Sunday, December 28, 2014

Unapomwacha Adui yako Fisadi Nyuma

Unapomwacha Adui yako Fisadi Nyuma

Chambi Chachage

Filamu ya Shaka Zulu ina ujumbe muhimu katika vita dhidi ya ufisadi. Kama tulivyoona katika makala ya Tunahitaji Viongozi Wenye U Tatu, tulipopata Uhuru tuliambiwa kuwa maadui zetu wakuu wa maendeleo walikuwa watatu – ujinga, umaskini na maradhi – ila baadaye tukajulishwa kuwa ameongezeka wa nne,yaani rushwa. Sasa rushwa imekubuhu na kuwa ufisadi ambao kwa hakika ni adui mkuu maana anakuza hao wengine watatu.

Katika filamu hiyo tunamuona Shaka akisema hivi: “Never leave an enemy behind or it will rise again to fly at your throat.” Maneno haya, kwa tafsiri ya haraka haraka, yanamaanisha: “Usimwache adui yako nyuma la sivyo ataibuka tena na kukurukia akukabe koo.” Shaka alisisitiza pia kuwa hiyo ndiyo pekee ya kumkabili adui.

Tatizo kubwa katika vita dhidi ya ufisadi ni kuwa maadui, yaani mafisadi, huachwa nyuma hivyo huibuka tena na tena kutukaba koo. Unakuta mtuhumiwa yule yule wa kupokea fedha za ufisadi wa rada ni mtuhumiwa huyo huyo wa kupokea fedha za ufisadi wa Escrow. Na unakuta mtuhumiwa yule yule wa ufisadi wa mgodi wa Kiwira ni mtuhumiwa huyo huyo wa kupokea fedha za kifisadi za Escrow. Tunamuacha tu.

Wahenga walinena, “akuanzaye mmalize”.  Na kuna njia nyingi za kummaliza adui aliyeanza kukufanyia ufisadi unaokuongezea ujinga, maradhi na umaskini pamoja na ufisadi zaidi. Katika nchi inayofuata utawala wa sheria, njia kuu ni kumshitaki na kumuadhibu vilivyo pale inapothibitika pasipo shaka kwamba amefanya ufisadi.

Lakini, je, ukimuadhibu kwa faini na kumfunga jela si atakulipa tu vijisenti na atatoka na kukukaba koo tena? Siyo rahisi hasa kama adhabu hiyo imejumuisha kumfilisi mali zake na kuvunja mtandao wa ufisadi unaoweza kumwezesha kulipiza kisasi. Ni vigumu kama utakuwa umemkata mabawa yanayoweza kumfana akurukie tena na kukukaba koo.

Si anyongwe? Hapana. Ya Uchina tuwaachie Wachina. Tuendelee na harakati zetu za kuondokana na adhabu ya kifo inayoondoa haki ya msingi kabisa ya mwanadamu yoyote yule, yaani kuishi. Tujikite kwenye kutunga na kutekeleza sheria zenye adhabu kali zaidi dhidi ya ufisadi, yaani, zitakazotufanya tuogope ufisadi kuliko hata tunavyoogopa kifo.

Mwanakijiji ameliweka hivi: “Kashfa ya akaunti ya Escrow ni miongoni mwa kashfa zinazotokana na watawala kuwadhania, kuwachukulia na kuwatenda Watanzania kwa ujinga. Kashfa kama hizi zinaishia mawaziri kung’oka, watu kushtakiwa na hata baraza la mawaziri kuvunjwa lakini chama kilichounda Serikali kinaendelea kwa kuruhusiwa kuingiza sura mpya. Tungekuwa na mfumo wa kumwajibisha Rais pale mawaziri wake wanapovurunda basi Baraza la Mawaziri linapovunjwa na yeye mwenyewe anaondoka nao na haruhusiwi kugombea na anapoteza mastahili yote ya ustaafu! Wangekuwa wanaogopa hata kudokoa ndotoni! Hata mawaziri wanaojiuzulu wangekuwa wananyang’anywa mafao yao na mali yote yenye utata kufilisiwa. Wangeona hela za umma chungu!” Hakika ufisadi ungegeuka shubiri ambayo tusingetaka kuichukua pima.

Ujumbe huo wa Shaka unawahusu pia wanasiasa na wanaharakati wapambanaji ambao aghalabu wanawaonea huruma baadhi ya mafisadi na kuwaach(i)a  kutokana na sababu mbalimbali. Kushughulikia baadhi ya mafisadi na kuwaachia wengine, kwa kisingizio kuwa makosa au maslahi yao ni madogo zaidi na/ama walijitahiditahidi kuzuia ufisadi ila wakazidiwa nguvu na wakuu wao wa kazi hivyo ufisadi huo ukatokea, ni kumwacha adui nyuma na kumpa nafasi ya kujipanga upya ili je kukukaba koo tena. Ni kubariki ufisadi.

Mafisadi wao hawana hulka ya kumuacha adui nyuma. Ndio maana mfuatiliaji mmoja wa ufisadi aliniasa hivi kwa Kiingereza, “it pays to watch your back.” Ila hatutakuwa na haja tena ya kutazama tazama nyuma kwa hofu na sisi tukiacha kuwaacha nyuma mafisadi.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP