Sunday, January 4, 2015

Kosa la Profesa Muhongo Escrow - Kudangany(ik)a?

Wadadisi tunahitimisha ukusanyaji wa dondoo/nukuu kutoka kwenye Hansard ya Majadiliano ya Bunge (Mkutano wa 15 Kikao cha 22) ya Mei 30, 2014 inayopatikana katika kiunganishi hiki cha Tovuti ya Bunge http://polis.parliament.go.tz/PAMS/docs/HS-15-22-2014.pdf na maneno ya Waziri wa Nishati na Madini. Tunaamini kwamba kosa - kama kwa hakika lipo - la Profesa Muhongo kuhusu Escrow linapatikana humo. Uchambuzi wa kina wa maneno hayo kwa kulinganisha/kuzingatia Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Utetezi wa Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini (MEM) Bungeni unatosha kabisa kuthibitisha kama kile Rais Kikwete alichokiacha "Kiporo" mwaka 2014 kwenye Hotuba yake kuhusu Escrow kinaweza 'kuchacha' au la. Wahenga walinena kwamba "njia ya mwongo ni fupi" na "penye ukweli uwongo hujitenga".  Isipochakachuliwa, historia - kama zilivyo rekodi/kumbukumbu sahihi - haidanganyi.
---

HANSARD UKURASA WA 314-319 

[MHE. PROF. SOSPETER MUHONGO (WAZIRI WA NISHATI NA MADINI):]

[...]

Sasa niwaeleze kitu ambacho kimeanza miaka ya 1990 mpaka leo hii eti tukijaribu kukitatua tukimalize kama Taifa twende mbele wengine hawataki kwa sababu ya mirija yao. Sasa niwathibitishie Watanzania mtu aje hapa na lori ya ma-documents na nini ni lazima kesi hii iishe. Kesi hii kutoisha madhara yake ni haya yafuatayo:- Kwanza heshima ya Taifa inashuka chini kwamba hili ni Taifa
ambalo kwanza ukienda kuwekeza huko utajiingiza kwenye migogoro ambayo haina mwisho. Halafu hawa watu wanaotupatia fedha wakitaka kutukomoa wanajishika kwa IPTL.

Sasa unaona hiyo ndiyo maana wewe kama ni mzalendo wa kweli
huwezi ukaja hapa unang'ang'ana na IPTL usioijua. Wote walioongea humu nawahakikishia hawajui mambo ya IPTL. Ni watu wamefungiwa chumbani wakakochiwa wakapewa, maana yake akapewa selective document. Mtu aliyempa document ni ile iliyokuwa inam-favour yeye. Kwa hiyo akachambua
hizi, ushahidi huu, nenda. Lakini upande wa pili unaufahamu? Inabidi watu wengine kusema kweli itabidi nitakuja na ku-check vyeti vya watu hapa kidogo. (Kicheko)

Sasa baada ya IPTL kuingia nchini hapa, hadithi ni ndefu sana, lakini mwisho wake ni kwamba MECMA alikuwa na asilimia 70 na Rugemalira alikuwa na asilimia 30 (VIP). Mimi mwenyewe documents nilizonazo, hizo asilimia 70 na 30 hawakubaliani, hawatambuani. Ukimwambia VIP, MECMA walikuwa na 70,
anasema hapana. Ukimwambia MECMA, VIP ilikuwa na asilimia 30 anasema hapana. Hiyo nayo ni kesi inaweza ikakuchukua miaka miwili mitatu au zaidi. Kwa nini Bunge letu lipoteze muda kuongea kitu kama hicho.

Ukiacha hao wanahisa hao, kwa hiyo hapa kitu ambacho kinaleta
mgogoro na msemaji mmoja amegusia, hapa ipo TANESCO, hapa ipo IPTL. TANESCO inanunua umeme kutoka IPTL. Lakini hawa wajanja ambao hawataki hii kesi isiishe wanazunguka na mikoba ya documents wanataka kuingiza TANESCO kwenye kesi za madeni ya IPTL. Ee, Profesa mwenzangu umenunua

daladala, mimi napanda daladala yako kweli mimi nina haki ya kujiingiza kwenye madeni ulikokopa fedha kununua daladala?Ndiyo hawa wanataka kutuingiza huku.

Halafu kitu kingine wanataka kutuingiza ambacho hakifai, sasa akatokea hii Standard Chartered, IPTL amekopa fedha huko ameshindwa kulipa, akajitokeza Standard Chartered akayanunua yale madeni. Hawa wajanja wanataka TANESCO na Serikali yetu iingie vilevile kwenye kesi ya Standard Chartered na IPTL kitu hakiwezekani.

Ndiyo maana nasema usikurupuke na vitu usipovifahamu, ni aibu sana. (Makofi)

Kingine ambacho lazima tuelewane, sasa baada ya IPTL kuja hapa,
mgogoro ulipoanzia sasa. IPTL ikaja ikajenga mitambo na sisi tuna ukame. IPTL ikasema sasa hii TANESCO ninavyoiona haina fedha nikiwauzia umeme ikishindwa kulipa nani atanilipa fedha zangu! Serikali kwa sababu ilikuwa inataka umeme ikaweka guarantee, lakini haikuweka guarantee kwenye madeni ya IPTL, iliweka guarantee kwenye mauziano ya umeme tu. Sasa wajanja wasiotaka kesi hii iishe wanataka kusema kwamba Serikali ilitoa guarantee kwa IPTL, kitu cha ajabu sana. Sasa kilichofanya mgogoro ukaanza ilikuwa ni tariff, hawa IPTL wakasema kwamba wamewekeza shilingi milioni 163.53, TANESCO ikakataa. Nasema lile deni langu mtalilipa, anasema ile internal rate of return, yaani namna ya kurudisha akawa anasema anataka asilimia 23.1, TANESCO wakakataa. Riba yeah!

Kwa hiyo wakapelekana huko Uingereza, EXCED na EXCED ikakubaliana na TANESCO kwamba kweli fedha za uwekezaji equity ikapungua mpaka dola milioni 121.83 na ile riba ikapunguzwa mpaka 22.31. Sasa wakati ule walikuwa hawakuelewana ndiyo ikaanzishwa hiyo ESCRO. Vijana wengi ambao wanakwenda kwenye kompyuta, nendeni mtafute definition ya neno ESCRO. Maana yake watu wanaongea hapa wanasema fedha za umma, fedha za walipakodi, hawajui hata simple English.

Fedha za ESCRO hizi ni fedha zilizowekwa baada ya hawa
wafanyabiashara wawili kutokubaliana na zingeweza zikawekwa popote. Zingeweza kuepelekwa CRDB, NBC, siyo lazima ziende BOT. Kwa hiyo hapo ndipo ESCRO iliwekwa. Sasa ESCRO kuwekwa kama mtu hujui hizo fedha TANESCO imeambiwa badala ya kumlipa IPTL kwa sababu unao mgogoro, basi
fedha zikae pale. Kwa hiyo hizo fedha ni za IPTL, yaani ni kitu ambacho ni rahisi kabisa, lakini mtu anataka kupotosha hapa anasema fedha za walipakodi, fedha sijui za wakulima, hakuna kitu kama hicho.

Sasa unataka utumie umeme wa IPTL bure! Kama hutaki alipwe fedha hizo, unataka utumie umeme wake bure?

Kwa hiyo toka ESCRO iwe established fedha zilizokuwa zimewekwa humo ndizo hizo wanazosema bilioni 200. Sasa maswali ya kujiuliza, nimeshasema hapa, namshukuru Mheshimwa Masele umesema, wote hao wa Upinzani wanafukuzana kwenda mahakamani kila siku, sasa huu ni uamuzi uliotolewa na
Mahakama. Mwingine anasema eti tungengoja hukumu ya Uingereza, hiyo unadhalilisha Mahakama yetu. Wewe kama unataka kungoja unawahusudu kawangoje huko, lakini Mahakama yetu ni lazima isonge mbele.

Hii ni hukumu ya mwezi Septemba inasema hivi: Judgement ya
Mahakama hii sikilizeni; ni kwa Kiingereza nitaitafsiri kidogo. That VIP has sold all its shares in IPTL to Pan African Power Solution and the former convince to the letter its 30 percent shares and rights title and interest in IPTL and any other interest connected to the shares including moneys or part their of which VIP is entitled in the Tegeta ESCRO account kept with the BOT. Haya maamuzi Gavana anaweza kuyazuia haya? Muhongo anaweza kuyazuia haya? Waziri wa Fedha anaweza kuzuia haya?

SPIKA: Kiswahili!

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Oo! Kiswahili ni kwamba Kampuni ya VIP imeuza hisa zake zote kwa kampuni ya Pan African Power Solution na kwamba hizo asilimia 30 sasa ni za hiyo Kampuni mpya na hii Kampuni mpya iliyochukua ina haki ya kila kitu ikiwemo na fedha za ESCRO. Hii ni hukumu ya Mahakama Kuu ya tarehe 5 Septemba, 2013. Kweli Bunge tunaweza kuburuzwa kuanza majadiliano ya hukumu ya Mahakama hapa na kila siku mnasema mihimili isingiliane! Sasa kama mtu alikuwa anapinga hii na wenye document hamjazuiwa nendeni Mahakama Kuu mkapinge. Siyo kuja hapa kupoteza fedha za walipakodi na muda wetu watu hapa walitaka kwenda kufanya vitu vya maana, kama unapinga Mahakama, nenda mahakamani siyo bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyingine inasema: “The provision liquidator shall handle over all the affairs of IPTL including the IPTL Power Plant to Pan African Power Solution which has committed to pay off all a legitimate creditors of IPTL and to expand the plant capacity to about 500 megawatts and sell power to
TANESCO at a tariff between US six cents per unit in the shortest possible time after taking over the public interest.”

Inasema kwamba, yule aliyekuwa mufilisi amkabidhi huyo mnunuzi mpya Pan African Power Solution ambaye amekubali kulipa madeni yote yaliyokuwa IPTL. Sasa kama wewe una boksi la ma-documents hapa una rafiki zako wanadai IPTL, yuko tayari mkamdai huko siyo Bungeni hapa, mkamdai huko, hii ni hukumu ya Mahakama. Halafu amesema akipata atatoka sasa hivi ni megawatt mia moja anakwenda megawatt mia tano, anauza umeme kwa senti sita mpaka senti nane. Huu ndiyo unakuwa ufisadi au nyie mnaotetea ndiyo mnatetea ufisadi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu umeme wa bei mbaya duniani kote
unapatikana Tanzania ni kati ya senti thelathini na tano mpaka senti hamsini na tano kwa unit, American cents, hata huyu sasa hivi wanayemtuhumu na kumtukana sijui Singasinga, kwanza siyo uungwana huo.

Mheshimiwa Spika, mimi nimekulia pale Uhindini, siwezi kuwachukia Wahindi, Mtaa wetu ulikuwa unaitwa William Street, kwa hiyo sikuzoeni lugha ya kusema huyu ni Singasinga huyu ni chotara na huyu ni nani, hii lugha ya ajabu sana hii. Hawa ni mafashisti, huwezi ukatumia lugha kama hiyo.
(Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hawa wanaowashabikia, wanaowapa hayo madocument, wanatuuzia umeme wa bei ya chini kati ya thelathini na tano na hamsini na tano yeye anauza ishirini na sita nani mbaya hapo? Ni nani wanaoumwa nchi? Kwa nini usiumwe nchi uwafuate hao uwaambie na wao washuke? Halafu hapa anataka kutupatia umeme wa senti sita mpaka nane, hizi imprest zingine muwe mnaziacha. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kuna mwingine akasema wanaosema wangengoja uamuzi wa Uingereza. Ndiyo maana nasema, mtu akikufungia chumbani akakupa documents kama wewe ni mtu makini usiende nazo nje hovyo hovyo kabla hujazifanyia utafiti, ni lazima zitakuwa zinampendeza yeye huyo na utakuwa embarrassed, hata ukiongea unataka kupasuka itakuwa ni mtu unaonekana ni mediocrity ya hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, kwanza TANESCO haijafungua kesi yoyote dhidi ya IPTL kule Uingereza sasa ingoje nini? TANESCO haijafungua kesi yoyote dhidi ya IPTL kule Exeed Uingereza, sasa unasema wangoje Mahakama wangoje nini hawajafungua kesi huko? IPTL haina kesi yoyote dhidi ya TANESCO kule Exceed
unataka ingoje nini? Aliye na kesi kule ni Standard Chattered, ndiyo maana kukurupuka na karatasi mtaaibika.

Mheshimiwa Spika, je, ilikuwa ni halali fedha kutoka? Ilikuwa ni halali fedha kutoka? Jibu ni ndiyo uhalali wake kwanza ni hukumu ya Mahakama Kuu, Gavana angeacha kutoa fedha hizi angeshtakiwa, hawezi kukaidi amri ya Mahakama Kuu. Sasa unayekuja hapa na karatasi sijui na nini, labda itabidi tucheck

vyeti kusema kweli hapa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushahidi, kwa hiyo kuna hii Mahakama. Ya pili, kama Mheshimiwa Masele na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha alisema, zimewekwa hapo kwamba mkikubaliana, mje mchukue hizo fedha. Sasa wamekubaliana nani tena akazichukue? Kulikuwa na conditions mbili; ya Mahakama hiyo na yenyewe hiyo.

Kukubaliana ndugu zangu acha niwaeleze ukweli ni kwamba, mpaka wakati fedha zinachukuliwa za Escrow zilikuwa bilioni mia mbili, lakini kutokana na mauziano ya umeme na capacity charge, IPTL ilikuwa inaidai TANESCO bilioni mia tatu sabini nukta nane, kwa sababu kuna wakati TANESCO haikulipa huko fedha. Kwa hiyo, deni sasa hivi IPTL inaidai TANESCO bilioni mia moja na
sabini nukta nane, sawasawa na dola milioni mia moja nne.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa majadiliano yao kabla hawajawekeana sahihi na kwenda BOT kuchukua fedha, wamefanya yamepungua mpaka milioni sabini na tisa, sasa hapo ni kipi bora? Je, wakati fedha za Escrow zinatoka kodi zililipwa? Mtu anakurupuka kodi zimeibiwa, zimefanya nini
.
Mheshimiwa Spika, aliyeuza 30% ya Hisa zake kwa IPTL ambaye ni VIP alilipa kwanza kodi, alilipa VAT za shilingi karibu bilioni 39.46. Akalipa ushuru wa stempu bilioni 1.27, akalipa capital gain ambayo ni Sheria mpya imeanza, 30% alilipa dola za Kimarekani milioni 24.2. Kwa hiyo, yule aliyeuza thelathini amelipa, aliyeuza sabini, sasa hivi TRA inafanyia kazi kwa sababu haijakubaliana
na kiwango kile walichosema wameuziana. Sasa ni nani ametoroka kodi?

Mheshimiwa Spika, halafu kuna kitu kizuri kabisa ambacho ni cha muhimu, walipokwenda pale kuchukua fedha kama Mheshimiwa Massele alivyosema, kwanza Gavana anasema umeniletea hukumu ya Mahakama sawa! Lakini niletee kithibitisho kwamba wewe na TANESCO mmekubaliana, wakaenda wakapeleka, bado Gavana akasema hapana, haitoshi, wewe ukishachukua hizi fedha, hivi kama kuna mwingine atakuja kutudai tutafanyaje?

Mheshimiwa Spika, ikawekwa kinga Serikali ina kinga, Wanasheria wanaifahamu indemnity ina kinga ambayo inasema chochote kitakachotokea baada ya hizo fedha kuchukuliwa atakayekuwa na jukumu la aina yoyote iwe kesi, iwe VAT, iwe nini huyu aliyenunua Pan African Power Solution ndiyo anahusika, sasa kuna wizi gani hapa? Kwa hiyo, nimalize kwa kusema kwamba
tuheshimu maamuzi ya Bunge letu hili, tungoje CAG na TAKUKURU wafanye kazi.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, nadhani inabidi tuwe waangalifu sana hapa, la sivyo hili Bunge litakosa hadhi. Kesi ya kuanzia 1998, hii kesi imeanza mwaka 1998, hadi leo hii sisi tumeamua ni lazima iishe, hatuwezi kuwa tunalipa mabilioni kila mwaka.

[...]

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP