Sunday, January 4, 2015

Standard Chartered - Mwizi Aliyezidiwa Spidi?

Wahenga walinena kuwa "anayekutwa na ngozi ndiye mwizi wa ng'ombe". Wengine wanatumia neno "anayekamatwa". Wadadisi tumejikita kwenye neno 'kukutwa' badala ya 'kukamatwa' maana mhusika mkuu ambaye amekutwa na ngozi bado hajakamatwa.

Wakati tunasubiri mhusika huyo na washirika wake wakuu wakamatwe, washitakiwe na wafilisiwe tunatatizwa na kujirudiarudia kwa madai kuwa kulikuwa na mwingine ambaye naye alijaribu ila alizidiwa spidi/kasi. Kama ni kweli naye alitaka kutuingiza mjini si ni vyema naye tumjadili, tumwelewe na tujihadhari naye hasa siku za usoni? Tunawezaje kupuuzia tu madai hayo ambayo kwa namna moja au nyingine yanadhihirika ndani ya maneno hayo hapo chini ya kizalendo ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) alipokuwa anawajibu - na papo hapo kutowajibu - watoaji wa madai hayo wakati anajumuisha Hoja ya Kamati yake iliyotusaidia kwa kiasi kikubwa sana kumjua mhusika mkuu wa wizi wa Escrow?

---
[MHE. ZITTO ZUBERI KABWE - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI:]

"Mheshimiwa Spika, Mheshimwa Waziri wa Nishati na Madini ukurasa wa ishirini amezungumzia suala la kwamba TANESCO haina mashtaka na ICSID ila mashtaka ni ya Standard Chartered. Napenda nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba IPTL kabla haijawekwa kwenye muflisi ilifungua kesi kupinga kitendo cha TANESCO ku-dispute zile invoices. Kesi ilipoendelea kule mahakamani ICSID baadaye IPTL ikawekwa chini ya muflisi na mahakama zetu za Tanzania baada ya maombi ya mbia mmoja, Ndugu James Rugemalila. Na wabunge wengi, wengine wameingia humu mara ya kwanza ndio maana wamediriki hata kunitukana, hawanifahamu. Nataka niwakumbushe na Waziri wa Mambo ya Ndani ni shahidi yangu. Fedha hizi zilitaka kuanza kuibwa toka mwaka elfu mbili na nane [2008], elfu mbili na tisa [2009]. Mahakamani Jaji akaenda akaondoa amri ya kuiweka IPTL kwenye muflisi wakati  tuna kesi ambayo kwa kujenga hoja kwamba hii kampuni iko kwenye muflisi ile kesi tungeweza kushinda. Leo kuna baadhi ya wabunge wanahoji kuwa labda tunatumwa na Uingereza. Huyu Chikawe ni shahidi. Balozi wa Uingereza alikuja na delegation yake ya watu wa Standard Chartered kuniona kama Mwenyekiti wa POAC ku-lobby kwamba tuwaachie Standard Chartered wachukue hela za Escrow. Nikatoka nje ya kikao nikampigia simu Chikawe, wakati huo ni Waziri wa Justice, nikamwambia Chikawe hawa wanavunja diplomatic protocol, hawawezi kuja kwa Mwenyekiti wa Kamati hawana kibali cha Wizara ya Mambo ya Nje, wanakuja ku-lobby. Chikawe ni shahidi yangu akatae hapa, anikane. Hamna kingine kilichonituma kufanya hivyo, ni uzalendo kwa nchi yangu. Kwa hiyo, siwezi kuwajibu watu ambao kwa njia moja ama nyingine wameniparuraparura, siwezi kuwajibu; siwezi kuwajibu hata kidogo kwa sababu hawajui nini nilichokifanya kwa nchi hii. Mheshimiwa Spika, shauri lile kule ICSD tukashinda kwa kuhoji ya kwamba IPTL iko chini ya muflisi. Mahakama ikairuhusu Standard Chartered waingie kwa nafasi ya IPTL kwa sababu wanaidai IPTL. Kwa hiyo ikaingia mahakama. Na hoja pale ilikuwa ni Capacity Charges, kwamba tumekuwa overcharged. Tumeshitakiwa sisi kwamba kwa nini tuna-dispute invoices. Kesi imekwenda. Mwezi Februari mwaka huu shauri limeamuliwa kwamba, kwanza, ni kweli tumekuwa overcharged na, pili, ifanyike recalculation. Mheshimiwa Spika, maamuzi ya kesi haya hapa na nayawasilisha mezani kwako. Serikali leo inakuja kukataa maamuzi ambayo sisi tumeshinda na imeamuliwa recalculation, kwamba bei mpya ya umeme, bei mpya ya Capacity Charges iangaliwe kulingana na uwekezaji ambao wale watu wameweka. Sasa tunakujaje kukataa kitu ambacho sisi tumeshinda? Sasa ngoja niwaambie madhara yake. Mkataba ule baada ya maamuzi ya mwaka 2001, Capacity Charges zikashushwa mpaka dola milioni mbili nukta sita kila mwezi, kama tulivyoeleza kwenye Taarifa ya Kamati. Usipofanya recalculation maana yake ni kwamba mpaka sasa hivi, hivi mwezi huu wa Novemba unakwisha, huyo anayesema ni mmiliki mpya analipwa Capacity Charges ile ile. Tungefanya recalculation, hata kama huyo mtoto mpendwa Seth angeachiwa hiyo mitambo, Capacity Charges ingekuwa chini. Hivi tunafikiria namna gani kama nchi?" - https://www.youtube.com/watch?v=wT_R40LcZpU
---

Wadadisi tunaona ni vyema kukusanya hapo chini kwa pamoja dondoo/nukuu zinazopingana kuhusu suala hili kutoka kwenye Hansard ya Majadiliano ya Bunge (Mkutano wa 15 Kikao cha 22) ya Mei 30, 2014 inayopatikana katika kiunganishi hiki cha Tovuti ya Bunge http://polis.parliament.go.tz/PAMS/docs/HS-15-22-2014.pdf. Japo wahenga wamenena pia kuwa "mwamba ng'oma ngozi huvutia kwake", kujitahidi kuchambua hoja hizi kinzani kwa pamoja na kwa uhuru kunaweza kumsaidia mchambuzi husika kuelewa nini kiliendelea/kinaendelea nyuma ya pazia. Na si ndio hao hao wahenga waliosema kwamba "siku za mwizi ni arobaini"!
---
HANSARD UKURASA WA 136 & 138

[MHE. JOHN J. MNYIKA – MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KWA
WIZARA YA NISHATI NA MADINI MHE. JOHN J. MNYIKA:]

Mheshimiwa Spika, mwaka 2011 Benki ya Standard Hong-Kong ambayo ni mdeni mkuu katika sakata la IPTL ilifungua kesi ya madai katika mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICSID case Na. ARB/10/20) inayodai kiasi cha dola za Kimarekani milioni 225, pamoja na riba katika kuendesha kesi hiyo. Kampuni ya
uwakili ya Mkono (inayomilikiwa na Nimrod Mkono Mbunge wa CCM) ilipewa zabuni ya kuitetea Serikali katika shauri hilo, na kwa kujiamini iliishauri Serikali kuwa kesi hiyo tutashinda pamoja na wanasheria wengine kuwa na maoni kinzani kuhusu suala hilo. Kampuni ya Mkono imekuwa ikiishauri Serikali isifanye
usuluhishi nje ya mahakama ya ICSID wakati wadai kupitia kwa Mfilisi wa Mali na Madeni za IPTL (RITA) wanakubali kusuluhishwa nje ya mahakama.

[...]

Profesa Muhongo alisahau kuwa Tanesco iliyoweka fedha hizo ni shilika la umma na hivyo ni fedha za serikali, pili madhumuni ya fedha hizo hayajafikiwa na Tanesco wenyewe wanasema kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Uhusiano Tanesco Makao Makuu, kuwa hukumu kati ya Tanesco na IPTL inasema: “Mahakama hiyo (ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya
Uwekezaji) haikutangaza aliyeshinda wala kushindwa.

“Ilichofanya ni kutoa muda wa miezi mitatu kwa pande zote mbili, (Standard Charted Bank Hong Kong (SCB-HK)) na Tanesco kwenda kukubaliana nje ya Mahakama… kwa sasa kuna mazungumzo yanayoendelea kuhusu taratibu za kukokotoa gharama halisi.


Mheshimiwa Spika, huku nyuma tayari mafisadi wa Taifa hili wameshakwapua fedha hizo, mbaya zaidi hakuna anayekanusha kuhusu kuibiwa kwa fedha hizo sipokuwa mkazo unatiliwa kuliaminisha taifa kuwa fedha hizi hazikuwa za

serikali [...]
---

HANSARD UKURASA WA 166

[MHE. DAVID Z. KAFULILA:]

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshindwa kujichunguza tangu mwaka 1995 mpaka leo, bado Bunge mnaamini kwamba Serikali ijichunguze? Msichanganye matatizo hapa. Watu wanasema ooh sijui mara Mengi, mara Standard Charted, mara Uingereza, hoja ya msingi iliyoko Mezani ni shilingi bilioni 200, bring back our money? Rudisheni na lazima zirudishwe. (Makofi)
---

HANSARD UKURASA WA 302-303

[NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (MHE. STEPHEN J. MASELE):]

Mheshimiwa Spika, lakini ni aibu kwa Serikali ya Waziri Mkuu David Cameron kwa Balozi wake kufanya uwakala wa Benki ya Standard Chartered, kuishawishi Serikali ya Tanzania ikope fedha ili zilipe madeni ya kampuni binafsi, jambo ambalo Mheshimiwa Rais Kikwete amelikataa kwa nguvu zote, Serikali yake haiwezi kubeba mzigo wa makampuni binafsi. Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa msimamo wa kizalendo na kuipenda nchi yake. (Makofi)

[...]

Mheshimiwa Spika, mtakuwa mnashuhudia matendo mengi
yanaendelea, lakini nashukuru sana Mheshimiwa Kafulila leo ameweza kutoa siri ya mambo ambayo yanaendelea. Balozi anafanya vitendo ambavyo havina hadhi ya ubalozi. Deni la Standard Chartered ambalo inadai IPTL ni za makampuni binafsi yaliyokopeshana kwa utaratibu wao. Inakuwaje unailazimisha Serikali yetu sisi ikope pesa Standard Chartered ikalipie deni la

kampuni binafsi? Hiyo kweli inaingia akilini? (Makofi)

[...]

HANSARD UKURASA WA 313-315 & 317

[MHE. PROF. SOSPETER MUHONGO (WAZIRI WA NISHATI NA MADINI):]

Mheshimiwa Spika, nilikuwa sipendi kuongelea mambo ya IPTL kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu alishatoa tamko na wote tukaafiki bungeni kwamba hii kazi tumuachie CAG na TAKUKURU halafu wailete hapa bungeni. Lakini kwa sababu mengi yameongelewa, nataka tu nitoe ufafanuzi mfupi kabisa. Kwanza hii document, niwaombe ndugu zangu Wabunge mimi
mwenyewe kwenye hili sakata nimeonana na Balozi ambaye amehamia Kongo, Balozi huyu wa sasa nimeshakaa naye vikao.

Nimekaa vikao na Mawaziri wawili wa Uingereza na wote wanaafiki kwamba siyo jambo jepesi. Kwanza tukianza kuongea nao, wengine wanasema tuachane nayo, tuongee mambo yetu ya ushirikiano wa Kiserikali kwa sababu haya ni makampuni kwa makampuni yanapambana. Hilo la kwanza.

La pili, hizi documents kila mtu anajidai anakuja nazo hapa, mimi nina documents ambazo nikileta hapa karibu zinajaza gari moja. Nina documents ambazo zinaweza zikajaza kigari kimoja cha tani moja hivi.

Kwa hiyo mtu kukurupuka tu anakuja hapa anaongea anataka kuruka hewani ana ushahidi, ni watu ambao siyo makini na hivi ni vitu vya Mahakama, unaweza ukajidhalilisha bure, unajidhalilisha, labda wameshakupatia imprest, ukija kui-retire humu unajidhalilisha. Na hili Bunge jamani tujitahidi tusiwe financial mercenaries hapa. (Kicheko/Makofi)

Kwa mfano hii aliyoileta huyu sasa hivi anaiacha hapa ambayo inatoka Power of Attorney ambayo imetolewa na Mike Joseph Monterino, haiwezi kukubalika. Kwanza haina tarehe, haijasajiliwa popote nchini hapa. Kati ya hao waliowasilisha hapa mojawapo imeshakuwa fake na mimi nadhani siihitaji labda muiweke kwenye dust bin tu. Kwa hiyo haya mambo ya kusema unaruka na document, mimi nadhani nina documents nyingi kuwazidi nyie wote ambao mnasema mna documents. Nina documents za IPTL, nina documents za MECMA, nina documents za VIP, za Standard Chartered, nina documents zote.

Sasa mtu ambaye ana busara na hasa mwenye elimu nzuri huwezi
ukakurupuka unakuja hapa umevimba kabisa una ushahidi na hapa siyo mahakamani na nashauri Bunge hili watu wasijaribu kulitumia vibaya na kuligeuza liwe Mahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika na Watanzania wote mnaonisikiliza, IPTL historia yake ni ndefu ilitokea miaka ya 1990 enzi ya awamu ya Serikali ya pili wakati tulikuwa na ukame. Lakini wakati huo sheria na sera za nchi zilikuwa haziruhusu mtu binafsi kufua umeme, ilikuwa ni TANESCO peke yake. Kwa hiyo sera ikabadilishwa na
sera ilivyobadilishwa, nadhani siku moja mlisikia ukame ukiwa mkubwa kweli kweli miaka ya mwanzoni ya 1990, aliyekuwa Waziri wa Mipango marehemu Kolimba ndiye alitumwa kwenda Malaysia kulishughulikia hili.

Sasa niwaeleze kitu ambacho kimeanza miaka ya 1990 mpaka leo hii eti tukijaribu kukitatua tukimalize kama Taifa twende mbele wengine hawataki kwa sababu ya mirija yao. Sasa niwathibitishie Watanzania mtu aje hapa na lori ya ma-documents na nini ni lazima kesi hii iishe. Kesi hii kutoisha madhara yake ni haya yafuatayo:- Kwanza heshima ya Taifa inashuka chini kwamba hili ni Taifa
ambalo kwanza ukienda kuwekeza huko utajiingiza kwenye migogoro ambayo haina mwisho. Halafu hawa watu wanaotupatia fedha wakitaka kutukomoa wanajishika kwa IPTL.

Sasa unaona hiyo ndiyo maana wewe kama ni mzalendo wa kweli huwezi ukaja hapa unang'ang'ana na IPTL usioijua. Wote walioongea humu nawahakikishia hawajui mambo ya IPTL. Ni watu wamefungiwa chumbani wakakochiwa wakapewa, maana yake akapewa selective document. Mtu aliyempa document ni ile iliyokuwa inam-favour yeye. Kwa hiyo akachambua hizi, ushahidi huu, nenda. Lakini upande wa pili unaufahamu? Inabidi watu wengine kusema kweli itabidi nitakuja na ku-check vyeti vya watu hapa kidogo. (Kicheko)

Sasa baada ya IPTL kuingia nchini hapa, hadithi ni ndefu sana, lakini mwisho wake ni kwamba MECMA alikuwa na asilimia 70 na Rugemalira alikuwa na asilimia 30 (VIP). Mimi mwenyewe documents nilizonazo, hizo asilimia 70 na 30 hawakubaliani, hawatambuani. Ukimwambia VIP, MECMA walikuwa na 70,
anasema hapana. Ukimwambia MECMA, VIP ilikuwa na asilimia 30 anasema hapana. Hiyo nayo ni kesi inaweza ikakuchukua miaka miwili mitatu au zaidi. Kwa nini Bunge letu lipoteze muda kuongea kitu kama hicho.

Ukiacha hao wanahisa hao, kwa hiyo hapa kitu ambacho kinaleta
mgogoro na msemaji mmoja amegusia, hapa ipo TANESCO, hapa ipo IPTL. TANESCO inanunua umeme kutoka IPTL. Lakini hawa wajanja ambao hawataki hii kesi isiishe wanazunguka na mikoba ya documents wanataka kuingiza TANESCO kwenye kesi za madeni ya IPTL. Ee, Profesa mwenzangu umenunua daladala, mimi napanda daladala yako kweli mimi nina haki ya kujiingiza kwenye madeni ulikokopa fedha kununua daladala? Ndiyo hawa wanataka kutuingiza huku.

Halafu kitu kingine wanataka kutuingiza ambacho hakifai, sasa akatokea hii Standard Chartered, IPTL amekopa fedha huko ameshindwa kulipa, akajitokeza Standard Chartered akayanunua yale madeni. Hawa wajanja wanataka TANESCO na Serikali yetu iingie vilevile kwenye kesi ya Standard Chartered na IPTL kitu hakiwezekani. 
[...]

Mheshimiwa Spika, sasa kuna mwingine akasema wanaosema wangengoja uamuzi wa Uingereza. Ndiyo maana nasema, mtu akikufungia chumbani akakupa documents kama wewe ni mtu makini usiende nazo nje hovyo hovyo kabla hujazifanyia utafiti, ni lazima zitakuwa zinampendeza yeye huyo na utakuwa embarrassed, hata ukiongea unataka kupasuka itakuwa ni mtu unaonekana ni mediocrity ya hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, kwanza TANESCO haijafungua kesi yoyote dhidi ya IPTL kule Uingereza sasa ingoje nini? TANESCO haijafungua kesi yoyote dhidi ya IPTL kule Exeed Uingereza, sasa unasema wangoje Mahakama wangoje nini hawajafungua kesi huko? IPTL haina kesi yoyote dhidi ya TANESCO kule Exceed unataka ingoje nini? Aliye na kesi kule ni Standard Chattered, ndiyo maana kukurupuka na karatasi mtaaibika.

[...]

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP