Sunday, December 14, 2014

Tuwaonao kwenye Ripoti ya CAG kuhusu ESCROW

Tuwaonao kwenye Ripoti ya CAG kuhusu ESCROW

Sasa macho na masikio ya wadadisi wa mambo yameelekezwa Ikulu. Juma hili Rais atawajulisha wananchi uamuzi wa Serikali kuhusu mapendekezo ya Bunge kuhusiana na utoaji wa fedha katika akaunti ya ‘Escrow ya Tegeta’. Yanatarajiwa maamuzi magumu.

Ili kutuandaa na kitakachojiri, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu ikatoa tamko siku ya sherehe za miaka 53 ya uhuru wetu – 09/12/2014 – lililobeba maneno haya: “….Kufuatia kupokea nyaraka hizo, Rais Kikwete ameelekeza kuwa Ripoti ya CAG iwekwe hadharani kwa ajili ya umma kuweza kuisoma na kujua nini hasa kimesemwa na kupendekezwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali [CAG]. Rais Kikwete ameelekeza kuwa Ripoti hiyo itangazwe kwenye magazeti yanayosomwa na watu wengi na kwenye mitandao ya kijamii, ili Ripoti hiyo iweze kupatikana kwa Watanzania wengi….”

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyotuchambulia ripoti ya CAG kwa umahiri mkubwa Bungeni naye akaandika maneno mazito kuhusu sakata hilo katika ukurasa wake kwenye mitandao ya jamii na kuhitimisha hivi: “….Ikulu imeagiza Taarifa ya CAG ichapwe kwenye magazeti, jambo ambalo halijapata kutokea huko nyuma kwani sio mara ya kwanza PAC kutumia Taarifa ya CAG kuwajibishana….”

Baada ya kusoma matamshi hayo na aliyoripotiwa akiyasema Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali aliyeteuliwa hivi karibuni, wadadisi tulihoji mtandaoni: “Ripoti ya CAG ina kitu tusichokijua kuhusu ESCROW?” Mwandishi mmoja mwandamizi akajibu bila kusitasita: “Ndiyo….Tatizo Watanzania huwa hatusomi ingawa ni wasemaji sana.”

Changamoto hii imetugusa na hivyo tumeisoma tujionee wenyewe nini kilichomo na nani waliomo humo. Ufuatao ni udadisi wetu kuhusu hayo. Tumezingatia kuwa, kwa kawaida, huwa kuna mstari mwembama kati ya hali halisi na tafsiri ya hali halisi hiyo unaopelekea kuwe na tofauti za kiuchambuzi na kimaoni. Hivyo, hii ni ‘tafsiri tunduizi’ tu ya kile tunachokiona na wale tunaowaona humo. Ni haki yetu sote kuhoji tafsiri na watafsiri.

Inaitwa “Taarifa ya Ukaguzi Maalum Kuhusiana na Miamala Iliyofanyika Katika Akaunti ya ‘Escrow’ ya Tegeta, Pamoja na Umiliki wa Kampuni ya IPTL.” Kuhusu “Madhumuni na Wigo wa Ukaguzi Huu” kipengele cha 1.4 katika “Utangulizi” kinatoa angalizo hili muhimu: “Madhumuni ya kufanya ukaguzi huu maalumu ni kumwezesha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kutoa mapendekezo yake kuhusiana na utaratibu uliotumika kutoa fedha kutoka akaunti ya Escrow ya Tegeta iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania. Ukaguzi huu maalum umefanyika kwa kuzingatia matakwa ya viwango vya kimataifa vya ukaguzi na kuzingatia hadidu za rejea kama zilivyoridhiwa na pande zote. Hata hivyo ukaguzi huu hautoi maoni ya ukaguzi (audit opinion) badala yake unatoa mapendekezo yanayolenga katika kushughulikia mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi huu. Ingawa matokeo ya ukaguzi huu yanajumuisha uchambuzi wa masuala ya kisheria, ukaguzi huu hautoi maoni juu ya kuwa au kutokuwa na hatia kwa mtu, chombo au taasisi yoyote iliyohusika katika ukaguzi huu.”

Hitimisho la kipengele hicho linatoa mwanya huu kwa wale ambao pengine wana asichokijua CAG: “Ukaguzi huu ulijikita katika uchambuzi wa nyaraka, taarifa na kumbukumbu kama tulivyozipokea kutoka katika taasisi husika ikiwa ni pamoja na kufanya mahojiano na wahusika mbalimbali katika suala la malipo yaliyofanyika kutoka katika akaunti ya Escrow ya Tegeta, umiliki wa IPTL na utekelezaji wa mkataba wa ununuzi wa umeme toka lPTL. Endapo nyaraka, taarifa ama kumbukumbu nyingine zitapatikana vinaweza kubadili mwelekeo wa maoni na hitimisho la ukaguzi huu.”

Kipengele cha 1.1 cha “Utangulizi” chenyewe kinatuelezea “Chimbuko la Ukaguzi” ambapo tunaona kuwa: “ Ukaguzi huu umetokana na barua…ya tarehe 10 Juni 2014 kutoka kwa Mh. Waziri Mkuu. Kabla ya barua hii, ukaguzi huu ulikwishaombwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kupitia barua…ya tarehe 12 Machi 2014 na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia barua … ya tarehe 20 Machi 2014. Barua ya Mh. Waziri Mkuu imefanya rejea katika maombi yaliyotangulia kutoka kwa Katibu wa Bunge na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini. Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi iliwasiliana na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini na Katibu wa Bunge kupitia barua…ya tarehe 17 Aprili, 2014 ili kukubaliana juu ya hadidu za rejea zitakazoongoza ukaguzi huu. Hadidu za rejea husika ziliridhiwa na taasisi hizo mbili kupitia barua…ya tarehe 5 Mei 2014 kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini na barua …ya tarehe 03/05/2014 kutoka kwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.”

Kwa maana nyingine, miongoni mwa waliooomba ukaguzi huo ufanyike ni walengwa wa ukaguzi huo. Je, walitaka ukaguzi uwasafishe? Au hawakujua wanaokaguliwa ni wao?

Sura ya pili ya Taarifa ya CAG inaanza kwa kurejea historia ya jinsi ambavyo uhaba wa maji na upungufu wa umeme ulipelekea Serikali kupitisha Sera ya Nishati ya mwaka 1992 “iliyoruhusu uwekezaji binafsi katika sekta ya nishati.” Huo ukawa mwisho wa “TANESCO pekee” kuwa “ndiyo iliyokuwa na jukumu la kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme.” Kwetu wadadisi wa wawekezaji huo ndio ulikuwa mwanzo wa Fungate la Uwekezaji na Migogoro ya Maslahi. “Katika kutekeleza sera hiyo na kuchukua hatua za dharura,” CAG anaendelea kututaarifu, “Serikali ilialika wawekezaji binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa umeme.”

Hivyo basi (inasemekana) “tarehe 27 Agosti 1994” ndipo “Wizara ya Maji Nishati na Madini iliingia katika Memoranda ya Makubaliano (MoU) na Kampuni ya Mechmar ili kuleta suluhisho la kukabiliana na upungufu wa umeme.” Mwaka huo huo “Kampuni ya IPTL ilianzishwa chini ya umiliki wa Kampuni ya Mechmar kutoka Malaysia na Kampuni ya VIP Engineering and Marketing (VIP) ya Tanzania. Kampuni ya MECHMAR ilimiliki asilimia 70 na VIP asilimia 30 ya hisa za IPTL.”

Hiki ni kile ambacho wadadisi wa wawekezaji tunakiita ‘Utanzaniashaji wa Uwekezaji wa Nje’ tukimaanisha kitendo cha kampuni ya nje kuingia ubia na kampuni ya ndani au yenyewe kujisajili kama kampuni ya ndani ili kupata faida ambazo ni mahsusi kwa makampuni ya ndani. IPTL ilizaliwa hivi ndio maana kirefu chake, kama kilivyo kwenye taarifa ya CAG, ni “Independent Power Tanzania Limited.” Ilibatizwa ‘Utanzania’.

Taarifa ya CAG ina “Jedwali T1” la mikataba 4 iliyoingiwa katika utekelezaji wa mradi wa uzalishaji umeme wa Megawati (MW) 100. Cha kudadisi kwa kina ni mwachano wa tarehe ambazo mikataba hiyo baina ya IPTL na TANESCO (wa kwanza na, kwa tafsiri yetu, wa nne) na baina ya IPTL na Serikali (wa pili na wa tatu) iliingiwa. Mkataba wa kwanza ni wa “Kununua Umeme” na uliingiwa tarehe “26 Mei 1995”. Wa pili ni wa “Utekelezaji wa Mradi wa Kufua Umeme Megawati 100” ulioingiwa tarehe “8 Juni 1995”. Kisha wa tatu ni wa “Dhamana” ulioingiwa tarehe hiyo hiyo ya “8 Juni 1995.” Halafu wa nne ni wa “nyongeza” na uliingiwa siku iliyofuata, yaani “9 Juni 1995.”

 Hii nyongeza ndiyo kiini kikuu cha utata na utatanishi. Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG, ni nyongeza “kwa” – ama kwenye – mkataba wa kwanza. Na inatutaarifu kuwa “Dhima ya Mkataba” huo wa nyongeza niKuelekeza ukokotoaji wa viwango vya tozo (tariffs) ya ‘capacity charges’” pamoja na “Kuainisha washirika wa Makubaliano ya “‘Escrow.’”

Lakini nini maana ya ‘Escrow’? Kwa tafsiri nyepesi kabisa ya kilei, tuchukulie kuwa Chaupele ana ugomvi na Chausiku kuhusu kibarua alichompa. Chaupele anataka kumlipa mwenzake kiasi anachoona ndicho kinachoendana na ubora wa kazi aliyoifanya kwa mujibu wa makubaliano yao. Lakini Chausiku hakubaliani na kiwango hicho maana anaona ni kidogo ukilinganisha na jasho alilovuja. Wakati wanaendelea kutafuta suluhu wanaamua hela ambayo Chaupele atakuwa anatakiwa kumlipa Chausiku ishikwe na mtu wa tatu asiye na maslahi yoyote au upendeleo wowote kwa mdau yeyote. Anachaguliwa Chaurembo na kuziweka kwenye kibubu.Wote wanakubaliana kuwa mara tu suluhu hiyo itakapopatikana ndani au nje ya mahakama, na kuthibitika/kuthibitishwa pasipo shaka kuwa hakuna mgogoro baina yao kuhusu malipo hayo, basi Chaurembo atazitoa hizo fedha kwenye kibubu na kumpa mhusika mmoja au kuwapa wahusika wote wawili kwa mujibu wa makubaliano ya suluhu. Hicho kibubu maalum ndiyo akaunti ya Escrow.

Mfano huo unatusaidia kuelewa kwa urahisi maelezo yafuatayo kutoka kwenye Taarifa a CAG tukichukulia kuwa Chaupele ni TANESCO, Chausiku ni IPTL na Chaurembo ni Benki Kuu ya Tanzania (BOT): “Kutokana na kutoridhika kwa TANESCO na viwango vya tozo vilivyokuwa vinatumiwa na IPTL, TANESCO ilisitisha kumlipa IPTL malipo ya ‘capacity charges’ badala yake tarehe 5 Julai, 2006 mkataba wa akaunti ya Escrow ulisainiwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya IPTL wakati Benki Kuu ya Tanzania ilikuwa Wakala wa utekelezaji wa mkataba huo kwa mujibu wa Kipengele Na.6.8 (b) cha Mkataba wa Kununua Umeme (PPA) ambapo fedha zote za ‘capacity charges’ zilikuwa zikilipwa katika akaunti hiyo.”

Labda tujiulize kwa nini Chaupele awe TANESCO na sio Serikali au Wizara ya Nishati na Madini? Tukiidadisi Taarifa ya CAG tutaona kuwa kwa kiasi kikubwa kwenye suala la akaunti ya Escrow ya Tegeta, TANESCO ndiye huyo huyo Wizara ya Nishati na Madini pia ndiye huyo huyo Serikali hivyo wote ni Chaupele tu. Tuanze na nukuu hii iliyopo ukurasa wa 11: “Kwa mujibu wa kipengele Na.1.1 na Na 7.1 cha Makubaliano ya Escrow Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilikubali kuwa wakala wa akaunti ya Escrow ambayo ilifunguliwa kufuatia makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Madini na Kampuni ya IPTL yaliyofikiwa tarehe 5 Julai, 2006.” Nukuu hii kutoka kwenye sehemu ya kwanza ya hadidu ya rejea ya tatu nayo inathibitisha hilo: “Kuchunguza sababu za kufungua akaunti maalum (Escrow Account) na pia chanzo cha mgogoro kuhusu tozo kati ya TANESCO na IPTL na kuthibitisha kuwa mgogoro uliamuliwa kwa faida ya pande zote mbili yaani Serikali (TANESCO) na IPTL.”

Ndio maana kwenye sayansi ya siasa ni vigumu kujibu swali la ‘Serikali ni Nani’? Huu mchanyato na mtanziko unajumuisha ukweli kuwa hata Chaurembo wetu BOT, pamoja na uhuru wake wote wa kitaasisi dhidi ya Wizara ya Fedha, naye ni (sehemu ya) Serikali. Miingiliano hii ya kitaasisi ndiyo imelifanya hili sakata la Escrow liwe tata na tete zaidi.

Tukumbuke kwamba tumeshaona kuwa mkataba huo wa kununua umeme ulisainiwa  Mei 1995 na kuwekewa nyongeza inayohusu Escrow Juni 1995. Japo Taarifa ya CAG inajichanganya kidogo kuhusu lini hasa – kati ya mwaka 1997 na mwaka 1998 – ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme hatimaye ulikamilika, inabainisha kuwa uzalishaji haukuanza punde. Kwa nini? Jibu mojawapo la moja kwa moja linapatikana kwenye nukuu hii iliyopo ukurasa wa 8 wa Taarifa hiyo: “Mwaka 1998 TANESCO ilifungua shauri dhidi ya IPTL Na. ARB/98/8 katika Baraza la Kimataifa la usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (International Centre for Settlement of Investment Disputes-ICSID) ikidai kusitishwa kwa PPA kutokana na ukiukwaji wa baadhi ya vipengele katika utekelezaji wake. Kutokana na shauri hilo, Mkataba wa uzalishaji umeme pamoja na kwamba uliingiwa mwaka 1995 na ujenzi wa mitambo kukamilika mwaka 1997, uzalishaji wa umeme ulianza Januari 15, 2002 (commercial operation date). Hivyo kwa kuwa mkataba ni wa miaka 20 unategemewa kuisha mwaka 2022.”

Labda jibu jingine linapatikana kwenye nukuu hii kutoka kwenye kipengele kinachoongelea “Historia ya Mkopo wa IPTL” kilichopo ukurasa wa 43 hadi 44: “Baada ya kuingiwa kwa Mkataba wa Kununua Umeme (PPA) baina ya TANESCO na IPTL; Kampuni ya IPTL iliingia mkataba na Umoja wa Mabenki ya Malaysia (Consortium of Malaysian Banks) tarehe 28 Juni 1997 kwa ajili ya mkopo wa jumla ya kiasi cha Dola za Kimarekani 105 ,000,000 ili kuwezesha ujenzi wa mradi wa ufuaji wa umeme uliopo Tegeta. Mabenki hayo ni Sime Bank Berhad (kiasi cha Dola za Kimarekani 10,000,000), BBMB International Bank Ltd (kiasi cha Dola za Kimarekani 55,000,000), na Sime International Bank (kiasi cha Dola za Kimarekani 40,000,000).”

Kwa mantiki hii, mwaka 1994 wakati IPTL inaanzishwa na mwaka 1995 wakati inaingia mikataba minne ama haikuwa na uwezo wa kifedha wa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme au kama ilikuwa nao, basi uwezo huo ulitoweka ilipofikia mwaka 1997. Lakini dhana za ubepari zinatufundisha kuwa eti biashara, hasa kubwa kubwa, hazifanyiki bila mikopo mikubwa. Hivyo, labda uwezo wa IPTL kuwekeza ulikuwa unapimika hivyo.

Cha kustaajabisha ni kuwa, kwa mujibu wa Taarifa ya CAG: “Jumla ya kiasi cha USD 85,862,022 kati ya USD 105,000,000 ndicho pekee kilichopokelewa na IPTL kati ya mwezi Agosti 1997 na Desemba 1999.” Jambo la kushangaza zaidi ni kuwa wakati wa lililokuwa zoezi la ufilisi wa IPTL mwaka 2012 wadeni wanne “waliojitokeza na kuainisha madai yao ya jumla ya Sh. 321,041,365,000, USD 145,628,784.43 na GBP 1,439,836.50” walikuwa ni pamoja na makampuni mawili ya ujenzi – “Watsila Tanzania Ltd” na “Watsila Netherlands B.V.” Wakati “Maelezo ya Deni” la huyo wa kwanza ni “Mkataba wa Uendeshaji na Ukarabati” ya huyo wa pili ni “Mkataba wa Ujenzi.”

Udadisi wa kina wa mikopo na madeni hayo unaweza kutusaidia kuelewa kwa nini, kwa mujibu wa CAG, wanasheria walioishauri TANESCO walitofautiana kuhusu kiwango ambacho kiliwekezwa na IPTL. Kampuni moja ya wanasheria iliona hivi: “Mapendekezo ya Mkono & Co. Advocates katika kipengele cha 7 na 8 katika taarifa yake kwa Bodi aliishauri TANESCO kuwataka IPTL kufanya marekebisho ya gharama za uwekezaji (Capacity Charges) kwa kuzingatia mtaji wa Shilingi 50,000 na kuanzisha madai dhidi ya IPTL ili kurejesha fedha zilizolipwa zaidi kutokana na kutumika kwa mtaji wa Dola za Kimarekani Milioni 38.16 katika ukokotoaji wa tozo za uwekezaji isivyo sahihi. Pia TANESCO ilishauriwa kutoa tamko la kutokubaliana na tozo hiyo (Invoice Dispute Notice) na endapo hakutakuwa na suluhisho, TANESCO na IPTL wangepaswa kufungua akaunti maalumu ya Escrow kwa haraka kwa mujibu wa Kipengele Na. 6.8 (b) cha PPA.”

Kampuni nyingine ya wanasheria iliona hivi: “Katika uchunguzi wao Hunton and Williams waliainisha kuwa ujenzi wa mitambo ya IPTL kwa kutumia mtaji (Owners Equity) wa TShs 50,000 haileti mantiki katika uhalisia wake kinyume na ilivyoainishwa na Mkono &. Co. Advocates. Vilevile Hunton and Williams ilibainisha kuwa mtaji wa USD 38.16 Milioni uliokuwa ukitumiwa na IPTL katika ukokotoaji wa ‘capacity charges’ haukuthibitika usahihi wake kama ilivyokuwa imeamuliwa katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi ICSID tarehe 12 Julai 2001 (ICSlD 1). Hata hivyo kwa kutolipa gharama za uwekezaji (capacity charges), TANESCO hawakuwa na nafasi ya kushinda katika shauri hilo na hivyo kushauriwa kukaa pamoja na IPTL kujadili na kukubaliana juu ya mtaji halisi uliowekezwa na wanahisa (Owners equity).”

Swali hilo bado linahitaji jibu sahihi: IPTL iliyokopa mabenki mwaka 1997 ilikuwa na mtaji kiasi gani na wanahisa wake – MECHMAR na VIP – waliwekeza mtaji halisi upi? Pia swali la kujiuliza ni kwa nini Taarifa ya CAG, japo haimtaji kwa jina Andrew Chenge kuwa ndiye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, inaonesha kuwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO hakupata jibu kuhusu maombi ya ushauri wa kisheria kuhusu maoni kinzani ya wanasheria hao binafsi waliolishauri shirika hilo umma. Hili ni muhimu maana Chenge ametajwa katika orodha ya waliopata fedha zilizotolewa katika akaunti ya Escrow, tena ‘vijisenti’ vingi sana – Shilingi bilioni 1.6 za Kitanzania.

Hebu turejee nukuu husika ukurasa wa 21 wa Taarifa ya CAG: “Kufuatia maoni ya kisheria ya Mkono & Co. Advocates kutofautiana na maoni ya Hunton and William LLP, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. …. Huysen alimuomba ushauri Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia barua …. ya tarehe 05 Julai 2004 ambapo ushauri wa Mkono & Co. na Hunton and William uliambatanishwa….Kufuatia kutojibiwa kwa barua…ya tarehe 05 Julai 2004 na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. …. Huysen alimuomba Katibu Mkuu Nishati na Madini kupitia barua ...ya tarehe 23 Septemba 2004...kuwasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupata majibu ya Barua ... ya tarehe 5 Julai 2004….Pia Mkurugenzi Mtendaji alimuomba ushauri Msajili wa Hazina kupitia barua…ya tarehe 16 Agosti 2004 kufuatia mgongano huo wa maoni ya kisheria….” Ni nani huyo alikuwa Msajili wa Hazina wakati huo?

Huysen na NetGroup Solutions (Pty) Ltd. yao ya Afrika Kusini walikuwa na matatizo yao ya uendeshaji wa TANESCO yetu na kina Rutabanzibwa wanastahili pongezi kwa (kulazimika) kuwaondoa nchini lakini kwenye hili la kutafuta bila ajizi ushauri wa wenye dhamana ya mali ya umma ni haki yake tumpe heko. Japo Rutabanzibwa ameorodheshwa  katika “Kiambatanisho Na. 1” cha “Mahojiano/Majadiliano yaliyofanyika wakati wa ukaguzi huu” katika Taarifa ya CAG, insha ya taarifa hiyo haisemi kama alitoa maelezo ya kwa nini Huysen hakujibiwa au/na kama hatimaye alijibiwa baadaye. Labda Hansard za mahojiano/majadiliano yake na CAG ina mwanga zaidi. Ila kilichopo kwa sasa kuhusu hilo ndani ya insha hiyo bado ni giza nene maana baada ya hapo kilichofuata ni Escrow.

Insha ya Taarifa ya CAG inasema hivi: “Barua…ya tarehe 06 Desemba 2005 kutoka kwa Mkono & Co. Advocates kwenda kwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini Bw. Patrick Rutabanzibwa ilirejea mazungumzo ya tarehe 05 Desemba 2005 ambapo iliamuliwa kuwa Kampuni ya Mkono & CO. Advocates iandae rasimu ya makubaliano kwa ajili ya ufunguzi wa akaunti ya Escrow.” Wale wanaoamini kuwa ‘njia ya kwenda kuzimu imenakshiwa na nia njema’ wanaweza kusema huko ndiko uamuzi mwema wa kuanzisha akaunti maalumu ya kutuokoa na kadhia ya kuilipa kupita kiasi IPTL unakotupeleka Watanzania. Hapa inabidi tuweke tuo na kurejea maneno haya ya mwandishi mkongwe, Nizar Visram,  katika makala yake ya IPTL haina jipya, tulipaswa kuwa wakali tangu 1994 ya kwenye  gazeti la Raia Mwema: “Mnamo…1994 mkataba wa maelewano (MoU) ulifikiwa na kuthibitishwa na mwanasheria mkuu wa nchi, kuwa ulikuwa mzuri na wa manufaa kwa nchi. Hatukujali tahadhari iliyotolewa na washauri wa TANESCO (kampuni za Acres kutoka Canada na Hunton and Williams kutoka Uingereza) kuwa uwekezaji huo ulikuwa ni kitanzi kwa sekta ya umeme na kwa uchumi wa nchi yetu.”

Kinachoshanganza sana ni kuwa, kwa mujibu wa Taarifa ya CAG, mwanahisa mmojawapo wa IPTL ndiye alikuwa wa kwanza kwanza kutujulisha kuwa kitanzi hicho kinatunyonga. Je, ni uzalendo ulimfanya afanye hivyo? Pengine aliona fursa inayoweza kujitokeza Escrow kutokana na migogoro? Au ni yale yale tu ya kumwona adui wa adui yako kuwa ni rafiki yako kwa kuwa mtasaidiana kupambana na adui wenu mmoja?

Taarifa ya CAG inaelezea hivi ‘kisa mkasa’ hicho cha kustaabisha kwenye ukurasa wa 18: “Ukaguzi umebaini kuwa katika kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO cha tarehe 01 Aprili 2004, TANESCO walifahamishwa na mmoja wa wanahisa wa IPTL, kampuni ya VIP kuhusu mambo kadhaa ambayo yanaashiria kuwa TANESCO inalipa viwango vya ‘tariffs’ vya juu isivyostahili. Baada ya kupata taarifa hiyo, Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO ilianza kuchunguza usahihi wake kwa kuiteua kampuni ya Mkono & Co. Advocates ili kufuatilia taarifa hiyo na kutoa ushauri. Pia Bodi iliwateua (miongoni mwa wajumbe wa Bodi) Bw. Anorld Kilewo, Dr. Enos Bukuku na Bw. B. Mrindoko kuunda kamati maalumu ili kufuatilia kwa ukaribu taarifa hizo.”

Wadadisi wa historia ya uwekezaji nchini Tanzania hawajasahau sehemu hii ya pili ya Azimio la 14 la Bunge Juu ya Mkataba Baina ya TANESCO na RICHMOND DEVEVELOPMENT COMPANY LLC la mwaka 2008: “Aidha, Kamishna wa Nishati, Ndugu Bashir Mrindoko naye achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kumshauri Katibu Mkuu wake mpya kuhusu udhaifu wa Richmond Development Company LLC ambao ulijulikana dhahiri na Wizara mwaka 2004 kwenye Mradi wa bomba la mafuta. Ndugu Mrindoko ndiye aliyeiandikia barua Kampuni hiyo kusitisha Mkataba wake na Serikali mwezi mmoja tu kabla ya mchakato wa Zabuni ya umeme wa dharura haujaanza.” Lakini watu wenye utu wanatuasa kuwa kosa moja lisiwe kisingizio cha kumhukumu mtu kwa kosa lingine. Kwa mantiki hii ya ‘ubinaadamu’, inashauriwa tusimhukumu, anayesemekana ukurugenzi wake ulileta tija na ufanisi TANESCO kuliko wa wengine, kwa sababu tu aliwahi kuhusishwa pamoja na Chenge kwenye kashfa ya Rada badala yake tumpongeze hasa ukizingatia Taarifa ya CAG imemuandika hivi: “Katika vipindi tofauti mwaka 2008, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dr. ldrisa Rashid alifanya mawasiliano mbalimbali na IPTL kuhusiana na madai ya TANESCO kwa IPTL yaliyotokana na kutozwa zaidi kiwango cha tozo ya uwekezaji (capacity charges)”. Ila  Dakta Bukuku ametajwa na kina Chenge kwenye orodha ya waliopokea fedha za Escrow kupitia akaunti ya James Rugemalila wa VIP iliyofunguliwa kwenye Benki ya Mkombozi, kiwango chake nacho si haba – Shilingi milioni  161.7 za Kitanzania. Pia kwa kuwa (bado) hatujui majina yote kabisa ya waliopokea fedha hizo kupitia benki hii ama ile ye Stanbic, mazingira haya ya iliyokuwa kamati maalumu ya kuishauri TANESCO kuhusu IPTL yanaibua maswali mengi kuliko majibu.

Ndio maana inabidi tujiulize sana kwa nini VIP ‘iliitonya’ TANESCO. Swali lingine la kujiuliza tena baada ya taarifa kinzani kujitokeza wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya PAC Bungeni na wa kile kilichoitwa utetezi wa Serikali ni kwa nini miaka 10 baadaye CAG anaelezwa yafuatayo kuhusu jinsi TANESCO ilivyojitokeza kama mmoja wa wale wadai 4 wa IPTL wakati wa jaribio la kuifilisi: “Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO kupitia barua…ya tarche 19 Agosti, 2014 iliyosainiwa na Mwenyekiti wake Jenerali Mstaafu Robert Mboma…kwenda kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilielezea kutokifahamu kiapo cha tarehe 12 Aprili , 2012 kilichotolewa na Bw. Godwin Simba Ngwilimi kwa niaba ya TANESCO kuthibitisha madai ya jumla ya Shilingi bilioni 321. Barua hiyo ilibainisha kuwa deni la TANESCO lililotolewa kiapo halifahamiki kwa Shirika na kwamba kiapo hicho kilikuwa ni matakwa binafsi ya Bw. Godwin Ngwilimi na ushauri wa wataalam wa masuala ya fedha kutoka Castalia LLC ambao walipewa kazi hiyo na Kampuni ya Wanasheria ya Mkono & Co, na kwamba TANESCO hawakuwahi kupokea ushauri rasmi kutoka kwa Castalia LLC kuhusiana na madai hayo kabla au baada ya notisi ya Mfilisi wa Muda. Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO alibainisha kuwa Menejimenti ya Shirika haikuidhinisha suala la Bw. Godwin S. Ngwilimi awasilishe madai yake kwa Mfilisi kwa niaba ya TANESCO. Pia ilielezwa kuwa madai haya yaliyowasilishwa dhidi ya IPTL ni madai ambayo yalikuwa tayari ndio msingi wa shauri la ICSID Na. ARB/10/20 (ICSID 2) ambalo lilikuwa bado halijaamuliwa hivyo TANESCO isingeweza kuwasilisha madai yanayohusu masuala ambayo bado hayajaamuliwa na ICSID.” Sasa aliwezaje kuapa kisheria hivi hivi tu?

Inakuwaje VIP hiyo hiyo iliyowahi kuiomba Mahakama iiweke IPTL iwekwe kwenye ufilisi na kukubaliwa ufilisi wa muda mwaka 2008 ndiyo hiyo miaka 5 baadaye inafanya hiki kinachoelezwa kwenye ukurasa wa 51 wa Taarifa ya CAG: “Katika vipindi mbalimbali kampuni ya IPTL iliwekwa katika ufilisi wa muda na ufilisi kamili, ambapo mnamo tarehe 30 Agosti 2013 VIP Engineering & Marketing kupitia Ngalo &. Co advocates kwa barua Na. NCA/DSM/1332/ 13 baada ya kutangazwa tarehe 26 Agosti 2013, iliwasilisha Mahakama Kuu ya Tanzania ombi la kuondoa shauri la ufilisi wa IPTL.”? Jibu tunalipata katika ombi la tatu kati ya matano iliyoyaomba mahakamani.

Ombi hilo linasomeka hivi kwenye Taarifa ya CAG: “Kwamba Mfilisi wa Muda akabidhi mali zote za IPTL, ikiwa ni pamoja na mtambo wa kuzalisha umeme kwa Pan Africa Power Solutions (T) limited [PAP] ambaye amedhamiria kuwalipa wadai wote halali wa IPTL na kuongeza uwezo wa mtambo hadi kufikia MW 500 na kuuza umeme kwa TANESCO kwa bei ya kati ya senti 6 hadi 8 za Dola za Kimarekani kwa uniti baada ya kuzingatia maslahi ya umma kama ilivyonukuliwa hapa chini: “that the provisional liquidator shall hand over oil the off airs of IPTL including the IPTL Power Plant (the plant) to PAP, which has committed to pay off all legitimate Creditors of IPTL and to expand the plant capacity to about 500MW and sale power to TANESCO at a tariff of between Us cents 6 and 8/Unit in the shortest possible time after taking over in the public interest.”

Utata unazidi kuigubuka jitihada hii pale tunapogundua kuwa miongoni mwa wale ambao walipata fedha zilizotolewa kwenye akaunti Escrow ni Phillip Saliboko ambaye alipata Shilingi milioni 40. 4 za Kitanzania. (Alikuwa) nani huyu? Taarifa ya CAG kwenye ukurasa wake wa 43 inamtambulisha hivi”: “Katika utekelezaji wa majukumu yake, Kampuni ya IPTL imekuwa ikidaiwa na wadai mbalimbali wa ndani na nje ya nchi. Tarehe 16 Machi 2012, Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya Mh. Jaji Kaijage ilitoa uamuzi kwamba kampuni ya IPTL iendelee na ufilisi kamili na kumteuwa aliyekuwa mfilisi wa muda wa IPTL, Bw. Phillip Saliboko Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA kuwa mfilisi kamili (Kielelezo 97). Kufuatia uamuzi huo, Bw. Saliboko alitoa notisi kupitia magazeti mbalimbali kati ya tarehe 3-5 Aprili, 2012 iliyowataka wadai wote wa IPTL kuwasilisha madai na taarifa zao kwake kabla ya tarehe 24 Aprili, 2012 ili kufanikisha zoezi la ufilisi lililotokana na amri tajwa ya Mahakama Kuu ya Tanzania.”

Suala la kuhuishwa huko kutoka kwenye umauti wa kufilisiwa linajitokeza kwa uwazi zaidi ukiyadadisi maelezo kuhusu mdai/mdeni mwingine miongoni mwa hao wadai/wadeni 4 tuliowagusia hapo juu, yaani Standard Chartered Bank Hong Kong (SCBHK). Katika ukurasa wa 45 Taarifa ya CAG inasema kwamba: “Ilibainika pia kuwa IPTL ilikuwa ikifanya marejesho hata baada ya deni kununuliwa na SCBHK. Kwa maelezo ya SCBHK katika kipindi cha Novemba 2005 mpaka Aprili 2007, IPTL ilikuwa ikifanya malipo moja kwa moja kwa SCBHK. Hili linathibitika katika barua ya ….ya 03 Februari, 2014 kwenda kwa Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, iliyosainiwa na Dr. Magesveran Subramaniam Mkurugenzi wa Uendeshaji na Bw. Joseph Makandege Mwanasheria wa IPTL, ilieleza kwamba hadi kufikia mwaka 2007 IPTL ilikwishalipa jumla ya kiasi cha Dola za Kimarekani 58.69 milioni, ambapo kati ya hizo Dola za Kimarekani 20 milioni zililipwa kwa SCBHK….Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mh. Jaji Frederick Werema pamoja na mambo mengine kupitia barua…ya tarehe 2 Oktoba, 2013 kwenda kwa Katibu Mkuu Hazina Dr. Servacius Likwelile akizungumzia deni la SCBHK alibainisha kuwa madai ya SCBHK hayana athari yoyole kwa Serikali baada ya uamuzi wa kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya Escrow kwenda IPTL, kwa msingi kwamba IPTL ni Kampuni iliyobaki kuwa hai. Hivyo SCBHK wanaweza kuendelea na madai yake kwa IPTL kama wadeni wengine.”

“Baada ya kuhakiki nyaraka za deni la SCB Hong Kong nchini China tarehe 14 Septemba, 2014” Taarifa ya CAG inasema kuwa “ilibainika kuwa SCB HK ilinunua deni hilo mwezi Agosti 2005” na kwamba “Hati halisi ya hisa saba (7) za Mechmar ambazo pia zilitumiwa kama dhamana ya mkopo ziliwasilishwa na kuhakikiwa.” Hivyo basi haishangazi kuiona Taarifa ya CAG nayo ikitoa pendekezo hili kwenye ukurasa wa 49 linaloonesha uhai wa IPTL na si wa PAP: “Ni vyema SCBHK ikafuatilia ulipwaji wa deni lake kutoka IPTL ambaye ndiye mdeni wake, kwa kuwa baada ya hukumu ya tarehe 5 Septemba 2013 ya Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo IPTL ilirejeshwa kuwa kampuni hai.” Sasa kwa nini kampuni iliyo(kuwa) hai iingie kivingine kwenye Escrow?

Tukirejea majina yetu ya mfano wa kutusaidia kuilewa ‘Escrowgate’, tujiulize ni nini hasa kilimfanya Chaurembo (BOT) wetu atoe hela za Escrow kwa mtu ambaye kwa jina siyo Chaupele (TANESCO) wetu wala siyo Chausiku (IPTL)? Kwa nini PAP ndiye alipwe na siyo IPTL kama kweli kulikuwa na suluhu na TANESCO? Ilikuwaje jitihada zote zile, udhibiti wote ule, mapambano yote yale na dhamana zote hizi zilizobainishwa kimamlaka na kimadaraka katika ukurasa wa 11 wa Taarifa ya CAG zishindwe kabisa kuzuia utoaji huo wa fedha uliofuatiwa na ugawanaji wa pesa nyingi sana na kwa kasi mno uliojumuisha watu wenye dhamana kubwa za mali ya umma wa Watanzania: “Kipengele Na 4.1 cha Makubaliano ya Escrow kinaipa mamlaka Benki Kuu kuwa mtoaji pekee wa fedha katika akaunti hiyo. Kadhalika Benki Kuu iliwajibika kutoa taarifa kila robo mwaka kwa pande zote za makubaliano kuhusiana na hali ya akaunti katika kipindi husika kama ilivyoanishwa katika Kipengele Na. 5. 3 na 5.4 cha Makubaliano ya Escrow. Kipengele Na. 7. 7 cha Makubaliano ya Escrow kinaeleza kuwa iwapo wakala wa Akaunti ya Escrow kwa nia njema asipokuwa na uhakika kuhusu upande unaostahili kulipwa fedha kutoka kwenye Akaunti ya Escrow kutokana na mgogoro baina ya pande hizo, atasubiri hukumu ya mwisho ya msuluhishi itakayomuelekeza upande stahili wa kulipwa fedha hizo ama makubaliano ya kimaandishi baina ya pande husika”?

 Pamoja na maelezo mengi yaliyotolewa na vyanzo mbadala mabarazani, mitandaoni na mitaani, wadadisi wa wawekezaji wakubwa tunaona kuwa jibu limejifichaficha katika maelezo haya yaliyopo kwenye ukurasa wa 15 na 16 wa Taarifa ya CAG: “Baada ya kupokea taarifa ya Stanbic tarehe 28 Novemba, 2013, Bw.Harbinder Singh Sethi alimjulisha Gavana Prof. Benno Ndulu kuwa afanye malipo husika kupitia akaunti za PAP zilizofunguliwa tarehe 28 Novemba 2013…. Baada ya Bw. Harbinder Sethi kuiandikia BoT kufanya malipo katika akaunti za PAP badala ya zile za IPTL, Mkurugenzi wa Fedha wa Benki Kuu Bw. J.R Angelo kupitia dokezo sabili katika ukurasa (folio) 12 aliomba muongozo kutoka kwa Naibu Gavana - FSD Bw. L.H Mkila na Mwanasheria wa Benki juu ya athari za kisheria endapo Benki Kuu ingelipa fedha husika katika akaunti zilizobadilishwa. Mwanasheria Bw. Mustafa Ismail alitoa muongozo juu ya agizo la Mahakama la tarehe 5 Septemba 2013 linaloelekeza kuwa ‘all affairs of IPTL should be handed over to PAP’ pamoja na stahili za IPTL katika akaunti ya Escrow. Pia alibainisha kuwa maelekezo ya malipo (payment instructions) husika yametolewa na IPTL hivyo ni vyema Benki Kuu ikafuata maelekezo ya
mwisho ya IPTL.”

Wadadisi tunashawishika kuona kuwa si kwamba ndugu Angelo tu alitumia taaluma yake ya masuala ya kifedha kuhisi – kama sio kubaini – kuwa kuna tatizo la kisheria katika kulipa fedha katika akaunti zilizobadilishwa kivile, bali pia alihisi/alibaini kuna tatizo katika kulipa fedha katika akaunti zilizofunguliwa ghafla kiasi hicho. Hapa uchambuzi wa mwachano/mpishano wa tarehe nao ni muhimu sana. Ukurasa wa 14 wa Taarifa ya CAG ambao inasemekana ni miongoni mwa kurasa zilizonyofolewa wakati kulipokuwa na jaribio la kuivujisha Bungeni Dodoma unamalizia na aya hii: “Kwa mujibu wa makubaliano ya kuhamisha fedha za Escrow yaliyoingiwa baina ya IPTL na Wizara ya Nishati na Madini tarehe 21 Oktoba, 2013 ilikubalika kuwa malipo yafanyike kupitia akaunti iliyoanishwa katika makubaliano hayo kama ifuatavyo:” Kisha kabla ya kueleza jina la benki – “UBL Bank (Tanzania) Ltd” – na nambari mbili za akaunti, ukurasa unaofuatia unamtaja “Mlipwaji” kuwa ni  “Independent Power Tanzania Limited (IPTL) C/o Pan Africa Power Solutions (T) Limited.” Kwa nini mlipwaji ilikuwa awe na “C/o”, yaani, ‘kupitia kwa’? Swali hili tutalijibu tutakapopitia ‘ufilisi’ na ‘uhuishaji’ wa IPTL.

Kwa sasa swali la kujiuliza ni kwa nini, kwa mujibu wa Taarifa ya CAG, takribani mwezi mmoja baadaye, yaani, “Tarehe 25 Novemba, 2013 Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu kupitia barua Kumb Na. NC.53/135/068/11/14 kwenda kwa Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL Bw. Harbinder Singh Sethi aliomba Taarifa za kibenki za IPTL ili kufanya malipo ya fedha za Escrow”? “Kupitia mahojiano,” CAG anatutaarifu, “Gavana Prof. Benno Ndulu alibainisha kuwa Benki ilihitaji maelekezo ya mlipwaji ili kufanya malipo husika.” Hivyo,  “Kwa mujibu barua ya tarehe 25 Novemba, 2013 Kumb Na. IPTL/BOT /001/2013 Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL Bw. Harbinder Singh Sethi alimuandikia Gavana wa Benki Kuu akiomba kuilipa IPTL fedha kutoka akaunti ya Escrow kupitia akaunti zilizoainishwa katika Makubaliano ya kuhamisha fedha baina ya Wizara na IPTL ya tarehe 21 Oktoba, 2013 ambayo yaliwasilishwa kwake. Pia alithibitisha kushiriki kikao cha tarehe 26 Novemba 2013 kilichoitishwa na Gavana.”

Sasa ikawaje tena siku tatu baadaye yanatokea haya yafuatayo yaliyomfanya hata ndugu Angelo aonekane walau akiliishi jina lake lenye maana ya ‘malaika’ kwa kuomba muongozo wa kisheria kutoka kwa wenzake wa BOT: “Baada ya kupokea taarifa ya Stanbic tarehe 28 Novemba, 2013, Bw. Harbinder Singh Sethi alimjulisha Gavana Prof. Benno Ndulu kuwa afanye malipo husika kupitia akaunti za PAP…zilizofunguliwa tarehe 28 Novemba 2013”? Kwa nini kwa ghafla hivyo hata jina la akaunti linabadilika na kuwa “Jina la akaunti Pan Africa Power Solutions (T) Ltd”? Udhibiti ule ukalishindwa hili?

Chausiku aliyekuwa IPTL akawa PAP au IPTL amekuwa huyo huyo PAP? Chaurembo – BOT – aliwezaje kumlipa ‘Chausiku II’ katika mazingira hayo tata ya kibenki/kifedha hata kama Chaupele – TANESCO – hakuhoji mabadiliko hayo ya ghafla? Iliwezekanaje?

Sasa tujikite tena kwenye suala la ‘uhai’ wa IPTL ili tuweze kujibu maswali hayo. Moja ya kurasa muhimu katika hili ni ule ule wa 14 wa Taarifa ya CAG ambao unasemekana ulinyofolewa – unasema yafuatayo mara tu baada ya kueleza kuwa “Gavana wa Benki Kuu, Prof. Benno Ndulu kupitia barua Kumb. Na. AC. 53/195/01 tarehe 24 Oktoba, 2013 kwenda kwa Katibu Mkuu Hazina, aliishauri Serikali kupata kinga kutoka IPTL dhidi ya madai yanayoweza kujitokeza baada ya fedha katika akaunti ya Escrow kulipwa”: “Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini alimwandikia Bw. Habinder Sigh Sethi Mwenyekiti na Mtendaji wa IPTL barua yenye Kumb. Na.SBD.88/147/01/4 ya tarehe 20 Septemba 2013 kumtaka kuthibitisha umiliki wake wa asilimia 70 na kutoa kinga kwa Serikali, Benki Kuu na kwa TANESCO…. Kupitia kikao cha tarehe 8 Oktoba 2013 TANESCO na IPTL walikaa na walikubaliana kuhusu madai ya IPTL kama ilivyonukuliwa hapa chini….”

Madai hayo yaliyonukuliwa kwa Kiingereza ni hayo hapo mbele yakimaanisha, kwa tafsiri yetu nyepesi ya kilei, kuwa fedha katika akaunti ya Escrow zitolewe na kupewa IPTL haraka iwezekanavyo ili IPTL ishughulikie masuala ya wadeni/wadai wake halali kwa mujibu wa agizo/hukumu ya Mahakama Kuu (Mh. Utamwa J.) ya tarehe 5 Septemba 2013. Malipo yote yaliyosalia yanayostahili kulipwa IPTL yalipwe kwa mujibu wa muda uliopendekezwa humu hapo juu ili kuiwezesha IPTL kupanga upya majukumu yake mengine: “Monies in the Escrow Account be released to IPTL as soon as possible to enable IPTL sort out its legitimate creditors as per the order of the High Court (Hon. Utamwa J.) dated 5 September, 2013. All other outstanding amounts payable to IPTL be paid in accordance with the timelines proposed herein above to enable IPTL restructure its other obligations.”

Taarifa ya CAG inaendelea kwa kusema hivi katika ukurasa huo: “Mnamo tarehe 27 Oktoba 2013, IPTL ilitoa hati ya kinga dhidi ya madai yoyote yanayoweza kujitokeza kwa Serikali na Benki Kuu kuhusiana na fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow mara baada ya fedha hizo kulipwa kwa PAP. Hati hiyo ilisainiwa na Bw. Harbinder Singh Sethi Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu na kushuhudiwa na Bw. Joseph Makandege Katibu na Wakili Mkuu wa Kampuni ya PTL.” Sasa hiyo kinga inatoka kwa IPTL au ya PAP ama kwa wote?

Hatuwezi kuhitimisha udadisi huu bila kugusia kile tukionacho na wale tuwaonao kwenye suala la kodi. Kuna mstari mwembamba kati ya kukwepa kodi (tax evasion) na kusamehewa kodi (tax exemption) achilia mbali kudanganya kodi (tax fraud). Ukurasa wa 24 wa Taarifa ya CAG ambao nao unasemekana ulinyofolewa ni somo tosha kuhusu mistari hii myembamba. Tunaunukuu wote hapa na hitimisho lake lililopo Ukurasa wa 25 ambalo kwa kiasi kikubwa ni muhtasari-hitimishi kuhusu kile kilichojiri katika Escrow:

“Katika kikao hicho [“cha dharura tarehe 19 Septemba 2013”], Bodi ya TANESCO ilikubaliana na ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ulioitaka TANESCO na IPTL kukaa na kutatua madai yanayohusu akaunti ya escrow na kubainisha kiasi kinachostahili kulipwa kwa pande husika. Baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO Jenerali Mstaafu Robert P. Mboma allmwandikia Katibu Mkuu wa Nishati na Madini barua…ya tarehe 19 Septemba 2013 akibainisha kuwa TANESCO itafuata maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kwamba washirika wa akaunti ya Escrow watakaa kwa pamoja kutatua mgororo wa tozo ya gharama za uwekezaji (Capacity charges) ili kubaini kiasi kinachopaswa kurejeshwa TANESCO na kile kinichostahili kulipwa IPTL. Hivyo Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO ilitoa mchanganuo wa madai yaliyopaswa kuhakikiwa kwanza ndipo yalipwe kwa IPTL... Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini kufuatia barua ya IPTL ya kudai kulipwa zaidi ya kiasi kilichokuwemo katika akaunti ya escrow, alimjulisha Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Felchesmi Mramba kuhusu madai ya IPTL kupilia barua…ya 9 Oktoba, 2013 na kuagiza TANESCO kufanya kikao na IPTL ili kujadili madai hayo na kuwa uamuzi utakaotokana na majadiliano hayo utasaidia utolewaji wa fedha katika akaunti ya Escrow....TANESCO na IPTL walikaa katika kikao cha tarehe 8 Oktoba 2013 na kukubaliana kuhusu madai ya IPTL ya USD 79,049,724.50... Katika kikao hicho TANESCO iliomba kuondolewa kwa kiasi cha USD 33,564,004.53 ambacho kilikuwa ni riba na adhabu itokanayo na malimbikizo ya tozo ya gharama za uwekezaji. IPTL ilikubaliana na ombi hilo endapo TRA ingeisamehe kodi ya kiwango sawa na hicho. Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Jenerali Mstaafu Robert Mboma kupitia Barua…ya tarehe 9 Oktoba 2013 aliijulisha Wizara kuwa IPTL ingeidai TANESCO kiasi cha USD 45, 485, 719.97 (endapo TRA itasamehe kodi kiasi cha USD 33, 564,004.53) ama USD 79,049,724.50 (endapo hakutakuwa na msamaha wa kodi) zaidi ya kiasi kilichopo katika akaunti ya Escrow ya Tegeta…. Baada ya kupokea mapendekezo ya Bodi ya TANESCO kuwa fedha katika akaunti ya Escrow zilipwe kwa IPTL, tarehe 21 Oktoba, 2013 Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Bw. Eliakim Maswi pamoja na Mwanasheria wa Wizara hiyo Bi. Salome Makange kwa niaba ya Serikali waliingia makubaliano na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji Bw. Harbinder Singh Seth na Mwanasheria wa IPTL Bw. Joseph Makandege juu ya utolewaji wa fedha katika akaunti ya Escrow (Agreement for delivery of funds to Independent Power Tanzania Limited (IPTL)”

Kuhusu Mama Profesa wetu mpendwa aliyetuongoza kwa ujasiri mkubwa katika harakati za Baraza la Wanawake (BAWATA) dhidi ya ukiritimba wa dola hatuna mengi ya kudadisi zaidi ya kumnukuu tena Nizar Visram: “Hawezi waziri kuchota dola milioni moja kisha akasema amepewa zawadi au msaada wa kirafiki au kibanadamu tu, hasa wakati waziri huyo ana dhamana ya kugawa viwanja kwa wawekezaji.”

Msemo kuwa kustaafu si kuchoka una nafasi kubwa katika nchi yetu ambayo bado haijafanikiwa kuwaandaa watu wengi wa kutosha kuchukua nafasi za wastaafu wenye utaalamu adimu. Lakini pamoja na kuwaenzi na kuwaheshimu wastaafu wetu, wakiwemo wale walioonyesha ujasiri mkubwa kwa kumng’oa Nduli Idi Amin aliyeivamia nchi yetu, kwa kuhakikisha wanapata shughuli ya kufanya uzeeni yasitufanye tufumbie macho kile ambacho wadadisi tunakiita dhana ya mgogoro wa kimaslahi katika mapana yake. Hili linawahusu pia watumishi wa umma na wanasiasa wakiwamo wale ambao wanaona wanaweza kuchanganya biashara na siasa na kuwa waadilifu badala ya mafisadi. Ni vigumu sana kutogonganisha maslahi, hata mtu uwe na nia njema kiasi gani, ukiwa kwenye wa bodi ya ukurugenzi wa shirika la umma na wakati huo huo upo kwenye bodi ya ukurugenzi wa kampuni binafsi kama mabenki na mashule huria hasa kunapokuwa na miingiliano ya uwekezaji kama iliyopo nchini. Ni heri tuwe kumoja – umma au binafsi.

Haya ndiyo tunayoyaona na hao ndio tunaowaona kwenye Taarifa ya CAG. Ni masuala na maswali yanayoumiza kichwa na yanayoutesa moyo. Ndio maana wadadisi wengi wa wawekezaji wanaogopa kufa kihoro au kifisadi. Unaoitwa ujasiri wa ufisadi una(tu)tisha.

Nani atatuokoa? Kuna mwenye ujasiri wa uwanamapinduzi? Yupo wa kujitoa mhanga? 

1 comments:

mtengera June 8, 2015 at 8:44 PM  

hey, they required red charge.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP