Wednesday, December 31, 2014

Wasomi Wanapowagombania Wakulima

Dastan Kweka:

Niliposoma mfululizo wa hii makala katika gazeti la Raia Mwema (katika awamu mbili), niliifurahia na kukereka. Niliifurahia kwa sababu inagusa jambo ambalo ni la msingi sana na lenye athari kubwa kwa watu masikini wa nchi hii. Na ililichambua kwa kina kwa kutazama historia na mifumo iliyochagiza mabadiliko kwa karne kadhaa. Jambo hilo ni mustakabali wa wakulima wadogo. Hata hivyo, kwa kiasi nilikereka pia hasa kutokana na namna vipengele kadhaa vilivyojikita katika fikra zilezile za kukosoa bila kuangalia mienendo mipya, kujifunza na kupendekeza mbadala.

Siku chache baada ya kusoma Makala ya ndugu Sabatho Nyamsenda, nilisoma pia makala ya Paul Sarawati (zote katika gazeti la Raia Mwema). Makala ya Ndugu Sarawati ilikua na kichwa, Wakulima Kilimanjaro wageukia kilimo cha parachichina iliandikwa kwa namna ya kumsifu muwekezaji mkubwa aliyeko sanya Juu (Wilaya ya Siha) na namna aalivyowawezesha wakulima wadogo kugeukia kilimo cha parachichi na kupata faida. Sikufurahishwa na makala hii hasa kutokana na kuwa nimeishi na kukulia Kilimanjaro na nimekuwa nikifuatilia mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea katika maisha ya wakulima wadogo mkoani humo na nafasi ya wawekezaji wakubwa katika mabadiliko hayo. Hivyo niliamua kuandika kidogo kuhusu suala hilo katika blogu yangu (Unaweza kufuata link hiyo na kusoma jibu langu fupi kwa makala hiyo). Hata hivyo sikumtumia mwandishi husika.

Sasa nitaenda moja kwa moja kwenye baadhi ya mambo ambayo yamejitokeza katika makala hii ya Ndugu Sabatho na ambayo nina mtazamo kinzani dhidi yake.

Kuhusu Kurasimisha  Umiliki wa Rasilimali (Hasa Ardhi)

Kuhusu hili mwandishi anaandika, “Hapa tunapaswa kujifunza kwamba wale wanaopigia debe urasimishaji wa rasilimali za wanyonge (mfano: kutoa hati za ardhi kwa wakulima) huwa la lengo la kurahisisha uporaji wa ardhi hiyo.”

Mimi nafanya kazi katika taasisi ambayo mojawapo ya miradi yake ni kuwawezesha wakulima kurasimisha umiliki wa ardhi wanayolima kwa lengo la kuikinga dhidi ya uporaji, kupata fidia stahili ikiwa inatwaliwa au kuwawezesha kutumia kupata mikopo ya kujiinua, pale inapobidi. Ingawa fikra za kina Hernando De Soto zilitawaliwa na haja ya kuwawezesha wakulima wadogo ‘kuchuma faida za uliberali mamboleo’, mapungufu yamekuwa makubwa hasa ya uporaji wa ardhi baada ya wakulima kuchukua mikopo na kushindwa kulipa (kama mwandishi alivyotoa mfano wa India). Hata hivyo, sisi katika NGO ninayofanyia, kwa kujifunza kutokana na mapungufu hayo, tunawawezesha wakulima kupata hatimiliki na kisha kuwahimiza kuanzisha SACCOS na VICOBA na kuendelea kujiinua wenyewe badala ya kuchukua risk kubwa kwa kukopa kwenye taasisi kubwa za fedha ambazo nyingi zina riba kubwa na siyo rafiki kwa mkulima mdogo. Kimsingi, faida za hatimiliki kwa wakulima wadogo ni zaidi ya hoja ya mikopo (hasa kutoka katika taasisi kubwa za fedha) na mara zote tunawaelimisha wakulima wadogo tunaofanya nao kazi kuhusu hili suala. Kwa mantiki hii, hilo tangazo la mwandishi kwa wakulima wadogo kuwa “wale wanaopigia debe urasimishaji wa rasilimali za wanyonge (mfano: kutoa hati za ardhi kwa wakulima) huwa la lengo la kurahisisha uporaji wa ardhi hiyo” ni upotoshaji na lina mapungufu makubwa hasa kwa vile ni jumuishi, lina mtazamo finyu na hasi kuhusu urasimishaji wa umiliki wa ardhi na linakosa kujadili mifano chanya (best practices) ya utekelezaji wa wazo hilo.

Nafasi ya NGOs katika Kuwaunganisha Wanyonge

Katika hili mwandishi anaandika;

“Kazi ya wanyonge kuungana isiachwe mikononi mwa mabwanyenye-uchwara kupitia vyama vya siasa au asasi zisizo za kiserikali (NGOs). Hawa wote, katika nafasi zao, ni watumishi wa mabepari wa kimataifa. Hata kama hapa na pale huonekana kuwa na ugomvi, ugomvi huo huwa haulengi katika kuubomoa ubepari. Wote hawa wanapigania nafasi ya kuwa mawakala wema wa mfumo wa kibepari. Ndio maana, hapa nchini, hakuna chama cha siasa chenye nia ya dhati ya kuleta mfumo mbadala, na harakati zao zinalenga kuepusha mapambano ya kitabaka katika jamii.”

Katika muda mfupi niliofanya kazi katika NGOs na uzoefu kwenye taasisi nyingine (zikiwemo za tafiti za kilimo), hakuna mahali ambapo pametawaliwa na mijadala inayohusu wanyonge na namna ya kuwasaidia (au kuwawezesha kujisaidia) kuliko kwenye NGOs. Tatizo kubwa ni kuwa wigo wa mijadala hiyo unadunishwa na namna NGOs zinapata fedha (funding system) ambayo pia hutegemea sana malengo ya wanaoitoa. Tunapoona maandamano ya wanaharakati Davos, Copenhagen na kadhalika, dhidi ya mikutano ya wakubwa na ajenda zao, lengo ni kuwa mawakala wema wa mfumo wa kibepari? Nafikiri, badala ya kurejea ukosoaji jumuishi wa kiwango hiki, ni vema kujikita katika mawazo mbadala ya namna gani ya kutatua matatizo ya kimfumo katika NGOs ili taasisi hizi ziweze kuchangia vyema katika kuung’oa mfumo kandamizi. Mchango wa taasisi hizi (hasa zile zenye kufanya kazi sawasawa) katika kupigania haki za kiraia (Civil rights), kupigania uwajibishwaji wa makampuni makubwa kama Monsanto, Shell, BP na kadhalika ni mkubwa.

Kiitikadi, NGOs ni sehemu ya uliberali-mamboleo na kimsingi kwa kiasi pia zimechangia kunawiri kwa mfumo. Lakini kama siyo jukumu letu kama wasomi kufikiri namna ya kuzibadili kiitikadi, mbadala wake ni upi? Tayari tumeshaona nyingi zikipigwa vita na dola kwa sababu ya misimamo yake na hasa kwa kupinga ukandamizaji na dhuluma. Tayari kuna maungio.

Lugha ya Mwandishi

Mimi ni mfuasi wa sera za Kisoshalisti (siyo ujamaa kama tunavyoujua). Hata hivyo, sina hakika ni kwa kiasi gani uandishi wa kebehi kwa wadau wengine unasaidia katika kuwabadilisha au kuwafanya waungane na wale wanaoonekana wanaendesha ‘harakati safi’ za kubomoa mfumo. Mfano mimi ninayetumia muda wangu mwingi vijijini nikijadiliana na kupanga mikakati na wakulima wadogo namna ya kuwajibisha makampuni makubwa ya madini yanayovuna utajiri katika ardhi yao bila kurejesha hata chembe, naweza kuwaita walioko vyuo vikuu wakifundisha (kama mwandishi wa hii makala), kuwa ni ‘watu wenye anasa ya kubwata bila kutenda’ - (Armchair advisors). Ndivyo vita vya maneno vinavyotumika. Kumbe kwa kiasi kikubwa wadau hawa wanategemeana. Kuna haja ya kuwa na mjadala mpana wa namna ambavyo lugha hizi na ‘kebehi za kisomi’ zinavyojenga kuta badala ya madaraja katika kufikia malengo mbalimbali, siyo tu ya kubomoa mfumo kandamizi wa kibepari.

Sabatho Nyamsenda:

Kwanza nikupatie pole kwa kukereka na lugha ya mwandishi. Yumkini ndilo lililokuwa lengo lake: kuwakera mabwanyenye na vijibwa vyao. Sasa wewe kama ulivyosema, sio bwanyenye. Lakini sina hakika kama sio mtumishi wao. Lugha ya mwandishi huwakera pia hata wasomi wenzake katika vyuo vikuu (soma http://www.raiamwema.co.tz/wasomi-kaeni-kando-wanyonge-shikeni-hatamu na hapa pia http://www.raiamwema.co.tz/elimu-yetu-izalishe-wasomi-wa-umma-si-makahaba-wa-kitaaluma). Huwakera wanasiasa, huwakera mawakala wengine wa ubepari, n.k. Kwa ufupi, wote hukereka na hawapendezwi na lugha ya mwandishi. Sio lengo la mwandishi hata kidogo kukufurahisha wewe, kwani hajioni kama mtumishi wako.

Tazama ilipo tofauti yako na mwandishi:
WEWE na NGO yako mnajiona kama wakombozi wa wanyonge. Mmewaona kuwa hawajiwezi, mbumbumbu, na hivyo mmejibatiza wajibu wa “kuwawezesha” na “kuwasaidia”.

Ngoja nisijeonekana nakubandikia maneno mdomoni. Hivyo nitakunukuu:

“Katika muda mfupi niliofanya kazi katika NGOs na uzoefu kwenye taasisi nyingine (zikiwemo za tafiti za kilimo), hakuna mahali ambapo pametawaliwa na mijadala inayohusu wanyonge na namna ya kuwasaidia (au kuwawezesha kujisaidia) kuliko kwenye NGOs”.

Sasa, hapo ndipo unapotofautiana na mwandishi. Na nikiri kabisa kuwa una haki ya kukereka.

Yeye mwandishi hata alipohudhuria kongamano husika, alijishusha, akajinyenyekeza na kusema kuwa amekwenda “kujifunza”. Eti anawaambia wanyonge kuwa wao ndio chanzo cha maarifa! Ujumbe wa mwandishi ni kwamba wanyonge watajikomboa wenyewe. Kwa bahati nzuri, kauli-mbiu ya MVIWATA ni “Mkombozi wa Mkulima ni Mkulima mwenyewe”. Mrengo huo wa wanyonge kujikomboa wenyewe unatumika sana katika mapambano ya nchi za Amerika ya Kusini.

Mwandishi huwaambia wanyonge kuwa kutokana na historia ya mapambano yao ni kosa kubwa sana kukasimisha mamlaka ya kujikomboa kwa “wasomi” kama yeye, wanasiasa, wana-ma-NGO kama wewe, kwani mwisho wa siku huishia kuwauza kwa mabepari.

Lakini huwakumbusha pia kuwa kabla ya majilio ya vyama vya siasa, vyuo vikuu na NGOs wanyonge wenyewe walikuwa wakipambana. Mapambano yalianza tangu siku ya kwanza pale wanyonge walipokutana na mkono wa damu wa ubepari kupitia biashara ya utumwa.

Nadhani hiyo inafafanua walau jambo moja katika majibu yako. Mengine yatafuata, kukiwa na haja ya kufanya hivyo.

CHANZO:

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP