Friday, January 2, 2015

Escrow – Vita vya Panzi au Tembo?

Escrow – Vita vya Panzi au Tembo?

Chambi Chachage

Wakati tunasherehekea kuingia mwaka mpya kadhia ya – ama sakata la – Escrow linazidi tu kuchukua sura mpya. Majibizano na vijembe vya hapa na pale vinaendelea huko na kule. Kulikoni?


Lakini wahenga waliosema “vita vya panzi furaha ya kunguru” ndio hao hao waliosema “wapiganapo tembo ziumiazo nyasi.” Swali la kujiuliza hapa ni, je, wananchi – yaani umma – ni nyasi au kunguru katika mpambano wa Escrow? Na, je, wanaojipambanua kama wanaopigana kwa niaba – na ajili - ya (fedha za) umma ni panzi au nao ni tembo?

Kama mawingu yaashiriavyo mvua, kuviziana ilikuwa ni dalili ya vita. “Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya Kamati” anayoongoza “ya PAC kuwasilisha Bungeni Taarifa Maalumu kuhusu ukaguzi maalumu wa akaunti ya Tegeta Escrow,” Mbunge Zitto aliujulisha umma, “kumekuwa na kampeni za chini chini zinazoendeshwa kwenye korido za Bunge na kwenye mitandao dhidi” yake “binafsi na baadhi ya wabunge waliosimama kidete dhidi ya wizi wa fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania akaunti ya Escrow”.

Mwenyekiti wa PAC pia alitujulisha kuwa “Waziri mmoja ambaye ni mtuhumiwa wa wizi wa fedha za Tegeta Escrow” alikuwa “anazunguka kwa wabunge akisema tuhuma hizi kupikwa kama njia yake ya kuhamisha mjadala kutoka uporaji wa Tshs 200 bilioni kwenda kwenye masuala binafsi.” Kisha Mwenyekiti huyo akazijibu ““Tuhuma hizi zenye kichwa cha habari “Zitto na Filikunjombe wanatumiwa na Kenya na Uingereza kuvuruga na kudhoofisha Uwekezaji nchini mwetu””.  Baadhi ya tuhuma hizi zilipotolewa Bungeni aliyekuwa Waziri mmojawapo alioneshwa runingani akigonga meza huku akicheka kwa furaha na kejeli.

Wakati anajibu bloguni tuhuma namba 6 kuwa “Uingereza imekuwa inamfadhili Zitto kwa miaka mingi kwa mambo yake ya kisiasa kwa hiyo sasa hivi Ubalozi wa Uingereza unamlipa Zitto na Kafulila kuhakikisha kwamba Standard Chartered ya Uingereza inalipwa deni lake lisilotambulika kisheria nchini mwetu”, Mwenyekiti wa PAC akasisitiza kuwa “kuna propaganda ambazo haziangalii hata diplomasia” na kuhitimisha kuwa “Kurudia kurusha tuhuma kwa Ubalozi wa Uingereza nchini ni kudhihirisha kwa mara nyingine kiburi cha kuwa na mamlaka…walichonacho wanaotuma tuhuma hizi.”

Tuhuma hii ina uzito wa pekee kwa kuwa hiyo barua inayosemekana iliandikwa na Standard Chartered Bank (Hong Kong) mwaka 2009 ina maneno haya: “Regrettably, the courts will not take notice of the fact that the Bank has appointed a Receiver over the shares (the Shares) held by (both Mechmar and) VIP in IPTI. The Bank has exercised its rights under Share security given to it by both Mechmar and VIP and now controls the Shares absolutely, through its Receiver. The Bank asserts that it has the power to, and it will if so advised, sell the Shares to a third party and pass good title to them…. The Bank has proposed to your legal advisers that the Government of Tanzania immediately consider Nationalisation of IPTL. This would be with the support of the Bank and with the express objective of implementing the Agreed Plan.... If Nationalisation were to be agreed upon and implemented.... The whole process could be conducted through the Tanzanian Parliament. There would be no need to involve the courts....”

Kwa tafsiri rahisi ya kimuhtasari, benki hiyo inaonekana haikupendezwa na maamuzi/mitizamo ya mahakama za Tanzania na katika kipande hicho kilichonukuliwa hapo juu inaziona mahakama zilikuwa hazizingatii kuwa benki ilimteua mkusanyaji wa hisa za Mechmar na VIP katika IPTL. Tukumbuke kuwa, kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu akaunti ya Escrow, benki hii ilinunua madeni ya IPTL, jambo ambalo pia limegusiwa katika barua hiyo. Pia tukumbuke kuwa Mechmar na IPTL ndio walikuwa wanahisa wa kwanza kabla hisa za Mechmar hazijauzwa kwa Piper Link na kisha PAP katika mazingira ya kutatanisha yaliyochangia kutolewa kwa fedha kwenye akaunti ya Escrow kabla ya kutatua utata huo.

Tukumbuke pia, kwa mujibu wa ukurasa wa 50 wa Taarifa ya CAG, benki hiyo na huyo mkusanyaji wake wametajwa katika baadhi ya kesi hizi ambazo hazikuchambuliwa kwa undani humo: “v. Standard Chartered Bank dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania- ICSID Case No. ARB /10/12, vi. Standard Chartered Bank (Hong Kong) Limited dhidi ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) ICSID case No ARB/10/20, vii. Martha Kaveni Renju the Administrator Receiver of IPTL dhidi ya IPTL Shauri Na.124 ya 2003, viii. Martha Kaveni Renju the Administrator Receiver of IPTL dhidi ya IPTL na VIP Engineering and Marketing ltd Shauri Na.98 la 2013, ix. Shauri la Mapitio Na.1 la 2012 kati ya Standard Chartered Bank (hong Kong) dhidi ya Mechmar Corporation, VIP Engineering and Marketing, IPTL, The Liquidator of IPTL, The Bank of Tanzania, TANESCO na TRA katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Pengine kwa kutambua kuwa hii ni tuhuma nzito inayohitaji majibu mazito, Mwenyekiti wa PAC alisema maneno yafuatayo kwa uchungu sana wakati anawasilisha majibu/ majumuisho ya Taarifa ya Kamati yake/yao tarehe 28 Novemba 2014: “Mheshimiwa Spika, Mheshimwa Waziri wa Nishati na Madini ukurasa wa ishirini amezungumzia suala la kwamba TANESCO haina mashtaka na ICSID ila mashtaka ni ya Standard Chartered. Napenda nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba IPTL kabla haijawekwa kwenye muflisi ilifungua kesi kupinga kitendo cha TANESCO ku-dispute zile invoices. Kesi ilipoendelea kule mahakamani ICSID baadaye IPTL ikawekwa chini ya muflisi na mahakama zetu za Tanzania baada ya maombi ya mbia mmoja, Ndugu James Rugemalila. Na wabunge wengi, wengine wameingia humu mara ya kwanza ndio maana wamediriki hata kunitukana, hawanifahamu. Nataka niwakumbushe na Waziri wa Mambo ya Ndani ni shahidi yangu. Fedha hizi zilitaka kuanza kuibwa toka mwaka elfu mbili na nane [2008], elfu mbili na tisa [2009]. Mahakamani Jaji akaenda akaondoa amri ya kuiweka IPTL kwenye muflisi wakati  tuna kesi ambayo kwa kujenga hoja kwamba hii kampuni iko kwenye muflisi ile kesi tungeweza kushinda.”

Mwenyekiti wa PAC akaendelea kujibu kama ifuatavyo: “Leo kuna baadhi ya wabunge wanahoji kuwa labda tunatumwa na Uingereza. Huyu Chikawe ni shahidi. Balozi wa Uingereza alikuja na delegation yake ya watu wa Standard Chartered kuniona kama Mwenyekiti wa POAC ku-lobby kwamba tuwaachie Standard Chartered wachukue hela za Escrow. Nikatoka nje ya kikao nikampigia simu Chikawe, wakati huo ni Waziri wa Justice, nikamwambia Chikawe hawa wanavunja diplomatic protocol, hawawezi kuja kwa Mwenyekiti wa Kamati hawana kibali cha Wizara ya Mambo ya Nje, wanakuja ku-lobby. Chikawe ni shahidi yangu akatae hapa, anikane. Hamna kingine kilichonituma kufanya hivyo, ni uzalendo kwa nchi yangu. Kwa hiyo, siwezi kuwajibu watu ambao kwa njia moja ama nyingine wameniparuraparura, siwezi kuwajibu; siwezi kuwajibu hata kidogo kwa sababu hawajui nini nilichokifanya kwa nchi hii. Mheshimiwa Spika, shauri lile kule ICSD tukashinda kwa kuhoji ya kwamba IPTL iko chini ya muflisi. Mahakama ikairuhusu Standard Chartered waingie kwa nafasi ya IPTL kwa sababu wanaidai IPTL. Kwa hiyo ikaingia mahakama. Na hoja pale ilikuwa ni Capacity Charges, kwamba tumekuwa overcharged. Tumeshitakiwa sisi kwamba kwa nini tuna-dispute invoices. Kesi imekwenda. Mwezi Februari mwaka huu shauri limeamuliwa kwamba, kwanza, ni kweli tumekuwa overcharged na, pili, ifanyike recalculation. Mheshimiwa Spika, maamuzi ya kesi haya hapa na nayawasilisha mezani kwako. Serikali leo inakuja kukataa maamuzi ambayo sisi tumeshinda na imeamuliwa recalculation, kwamba bei mpya ya umeme, bei mpya ya Capacity Charges iangaliwe kulingana na uwekezaji ambao wale watu wameweka. Sasa tunakujaje kukataa kitu ambacho sisi tumeshinda?”

Kisha Mwenyekiti wa PAC akahitimisha hivi: “Sasa ngoja niwaambie madhara yake. Mkataba ule baada ya maamuzi ya mwaka 2001, Capacity Charges zikashushwa mpaka dola milioni mbili nukta sita kila mwezi, kama tulivyoeleza kwenye Taarifa ya Kamati. Usipofanya recalculation maana yake ni kwamba mpaka sasa hivi, hivi mwezi huu wa Novemba unakwisha, huyo anayesema ni mmiliki mpya analipwa Capacity Charges ile ile. Tungefanya recalculation, hata kama huyo mtoto mpendwa Seth angeachiwa hiyo mitambo, Capacity Charges ingekuwa chini. Hivi tunafikiria namna gani kama nchi?”

Pamoja na majibu hayo, Rais ametoa Hotuba inayoonekana imeegemea zaidi upande wa Utetezi wa Serikali uliowasilishwa Bungeni na Waziri wa Nishati na Madini tarehe 27 Novemba 2014. Na pengine Hotuba hiyo ndiyo imeipa Wizara hiyo ujasiri wa kutoa Tamko la kuijibu Nipashe linalojumuisha jibu hili: “Waziri wa Nishati na Madini ndiye msimamizi mkuu wa masuala yanayohusu sekta za Nishati na Madini nchini. Mtambo wa IPTL ulijengwa kwa ajili ya kufua umeme unaotumiwa na jamii ya watanzania. Kuwepo kwa mgogoro kungeweza kuondoa azma ya uwepo wa mtambo huo ya kufua umeme ili kuliepusha Taifa kuingia katika mgawo wa umeme kutokana na upungufu wa upatikanaji wa nishati hiyo, hivyo lilikuwa ni jukumu lake kuona kuwa mgogoro wa wawekezaji wa mitambo ya IPTL unakwisha ili mitambo iendelee kutoa huduma ya umeme kwa Taifa. Jukumu la Waziri ni kusimamia Sera, Sheria na taratibu katika sekta anazozisimamia.”

Kuhusu hizo tuhuma za Waziri kuwa “Dalali wa Fedha wa Escrow”, Kanusho hilo la Wizara linaendelea kwa kusema kuwa: “Katika kufanya hivyo, Waziri hukutana na wadau na kujadili masuala kwa uwazi bila kificho kwa nia ya kujenga nchi na kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa ndiyo kipaumbele. Kwa hiyo mikutano na Wadau ikiwa ni pamoja na wawekezaji hufanyika si kwa udalali. Suala la fedha za akaunti ya Escrow lilihusu uamuzi wa mahakama iliyojiridhisha kuwa mnunuzi wa hisa zote za VIP na MECHMAR ni halali na alitakiwa kukabidhiwa mali na madeni ya IPTL. Mali ni pamoja na kiasi cha fedha stahiki kwenye Akaunti ya Escrow ambazo hata hivyo ilidhihirika kuwa hazitoshi kukidhi deni halali. Akaunti hiyo ilikuwa na Sh. 182 bilioni wakati malipo yaliyokubalika kwa pande zote (IPTL na TANESCO) kwa mujibu wa maamuzi ya ICSID I yalikuwa Sh. 306 bilioni. Kumwita Waziri wa Nishati na Madini kuwa ni dalali ni kupotosha ukweli.”

Lakini siku moja tu baada ya Hotuba ya Rais, Mwenyekiti wa PAC aliandika maneno haya katika Ukurasa wake wa Facebook: “Kuweka rekodi sawa, PAP (sio IPTL) wamelipwa tshs 306 bilioni. Alizosema Rais ni zile zilizokuwa Benki kama taslimu na dhamana za Serikali. Ambazo hakusema ni zile ambazo zililipwa na TANESCO baadaye. Ifahamike hadidu rejea (Terms of References) kwa CAG kufanya uchunguzi zilitolewa na PAC, hivyo PAC ndio yenye mamlaka ya kuzisemea, kuzielezea na kuzitolea ufafanuzi. Kwenye eneo hili Rais hakuwa sahihi na Ikulu inapasa kurekebisha. Jumla ya fedha ambayo PAP wamelipwa kutoka akaunti ya ‪#‎TegetaEscrow Ni tshs 306 bilioni.”

Pia akarejea na kuiboersha hii hoja yake ya awali na kusisitiza kuwa hili ni “Muhimu sana”:  “Mamlaka ya Kutafsiri Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali haipo kwa mkaguliwa (Serikali) Bali kwa Bunge. Bunge hufanya kazi hiyo kupitia Kamati ya PAC”. Hili tumelidadisi katika makala ya Hotuba ya Rais na Hatma ya Udhibiti na Ukaguzi wa Fedha za Serikali. Tulichoona ni kuwa migongano ya kimamlaka katika suala la Escrow inachangia kuleta utata hivyo ni vyema tukaondoa miingiliano ya aina hii ila tuhakikishe pia kuwa kikundi kimoja au mtu mmoja – Bungeni ama Serikalini – asiwe na nguvu sana na madaraka makubwa kupita kiasi ya kitafsiri na kimaamuzi.

Wakati ‘Serikali’ inaonekana kuendelea tu kushikilia ‘tafsiri yake’ kuhusu fedha hizo iliyopelekea kuiweka wazi kwa mara ya kwanza Taarifa Maalum ya CAG magazetini na mitandaoni ili tuisome, tarehe 31 Desemba 2014 Mwenyekiti wa PAC aliibukia huko Mtwara na Hotuba yenye jibu hili (kinzani) la nyongeza: “Katika shilingi bilioni 306 zilizokuwa na zilizopaswa kuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow kuna fedha za Umma. Serikali inasema hazikuwa 306 bilioni bali 202 bilioni! Hii sio hoja ya msingi. Hoja ya msingi ni kwamba hata zingekuwa bilioni moja, bado ndani yake kuna fedha za umma na ilipaswa utekelezaji wa hukumu ya kupunguza kiwango cha tozo ya uwekezaji kufanyika ili kujua kiasi cha fedha za umma. Tapeli Harbinder Singh Seth alilipwa hizo zilizokuwemo katika akaunti na akaendelea kulipwa bakaa na TANESCO kiasi kwamba shirika hili linalofilisika linamlipa kila siku bwana huyu shilingi milioni 400. Kila siku inayokwenda kwa [M]ungu tunamlipa mtu ambaye hajawekeza hata senti tano nchini mwetu. Alikuja na briefcase tu. Kule Kigoma kuna neno jipya siku hizi, linaitwa umazwazwa. Ni kama ujuha hivi. Huu ni umazwazwa ambao wananchi hawapaswi kuukubali.”

Kana kwamba inalifufua Azimio la Songea la enzi za sakata la Buzwagi kupitia Azimio la Mtwara, Hotuba hiyo inaendelea kwa kusema hivi: “Watu watatu tu ambao ni raia wa kigeni walichora wizi huu kwa miaka mitatu. Mtu mmoja anaitwa Bwana Baharuddin kutoka Malaysia, Bwana Issa Ruwaih kutoka Oman na Bwana Singh kutoka Kenya na anaishi Afrika Kusini. Walidanganya nyaraka za kuuziana makampuni, bwana Baharuddin akauza hisa za IPTL kutoka Mechmar kwenda kwa Bwana Issa wa kampuni ya PiperLink na Bwana Issa naye akauza hisa hizo zikiwa zimezuiwa na Mahakama kwa Bwana Seth wa kampuni PAP.  Mabwana hawa wanajua Watanzania ni mazwazwa na hawafanyi uchunguzi wa kina, yaani ‘due diligence’ kwani hata kwenye EPA fedha ziliibiwa kwa kutofanya due diligence na kwa kutumia kitu kinaitwa ‘deed of assignment’. Mabwana hawa wanajua kuwa Watanzania wenye ofisi za umma wana njaa na watawahonga kidogo tu na kupitisha kila kitu. Ndivyo ilivyofanyika. Kama viongozi wetu wangefanya ‘due diligence’ kwenye manunuzi ya makampuni haya kama Sheria ya Kodi ya Mapato inavyowataka, tusingekuwa na skandali ya Tegeta Escrow. Mfumo uliganzishwa kwa rushwa. Ukitazama miamala ya malipo kutoka akaunti ya Bwana Seth katika akaunti ya StanBic utaona fedha zimekwenda benki za UAE na baadaye Oman na Malaysia. Fedha hizo zilikwenda kuwalipa mabwana Baharuddin na Issa.”

Hotuba hiyo inayoutangaza 2015 kuwa “Mwaka wa Kuwajibishana” inahitimisha jibu (mbadala) hilo kwa msisitizo huu: “Serikali lazima ichukue hatua mara moja kuhakikisha fedha zilizokuwamo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zinarudi, uamuzi wa mahakama ya kimataifa unatekelezwa na fedha za umma zinarejeshwa TANESCO na zile za binafsi zinalipwa kwa wamiliki halali. Tanzania haiwezi kuwa nchi ya kubariki utapeli wa kimataifa na kuchafua sura ya nchi yetu mbele ya jamii ya kimataifa. Baraza la Taifa yaani Bunge, kupitia wawakilishi wa wananchi, tayari wameamua na kupitisha maazimio. Kilichobakia ni maazimio hayo kutekelezwa na Serikali. Hakuna mjadala katika maazimio ya Bunge, maana katika maazimio hayo Serikali nayo imo; ilishiriki kikamilifu katika kuyandaa na hatimaye kupitishwa na Bunge. Hakuna namna ya kukwepa kutekeleza maazimio ya Bunge kwa ukamilifu wake; nasema hakuna, ni utekelezaji tu.” 

Mtaalamu mmoja aliyebobea katika kufuatilia kwa undani sakata la Escrow anashauri kuwa, kimkakati, kwa sasa suala la Standard Chartered Bank siyo muhimu kulishikilia bango maana kwa kufanya hivyo mwanaharakati unaweza kujikuta unatumiwa na mafisadi hata bila kujijua. Kilicho muhimu, kwa mujibu wa mfuatiliaji huyo, ni kulivalia njuga suala kuu tu nalo ni la PAP/VIP kuchota kilichokuwa Escrow ili fedha zetu zirudi na gharama za umeme zipungue. Wito wake unaonekana una mashiko ukizingatia kuwa matamko ya VIP yaliyotolewa katika gazeti la Serikali la Daily News yamejikita katika kuishambulia Benki hiyo ya Standard Chartered kuwa ndiyo iko nyuma ya harakati dhidi yao.

Lakini baadhi ya wananchi wadadisi tuko njia panda. Kwa nini tuangalie tu upande mmoja wa shilingi na sio mkanda mzima? Kama hao wote ni tembo – yaani VIP/PAP na Standard Chartered Bank (ya Uingereza au hiyo ya Hong Kong) – tunaoumia si ni sisi nyasi? Au hao ni panzi tu ilhali sisi na wapambanaji wetu ndio kunguru? Kama ni hivyo, je, na hili lililonenwa na wahenga  wetu nalo linatuhusu pia: “kunguru mwoga hufukuza mbawa zake”?

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP