Sunday, January 4, 2015

Escrow-Kwa nini Haiundiwi Kamati Teule ya Bunge?

Mjadala mkali Bungeni kuhusu Escrow na mijadala inayoendelea mitandaoni na mitaani inadhihirisha kuwa bado kuna maswali mengi (pengine) kuliko majibu. Pamoja na jitihada kubwa zilizofanywa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambazo hakika zinastahili pongezi kubwa kutoka kwa wapinga ufisadi kote nchini, bado kuna utata mwingi. Kwa mfano, kwenye Mtandao wa Wazi wa Wanazuoni, Mwenyekiti wa PAC amenukuliwa akisema hivi: "Mpaka sasa hakuna anayejua 50% ya PAP chini ya Simba Trust ni Mali ya nani."

Katika kujiuliza "Kwa nini Haiundwi/Haikuundwa Kamati Teule ya Bunge Kuhusu Escrow?" Mdadisi anahoji: "Hayo maswali mengine mazito ambayo majibu hayajapatikana kupitia CAG na PAC nani atayajibu? Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB)? Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP)?" Bahati nzuri Hansard ya Majadiliano ya Bunge (Mkutano wa 15 Kikao cha 22) ya Mei 30, 2014 inayopatikana katika kiunganishi hiki cha Tovuti ya Bunge http://polis.parliament.go.tz/PAMS/docs/HS-15-22-2014.pdf inatoa mwanga mkubwa wa kusaidia kupata majibu ya maswali hayo.

Zifuatazo hapo chini ni baadhi ya nukuu kutoka katika Hansard hiyo. Tukumbuke kuwa mjadala huo ulitokea katika muktadha wa uwasilishaji wa Hoja ya Serikali kuhusu Makadirio ya Matumizi ya kwa Mwaka wa 2014/2015 Wizara ya Nishati na Madini  ambapo kulikuwa na tuhuma kinzani kuwa rushwa ilitolewa kwa baadhi ya wabunge ili waipitishe/wasiipitishe. Kilicho muhimu ni kuangalia uzito wa hoja zilizotolewa kupinga au kukataa uundwaji huo wa Kamati Teule ya Bunge. Pia ni muhimu kurejea hoja hii katika blogu yetu ya Udadisi: Tofauti Kati ya Ripoti ya Escrow na ya Richmond. Vile vile ni muhimu kuzingatia maoni haya ya Mhariri mmojawapo wa gazeti la The Citizen katika Mtandao wa Wazi wa Mabadiliko: "... unaweza kumtetea Muhongo kutokana na weledi na uchapakazi wake na kasoro zilizomo kwenye ripoti za CAG na PAC lakini unaweza kubadili msimamo iwapo...."
---

HANSARD UKURASA WA 77-80

MHE. JOHN J. MNYIKA – MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KWA WIZARA YA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, nasoma kwenye kitabu na naomba nisome kwenye kitabu kama ilivyoandikwa kwenye kitabu (Kicheko/Makofi)

Tatu, mara baada ya hoja hii kuamuliwa naeleza kusudio la kuwasilisha hoja Bungeni kutaka kuundwe Kamati Teule kuchunguza masuala yote tete na tata tuliyoyaeleza ndani ya kitabu hiki yanayohitaji uchunguzi maalum wa Kibunge. (Makofi)

[...]

HANSARD UKURASA WA 159-160

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nchi yetu inapita katika kipindi kigumu, kipindi ambacho kinahitaji umoja wa watoto wa Tanzania katika kusema kweli na kuitendea Tanzania haki. (Makofi)

[...]

Mheshimiwa Spika, nataka wana-CCM wenzangu tuliokula kiapo kwamba nitasema kweli daima, rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa, mtoke na vielelezo vya kukanusha hoja aliyoitoa Mnyika na ambayo na mimi nitatoa ushahidi wa nyaraka zote zinazohitajika juu ya uhalifu uliofanywa wa kutorosha shilingi bilioni mia mbili za Watanzania kutoka Akaunti ya BOT na
kuipeleka Stanbic na wakubwa waliopelekewa fedha zile walikwenda kuchota fedha hizo. Imagine mtu anaingia benki anaondoka na dola milioni tano kwa mfuko wa sulphate. Tunataka iundwe Kamati Teule ya Bunge ione ukweli huu. Tunataka tuthibitishe juu ya watu wenye uhusiano na wakubwa katika nchi hii, waliokwenda katika benki ya Standard Chartered na kusafirisha dola laki mbili kwa siku mara tano, dola milioni mbili kinyume cha Sheria ya Money Laundering na watu hawa hawajakamatwa mpaka leo, fedha hizi naamini zimetoka katika mgawo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka mtueleze Serikali ilikuwa wapi wakati imepewa tahadhari na VIP, imepewa tahadhari na ninyi mkaishinikiza BOT itoe fedha kutoka katika akaunti hiyo ya BOT na kuipeleka kwenye akaunti ya PAP, PAP ambayo mhusika wake Mkuu anahusika katika kashfa iliyoiangusha Serikali ya KANU ya Goldenberg. Nataka niwaambie ni lazima tuchunguze hili maana mitandao inasema hivyo, tuthibitishe kama mhusika huyu anahusika na Goldenberg skendo ya milioni mia sita dola za Marekani. Ni lazima Kamati Teule iundwe iwaeleze Watanzania ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakusudia baadaye kutoa hoja ili iundwe Kamati Teule ya Bunge ijiridhishe juu ya masuala haya. Sioni sababu kwa Mbunge yeyote wa Chama chochote kukataa kuundwa kwa Kamati Teule ichunguze jambo hili. Hatumvizii mtu, tunataka ukweli ujulikane. (Makofi)

HANSARD UKURASA WA 161-162

MHE. NIMROD E. MKONO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona na kunipa nafasi nami niweze kuchangia machache kuhusu hoja iliyo mbele yako. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nataka niwatoe hofu iliyosambaa kwamba mimi sitaunga mkono hoja hii. Nataka niseme kabisa, mimi ni mwana-CCM halisi, napenda Chama changu na nitasema ukweli daima. Mheshimiwa Spika, siwezi kuchangia hoja ya mfuko wa Escrow kwa sababu moja kubwa. Nimekuwa mshauri wa Serikali kwa miaka kama 15, nikianza kuzungumzia mambo ya IPTL hapa, nitakuwa nimekiuka utaratibu wetu wa kisheria. Ni lazima nipate kibali cha Mwanasheria Mkuu niweze kuzungumza na siyo wakati wake, kwa hiyo mtanisamehe sana. Zile taarifa kwamba Mkono anasema bajeti isipite huo ni uwongo na uhuni wa mjini tu, wananichonganisha mimi na Muhongo, sina ugomvi na Muhongo. Sina ugomvi wowote na Muhongo, ni rafiki yangu, anafanya kazi yake na mimi nafanya kazi yangu ya Uwakili. (Makofi)

[...]

HANSARD UKURASA WA 163-166

MHE. DAVID Z. KAFULILA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi.

[...]

Mheshimiwa Spika, ukiacha mgodi wa Mwadui, mimi wakati nachangia hotuba ya Waziri Mkuu nilizungumza kuhusu tatizo la ufisadi wa Escrow, narudia tena kuzungumza. Narudia tena kusisitiza, kama kweli Bunge hili ni la wawakilishi wa Watanzania wanaothamini mali na utajiri wa nchi yao, ni lazima iundwe
Kamati Teule kuchunguza jambo hili. Sielewi anayepinga Kamati Teule ana wasiwasi gani. Kama wewe upo clean una wasiwasi gani wa kuchunguzwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ufisadi huu umeanza tangu mwaka 1995 ukaja mwaka 1998, ukaja miaka ya 2000 na kwenye Escrow ndiyo unahitimishwa sasa bilioni mia mbili amepewa Singasinga anayefanya biashara Kenya, ambaye hata Bunge la Kenya walishampiga burning baada ya kupewa mradi na kushindwa ku-perform. Huyu ameshiriki kwenye Goldenberg scandal, scandal kubwa ambayo iliangusha Chama cha KANU, leo anakuja hapa tunaambiwa eti ndio mwekezaji! Hivi hii nchi mnataka muipeleke wapi, bilioni 200 nchi inakosa kutengeneza madawati kwa miaka hamsini, mahitaji ya madawati ni 1,500,000, kama kila dawati ni Sh.100,000 maana yake ni kwamba shilingi bilioni 150 zingetosha.

Mheshimiwa Spika, miaka hamsini nchi ambayo ni miongoni mwa nchi kumi zenye misitu ya mbao duniani lakini leo mnapoteza bilioni 200 kipuuzi, anapewa Singasinga kwa kushirikiana na vigogo wa Serikali. Mimi sina ugomvi na Muhongo, Muhongo is my friend! Sina ugomvi na Maswi, wala sina ugomvi na Waziri wa Fedha, wala sina ugomvi na Gavana wa Benki Kuu, wala AG mimi sina ugomvi naye. Nachokisema ni kwamba, Bunge ni lazima lifanye uchunguzi kuhusu suala hili kwa sababu linagusa pesa nyingi za Serikali, haiwezekani! Mimi ushahidi ninao, nawaambia niwapeni ushahidi hapa, Spika unakata kona tu, unakata kona tu, Spika nchi hii itakuhukumu! (Makofi)

SPIKA: Eeeh weka hapa ushahidi, weka hapa tuuone, siyo kusema Spika, weka.

MHE. DAVID Z. KAFULILA: Ndiyo, ndiyo naweka ushahidi wote uko hapa. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Weka!

WABUNGE FULANI: Endelea.

MBUNGE FULANI: Muda wake ulindwe.

MHE. DAVID Z. KAFULILA: Mheshimiwa Spika, sasa …

SPIKA: Naomba ukae chini.

MHE. DAVID Z. KAFULILA: Naomba muda wangu ulindwe.

MBUNGE FULANI: Ndiyo, muda wake ulindwe.

SPIKA: Naomba ukae chini na uzime kipaza sauti.


MBUNGE FULANI: Chukua umpelekee.

SPIKA: Waheshimiwa emotions zingine hazina sababu, utaratibu upo, kama una ushahidi weka hapa. Hivi sasa nasubiri ushahidi wa Mheshimiwa Mnyika, anasema ana-lay on the Table, let them lay on the Table, kwa nini mnakuwa na vitu ambavyo havina maana?Kwa hiyo, mwenye ushahidi wowote a-lay on the Table sasa (Makofi)

WABUNGE FULANI: Peleka!

SPIKA: Aah, aah, mimi ndiye ninayesimamia Bunge, nimemwambia alete, ataleta sasa ninyi mna tatizo gani?

MBUNGE FULANI: Waambie!


MHE. DAVID Z. KAFULILA: Huu hapa, huu hapa ushahidi. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Endelea.

MHE. DAVID Z. KAFULILA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba muda wangu ulindwe.

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi, unajua kwamba ni Bunge hilihili lilishindwa kusimamia fedha ya rada ilirejeshwe ndani ya nchi yetu. Bunge la Uingereza ndiyo likaja kuchachamaa, Bunge la Uingereza, ndio tukarudishiwa chenji ya rada. Hivi leo, Clare Short mnataka ndiyo aje tena aturudishie pesa za nje za Escrow? Balozi wa Uingereza anakwenda front anazungumza na Gazeti la Mwananchi, The Citizen anawaambia kwamba hapa kuna tatizo. Hivi kweli Uingereza walioturudishia hela ya rada ndiyo mnataka waturudishie ya Escrow, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili Bunge ni lazima tujitambue. Kuna akina mama, kuna vijana, kuna akina baba ambao mmesoma, mnajua wajibu wa Bunge. Uchunguzi siyo kutafuta mchawi, uchunguzi ni kutafuta ukweli, kama Muhongo is clean hawezi kukutwa na kasoro, kama Maswi is clean hawezi kukutwa na kasoro, kama AG is clean hawezi kukutwa na kasoro, wasiwasi ni wa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshindwa kujichunguza tangu mwaka 1995 mpaka leo, bado Bunge mnaamini kwamba Serikali ijichunguze? Msichanganye matatizo hapa. Watu wanasema ooh sijui mara Mengi, mara Standard Charted, mara Uingereza, hoja ya msingi iliyoko Mezani ni shilingi bilioni 200, bring back our money? Rudisheni na lazima zirudishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati nilipozungumza Bungeni hapa, lazima
ukumbuke, wakati pressure ya kuzitoa hizi pesa inafanyika ndiyo kipindi ambacho Waziri wa Fedha alikuwa Afrika Kusini yuko hoi taabani, amekata kauli. Kwa Bunge makini ilipaswa hata kifo cha Mheshimiwa Mgimwa kichunguzwe. Hawa watu hawa ndugu zangu ni maharamia. Huyu Seth siyo mfanyabiashara sahihi.

[...]

HANSARD UKURASA WA 174-177

SPIKA: Ahsante, muda umekwisha, ni kengele ya pili. Mheshimiwa Kangi Lugola?

MHE. ALPHAXARD K.N. LUGOLA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nizungumze machache. Kwa vile ninaumwa na sauti yangu sio nzuri, nitazungumzia mambo mawili tu. La kwanza, niliwahi kusema hapa Bungeni kwamba Rais alipomteua Profesa Muhongo kuwa Waziri wa
Nishati na Madini, aliteuwa gate valve ya kusigina mirija ya mafisadi ndani ya TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina makabila mengi sana. Kuna kabila moja kuku akifa wao ni msiba na ni kilio kikubwa. Sasa kuna watu humu wanataka kuwafanya Wabunge wote tulioko humu kwamba ni kabila moja na sisi tulie kwenye msiba wa kuku, Bunge hili hatutakubali. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye Hotuba ya Kambi ya Upinzani, rafiki zangu hawa na mimi Mnyika namheshimu sana, ripoti yao imejaa mambo mengi yanayohusu Ripoti ya CAG na wakasema wameitengeneza wao Kambi ya Upinzani kwa ushirikiano. Sasa leo kama hotuba yenu mnamheshimu CAG, mnaheshimu taaluma yake, inakuwaje leo tena mnasimama hapa mnasema kwamba hamtaki tena mambo haya yachunguzwe na CAG mnataka Kamati

Teule ya Bunge? Huu sio unafiki ni nini Waheshimiwa Wabunge (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bunge letu sasa linaanza kupoteza mwelekeo,
linaanza kupoteza heshima. Kama Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, baada ya kusikia jambo hili ikachukua hatua kwa niaba ya Bunge na wakaelekeza suala la Escrow Account, TAKUKURU na CAG wachunguze mara moja na Taarifa zao ziletwe Bungeni ili yeyote atakayebainika; nawahakikishieni

hapa patachimbika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa leo mnasimama mnasema hamuamini CAG, hamuamini TAKUKURU, mnataka tuunde Kamati Teule ya Bunge. Kwanza humu ndani wapelelezi, wachunguzi, mapolisi tuko wawili tu, mimi na rafiki yangu Mheshimiwa Deo Filikunjombe; ninyi mnasema mnataka mkachunguze, hata neno Escrow Account hamlijui. Kwa taarifa yenu hakuna fedha za Serikali zinazotunzwa kwenye Escrow Account. Zile sio fedha za Serikali, sio fedha za umma…

MBUNGE FULANI: Hawajui!

MHE. ALPHAXARD K.N. LUGOLA: Sasa hamjui, msidandie mambo, niulizeni mimi niwafundishe mambo haya (Kicheko/Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, nimesema nitaongea machache sana. Rafiki yangu Ole-Sendeka kwa bahati mbaya naona ametoka, amesema ana ushahidi, umtake alete ushahidi na wale wote mnaosema mna ushahidi, mna makaratasi, hayo ma-photocopy yenu, hayo makaratasi ya kufungia maandazi na vitumbua, sisi wenye taaluma ya upelelezi huo sio ushahidi. Kama mnadhani huo ni ushahidi pelekeni TAKUKURU na kwa CAG, ili waweze kuchunguza hayo

makaratasi yenu hayo badala ya kubaki nayo mfukoni hapo (Makofi/Kicheko)

Waheshimiwa Wabunge wenzangu, naomba tusiwayumbishe
Watanzania…

MBUNGE FULANI: Kweli!

MHE. ALPHAXARD K.N. LUGOLA: Tusiwaghilibu Watanzania. Watanzania sasa wanataka umeme, Watanzania wanataka nishati, Mwibara kule mpaka sasa mkandarasi yuko site; kwa mara ya kwanza, Mwibara hawajawahi kuona umeme, umeme unataka kuwaka, halafu mnaanza kusumbuasumbua Profesa
na Mawaziri wenzake na akina Maswi? Tuache nongwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bunge hili litatumika vibaya, kwa nini kila wakati Wizara ya Nishati na Madini ni migogoro isiyoisha? Kuna nini Nishati na Madini? Nawaambia ndugu zangu mafisadi wataendelea kututumia, tutaleta matatizo makubwa katika nchi hii. Tukatae kutumika ndugu zangu, tukatae kutumika, Bunge hili tusikubali. Nilisema mwanzoni, ukienda nje kule utakuta kila watu tuna makundi kule, tuko makundi tunatetea wafanyabiashara, tuko makundi tunatetea mafisadi na tunataka kuingia kwenye Bunge hili; nawaambieni Watanzania tusikubali Bunge hili kutumika vibaya.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi mwenyewe ni mwana-CCM halisi, ni mwana-CCM nisiyeyumba, ni mwana-CCM ninayeitakia mema nchi hii. Leo wanapoanza kusimama watu humu wanasema ni wana-CCM wana uchungu, wanatokwa machozi kwa mara ya kwanza tuwaogope kama ukoma.(Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, wanakuwa wapi kama ni wana-CCM nchi inaibiwa? Uko wizi wa dhahiri, lakini hawasemi, hawapigi kelele? Leo hapa wanaanza kupiga kelele fedha za Escrow ambazo sio fedha za Watanzania, ni fedha za IPTL, ameuza umeme, lazima TANESCO wamlipe pesa, sasa haya mambo yanatoka wapi katika nchi hii kama kweli ninyi ni wana-CCM halisi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wana-CCM wenzangu, ambao tuna uchungu na nchi hii, inakuwaje katika masuala ya msingi ambayo kila siku nasema mniunge mkono wana-CCM wenzangu, haohao wanabaki nyuma kule wanakimbia leo wanakuja humu na vikaratasi wanasema kwamba wana ushahidi wa wizi wa fedha za Escrow Account, ni uwongo na unafiki mtupu, ni uwongo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa busara za Bunge hili na Wabunge tusikubali kuyumbishwa, tusubiri CAG na TAKUKURU wachunguze mambo haya, watuletee na kwa kweli, kama nitakuta Mheshimiwa Muhongo unahusika sitakuangalia usoni, nitakushughulikia. Nikiwakuta akina Mheshimiwa Masele na Kitwanga mmehusika, sitawatazama usoni nitawashughulikia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha
kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Haya, ahsante, muda wako umeisha.

MHE. ALPHAXARD K. N. LUGOLA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja
nipate umeme. (Makofi)

HANSARD UKURASA WA 198-200

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Awali ya yote, nitumie fursa hii kumshukuru Mola Manani, kwa kutuwezesha tena kwa mara nyingine, kuwa mbele ya Bunge lako Tukufu kujadili hoja hii ya Wizara ya Nishati na Madini. Nianze kwa kusema kwamba, kwanza, nitakuwa mgumu sana kuunga mkono hoja hii kwa sababu ambazo nitazitaja baadaye.

[...]

Nimalizie kwa kuzungumzia IPTL. Si Uwana-CCM ulio mahili ama uliodumu katika misingi, kukubali kushangilia wizi, ama kukubali kufumbafumba mambo mazito kama hili la IPTL. Huo si Uwana-CCM na wala siyo kuyaweka masilahi ya Watanzania ndani ya mioyo yetu; na wala si kuyaweka masilahi ya Chama
chetu cha Mapinduzi ndani ya mioyo yetu. Kule nje Wananchi wanafahamu, kuna Viongozi wakubwa ndani ya Serikali wala siyo wa kisiasa, walionekana katika Benki ya Stanbic, wakichukua mabegi ya fedha zinazotoka kwenye akaunti hii ya IPTL. (Makofi)

Sasa leo hii hatutaki kulizungumza hili kwa sababu gani? Nina details za kutosha, nimefanya uchunguzi wa kutosha, nimejiridhisha Rais hahusiki, Waziri Mkuu hahusiki, Spika hahusiki, Katibu wa CCM hahusiki. Wanaohusika ni watu
ambao hata hawatafuti kura za CCM. Kwa nini sisi tunakuja kukaa hapa tunashabikia na kushangilia, wakati hatujapewa chochote, waliokula wanajulikana na wapo na hawapelekwi kwenye Kamati Teule ya Bunge kwenda kujibu maswali haya ili ushahidi wote tulio nao uweze kupatiwa majibu?

Mheshimiwa Spika, kama hili linapingwa, naomba nipatiwe majibu na Waziri wakati ana-wind up hapa, kwamba ni kwa nini waliamua ku-release mzigo kutoka kwenye Account ya ESCROW, wakati walijua kabisa TANESCO imefungua kesi kwenye Mahakama ya Kitaifa ya kule Marekani?

Kwa nini hawakuanza kuiondoa kesi Mahakamani ndipo wa release huu mzigo kwenye Account ya ESCROW? Ni sababu zipi ziliwafanya wafanye hivyo?

Napenda nijibiwe swali hili pia; ni kwa nini Viongozi wa Wizara wanamshambulia sana Mzee Mkono wakati walimpa mkataba wao wenyewe kinyume kabisa na Kanuni za Gharama za Mawakili?Kwamba, kama fedha inayodaiwa inazidi bilioni kumi, basi kiwango cha gharama ya Wakili kisizidi asilimia tatu. Leo hii mzee Mkono akilipwa bilioni 18 kuna hasara gani wakati walimpa mkataba? (Makofi)

[...]

HANSARD UKURASA WA 305-307

MHE. CHRISTOPHER O. OLE – SENDEKA: Kwamba mara baada ya mimi kuchangia na Wabunge kadhaa, Mheshimiwa Kangi Lugola alisimama hapa na kuelekeza shutuma kwetu hasa baada ya kulitaja jina langu na kusema kwamba tulichokuwa tumeleta au tulichonacho kama ushahidi ni makaratasi ya kufungia mandazi au vitumbua.

[...]

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitakupa karatasi 10 kama ushahidi hapa mbele yako na nitaendelea kutoa ushahidi utakaohitajika kama Kamati Teule itaundwa. Kama itashindikana uamuzi wowote utakaofanyika kama ni wa CAG, kama utakuwa ni wa Mkurugenzi wa TAKUKURU au chombo chochote, niko tayari kushiriki.

Mheshimiwa Spika, nilichosimama kufuta ni kuthibitisha kwamba ushahidi tulionao juu ya uhalifu huu ninaouzungumza ambao nitautetea katika kipindi cha maisha yangu yote kwamba nilikuwa sahihi, naweka mezani kwako.

Ninachoomba tu ni kwamba hili la TANESCO ambalo wahalifu wakubwa wamepandishwa madaraka, nitaomba photocopy ili niweze kuwa na nakala halisi. Hizi zingine nimepiga photocopy, lakini hiki kitabu kwa sababu ni kikubwa nitaomba wasaidizi wako wapige photocopy ili uone wale walioiba raslimali za nchi walivyopandishwa vyeo na wengine bado wamekalia viti kama Muhongo na Maswi. Nitathibitisha katika kitabu hiki, Ripoti ya Controller and Auditor General. Anayeguna, natoa ushahidi, simama pinga.

[...]

HANSARD UKURASA WA 341-343

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nitatumia dakika kidogo, lakini nafikiri ni vizuri niseme mawili, matatu. Moja, nataka tu kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba maelekezo ambayo yalikwishatolewa kuhusu namna tutakavyoshughulikia IPTL, naomba kila Mbunge kwa kweli alipokee jambo hili kwa moyo mkunjufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yuko pale kwa mujibu wa Katiba yetu, Ibara 143, ni Ofisi Kuu na ni Ofisi ambayo kwa miaka ndiyo tumeitegemea tunapokuwa na tofauti zetu katika masuala yanayohusu fedha. Nataka niwasihi sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tusianze kuonesha dalili za kwamba pengine hatuna imani na chombo hiki,.
itatuletea tabu sana katika kusaidia Serikali kuweza kutimiza majukumu yake. (Makofi)

Tumeshakubaliana taarifa ile akishaikamilisha tutaileta kwako,
itatazamwa na kama kutakuwa na jambo lolote lile sisi kwa kweli hatutajali kitu gani amesema, hatua stahiki zitachukuliwa kwa yeyote yule Mdhibiti atakayemwonesha kwamba ameingia katika mgogoro wa ama ubadhirifu ama rushwa ama jambo lolote. Kwa hiyo, nataka niliseme hilo kama jambo moja la msingi sana.

[...]

Mheshimiwa Spika, mwisho, naomba niseme kwa dhati, Wizara hii ya Nishati na Madini, tangu wameshika Ofisi hii, Profesa Muhongo na Naibu wake wawili, kama kuna jambo ambalo tulitakiwa kwa kweli tukubali ni kuwapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafuatilia sana kazi yao karibu kila siku kwa dhati kabisa. Nimetembea nchi hii sana, nimeona juhudi wanazozifanya kwenye umeme vijijini. Nimekwenda kutembelea bomba lile la Mtwara, tuko na Muhongo, unafarijika kuona kwamba Wizara hii iko makini na inajitahidi sana.

(Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa sipendi tuwavunje moyo, lazima tuwatie moyo, sana tu, ndiyo maana leo nilishindwa kuvumilia nilipoona Mheshimiwa Kafulila pale anasema ninao ushahidi, ninao ushahidi, nikasema utoe basi. Unajua vitu hivi, hawa ni binadamu, mimi siyo Mwenyezi Mungu. Sijui yaliyomo moyoni mwake na hakuna hapa ambaye anajua yaliyomo moyoni mwake. Ndiyo maana inabidi mfike mahali kama kuna mashaka mazito yenye ushahidi, toeni
kwa utaratibu wa kawaida, ndiyo maana nikasema mwacheni na CAG naye atusaidie, Muhongo akionekana kachukua rushwa, kaiba, kafanya nini, hatua stahiki zitachukuliwa, lakini in the meantime kwa yale wanayofanya mazuri, tukubali wanafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sitaki nichukue muda wako mwingi, lakini naomba tu nirejee kusema, kwa kweli nafarijika sana na utendaji wao na nitaendelea kushirikiana nao sana na naomba Wabunge wenzangu tuwasaidie. Kama watakuja kuteleza kama binadamu, hakuna tatizo, watachukuliwa hatua stahiki bila kuwaogopa bila kujali. Sasa kwa kuwa bado ni tuhuma tu, maneno, maneno tu na baadhi ya makaratasi wanayotoa kwamba ndiyo ushahidi wa
rushwa, aah unashangaa haya. Kwa hiyo, nadhani twende nalo hili nafikiri tutalimaliza vizuri na naomba nishukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)

HANSARD UKURASA WA 343-345

SPIKA: Naona umesimama Mheshimiwa Ole-Sendeka. Ninazo dakika zangu tano. Mheshimiwa Ole-Sendeka. Nimemwita Mheshimiwa Ole-Sendeka, kwa hiyo ninyi wengine mnakaa.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

SPIKA: Msichafue hali ya hewa. (Kicheko)

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme naungana na Mheshimiwa Waziri Mkuu, nilikusudia kuomba kuundwa Kamati Teule na baada ya maelezo yake, nataka niseme baada ya Msemaji wetu Mkuu kusema hivyo nami nataka niseme kwanza naondoa hoja yangu ile.

[...]

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP