali ni Nani’?” Ugumu wa swali hilo usituzuie kujibu ni nani na nani katika Serikali ana jukumu lipi na lipi katika mchakato wa ukaguzi na udhibiti wa fedha za Serikali. Na jibu hilo linapaswa kuzingatia uhuru wa mihimili ya Serikali na Bunge kuzuia miingiliano.

Ukurasa wa 5 wa Taarifa ya CAG kwenye Kipengele 1.7 chenye kichwa cha habari “Matumizi ya Taarifa Hii” unatujulisha hivi kuhusu wajibu:Taarifa hii ni kwa ajili ya matumizi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ndiyo waliomba kufanyika kwa ukaguzi huu maalum. Taarifa hii yaweza kutumika kama ushahidi katika mashauri ya madai au jinai. Pia taarifa hii yaweza kutumiwa na Mamlaka, taasisi za Serikali au vyombo vya kusimamia utekelezaji wa sheria kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki pale itakapotakiwa kufanya hivyo. Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi haitahusika na matumizi ya taarifa hii na chombo, taasisi au mtu mwingine zaidi ya vyombo au taasisi zilizotajwa hapo juu.”

Hatma ya ukaguzi na udhibiti wa fedha za umma itakuwa mashakani kama uhalali wake na wa mchakato wa utekelezaji wake utatiliwa mashaka. Hata ukaguzi ukifanywa kwa dharura, haraka hiyo isiwe sababu ya kufanya tuhoji nani atamkagua mkaguzi kama tunavyohoji nani atamhariri mhariri. Uhakiki ni kupata uhakika. Ni kupata majibu siyo kuongeza maswali. Kukiwa na majibu ya hakika hata uwajibikaji utakuwa wa hakika.

Wawajibikaji wawajibike. Wasiowajibika wawajibishwe. Wawajibishaji wawajibishe.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP