Saturday, January 24, 2015

Upya wa January Makamba

Upya wa January Makamba

“Mabadiliko haya tuyatakayo yana sura ipi?” – Padre Privatus Karugendo

Chambi Chachage

Siasa za Urais zimechukua sura ‘mpya’. January Makamba ameibuka na kitabu kipya. Ni cha mazungumzo Kuhusu Tanzania Mpya aliyoyafanya na Padre Privatus Karugendo.

Ndani ya kitabu hicho kuna maneno mengi tu matamu yanayoweza hata kumtoa nyoka pangoni. Jukumu langu katika uchambuzi huu siyo kuyaimba kama kasuku. Kazi yangu  ni kudadisi na kuibua maswali zaidi ili tumfahamu kwa kina mgombea Urais mtarajiwa.

Maadam kina maswali na majibu 40, uchambuzi huu utajikita katika hoja mbalimbali zilizoibuka humo. Lakini kwa kuzingatia maangalizo ya wanazuoni wawili, udadisi huu hautajibana tu kwenye kitabu hicho na kuishia tu kujadili masuala ndani ya mabano aliyoyaweka January. Bali kitapitia vyanzo vingine mbadala hasa vilivyopo mitandaoni.

Pia maadam mdadisi anasisitiza kuwa Tunahitaji Viongozi Wenye U Tatu, yaani “Utu”, “Uadilifu” na “Utaalamu” basi udadisi huu utapima majibu ya January kwa kuzingatia U hizo. Kazi hiyo haitakuwa ngumu sana maana majibu hayo yanajadili U nyingi – “Uthubutu”, “Uzoefu”, “Ujana”, “Ujasiri”, “Ubora’, “Uadilifu” na kadhalika.

Lakini vivumishi vilivyojazana kitabuni ni vinavyotokana na mzizi “-pya-”.  Humo kuna “upya”, “mpya”, “jipya”, “vipya”, “mapya” na “kipya”. Maneno hayo yanayoashiria upya yapo 156 katika kitabu hicho chenye kurasa 196. Hivyo, tuanze kwanza kuidadisi U hiyo.

Upya
Wachambuzi wa masuala ‘mapya’ huwa tunashtuka tunapoona matumizi ya kivumishi chenye ‘-pya-’ hasa kwenye kichwa (kikuu) cha habari. Kwa kawaida swali la kwanza tunalojiuliza lina muundo huu: “Ni nini kipya kuhusu kinachosemwa kuwa ni kipya?

Je, ni nini kipya katika “Tanzania Mpya” anayoiongelea January? Anatuambia hivi: “Rais ajaye ana kazi kubwa zaidi ya kusimamia umoja wa nchi yetu na usalama, amani na utulivu kuliko viongozi waliopita. Huu ni msitu mpya kabisa” (Uk. 3).

Kwa maana nyingine, Tanzania ya sasa ina hatari zaidi kuliko ya enzi za majaribio ya mapinduzi ya miaka ya 60, vita dhidi ya Nduli Idi Amin vya miaka ya 70, uhujumu uchumi wa miaka ya 80, na machafuko ya kidini ya Mwembechai ya miaka ya 90.

Yaani, huyo Rais mpya ajaye wa awamu ya tano atakabiliana na “msitu mpya kabisa” na hivyo kuwa na “kazi kubwa zaidi” (kuliko marais wa awamu ya kwanza hadi ya nne) ya kukabiliana na hatari iliyopo “ya taifa letu kupasuka - kutokana na dalili za mpasuko wa kidini, mmomonyoko wa maadili kwenye jamii, kuporomoka kwa imani ya wananchi kwa Dola, ufa katika Muungano na umasikini na tofauti kubwa ya kipato baina ya watu na hali ya kukata tamaa miongoni mwa wananchi” (Uk. 2).

Kwenye suala mmojawapo katika huo anaouita “msitu mpya kabisa”, January anasema hivi: “Changamoto ya Rais ajaye ni kufufua ndoto na dhamira ya Muungano kwa kuupatia sababu mpya.” (Uk. 5). Lakini kitabuni hatuoni hizo sababu mpya. Ni tamanio tu.

Tunachoona kitabuni ni hiki: “Muungano wetu umetikiswa. Nimejiridhisha kwamba kiongozi ajaye lazima ahakikishe Muungano wetu unajibu changamoto za umasikini na changamoto za kimuundo, mambo ambayo yamezaa hoja na kelele za kuuvunja. Uhai wa Muungano utategemea sana ni kwa jinsi gani unawasaidia Watanzania wa pande zote kwa kuwapa fursa ya kuendeleza ndoto zao za kiuchumi na kijamii. Kinyume na hapo, Muungano utakuwa mali ya viongozi na wanasiasa na hautadumu” (Uk. 5).

Maono mapya hapo ni matamanio tu maana tunaendelea kusisitiziwa kuwa “Ubunifu unahitajika katika kuweka taasisi na miundo itakayotoa fursa zaidi kwa wananchi wa Tanzania na haswa Wazanzibari kuondokana na umasikini, na kuondoa mpasuko miongoni mwa jamii ya Wazanzibari” (Uk. 5). U nyingine hiyo ya Ubunifu ila uko wapi humo?

Ili walau tuone ubunifu huo mpya kuhusu Muungano Wadadisi tunalazimika kurejea mchango wake kwenye Bunge Maaalum la Katiba kama ulivyorekodiwa kwenye video iliyopo mtandaoni. Hayo aliyasema mwaka 2014 na maadam hajayakanusha kwenye kitabu basi ndiyo angalau yanaweza kutupa picha ya maono yake kuhusu hiyo miundo anayoiongelea kitabuni na inayomfanya aseme kuwa “Rais ajaye afanikiwe kuwashawishi Watanzania kuhusu azma yake ya kusimamia Muungano usivunjike kutokana na mashinikizo ya viongozi wachache wenye ajenda binafsi na uchu wa madaraka” (Uk. 6).

Baadhi ya maneno aliyoyasema January humo Bungeni ni haya: “Ndugu Mwenyekiti, waasisi wetu walitazama miundo yote, walitafakari miundo yote kwa kina. Nilipata bahati ya kukaa na Mzee Lusinde, Mzee Job Lusinde ambaye alikuwepo kwenye majadiliano ya kuamua aina ya Muungano ambao tuwe nao. Dhana inayojengeka hapa ni kwamba wale wazee hawakuwa na maarifa, walirukia tu kwenye muundo wa Serikali Mbili. Walitafakari miundo yote ya Muungano iliyopo: walitafakari Serikali Moja, walitafakari muungano wa Serikali Tatu, walitafakari Shirikisho na mingine mingi; na wakaamua, baada ya tafakuri ya kina, kwa kutazama mazingira yetu, kwa kutazama mazingira mahususi ya nchi zetu, kwamba muundo wa Serikali Mbili ndiyo ambao ungetufaa. Ndugu Mwenyekiti, katika azma ile ya kuunda taifa lenye nguvu, ya kurasimisha udugu, waliona kwamba wangeenda na Serikali Tatu, azma ile ingeisha, ingeishia katikati, tusingefika mbali, tusingefika leo kwenye Muungano wenye umri wa miaka 50”.

Sehemu ya hitimisho la utangulizi huo wa hoja ya January ni hili: “Ndugu Mwenyekiti , kama tunataka kuvunja Muungano wetu, kama tunataka kuvunja Muungano wetu – maanake lazima tuwe wakweli sisi ni viongozi hapa – basi twende kinyume na ile busara; kama tunataka Muungano wetu uvunjike ndani ya mwaka mmoja, ndani ya miaka miwili, tuingie kwenye Serikali Tatu”.

Mti mwingine kwenye “msitu mpya kabisa” wa January ni tishio la udini. Suluhisho lake analielezea hivi: “Tatizo ni viongozi wachache, wa kisiasa na kijamii, ambao wanatumia dini kufanikisha malengo yao ya kisiasa na kijamii kwa kuchochea chuki baina ya watu wa dini tofauti. Watu hawa ni hatari sana ni lazima tuwabaini, tuwatenge, tuwadhibiti na tuwaadhibu haraka sana. Serikali yetu inao wajibu katika hili lakini pia jamii inao wajibu” (Uk. 132).

Pia anasema: “Kama kuna hujuma inafanyika ili kutugawa kwa misingi ya kidini vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vifanye kazi ya kubaini hujuma hizo na kuzidhibiti” (Uk. 133). Na anatoa wito huu pia: “sisi viongozi wa siasa tutimize wajibu wetu” (Uk. 132).

Rai nyingine anayoitoa January ni hii: “Na wale wanasiasa wanaoomba nafasi za kisiasa kwa misingi ya dini nao wanapaswa kuwekwa pembeni, kama ambavyo Mwalimu Nyerere alituasa” (Uk. 133).

Hakuna maono mapya hapo kuhusu suala la udini. Sana sana tunachokiona ni kitabu ambacho kimeandikwa na Padre na Alhaj na picha za January akiwa na viongozi wa dini mbalimbali, kitu ambacho labda kinajaribu kutuambia kwamba January siyo mdini. Lakini uchambuzi wa picha zilizopo kitabuni nao unaibua maswali ya kidadisi: Kwa nini kuna picha kadhaa akiwa na viongozi wa dini ya Kikristo au akiwa kwenye taasisi mbalimbali za Kikristo ilhali inapokuja kwa Waislamu/Uislamu kuna picha moja tu “akiwa kwenye Maulid jimboni Bumbuli” (Uk. 135).

Jibu pengine ni rahisi maana hizo picha na viongozi wa Wakristo ni za kutoka kwenye madhehebu mbalimbali. Lakini kwani Waislamu hawana madhehebu mbalimbali yenye viongozi wao? Picha kama ya “January Makamba alipotembelea shule [ya] Sekondari ya Mtakatifu Maria Mazinde Juu, Lushoto” (Uk. 99) inaweza kuelezewa kirahisi maana huko ndiko maeneo ya jimboni kwake yalipo. Lakini tunapata shida kuelezea picha ya “January Makamba akisalimiana na wanafunzi wa Sekondari ya Mtakatifu Agnes inayomilikiwa na Kanisa Katoliki la Jimbo la Mahenge” (Uk. 44). Ni vigumu kuelezea picha ya “January Makamba akihutubia katika mkutano wa vijana wa makanisa ya Pentekoste” (Uk. 96) ilhali hatuoni picha zingine akiwa kwenye mikutano ya vijana wa dini zingine.

Pamoja na hayo hivi ndivyo January anavyohitimisha maono yake kuhusu dini na uongozi: “Nchi yetu ili istawi na kushamiri ni muhimu kwa viongozi wake na watu wake kumpenda Mungu na kufuata mafundisho yake. Dini ya kiongozi haipaswi kuongoza nchi lakini imani kwamba Mungu yupo ni muhimu kiongozi awe nayo. Mtu ambaye hamjui wala hamuogopi Mungu hafai uwa kiongozi” (Uk. 134); “Kiongozi anaweza kuwa wa dini yoyote lakini cha muhimu asiwe mdini. Watanzania wa dini yoyote wapo tayari kuchagua kiongozi wa dini yoyote. Ambacho hawataki ni kiongozi mdini. Naomba nimalize kwa kusema, Tanzania ni nchi yenye waumini wa dini tofauti ila misingi ya upendo, heshima, amani, umoja, mshikamano, ujirani mwema ipo kwenye vitabu vyote vya Mungu lakini pia ipo kwenye katiba na sheria zetu. Hivyo sisi kama viongozi tutahakikisha kwamba misingi hii muhimu ya dini na katiba tunaisimamia” (Uk. 136).

Uadilifu
Kwenye “msitu mkubwa mpya” wa January pia kuna U ya uadilifu. Hivi ndivyo anavyouhusianisha na uongozi: “Watanzania hawatafuti mwanasiasa mkongwe kuwaongoza, wanatafuta kiongozi mahiri na mwadilifu wa zama mpya” (Uk. 28).

Pia anasisitiza kuwa “Ukomavu wa kiongozi haupo kwenye umri wake bali kwenye maarifa yake na busara zake na malezi yake na uadilifu na uzalendo wake” (Uk. 30).

Uadilifu, kwa mujibu wa dhana ya Udadisi wa Viongozi Wenye U Tatu, ni kigezo muhimu sana. Kigezo hiki kinaendana na U za ‘Ukweli’, ‘Uwazi’, na ‘Ujasiri’.  Japo majibu ya January hayatuambii moja kwa moja kuwa ‘Mimi, January, ni mwadilifu’, uchambuzi wa matumizi yake ya neno hilo yanayoonyesha kuwa anajibainisha/anajitambulisha hivyo.

Ni kazi ngumu sana kwa mwananchi ambaye hamjui January binafsi kuthibitisha kuwa ni mwadilifu au la. Kwa kuanza jaribio hili labda ni vyema kulirejea jibu lifuatalo na kisha kumuuliza maswali ya nyongeza: “Kwa hiyo, wakati mwingine napata shida kidogo kutoka kwa ndugu na jamaa na marafiki kwa sababu katika vitu ambavyo binafsi havinisumbui ni haja ya kukusanya mali, majumba, magari ya kifahari na kadhalika. Falsafa yangu ni kwamba hapa duniani tunapita tu kutimiza mapenzi ya Mungu na kwamba hakuna mtu atakayekumbukwa kwa mali zake bali kwa mchango wake kwa jamii pana na labda pia kwa uadilifu wa watoto aliowakuza na kuwalea. Hii haipaswi kuwa kauli-mbiu tu ya kisiasa kwa ajili ya kufurahisha watu bali inapaswa kuwa imani ya ndani ya moyo kabisa” (Uk. 21).

January, je, umeorodhesha mali zako kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia maadili ya viongozi? Kama ndiyo, je, mali hizo zina thamani ya shilingi ngapi? Na kama bado, kwa nini? Unaweza kutuwekea wazi magazetini na vitabuni vielelezo tuthibitishe pasipo shaka?

Majibu yake ya maswali hayo ya nyongeza yatatusaidia wadadisi kuelewa haya maelezo yake mengine kitabuni kuhusu Kampuni/Shirika la Maendeleo la Bumbuli: “Shirika hili nililianzisha kwa mtaji wa fedha yangu ya mfukoni ambayo ilikuwa ni mkopo wa magari ya Wabunge. Tumefanikiwa sana kwenye mambo kadhaa lakini pia tumekabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo fedha za uendeshaji wa shughuli zetu. Kwa kiasi kikubwa bado natumia fedha zangu kusaidia shughuli za Shirika. Tulitegemea misaada kadhaa kutoka maeneo mbalimbali lakini imechelewa” (Uk. 31).

Sijui wabunge wanakopeshwa shilingi ngapi, niliwahi tu kuambiwa na Mbunge mmoja kuwa aliwahi kukopa shilingi milioni 30. Ila jibu la January litatusaidia kujua ni namna gani huo mkopo – pengine na vyanzo vyake vingine vya mapato ambavyo navyo ni haki yetu wananchi/wapiga kura kujua – umetosha kupata fedha hizi zilizoelezwa kitabuni: “Hata hivyo, nafarijika kwamba program tulizozianzisha zinaenda vizuri. Program kubwa ni ile ya ukopeshaji, ambapo hadi sasa tumekopesha karibu shilingi milioni 250 kwa vikundi vya wajasiriamali Bumbuli, wengi wao wakiwa kina mama” (Uk. 31).

Hali kadhalika tungependa kujua gharama za kuchapisha hiki kitabu zimetoka wapi maana japo kinauzwa shilingi 5,000 kwenye duka la vitabu la TPH, kuna watu wengi sana ninaowajua – nikiwemo mimi mwenyewe – ambao tumeletewa nakala za bure na pia kimetolewa kwenye magazeti na kwa uelewa/uzoefu wangu mara nyingi huwa ni lazima ulipie kufanya hivyo au wamiliki wenyewe wa gazeti wasamehe malipo. Je, ni nakala ngapi za bure zimetolewa? Gharama zake ni shilingi ngapi? Nani anazigharamia?

Kwenye hili pengine rafiki yangu Padre Karugendo naye anaweza kutusaidia kulijibu maana kwenye utangulizi wa kitabu hicho ameandika maneno haya: “Nilifaidi mazungumzo yetu na nikaona makala peke yake haitatenda haki juu ya kina na mapana ya mazungumzo yetu. Nilipenda watu wayapate kama nilivyoyapata mimi bila ya kupunguza au kuhariri chochote. Nikaamua nichukue muda, kwa kushirikiana naye, kutafuta uwezo wa kuchapisha hiki kitabu” (Uk. ix ). Uwezo huo mliupatapataje?

Kulinda maadili kunaendana na kuzuia migongano wa maslahi. Na tafsiri ya Udadisi ya mgongano wa maslahi, kama ilivyochambuliwa kwenye Fungate la Uwekezaji na Migogoro ya Maslahi pamoja na Lionel Cliffe na Mgongano wa Maslahi Tanzania, inagusa hata maslahi yasiyo ya kifedha kama vile ‘umaarufu wa kisiasa’, au ‘kiki’ kama wanavyosema vijana wa ‘kizazi kipya’. Hivyo, ni vyema tukaelewa ni kwa misingi gani mtumishi wa umma anaweza kutumia pesa zake kama kisa hiki kinavyoonyesha na anazuiaje/anadhibitije kitendo hicho kisimpatie maslahi ya umaarufu wa kisiasa: “Katika kampeni za uchaguzi za mwaka 2005, ambapo nilishiriki kama Msaidizi wa Mgombea Urais wa CCM, Mheshimiwa Kikwete, nilishauriana naye na tukaamua tuwashirikishe hawa wasanii kwenye mikutano yetu na shughuli zetu. Tukaanza na Bushoke. Akabadilisha wimbo wake wa Mume Bwege na kuweka maneno mapya na ukawa wimbo wa kampeni za CCM. Nakumbuka pesa ya kwenda kurekodi upya nilitoa mfukoni mwangu. Baada ya hapo, wasanii wengine karibu wote nao wakaingia. Rais akawapenda wote. Akawa anakula nao chakula, anapiga nao picha. Alivyoingia madarakani, kwa mara ya kwanza kabisa, wanamuziki hawa tukawaalika Ikulu. Mwanzo jambo hili lilistua wengi na kuzua mjadala lakini baadaye likaonekana ni jambo la kawaida. Na Serikali nzima ikaona ni sawa kuwashirikisha kwenye shughuli za kiserikali. Baadaye ikawa hivyo hivyo kwa wasanii wa filamu na wengineo. Kwa hiyo, nilifungua mlango kwa wasanii vijana kuanza kutambuliwa na Serikali na viongozi wa Serikali. Lakini pia nilikuwa mfadhili wa mwanzo kabisa wa Tanzania House of Talent” (Uk. 138-139).

Hilo ni muhimu hasa ukizingatia kuwa kampeni ya Ubunge wa January zilihanikizwa/zilitumbuizwa na wimbo wa Bumbuli Songa ulioimbwa na msanii Jobiso. Umuhimu huo ni mzito zaidi sasa hivi ambapo January ni Naibu Waziri na ‘Rais Mtarajiwa’ ilhali anafanya vitu kama hivi vifuatavyo ambavyo hata kama kweli ni vya ‘nia njema’ vina(fungua mianya ya) migongano ya maslahi: “Lakini vilevile kwa nafasi yangu ya sasa, nimefanya vikao na wahusika, hasa makampuni ya simu, kuhusu utaratibu wa malipo kwenye miito ya simu. Bado hatujamaliza lakini mambo yamebadilika kidogo na yataendelea kubadilika. Lakini pia nimeshiriki katika kuweka presha ya mwanzo kwa vyombo vya habari, redio na televisheni, kuwalipa wasanii pale wanapopiga nyimbo zao. Nilitambulisha kwa Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Kigoda, vijana wenye teknolojia na utaratibu wa kuweza kubaini nyimbo zote zilizopigwa na redio na luninga zote, au filamu zote zilizoonyeshwa kwenye luninga, siku gani na kwa muda gani. Mazungumzo kati ya COSOTA, wenye redio na TV na wasanii yamefanyika mara kadhaa na mradi mpya umeanzishwa na Ndugu Rashid Shamte na unaosimamiwa na produsa mkongwe hapa nchini, P-Funk, kwa ajili ya kufanikisha jambo hilo. Pia nimeendelea kuwasaidia wasanii hawa mmoja mmoja kwa shida zao mahsusi. Nisingependa kuwataja na kuzitaja hapa kwa sababu sio ustaarabu ila wasanii wengi wanajua kwamba mimi ni rafiki yao na mtu wao na nitaendelea kuwa hivyo. Yapo mengi nimeyafanya kimya kimya kusaidia tasnia hizi, ambayo siwezi kuyaorodhesha yote hapa” (Uk. 139).

Pia ni vyema tukaelezwa na tukaelewa jinsi ‘ushiriki/umiliki’ wa January katika Kampuni/Shirika la Maendeleo la Bumbuli hauleti mgongano wa kimaslahi hasa ukizingatia yeye ni kiongozi wa umma ihali taasisi hiyo ina mwonekano mwonekano wa ‘sekta binafsi’ na kutuletea hisia kuwa ni ‘kampuni binafsi’.

Ni vyema hilo likawekwa wazi mapema kabisa maana humo kitabuni kuna majibu kama haya kutoka kwa January: “Pia tunatoa ushauri na kushirikiana na Halmashauri ya Bumbuli kuiwezesha kupata mtaji wa shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuwekeza kwenye shughuli za maendeleo” (Uk. 32);  “Shirika la Maendeleo la Bumbuli litaendelea kubaki milele na kuwasaidia wananchi” (Uk. 36).

Sasa January akishinda Urais umelele huu utakuwaje? Je, atamrithisha mtu mwingine (binafsi) kampuni/shirika? Atazuiaje upendeleo unaoweza kutokea kwa kuwa yeye amekuwa Rais?

Ukweli
Ukweli ni nguzo muhimu sana ya uadilifu, hivyo, itakuwa vyema January akatusaidia kujua kama baadhi ya majibu yake kwa hakika ni ya ukweli – au ni ya uwongo (wa kisiasa). Pia ni vyema kujua kama utata wa baadhi ya majibu yake unatokana na tatizo la uelewa – ama wa msomaji, mwandishi au ‘mwandikwa’. Na pale ambapo inaonekana hakuna ‘uwazi’ kwenye majibu yake, je, ni kwa sababu ya propaganda za kisiasa?

Tuanze na historia ya elimu. Kwenye kitabu anatuambia hivi: “Nilipata daraja la kwanza kwenye mtihani wa kanda wa mock wa kidato cha nne, nikiwa na uhakika wa kuendelea na A-Level katika Shule ya Sekondari Kibaha, shule pekee iliyokuwa inafundisha mchepuo wa CBA hapa nchini. Hata hivyo, nilifanyiwa hujuma kubwa kutokana na siasa zinazomhusu Mzee wangu na kufutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne. Sikufa moyo, nilirudia mtihani kama mtahiniwa binafsi na kufaulu na kuweza kusoma A-Level katika Shule ya Sekondari Forest Hill Morogoro na nikapata Daraja la Pili kwenye mtihani wa Kidato cha Sita” (Uk. 14-15).

Lakini kwenye tovuti yake aliwahi kutuambia hivi: “So, we did our exams – and the day to go and look for the result came. And, to the shock of friends and family and teachers, my name was not there in the results sheet. I felt like collapsing. I went to another result centre thinking that there was a mistake – again, nothing. Inquiries to the reasons were not responded to immediately. Later we learnt that I was mistakenly linked to a cheating scam that one of the teachers was involved in. I was a pawn in a terrible mistake. A really long and painful story”.

Sasa swali la kiudadisi ni: Hiki kisa cha mwalimu aliyeshiriki katika huo ufisadi wa  mitihani kina uhusiano gani na kisa cha siasa za Mzee Makamba hadi uhusiano huo ukapelekea mtoto wake afutiwe matokeo? Ni watu wangapi ‘huria’ ambao wamedhibitisha kuwa kisa cha kweli ni kipi hasa? Ni swali muhimu kwa sababu kwa wale tuliosoma sekondari miaka hiyo tunakumbuka kuwa uwizi wa mitihani (‘mafeki’) ulikuwa umeshamiri na kuna wakati hata wanafunzi wenye akili nao walishiriki kuiba ili wasipitwe.

Kwa wale ambao tulikuwa tunafuatilia sana mfumo wa elimu ya Vyuo Vidogo vya Jamii (Community Colleges) nchini Marekani katika miaka ya 90, tunafahamu kuwa moja ya mbinu za Watanzania kufika Marekani na baadaye kupata udahili katika Chuo Kikubwa Kiasi (College) au Chuo Kikuu (University), hasa pale matokeo yetu ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita yanapokuwa siyo mazuri, ni hiyo ya njia ya ‘Community Colleges’. Hivyo, ni vyema pia January akawa muwazi zaidi kwenye haya maelezo yake ya ziada ili kuondoa utata hasa kwa wale ambao wanashuku ukweli kuhusu historia ya awali ya elimu yake ya juu, jambo tete ambalo tunaona linatikisa sasa hata kampeni kali za Urais huko Nigeria: “Lakini kilikuwa Chuo aghali kidogo, kwa hiyo nikaanza kusoma masomo ya awali kwenye Chuo kingine kidogo katika jiji la Boston kinachoitwa Quincy College na baadae nikajiunga na St. John’s University na kupata shahada ya kwanza ya sayansi ya masomo ya amani (Bachelor of Science in Peace Studies)” (Uk. 15).

Ni vyema January atoe jibu thabiti na vithibitisho ili wapiga kura wake tusije tukaona kwamba na yeye ni miongoni mwa wale wale ambao Jenerali Ulimwengu amewaelezea hivi: “Tumeona…. jinsi kitoto kilichozaliwa katika familia ya mafisadi kinavyolelewa kifisadi, kinavyosomeshwa kifisadi, kinavyofanywa ‘kifaulu’ kifisadi, kinavyoajiriwa kifisadi, kinavyoozeshwa kifisadi na kinavyokuwa kitu kingine cha ufisadi katika mwendelezo wa utamaduni wa ufisadi kilimozaliwa. Sidhani kwamba tunaweza kuwa na matumaini ya kupata lo lote la maana kutoka kitoto hicho kwa maana ya kuiendeleza nchi na kuwaendeleza watu wake. Watu wa aina ya kitoto hicho hawawezi kuijenga wala kuiongoza nchi, kwa sababu wao hawajajengwa wala kuongozwa katika misingi ya kujenga lo lote la maana isipokuwa kuendeleza utamaduni uliowazaa na kuwalea”.

Ni ushuhuda kama huu ufuatao ambao January ameutoa kuhusu safari yake ya kisiasa na vyanzo vilivyolipia shahada yake ya umahiri ndiyo utatusaidia kuhisi hizo zinazotajwa kuwa zama mpya za kizazi kipya cha viongozi zitazifunika hata zile zama za ‘ukweli na uwazi’ za awamu ya tatu: “Nilipata wakati mgumu kulipa ada, kiasi cha kukaribia kufukuzwa shule. Niliomba msaada kwa watu mbalimbali akiwemo Rais wa wakati ule Mhe. Benjamin William Mkapa. Bahati nzuri, alikubali kusaidia kwa sharti kwamba nije kutumia utaalamu wangu Serikalini nitakapomaliza masomo. Na ndivyo nilivyofanya. Baada ya masomo hayo, nikajiunga na Wizara ya Mambo ya Nje…. Pale Wizarani, nilipata fursa ya kufanya kazi na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. Nahisi alipenda kazi zangu na mara alipoamua kuwania nafasi ya Urais akanitaka nichukue likizo isiyo na malipo Serikalini ili niwe msaidizi wake kwenye kampeni zile. Siwezi kusahau maishani mwangu ile fursa kubwa kwani niliweza kuijua kwa kina nchi yangu na watu wake. Baada ya Rais Kikwete kushinda aliniteua kuwa Msaidizi wake Ikulu, nikiwa na jukumu la kumsaidia kuandika hotuba zake, pamoja na mambo mengine mengi ya uendeshaji wa shughuli zake za kila siku” (Uk. 15-17).

January mwenyewe anasisitiza kwamba “Rais ajaye asiwe na chembe hata kidogo ya kuhisiwa kunufaika na fursa ya muda mrefu wa uongozi katika Serikali” (Uk. 5). Wadadisi tunakubaliana naye. Ila tunapenda kuifanyia ‘fomuleshini’ ‘mpya’ kidogo hiyo kauli ili isomeke hivi: ‘Rais ajaye asiwe na chembe hata kidogo ya kuhisiwa kunufaika na fursa ya muda mrefu au mfupi wa uongozi katika Serikali ama taasisi yeyote ya umma’.

Tusogee kwenye hili jibu lake kuhusu suala lingine: “Tumejenga Chuo Kikuu kikubwa cha Sayansi na Teknolojia na chenye hadhi ya kimataifa pale Arusha ambacho kinafundisha wanasayansi na watafiti wa ubora wa juu, waliojikita katika kutumia elimu ya sayansi kutafuta majawabu ya matatizo ya msingi ya Watanzania. Kuanzia mwakani tutakuwa tunatoa wahitimu watafiti wa sayansi, yaani PhDs, 500 kila mwaka na tutaendelea kuongeza” (Uk. 35 ). Hivi kweli kuna chuo (kipya) na kidogo duniani kinatoa shahada za uzamivu – PhDs – ambazo kwa kawaida zinachukua miaka 3 na kuendelea kwa wingi kiasi hicho kwa mwaka? Hii ni kosa la uandishi au ndilo jibu halisi alilolitoa ‘mwandikwaji’ January?

Pengine kwa kutambua kwamba wengi hatupendi wanasiasa wahodhi sifa hasa pale ambapo wameshirikiana na wenzao kufanikisha jambo fulani, January analijibu swali mojawapo hivi: “Umeuliza pia kuhusu mafanikio ambayo tumeyapata Wizarani hadi tuaminiwe kwa nafasi za juu. Labda niseme kwamba Wizara haiendeshwi na mtu mmoja au wawili. Kuna timu ya watendaji, wataalam na watumishi wa Wizara pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara. Na pia kuna wenzetu wengine ndani ya Serikali nzima ambao bila wao Wizara moja haiwezi kutimiza majukumu yake. Mara nyingi sijisikii vyema pale Wizara moja au Serikali inapotimiza majukumu yake, basi hujitokeza mtu mmoja kusema yeye kafanya – kwamba ni mafanikio yake” (Uk. 32-33).

Lakini anapoelezea mafanikio ya Kamati yake, kuna sehemu anasema hivi: “Kuhusu gesi, kabla Kamati yetu haijaundwa, hapajawahi kuwa na mjadala Bungeni kuhusu masuala ya gesi. Niliunda Kamati Ndogo ya Kamati yangu ili kulichunguza kwa kina suala la gesi. Kamati ile ilifanya kazi nzuri na kwa kweli napendekeza watu waitafute ile ripoti ya kizalendo na kuisoma” (Uk. 59).

Ukiisoma ripoti hiyo iliyopo kwenye tovuti ya Bunge na iliyowasilishwa na Mbunge wa Bukene, Selemni Jumanne Zedi kwa niaba ya Mwenyekiti unakutana na maneno haya: “Mheshimiwa Mwenyekiti, chimbuko la Kamati Ndogo ni hoja zilizojitokeza wakati Kamati ilipokuwa inajadili na kuchambua Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. Wakati wa mchakato huo Kamati ilipata taarifa kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu mapungufu mbalimbali yanayolenga sekta ya gesi katika mahusiano ya wadau wa gesi. Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 15 Julai, 2011 wakati Kamati ya Nishati na Madini inawasilisha taarifa yake ya Bajeti ya Mwaka 2011/2012, Bungeni katika sehemu ya Maoni na Ushauri wa Sekta ya Gesi, Kamati ilitoa hoja ya kuunda Kamati Ndogo kufuatilia suala hili. Wabunge waliunga mkono hoja hii na Mheshimiwa Spika alikubaliana na ushauri huo wa Kamati. Aidha, Katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa ufasaha, Kamati Ndogo ilipewa Hadidu za Rejea (Terms of Reference) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini”.

Hata ukisoma ukurasa wa 67 wa Hansard ya 15 Julai 2011 unakutana na maneno haya aliyoyasema January akiwa Mwenyekiti: “Kamati haijaridhishwa na ushiriki, ufanisi na uadilifu wa Kampuni ya Pan African Energy Tanzania katika mchakato wa uendelezaji gesi nchini. Hivyo basi, kufuatia utata huu uliopo, Kamati ya Nishati na Madini inaunda Kamati yake ndogo ili kufuatilia utata huu na tutadhihirisha wazi mambo”.

Japokuwa kwa kawaida Wenyeviti wa Kamati au Tume wanakuwa ndiyo vinara wa kushawishi maamuzi yaelekee upande gani, ni dhahiri kuwa matumizi ya maneno yenye muundo wa ‘nilifanya hiki au kile na kile’ badala ya ‘tulifanya hiki au kile’ ni uwongo na kama siyo uwongo, basi ni kile kilichobatizwa jina la ‘propaganda’ au ‘jibu la kisiasa’.

Kuhusu baadhi ya mafanikio kwenye sekta ya elimu, January anasema hivi: “Katika miaka 46, yaani tangu uhuru mwaka 1961 hadi mwaka 2004, tulikuwa tumejenga shule za sekondari takriban 1,200. Katika miaka nane tu, kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2013, tumejen[g]a shule zaidi ya 3,500. Mwaka 2004, kulikuwa na wanafunzi wa sekondari kama 400,000 hivi leo hii wanakaribia milioni mbili. Nakumbuka wakati nikiwa Msaidizi wa Rais Ikulu, Rais Kikwete alipoingia madarakani mwaka D[e]semba 2005, moja ya vitu vya kwanza alivyoagiza ni kupewa taarifa ya wanafunzi wali[o]faulu mtihani wa darasa la saba na ni wangapi wamepata nafasi za kwenda Sekondari. Taarifa iliyokuja ilionyesha kwamba karibu nusu ya wanafunzi waliofaulu hawakuwa wamepata nafasi na ilikuwa ndio basi wanabaki nyumbani. Hakuridhika na hali hiyo, kwamba wapo watoto wenye vipaji, waliofaulu, lakini kwa kuwa tu hakuna shule basi wanarudi nyumbani. Na hawa ni watoto wa miaka 13 na 14. Hakuna aliyekuwa na jawabu kwamba wakibaki nyumbani wanafanya nini. Ndipo akaagiza kwamba yajengwe madarasa na shule mpya haraka na kwa mtindo wa operesheni ili walau ifikapo mwezi Machi watoto hawa wawe wamepata nafasi” (Uk. 97).

Hapa kwa kweli tunaona kana kwamba historia inaandikwa upya japo siyo kwa usahihi (kamili). Pengine ni kwa sababu za ‘ajali ya kisiasa’ ndiyo maana January hayasemi yale ambayo tunayakumbuka tuliokuwa kwenye harakati za HakiElimu miaka hiyo ya 2005 na 2006 tukihoji maagizo tete/tata ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Kwa kumbukumbu tulizo nazo, kama zilivyorekodiwa katika taarifa mbalimbali kama hii ya Raising The Stakes: The Impact of HakiElimu’s Advocacy Work on Education Policy and Budget in Tanzania, maagizo mawili ya kiongozi huyo aliyejiuzulu kufuatia kashfa ya ufisadi wa Richmond ndiyo yaliyopelekea ujenzi wa shule nyingi za sekondari (hasa zijulikanazo kama za kata) na udahili wa wanafunzi hao waliofaulu ila wakakosa nafasi. Hivyo, ni vizuri kuuenzi ukweli kwa kueleza sehemu yake ya kufanikisha hayo anayoyasifia January.

Dalili hizo za uchakachuaji wa historia ya elimu nchini zinazidi kuonekana tunapokutana na ‘vijembe vya kampeni’ kama hivi ndani ya kitabu hicho cha mazungumzo na January: “Rais Ajaye anatakiwa aje na majawabu kuhusu namna gani ataendesha mageuzi makubwa na machungu katika sekta ya Elimu. Kauli za juu juu tu za kuboresha elimu tunazosikia kutoka kwa baadhi ya watarajiwa hazitoshi. Lazima kwenda kwa kina zaidi” (Uk. 7); “Kuomba uongozi hakuanzii na kuishia na kauli-mbiu rahisi za afya bure, elimu bure ambazo hazina ufafanuzi wala maelezo – ambazo ni rahisi kuvutia na kuhadaa watu. Hazishii na kauli za juu juu kwamba tutaongeza ajira au tutaboresha elimu. Kila mtu aweza kusema haya. Swali kubwa ni kivipi? Kwa maarifa gani mapya?(Uk. 11)

Uwazi
Kuna baadhi ya majibu ya January yanatuacha na maswali zaidi. Ni vyema akawa wazi ili ukweli uwe dhahiri. Hili litazaidia kudumisha ukweli na kukuza uwajibikaji.

Wapo, kwa mfano, ambao tunapenda kujua ni akina nani hawa na walifanya nini hasa hadi January akasema hivi kuhusu shirika/kampuni ya maendeleo ya Bumbuli:  “Kuna baadhi ya maeneo watu niliowaamini kuendesha shughuli za ukopeshaji wametuangusha na wamewaangusha wananchi kwa hiyo tunalazimika kurekebisha hali hiyo” (Uk. 32).

Pia tungependa kujua ana maana gani hasa anapohitimisha aya ifuatayo kwa kusema maneno yanayoonyesha kana kwamba kuna wajumbe wa kamati aliyokuwa anaiongoza ambao walizidiwa na vishawishi: “Kama Kamati tulipata changamoto nyingi mara kwa mara. Sekta ya Nishati ni nyeti na kuna watu wengi wenye maslahi makubwa katika sekta hii. Sekta hii inahusisha fedha nyingi na kumekuwa na historia ya rushwa na ubadhirifu. Kazi kubwa tuliyofanya ni kuhakikisha wajumbe wote tunasimama pamoja na kuepuka ushawishi unaoweza kutupeleka pabaya. Katika kipindi changu tulifanikiwa kwa kiasi fulani” (Uk. 59).

Hili ni suala muhimu kwa sababu hitimisho la hilo jibu lake katika aya inayofuata linatumia neno lenye muundo wa ‘inaonekana’ ambalo kwa kawaida katika tasnia ya uandishi huashiria kukosa uhakika au ‘kupotezea’: “Binafsi nilipata changamoto kubwa za kuchafuliwa. Kwa kuwa nilikuwa mkali sana na niliharibia baadhi ya watu mianya yao ya kula na kwa sababu nilibainisha udhaifu katika utendaji na kwa sababu niliweza kuaminiwa sana na Watanzania, zikafanyika jitihada kubwa kunichafua. Nakumbuka mojawapo ni watu walitengeneza barua pepe ikidaiwa inatoka kwa dada yangu kwenda kwa mpenzi wake wa kufikirika eti akiomba pesa kwa ajili yangu na kisha hiyo barua pepe ikazungushwa dunia nzima. Barua pepe ile ilibainika kwamba ni ya kugushi. Wahusika wa ile barua pepe hadi leo tunasalimiana lakini wanaamini siwafahamu. Kamati ile ilivunjwa baada ya mimi kuondoka kwa tuhuma za rushwa dhidi ya wanakamati wachache, ingawa baadae tuhuma zikaonekana za kusingizia” (Uk. 59).

Na kama tunavyojua, John Mnyika ambaye alikuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ile iliyovunjwa aliendelea kuashiria kulikuwa na vitendo vya rushwa kamatini na kutaka ripoti ya uchunguzi wa tuhuma hizo ijulikanayo kama ‘Ripoti ya Ngwilizi’ iwekwe wazi. Zitto Kabwe naye alikuwa ni miongoni mwa wabunge waliotaka iwasilishwe na ijadiliwe kiuwazi Bungeni.

Pengine tunamdai January mengi kwenye hili la uwazi kuliko anayoweza kuyaweka kiuwazi hasa ukizingatia kuna sehemu amekuwa muwazi kutueleza yafuatayo kuhusu usiri: “Kama Msaidizi wa karibu wa Rais unapata fursa ya kujifunza kwa karibu jinsi siasa na uongozi wa nchi unavyoendeshwa. Kila kiongozi huwa anapitia vipindi vigumu katika uongozi wake. Na kwa Rais Kikwete ilikuwa hivyo hivyo. Zipo nyakati nyingi nilikosa usingizi. Zipo nyakati tulipaswa kuandika hotuba ngumu kukabiliana na mazingira magumu na masuala mazito yaliyokuwepo kipindi hicho. Kwa mfano, wakati wa ukame na njaa kubwa iliyoikumba taifa mwaka 2007, kipindi cha kashfa za EPA na Richmond, na pia kipindi ambacho taifa lilikumbwa na wimbi kubwa na kutisha la ujambazi. Unapata fursa ya kujua siri nyingi za nchi na lazima uwe na ukomavu na uwezo wa kuzitunza. Yapo mambo mengine niliyoyaona na kujifunza ambayo nitakwenda nayo kaburini lakini yalinipa elimu tosha ya uongozi” (Uk. 68).

Uzoefu
Katika majibu yake January ametumia nafasi, muda na nguvu nyingi kujibu madai – ama mashambulizi – kuwa hana uzoefu. Hoja hii ya uzoefu imefungamana na hoja ya ujana na kwa kiasi kikubwa sana amefanikiwa kuupangua ‘mfungamano’ huo kwa kutumia dhana ya rika. Tatizo lipo kwenye mifano anayoitoa kushibisha hoja yake kuwa amekomaa na ana uzoefu wa kutosha.

Tuanze na mfano ulio karibu na nyumbani kabla hatujaenda huko Ughaibuni. January anatuambia hivi: “Wakati wazee wanamchagua Mwalimu Julius Nyerere kuwa Rais wa TANU mwaka 1954 ili aongoze harakati za uhuru, ambazo ni ngumu na hatari kuliko hata uongozi wa nchi, ukomavu wake haukutazamwa kwenye umri wake mdogo wa miaka 32” (Uk. 30).

Mahali pengine humo kitabuni anasema hivi: “Wakati Mwalimu Nyerere anachaguliwa kuwa Rais wa TANU mwaka 1954, akiwa na miaka 32 tu, ili kuongoza harakati za kutafuta uhuru wa nchi yetu, kama kungekuwa na swali kwamba kwani kafanya nini hadi awe Rais wa TANU, kwamba kuna wanaostahili zaidi Urais wa TANU kwa sababu wamefanya makubwa zaidi hata kabla Mwalimu hajatia mguu Dar es Salaam, basi historia ya nchi yetu ingekuwa tofauti na ilivyo leo” (Uk. 33).

Hapo tatizo la kwanza ni hoja ya awali kuwa harakati za uhuru zilikuwa ngumu na hatari kuliko hata uongozi wa nchi (tena nchi changa). Hapa tunamwongelea Nyerere aliyetaka kupinduliwa na (wana)jeshi mwaka 1964 na kutaka kupinduliwa tena kwenye miaka ya 70 na miaka ya ya mwanzo ya 80. Pia tunayemwongelea ni Nyerere aliyeongoza nchi kwenye vita dhidi ya Nduli Idi Amin. Hali kadhalika huyu ni Nyerere aliyeongoza nchi katika kipindi ambacho wengi wa viongozi wakuu wenzake wa nchi za Afrika walipinduliwa ama kuuwawa – kina Patrice Lumumba, Sylvanus Olympio na Kwame Nkrumah. Baadhi ya magumu haya January anayaelezea kwa ufasaha mwishoni mwa kitabu anapojibu swali la 39 kuhusu Rais aliyeacha historia kubwa ila hapa mwanzo halitilii mkazo kwa kuwa (inaonekana) anajenga madai kwamba kama ni uzoefu hata Nyerere wa 1954 hakuwa tofauti na January wa 2014.

Kisha tatizo la pili ni hiyo hoja kuhusu Nyerere na uongozi wa TANU. Huyo ni Nyerere aliyekuwa ‘Mwenyekiti Mwanzilishi’ wa tawi la AA akiwa katika Chuo cha Makerere, hii ikiwa na maana alikuwa anawaongoza wenzake ambao wengi wao ndiyo walikuwa wawe viongozi wa serikali itakayopata uhuru kutoka kwa wakoloni. Huyo huyo Nyerere alikuwa ni ‘Mwenyekiti Mwanzilishi’ wa TAA ambayo ndiyo iliizaa TANU. Maswali hayo kuhusu uzoefu wa Nyerere hasa ukimlinganisha na Abdulwahid Sykes yameshaulizwa na kama tujuavyo Mohamed Said amelishikilia sana hilo bango katika vitabu na makala zake. Lakini sababu maalumu iliyopelekea Nyerere kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti badala ya Sykes sote tunaifahamu.

Ukishajenga msingi wa hoja yako kwa kusema kwamba kuongoza harakati za uhuru ni kazi ngumu kuliko kuongoza nchi basi unajikuta unaacha kabisa kuongelea ni uzoefu gani Nyerere aliupata kabla hajawa Waziri Mkuu na Rais tulipopata uhuru na kuwa jamhuri mwanzoni mwa miaka ya 60 – ukifanya hivyo unaacha kuongelea yafuatayo:

Kwa mujibu wa mwanahistoria mmoja wa nchi yetu, John Iliffe, kama kiongozi wa TANU, Nyerere  alishirikiana na wenzake kufungua matawi nchini kote na kufikia mwaka 1955 walikuwa wakipata wanachama wapya 100 kila siku; mwaka huo huo Nyerere alishiriki kwenye Baraza la nchi zilipo chini ya Uangalizi wa Umoja wa Mataifa jijini New York ambapo alitoa tamko liloipaisha TANU ndani na nje ya nchi; mwaka 1958 Nyerere alijiuzulu kwenye Baraza la Kutunga Sheria kupinga mfumo ‘pendekezwa’ wa uchaguzi; mwaka huo huo Nyerere alimshinda Kunambi kwenye uchaguzi kwa kura 2,628 dhidi ya 802 na wala hakupita bila kupingwa tu kama baadhi ya wanasiasa wetu; mwaka  1960 Nyerere na wenzake walishinda uchaguzi wa Septemba na kisha (w)akaunda Baraza lake la kwanza kabisa la Mawaziri.

Ukiacha kuongelea historia hiyo ya kabla ya Urais wa Nyerere basi inakuwa siyo vigumu kudiriki kusema maneno haya kitabuni: “Jingine ninaloweza kusema ni kwamba hakuna kazi yoyote inayomuandaa au kumkomaza mtu kuwa Rais wa Tanzania. Kuna watu wanne tu hapa Tanzania ambao tunaweza kusema kuwa wana uzoefu wa Urais: Mwalimu Nyerere, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin William Mkapa, na Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Kinachomfanya mtu awe tayari ni makuzi yake, maadili yake, busara yake, hekima zake, dira yake pamoja na vipaji na talanta na karama alizojaliwa na Mungu” (Uk. 30).

Mifano ya ugenini ndiyo inaongeza utata. Tunaambiwa hivi kitabuni: “Moja ya mijadala mikubwa kwenye uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2008 ilikuwa ni hili la uzoefu. Obama alikuwa Mbunge kwa miaka mitatu tu, basi. Hajawahi kuwa hata Naibu Waziri. Viongozi wenzake na wengine waliompinga wakasema hana uzoefu. Wamarekani wengi wa kawaida wakasema kwamba sifa na ubora wa uongozi haupimwi kwa miaka mingi na nafasi za ndani ya Serikali. Wakampa kura nyingi kuongoza taifa kubwa duniani” (Uk. 25-26).

Wadadisi tunagoma kukubali tu tunachoambiwa na kupumbazika hivyo tunaingia mtandaoni kusoma historia ya Obama. Humo tunakuta yafuatayo: Mwaka 1992 Obama ni Mkurugenzi wa Mradi wa Kura katika jimbo la Illinois na anafanikisha uandikishwaji wa wapiga kura 100,000 hasa kutoka kwenye jamii zilizoko pembezoni; Mwaka 1996 Obama anagombea kuwa Seneta wa jimbo la Illinois na kushinda. Anachaguliwa tena mwaka 1998. Mwaka 1999 anagombea Ubunge na anashindwa kwa uwiano wa 2 kwa 1 baada ya kutokuwepo wakati wa kutopitishwa muswada wa kudhibiti matumizi ya bunduki maana alikuwa anamuuguza binti yake jimboni Hawaii, hivyo anaendelea na useneta na kufanikisha kupitishwa kwa miswada ipatayo ishirini kuwa sheria.

Hapa inabidi tutulie na kutafakari kidogo maana kuna madai kuwa huo Useneta wa Illinois ni sawa tu na Udiwani wa Bumbuli hivyo kumlinganisha January katika hilo ni sawa na kusema alipaswa kuwa Diwani kwanza kabla hajawa Mbunge. Kwanza, siyo sahihi kwa kuwa kwa kiasi kikubwa jimbo moja la Marekani ni kubwa kuliko Wilaya ya Tanzania na lina(hitaji) ugatuzi mkubwa wa madaraka  hivyo ni kama vile nchi/dola iliyo ndani ya nchi/dola ambayo kwa kiasi kikubwa inajiendesha yenyewe. Pili, maneno hayo ni dharau kubwa sana kwa Udiwani na sera/dhana nzima ya kugatua/kupeleka madaraka zaidi mikoani, wilayani na vijijini.

Tukirudi mtandaoni tunaona kuwa mwaka 2003 Obama hatimaye anashinda Ubunge, hii ikiwa ni baada ya kushinda Useneta kwa mara nyingine mwaka 2002. Hivyo, Obama hadi kufikia hapo alikuwa na uzoefu mkubwa wa siasa za ushindani na siyo za kupita tu kwenye uchaguzi bila kupingwa kwa sababu wagombea wamejitoa, wametolewa au wamelazimika kujitoa. Kwa kushirikiana na wenzake akiwamo mbunge wa kilichokuwa chama tawala nchini Marekani, mwaka 2006 Obama anafanikiwa kupitisha muswada kuwa sheria inayoruhusu Wamarekani kuingia mtandaoni na kuona matumizi ya kodi zao.

Huyo ni Obama aliyekuwa kwenye chama kilichokuwa cha upinzani. Lakini akaweza kufanya ushawishi wa kimkakati mpaka muswada wake ukapita na kuwa sheria ya nchi. January yuko chama tawala, analeta muswada mwaka 2012, leo mwaka 2015 jibu lake kuhusu ulipoishia ni hili: “Nilipowasilisha Muswada [wa Sheria ya Kudhibiti Shughuli za Upangaji wa Nyumba (Rental Housing Act)] ulipokelewa vizuri na Wabunge wote. Serikali pia iliupokea vizuri na ikaahidi kwamba kabla ya Sheria hii kutungwa basi lazima kuwe na Sera ya Nyumba kwanza. Hivyo ndivyo alivyoahidi [aliyekuwa] Waziri, Mheshimiwa Profesa Bungeni. Mimi naamini swala hili litatekelezwa mapema” (UK. 123).

 Mapema ipi ilhali Bunge karibia linavunjwa na lina viporo vingi vimeachwa baada ya mjadala mkali wa ESCROW? Au utapitishwa atakapopata makazi ‘mapya’ Ikulu?

Mfano huu wa January kuhusu Tony Blair ambaye kumbe alikuwa Mbunge wa kugombea toka mwaka 1983 na Waziri Kivuli pamoja na Kiongozi wa Upinzani Bungeni kuanzia1994 baada ya kugombea/kushinda unafurahisha zaidi: “Majuzi kuna rafiki yangu alitumia nukuu ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair aliyoitoa mara baada ya kuchaguliwa kuongoza Serikali mwaka 1997. Tony Blair, aliyechaguliwa kuongoza Uingereza akiwa na miaka 43 tu, alisema kwamba “wakati nachaguliwa kama Waziri Mkuu, nilikuwa sijawahi kushika nafasi yoyote Serikalini. Sikuwahi kuwa hata Naibu Waziri. Na Uwaziri Mkuu ndio kazi yangu ya kwanza na pekee Serikalini””(Uk. 26).

January naye anatuambia anakijua chama chake “vizuri sana” (Uk. 29). Kwa nini? Kwa sababu ya nyadhifa alizoshika:“Naweza kuelewa kwamba, bila hata kujali umri, mtu ambaye hajawahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu au Halmashauri Kuu ya Taifa anawezakupata changamoto ya uelewa wa namna ya kukiongoza Chama chetu. Lakini kama umeshakuwa Mjumbe wa Sekretarieti, Mjumbe wa Kamati Kuu, Mjumbe wa Halmashauri Kuu, kama ambavyo nimeshawahi kushika nafasi zote hizo, utakuwa umepata uelewa madhubuti wa uendeshaji na uongozi wa Chama” (Uk. 166).  Je, ni kwa muda gani na nini hasa alifanya katika kila kipindi? Hatuelezi moja kwa moja, tunaambulia neno ‘kitambo’ maana kati ya mwaka 2010 na 2015 hajatulia kwa muda kenye wadhifa mmoja. Au ndiyo masuala ya kasi ‘mpya ya upya’?

Hebu tumsikilize: “Baada ya kitambo kidogo, nikateuliwa kwenye Sekretarieti ya Chama nikiwa kama Katibu wa NEC wa Siasa na Mambo ya Nje, na nikawa Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Nilishika nafasi hizi katika kipindi kigumu sana kisiasa kwa Chama chetu na nilijifunza mambo mengi  mchango wangu kwenye kukijenga na kukiimarisha” (Uk. 17-18).

Pengine haya maandalizi ya “kitambo kidogo”,  ama ‘voda fasta’ kama tukitumia lugha ya vijana wa ‘kizazi kipya’ cha ’dot com’, ndiyo haya anayoyaongelea Mzee Mwinyi kwenye Dibaji ya kitabu hicho: “Nilimteua Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mbunge na Naibu Waziri akiwa na umri wa miaka 38 tu na baadaye Waziri wa Wizara muhimu ya Maji, Nishati na Madini akiwa na umri wa miaka 40 na baadaye Waziri wa Fedha. Sikufanya hivyo kwa sababu tu ya umri wake bali kutokana na kuamini katika msingi wa kuandaa viongozi wa vizazi vijavyo kwa kuwapa majukumu katika Chama na ndani ya Serikali” (Uk. vii-viii).

Ubunifu
Kuna tofauti kati ya uvumbuzi (invention) na ubunifu (innovation). Kwa tafsiri rahisi, uvumbuzi ni ugunduzi wa kitu kipya na ubunifu ni ubadilishaji/uendelezaji wa kitu kwa namna ‘mpya’ au nzuri zaidi. Kwenye kitabu cha January kivumishi kitokanacho na mzizi ‘-bunif-’ kimetumika mara 22 na majibu yake yamemtambulisha kama mbunifu.

Kwa mfano, kwenye ukurasa wa 89 January anatujulisha hili kuhusu kutuzwa na taasisi ya National Democratic Institute inayoongozwa na Waziri mstaafu wa Mambo ya Nje wa Marekani, Madeleine Albright: “Tuzo niliyopewa mimi inaitwa Democracy Award ambayo nilishinda kutokana na ubunifu wa kutengeneza mfumo wa kuwasiliana na wapiga kura wangu wa Bumbuli kwa kutumia SMS. Tuzo hii nilishinda pamoja na Rais wa nchi ya Estonia na mwanzishaji na mmiliki wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Jack Dorsey. Nilipewa heshima ya kuzungumza katika halfa hiyo iliyokuwa na viongozi wakubwa katika Serikali ya Marekani. Ilikuwa heshima kubwa kwa sababu huko nyuma waliopata kushinda tuzo hii ni pamoja na Kofi Annan na Desmond Tutu” (Uk. 89).

Anastahili pongezi kwa hilo hasa kutoka kwa waumini wa ‘demokrasia ya kiliberali’ (liberal democracy). Wakati ubunifu huo ulipofanyika kulikuwa na msisimiko na mvuto mkubwa mtandaoni miongoni mwa watumiaji wa twitter nchini Tanzania. Tulipewa taarifa ya jinsi Wanabumbuli walivyokuwa wanautumia na hata kuwekewa nukuu kutoka kwenye SMS zao. Pengine itakuwa vyema kama January atatueleza uendelevu wa ubunifu huo na kama umeweza kufikia maeneo mengine ya Tanzania. Hili ni muhimu maana kuna vitu vingi sana vizuri vimebuniwa ulimwenguni lakini kutokana na sababu mbalimbali havitumiki.

Maadam January tayari ni kiongozi mkubwa wa Serikali katika sekta ya mawasiliano ni vyema pia akaufanyia na majaribio ya awali na huu ubunifu mwingine anaouelezea ili angalau tupime kama unafanya kazi kweli/kiuhalisia badala ya kusubiri mpaka atinge Ikulu ndiyo tufanywe kuwa sehemu ya maabara ya majaribio: “Nimefarijika kuanza kuona kwamba kuna makampuni kadhaa yameanza shughuli za kuweka rekodi za ukopaji, yaani Credit Reference, kwa ajili ya matumizi ya mabenki na taasisi nyingine. Hili ni jambo jema. Lakini mimi naamini kwamba kuna fursa ya ubunifu zaidi. Kwa mfano, karibu kila Mtanzania anatumia simu ya mkononi na kila siku anatumia airtime au anahifadhi pesa kwenye simu na kuhamisha na kufanya manunuzi mbalimbali. Simu ni kama akaunti ya benki siku hizi. Na kwenye simu kuna taarifa muhimu ya kujua nguvu ya kiuchumi ya kila mtumiaji simu. Makampuni ya simu, kwa ruhusa ya watumiaji, yanaweza kutumia taarifa hizi kama credit reference na kuwezesha watu wasio kwenye sekta rasmi lakini wenye nguvu ya kiuchumi kuweza kukopesheka na kupata mikopo nafuu ikiwemo ya ununuzi na ujenzi wa nyumba au mikopo ya biashara” (Uk. 124).

Au kwa kuwa hatuna Waziri wa Ardhi kwa sasa pengine Rais amteue January kuziba nafasi hiyo ili afanye na hili jaribio lake la kibunifu tuone kama litawezekana: “Asilimia zaidi ya 60 ya wakazi wa Dar es Salaam wanaishi kwenye makazi yasiyo rasmi na wanalipa kodi kubwa kuliko hali ya nyumba wanazoishi. Jawabu ni kujenga nyumba zaidi. Jawabu la haraka ninalolifikiria ni kubadilisha kabisa maeneo yanayoonekana kama ni mabaya – Manzese, Tandale, Mbagala, Vingunguti na kwingineko – kuwa mazuri. Kwa mfano, ukienda Manzese ukaainisha eneo lenye nyumba duni la ukubwa wa uwanja wa mpira wa miguu, ambalo linaweza kuwa na familia kama 200, halafu ukazungumza na wakazi hao na kuwashawishi wakubali kuhama na kuwalipia makazi ya muda kwa miezi kumi na nane ili kuliendeleza. Wakihama, lile eneo unalivunja na kujenga nyumba za ghorofa tatu au nne zitakazochukua familia si chini ya 800, kuweka mifereji, bustani, maduka, na shule. Ukimaliza unazirudisha zile familia 200 katika nyumba hizi mpya bora zaidi na unakuwa umepata nafasi mpya kwa familia 600 zaidi katika eneo lile lile. Halafu unaendelea kwa kukata kipande kingine tena sawa na uwanja wa mpira wa miguu ambapo utapata familia nyingine 200 na safari hii huna haja tena ya kuzihamisha familia za eneo hili kwenye makazi ya muda kwa miezi kumi na nane, kama ulivyofanya mwanzo, kwa sababu tayari una nafasi za familia 600 – kwa hiyo utatoa nafasi 200 na kubakiwa na nafasi 400. Kwa hiyo utajenga kwenye eneo hilo na kupata nafasi nyingine mpya za familia 800 halafu ukijumlisha na zile 400 utakuwa na nafasi za familia 1,200. Familia 400 za kwanza zilizohamishwa zitalipa kodi sawa na waliyokuwa wanalipa zamani na nafasi mpya zilizobaki zitauzwa au kukodishwa kwa gharama nafuu. Ukiendelea hivi na mpango huu katika maeneo yote tunayoyaita ya uswahilini katika miji yetu utapunguza sana tatizo la makazi, utapendezesha mji na utawezesha watu wanaoishi kwenye miji kuishi kwenye nyumba zenye hadhi zinazohifadhi utu wao” (Uk. 119-120).

Inaonekana bila madaraka makubwa au fursa ya kuwa karibu na wenye madaraka makubwa inakuwa vigumu kutekeleza kilichobuniwa pengine ndiyo maana ni muhimu mtu awe Rais au awe karibu na Rais. Mfano ufuatao unaonekana kudhihirisha hilo: “Kwa kifupi sana, nimefanya mambo kadhaa: kwanza, ingawa hili halijatangazwa sana, lakini watu wa TRA, BASATA, COSOTA na wengineo wanafahamu kwamba kuanzia mwaka 2008 nikiwa Msaidizi wa Rais, niliitisha vikao vya wadau wa muziki na filamu, ikiwemo wasambazaji wote wa filamu, ili kuangalia namna ya kuisaidia tasnia hizi. Katika kikao nilichoongoza, ndipo wazo la stika za TRA tulipolibuni kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, suala hilo lilihitaji utafiti kidogo, na utafiti huo ulihitaji pesa. Nikaenda kumuomba Rais Kikwete pesa hizo, akakubali kutoa shilingi milioni 20, ambazo zilipelekwa TRA ambao ndio waliosimamia utafiti huo. Dhana nzima ya kuanzisha stika ilikuwa ni kwamba kazi za wasanii lazima zitambuliwe rasmi na kuwe na taasisi Serikalini inayosimamia uchakachuaji wa kazi hizo kwa kuwa huko nyuma ilikuwa ni holela tu na ilionekana kama halali kufanya uharamia kwenye kazi za wasanii. Tukaona kwamba, kwa kuwa, ukiwa na sigara feki, mvinyo feki au konyagi feki, unakamatwa na Serikali, basi tuweke utaratibu kwamba ukiwa na CD feki basi pia ukamatwe na Serikali. Na kwa kuwa sigara, konyagi na mvinyo zinawekwa stika ili kuzitambua halali na feki, basi na kwenye kazi za wasanii na kwenyewe tuweke stika za TRA ili Serikali iwe na wajibu wa kusimamia kazi hizi. Bahati nzuri tukaanza utekelezaji. Imechukua muda na mwanzo tumeanza kwa kusuasua na kukiwa na changamoto za hapa na pale lakini naona sasa TRA wameamka na kuanza kukamata kazi feki. Kwa hiyo, naona fahari kwamba
 hili ni jambo nililianzisha, kwa maelekezo ya Rais, nikiwa Ikulu na likaingizwa kwenye mfumo wa Serikali na kupelekwa Bungeni na sasa ni utaratibu rasmi” (Uk. 137-138).

Masuala mengine kama haya inaonekana hayahitaji mpaka mtu uwe na (ukaribu na) madaraka ya Kiikulu/Kirais: “Nilishawahi kwenda pahala kwenye shule ya sekondari nikapewa kero ya maji, kwamba yapo mbali na sio masafi. Lakini nikaangalia ile shule ina majengo makubwa zaidi ya 9. Nikauliza hali ya mvua huwa ikoje. Nikaambiwa huwa zinanyesha sana, hasa wakati wa masika na vuli. Tukaanzisha harambee ya kujenga kata za kukinga maji na matenki ya kuhifadhi maji. Siku hizi naambiwa kwamba mvua zinakuta bado maji ya msimu uliopita yapo na wanakijiji pia wanayatumia. Kwa hiyo, kwanza, katika masharti ya kutoa vibali vya ujenzi, kuwepo na kanuni mahsusi za kulazimisha uwepo wa miundombinu ya kukinga maji katika majengo na kuyahifadhi” (Uk. 157).

Kwenye suala la “majimbo ya kiuchumi”, January anasema anaamini “kwamba kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukitazama mgawanyo wa maeneo ya nchi yetu katika misingi ya kiutawala au kiuongozi zaidi kuliko kiuchumi” (Uk. 45). Tatizo linakuja kwenye uchambuzi wake wa kihistoria ambapo anasema “Mfumo wa uchumi wa kikoloni uliitazama nchi yetu kama eneo la uzalishaji mali, kama vile shamba tu la Malkia. Wakoloni hawakujali maendeleo ya watu wetu. Ndio maana kuna baadhi ya maeneo ya nchi yetu yalitengwa tu kwa ajili ya kutoa manamba kwenye mashamba, na kuna baadhi ya maeneo yalitoa askari tu katika jeshi la mkoloni. Miundombinu yote iliyojengwa na mkoloni ilikuwa ni kwa ajili ya kusafirisha bidhaa ghafi kuja bandarini kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi” (Uk. 45).

 Lakini huo ndiyo mfumo wa ‘siasa uchumi’ wa kikoloni ambao ulijikita katika majimbo 9 ya kiutawala/kiuchumi wakati wa ukoloni wa Mwingereza. Wakati tunapata uhuru mwingereza mmojawapo, Kathleen Stahl, alitembelea majimbo hayo na kuandika kitabu cha Tanganyika: Sail in the Wilderness ambapo alijaribu kuelezea uchumi wa kimajimbo. Tulipopata uhuru ilibidi tuamue kubaki na mfumo huo au kujaribu kujenga mwingine wa mikoa hasa kwa kuzingatia kuwa uchumi unaingiliana na siasa.

Sasa wazo la January ni lile lile la wakati wa ukoloni ila safari hii limebeba hoja kwamba majimbo/kanda ziwe 6 na, kwa kuzingatia maneno yake yafuatayo kuhusu jimbo/kanda ya Dar es Salaam, pia maendeleo ya jimbo mojawapo yasififishe ya lingine: “Cha msingi ni kwamba maendeleo na uwekezaji katika ukanda huu yasiwe na yasionekane kuwa na athari kwa maendeleo na uwekezaji kwenye kanda nyingine za kiuchumi. Maendeleo na uwekezaji kwenye kanda hii yawe ni sapoti kwa maendeleo ya nchi nzima” (Uk. 56).

Hayo mawazo yake pia ni mwendelezo wa sera ya majimbo ya chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, ambacho hata nacho kinayaangalia majimbo kiuchumi na si kiutawala tu. Ukiyasoma maandishi ya wanasiasa vijana wenzake, John Mnyika na Zitto Kabwe,  hasa waliyoyaandika kabla ya 2014, kuhusu majimbo au mikoa fulani ndani ya majimbo na kuyalinganisha na haya ya January ni kana kwamba kuna ‘kuegelezeana’.

Kwa mfano, mnamo tarehe 11 Januari 2013 Mnyika aliandika hivi kwenye makala yake yenye kichwa cha habari Sera ya Majimbo ya CHADEMA Siri ya Maendeleo: “Mwaka 2005 wapinzani wa hoja hii walitoa hoja kwamba lipo jimbo ambalo halina rasilimali na walitolea mfano wa jimbo la kusini. Hawa ni watu ambao pengine walikuwa hawafahamu kwamba Tanzania ina rasilimali kila mahali. Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa mikoa ya kusini haina maendeleo.Wakati huo tuliwaeleza ukweli ni kwamba tafiti zinaonyesha mikoa ya kusini ina rasilimali na mali asili nyingi sana tatizo kubwa ni miundo mbinu. Tuliwapa mfano kuwa Jimbo la Pwani ya Kusini kwa mfano lina mikoa ya Lindi, Mtwara na maeneo mengine yana rasilimali kama madini, bandari, uvuvi, nishati ya gesi, kilimo cha korosho, mikoko pamoja na utalii. CHADEMA imeendelea kuwaeleza wananchi umuhimu wa mfumo mpya wa utawala kwani kila jimbo lina rasilimali za kutosha ila kwa kuwa serikali ya CCM imekuwa ikiwahadaa wananchi na kuwafanya wabweteke kisaikolojia ili wasijiletee maendeleo, imekuwa ikipinga vikali serikali ya majimbo. Baada ya ugunduzi wa ziada wa gesi, sasa hoja imebadilika kutoka kusini haina rasilimali; sasa lugha ni kuwa kusini haipaswi kudai manufaa ya rasilimali hizo kwa kuwa ni za nchi nzima”.

Linganisha na haya ayasemayo January kitabuni mwaka 2014/2015: “Kanda nyingine ni Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Mtwara, na Lindi. Kwa miaka mingi mikoa hii imeonekana kama imesahauliwa kimaendeleo ingawa inazo fursa nyingi za kiuchumi zinazoweza kutumika kuinua kipato cha watu wake. Kutokana na historia ya mikoa hii Serikali ina wajibu kufanya juhudi za maksudi za kuhakikisha maendeleo ya mikoa hii inapatikana. Mwanga mpya umepatikana kutokana na uvumbuzi wa gesi ambayo inapaswa kuwanufaisha wananchi wa mikoa hii na taifa kwa ujumla…. Mikoa ya Lindi na Mtwara pia sasa imepata fursa mahsusi ya kiuchumi kutokana na upatikanaji wa gesi. Fursa za kuwepo kwa gesi ikiwemo viwanda vya kuchakata gesi kwa ajili ya kuiuza nje ya nchi ni muhimu pia ikatumika kuipa Kanda hii mwamko mahsusi wa kiuchumi wa kuweza kubadilisha maisha yawatu wa kawaida. Ni muhimu kutengeneza maarifa mahsusi ya kuwashirikisha wananchi katika uchumi huu” (Uk. 48).

Baada ya CHADEMA kushindwa kuiuza sera yao ya majimbo mwaka 2005-2010 kwenye Ilani yao ya Uchaguzi ya 2010-2015 wakaja na gia ya maeneo maalumu. Hivi ndivyo inavyosema kuhusu eneo hilo: “Mikoa ya Mtwara na Lindi ni mikoa ambayo bado haijachangia inavyostahili katika masuala ya uchumi na imekuwa bado ikikimbiwa kutokana na kile kinachoaminika kuwa ni ugumu wa maisha na umbali uliopo na maeneo yaliyofanikiwa zaidi. Chini ya serikali ya CHADEMA hili halitakuwa hivyo kwani mikoa hii ndio itaunda kile ambacho tunakiita kuwa ni “Makao Makuu ya Mapumziko Afrika” (Africa’s Vacational Capital). Lengo ni kuhakikisha kuwa miji hii inavutia uwekezaji mkubwa katika masuala ya mapumziko (Leisure). Katika kutekeleza azma hii, Serikali ya CHADEMA itachukua hatua zifuatazo…. Serikali itaanza ujenzi wa barabara za kisasa ndani ya mikoa hiyo na za kwenda nje ya mikoa hiyo ili hatimaye kuinganisha mikoa hiyo na mikoa ya Morogo[ro], Pwani, na Ruvuma….” (Uk. 90)

January naye anasema hivi: “Moja ya sehemu zenye fukwe nzuri zaidi katika ufukwe mzima wa Bahari ya Hindi kutoka Djibouti hadi Cape Town ni kipande cha kutoka Kilwa hadi Mtwara. Kipande hiki hakijaendelezwa sana kiutalii. Inawezekana kabisa kujenga mahoteli makubwa ya kitalii na viwanja vya kisasa vya mchezo wa gofu na uvuvi wa kitalii (sports fishing) kwenye kipande hiki lakini cha kwanza ni kuboresha miundombinu ya kufika huko, ikiwemo barabara na viwanja vya ndege. Ajira na
kodi na manufaa mengine yatakayopatikana kutokana na kufunguka kwa eneo hili kutabadilisha kabisa hali za maisha za watu wa kanda hii” (Uk. 50).

Tunaiona pia Ilani ya CHADEMA ya 2010-2015 ikisema hivi: “Mkoa wa Kigoma utapewa kipaumbele cha kuwa kiunganish[i] cha Tanzania na nchi ya DRC. Hivyo, mikakati ya makusudi itafanyika kama ambavyo tumedokeza awali lakini vile vile pia kuhakikisha kuwa mji huu unafikika kirahisi kutoka maeneo mengine ya Tanzania. Kipaumbele kikubwa kitakuwa ni katika kuboresha usafiri wa Reli ya Kati na Ujenzi wa barabara za kisasa za kuunganisha mkoa huo na Tabora na Shinyanga na kuunganisha na Mwanza kupitia Shinyanga Magharibi. Serikali ya CHADEMA …. Itahakikisha…. Kunakuwa na mapunguzo ya kodi mbalimbali za viwanda ili kuchochea ujenzi wa viwanda mbalimbali hasa vile vya kuhifadhia chakula, nyama na matunda. Tutahakikisha kuwa kilimo cha mawese kinapata mwamko mpya na kuwa chanzo kikubwa cha mapato” (Uk. 91).

Halafu tunamwona January akisema hivi kitabuni: “Kigoma inaweza kuwa kituo kikubwa cha biashara na uwekezaji kinachohudumia nchi jirani za Burundi na Kongo. Moja ya njia ya kufanya hivyo ni kuipanua Bandari ya Kigoma ili iwe bandari huru na bandari kubwa ya mizigo – na uchukuzi, kwa nchi za Burundi na Kongo, kwa kuwa Kongo ya Mashariki inategemea upande wa Tanzania kwa karibu bidhaa zote. Hili lazima liende sambamba na kuimarisha reli ya kati ili iwe ya kisasa ikiwa na treni ya abiria na mizigo karibu kila siku…. Mkoa wa Kigoma pekee unaweza kuzalisha mafuta ya kula ya kutosha ya kulisha nchi nzima kutokana na kilimo cha mawese. Kwa hiyo, lazima kuanzisha kilimo kikubwa cha mawese na viwanda vya kusindika mawese na bidhaa … nyingine za mawese, ikiwemo sabuni na umeme kutoka katika kanda hii. Kilimo hiki pia kinaweza kumaliza tatizo la ajira katika kanda ya magharibi….” (Uk. 52-53)

Utaalamu
Kwa kiasi kikubwa utaalamu ambao ni pembe mojawapo katika dhana ya Udadisi wa Viongozi Wenye U Tatu imejadiliwa kwenye sehemu ya uzoefu na ubunifu hapo juu na kugusiwa kwenye sehemu zingine. Hapa tunajikita kwenye kuhoji baadhi ya majibu ya January yanayogusa taaluma/utalaamu mbalimbali. Msingi hasa wa hoja hapa siyo kuonyesha alichosema ni ukweli au uwongo bali kudadisi kama kina ‘mashiko’ kitaaluma.

Tuanze na sekta ya Wizara yake, yaani mawasiliano. January anatujulisha kuwa “Ndio sekta inayoongoza kwa kukua kwa kasi na kwa muda mrefu – kwa kiwango cha wastani wa asilimia 20 katika kipindi cha miaka saba. Hakuna sekta yoyote ya uchumi iliyokuwa kwa kasi hiyo na kwa kipindi kirefu kama hicho” (Uk. 33 ). Sasa sijui hii ni taarifa ya kisiasa tu au vipi maana hatuambiwi mchango wake hasa kwenye uchumi ni kiasi gani ukilinganisha na hizo sekta zingine anazodai (bila kusema moja kwa moja hapo) kuwa hazikui/hazijakua kwa kiasi/kasi hiyo katika kipindi hicho.

Shida inaanzia pale unaposoma maneno haya ya Mchumi Aidan Eyakuze kwenye jalada la kitabu cha January: “Ni jambo la nadra sana kwa wanasiasa wa Tanzania kutoa ufafanuzi wa kina wa mipango na maono yao ya kiuchumi kwa uwazi na kwa kujiamini. Katika kitabu hichi, January Makamba amefanikiwa kufanya yote haya, tena kwa ujasiri mkubwa”. Maadam ‘mchumi mahiri’ kanena na wewe ni ‘mchumi kanjanja’ basi unaenda walau kutafuta machapisho ya mchumi huyo uone anasema nini kuhusu sekta zetu za uchumi zilizopo katika muktadha wa ‘uliberali mamboleo’.

Huko kwenye kabrasha la ‘The State of East Africa 2013’ (yaani ‘Hali ya Afrika Mashariki Mwaka 2013’) ambalo mmoja wa watunzi wake wakuu ni huyo Aidan Eyakuze unakutana na picha/grafu nzuri yenye kichwa cha habari “Evolving Structure of Tanzania’s Economy (2005-2012)” yaani ‘Mabadiliko ya Muundo wa Uchumi wa Tanzania’ iliyoambatana na maneno haya: “In 2012 the service industry in Tanzania accounted for 49 per cent of the economy, a 3 per cent increase from 2005, while agriculture’s share shrank from 28 per cent to 24 per cent during the same period. Industry grew its share of the economy from 20 per cent to 22 per cent in 2012” (p. 71). Unajiuliza nafasi ya sekta ya mawasiliano katika muundo huo iko wapi? Au bado kulikuwa hakuna takwimu? 

Au pengine ni kwa sababu sekta yenyewe imejifichaficha kwenye sekta nyingine na hivyo (labda) kupelekea January aielezee hivi baadaye humo kitabuni: “Zipo sekta kadhaa – ambazo zenyewe ni shughuli za uchumi lakini pia ni viwezeshi, yaani huduma, kwa shughuli nyingine za uchumi. Sekta hizo ni uchukuzi, kwa maana ya bandari, reli, barabara na usafiri wa anga; huduma za fedha, kwa maana ya upatikanaji rahisi na kwa unafuu wa mikopo ya biashara; nishati, kwa maana ya upatikanaji wa umeme wa uhakika na gesi viwandani kwa bei nzuri; mawasiliano, kwa maana ya huduma bora za simu na miundombinu ya TEHAMA; na huduma za utawala, kwa maana uwezo na weledi wa serikali kuwezesha biashara kuanzishwa na kuendeshwa bila vikwazo vya rushwa na urasimu, pamoja na usimamizi bora wa uchumi au sound economic management, ikiwemo sera wezeshi na rafiki kwa biashara na uwekezaji. Sekta hizi zinazohudumia uchumi ni muhimu sana ziwe bora na imara” (Uk. 81)?

Unatoka hapo unaenda kutafuta makabrasha ya mchumi mwingine mahiri, Profesa Benno Ndulu ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), huko unakutana na taarifa hizi kutoka kwenye kabrasha ‘aliloliandika’ na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, na kuliwasilisha kwa Mkurugenzi wa IMF, Christine Lagarde tarehe 18 Desemba 2014: “The structure of the economy is broadly unchanged with agriculture being the largest sector (23.8 percent) followed by trade (10.1 percent), construction (9.6 percent) and manufacturing (7.6 percent)” (Uk. 11). Unajiuliza kama sekta ya mawasiliano imekuwa kwa kasi kubwa kiasi kile kwa miaka 7 inakuwaje wachumi wanatuambia bado sekta kubwa nchini ni kilimo, ikifuatiwa na biashara, ujenzi na uzalishaji viwandani?

Ama hiyo sekta ya biashara iko juu kwa sababu ya sekta ya mawasiliano ndiyo maana January anatuambia “Kwamba sasa hivi karibu kila mtu ana simu ya mkononi na anaweza kumudu kuitumia sio jambo lililotokea lenyewe tu kwa ajali – ni matokeo ya uamuzi wa Serikali, ni matokeo ya Sera za Serikali, ni matokeo ya Sheria na Kanuni tulizoziandika Serikalini. Maisha ya Watanzania yamebadilika kwa kiwango kikubwa sana kutokana na sera muafaka tulizoweka, zilizowezesha uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya mawasiliano ikiwemo kwenye mitandao ya simu za mikononi. Huduma ya fedha, kutuma na kupokea fedha, sasa inapatikana kwa Watanzania karibu wote – hata wale wasio na akaunti za Benki. Biashara za aina zote zimeshamirishwa kutokana na urahisi wa mawasiliano – jambo lililowezeshwa na uwekezaji wa Serikali kwenye kujenga mkongo wa mawasiliano wa taifa” (Uk. 33)?

Pengine kwa kutambua kuna tatizo katika kuthibitisha ni kwa kiasi gani hasa sekta ya mawasiliano inachangia pato la taifa, January anatupiga ‘chenga ya mwili’ na ‘kuitupia mpira’ wizara nyingine kama ifuatavyo japo humo humo kitabuni anadai Serikali ni timu: “Kumekuwepo na mashaka kwamba Serikali haipati mapato stahiki kutoka kwenye makampuni ya simu. Suala la usimamizi wa kodi na mapato ni suala la Wizara ya Fedha sio la Wizara za kisekta. Hata hivyo, mwezi Oktoba 2013, tumefunga mtambo wa kisasa wa kufuatilia mapato ya makampuni ya simu na sasa mapato ya Serikali yameongezeka kwa kiwango kikubwa. Pia, kutokana na usimamizi mzuri wa sekta hii, ajira zimeongezeka sana – kwanza kwenye makampuni yenyewe lakini pia kwa Watanzania wengi hasa kina mama walioingia kwenye biashara za kuuza vocha na huduma za kuhamisha fedha. Karibu katika kila kona ya nchi yetu wapo watu wanaofanya biashara hizi – na hizi ni ajira nyingi sana zinazowasaidia Watanzania wa kawaida” (Uk. 33-34).

Msomaji unazidiwa kuchanganyikiwa – ama kuchanganywa – pale unapokutana na majibu haya ya January kwa swali mahsusi la Padre Karugendo kuhusu uchumi wa Tanzania: “Kwanza, shughuli za uchumi zilizokua kwa kasi katika miaka kumi na tano iliyopita ni zile ambazo hazijawagusa au haziwahusishi watu wengi – kwa maana ya ajira na kipato. Kwa mfano, mtaji uliowekezwa kwenye sekta ya madini ni mkubwa na mtaji huo umejumlishwa kwenye mchango wa Pato la Taifa, hivyo kuleta taswira ya ukuaji wa kasi wa uchumi, lakini ajira, kodi na manufaa mengine hayakuwa makubwa sana. Kwa kifupi ni kwamba uchumi wetu umepanuka katika sekta ambazo haziwagusi wananchi wengi moja kwa moja. Shughuli ambazo zinawagusa au zinawahusisha watu wengi ni kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi – shughuli ambazo zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanajihusisha nazo. Lakini ukitazama kasi ya ukuaji [wa] shughuli hizi, bado sio ya kuridhisha” (Uk. 79-80).

Unabaki unajiuliza hivyo hizo sekta zilizotajwa hapo juu na wachumi kuwa ndiyo sekta kubwa katika muundo wa uchumi – hasa hizo ya biashara na ujenzi – au hiyo ya huduma inayosemekana kukua kwa kasi, je haziwahusishi/haziwagusi watu wengi? Kwa nini? Na inakuwaje hata hiyo ambayo ‘imefagiliwa’ sana na January – yaani mawasiliano – kuwa imekuwa kwa kasi kubwa na kugusa watu karibia wote Tanzania haina jipya hapo?

Unabaki kujiuliza January aliona nini hasa kuhusu hayo yote wakati anafanya hivi: “Majuzi nilikuwa natazama kitabu cha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa na nikaona takwimu kwamba mwaka 2013, tumeuza nje huduma na bidhaa za thamani ya dola bilioni 6 na tumeagiza kutoka nje bidhaa na huduma za thamani ya dola bilioni 11” (Uk. 83).

Chambuzi za kitaalamu za January pia zinaibuka na hili ambalo pia tungeweza kulijadili kwenye sehemu ya upya na ya ubunifu: “Ukiwa unamiliki mashirika haya haupaswi kushindwa kununua vitabu vya watoto mashuleni, haupaswi kukosa madawa kwenye zahanati na hospitali. Lakini ili tufanikiwe lazima tubadili mfumo wa umiliki na usimamizi wa mali za Serikali. Kwa sasa mwenye mali ni Msajili wa Hazina lakini anayesimamia uendeshaji wa mashirika ni Wizara za Kisekta. Huu ni mkanganyiko wa kwanza. Shirika moja lina mabwana wawili. Suala hili aliwahi kulizungumzia kwa ufasaha zaidi rafiki yangu Ndugu Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma. Ni vyema basi tukaanzisha Kampuni kubwa tanzu, kwa Kiingereza wanaita a Holding Company, itakayomiliki na kusimamia uendeshaji wa Mashirika ya kibiashara ya Serikali kwa weledi, maarifa ya kisasa na kanuni ya kibiashara bila kuingiliwa na siasa. Singapore wamefanya hivyo na wamefanikiwa sana. Msajili wa Hazina ameelemewa na majukumu mengi, ikiwemo kushiriki kwenye bodi za mashirika zaidi ya 100. Pia baadhi ya Wizara za kisekta zimeishia kuwa waendeshaji na wasemaji wa mashirika yaliyo chini ya Wizara hizo badala ya kutoa uongozi wa ujumla wa kisera na kimkakati wa maendeleo ya sekta husika” (Uk. 183).

Mdadisi wa historia ya Ujamaa na Ubepari nchini unajikuta unajiuliza hiyo kampuni kubwa tanzu ina/itakuwa na tofauti gani hasa na Shirika la Maendeleo la Taifa ambalo Idrian Resnick alilielezea hivi katika kitabu chake cha mwaka 1981 kijulikanacho kama The Long Transition: Building Socialism inTanzania: “A new parastatal organization (state-owned corporation), the National Development Corporation (NDC) was created in 1964 to manage government’s holdings in manufacturing and primary product companies…[it] grew enormously during its first five years, becoming the channel through which imperialism made substantial gains…. By 1966, the NDC wholly owned or held shares in thirty-seven companies” (Uk. 52). Kwa tafsiri rahisi ya kimuhtasari, shirika hilo lilianzishwa umnamo mwaka 1964 kama kampuni kuu ya kumiliki makampuni mengine na lilikua kwa kasi sana na kuwa sehemu ya kuuwezesha ubeberu kupenya nchini ambapo kufikia mwaka 1966 likawa na hisa au umiliki kamili wa makampuni 37.

Kivumishi mtambuka ndani ya kitabu cha January kinaonekana kwa mara nyingine tena pale anapotuambia hivi: “Kwanza kabisa, ni muhimu kubadilisha mtazamo na kuondokana na dhana ya ajira au dhana ya kuajiriwa. Tuchukue dhana mpya ya kipato. Kimsingi watu hawatafuti ajira bali wanatafuta kipato cha kujiendeleza kimaisha. Kuajiriwa ni moja tu ya njia ya kutafuta kipato. Tukiwa na dhana ya kipato itaweza kutusaidia kupanua wigo wa mawazo na fikra kuhusu mambo tunayoweza kuyafanya” (Uk. 38-39). Lakini mipango yake mikubwa – kama wa “Muswada na Mpango Mahsusi” wa kutenga shilingi trilioni 3.6 kwa miaka 3 ili kuwezesha vijana – umejikita katika kuongeza ajira. Hapa tunapata utata kuhusu upya wa dhana yake maana kwa kawaida dhana ya ‘kipato’ (income) na ‘ajira’ (employment) zimefungamana hasa mtu anapoitazama ajira katika upana wake, yaani, ajira za kuajiriwa na za kujiajiri, ambapo kwa mtazamo huu ajira inaweza kutafsiriwa pia kwa Kiingereza kama ‘income generating activities’, yaani ‘shughuli za kujipatia kipato’. Tungependa kuulewa huu utalaamu unaodai unatuletea dhana mpya itakayotupanulia mawazo (mapya).

Pia tafiti mbali mbali za biashara barani Afrika na kwingineko zinaonesha kuwa siyo kila mfanyabiashara wa kati (au hata mdogo) anataka kuwa mfanyabiashara mkubwa hasa ukizingatia kuwa kuna wafanyabiashara ambao lengo lao ndilo hilo la ‘kati’ au ‘udogo’ ili mradi lina tija kwa familia zao na kwa taifa. Lakini January anatuambia kuwa “Rais ajaye lazima awe karibu na aongoze jitihada za dhati za kuwasaidia wafanyabiashara wa kati, wengi wao waliopo huko mikoani, wengi wao wakiwa wasafirishaji, wanunua mazao, wenye viwanda vidogo vidogo, ili nao wawe wafanyabiashara wakubwa” (Uk. 10). Hivyo, tungependa kujua pia utaalamu huu wa biashara unaopelekea kuwa na hitimisho hili msingi wake ni nini hasa isije ikawa ndiyo itikadi/sera zile zile za kuua biashara ndogo ndogo ili kufungua njia kwa biashara kubwa kubwa tu. Hili ni muhimu maana January mwenye anakiri kwamba “Kote duniani, biashara za kampuni ndogo na za kati ndio injini ya uchumi wa nchi” (Uk. 43).

Suala hili tutalijadili zaidi kwenye sehemu ya ‘uitikadi’. Lakini ni dhahiri kuwa kwa kiasi kikubwa utaalamu huu wa January unapata ushawishi mkubwa kutoka kwenye taasisi kubwa za kifedha duniani kama haya maneno yake kitabuni yanavyoonesha: “Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, asilimia 20 tu ya biashara na kampuni ndogo zikiongeza mfanyakazi mmoja kwa mwaka, ajira 400,000 zitazalishwa. Je asilimia 80 za biashara hizi zikiongeza watu watatu kwa mwaka?” (Uk. 43); “Asilimia zaidi ya 80 ya biashara za jijini ni biashara ndogondogo zinazoajiri watu wasiozidi wawili. Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, asilimia 20 tu ya biashara hizi zikiongeza mfanyakazi mmoja tu, ajira zitakazopatikana ni 400,000 kwa mwaka. Kwa hiyo kuna haja kwa Serikali kuhakikisha kwamba biashara ndogo katika miji yetu zinapanuka na kuwa biashara kubwa na za kati na kuongeza watu wanaojishughulisha na biashara” (Uk. 120).

Kabla ya kumaliza kuudadisi utaalamu wake uchumi, mdadisi unayasoma kwa kina maneno haya ya nguli wa ‘sayansi ya siasa’ kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam/Mkwawa, Profesa Bernadeta Killlian, yaliyopo kwenye jalada la kitabu cha January kujaribu kubaini nini hasa kilimgusa humo: “Je, uchumi wa Tanzania unaweza kuwafanya Watanzania waondokane na umaskini? January Makamba ameainisha mawazo yake makubwa na mapya ya kiuchumi pamoja na mipango yake madhubuti ya maendeleo katika kitabu hiki ambacho kimejaa matumaini juu ya uwezekano wa Tanzania Mpya”.

Maneno ya Profesa yanakufanya ujiulize wataalamu wetu kutoka kwenye vyuo vikuu vyetu wana nafasi gani, kitaalamu na kiitikadi, katika safari (fupi na ya haraka) ya January ya kuuelewa uchumi. Unarudi kitabuni na kukutana na shuhuda hizi: “Kwa mfano, kutokana na kazi ile [ya Msaidizi  wa Rais], nililazimika kwa haraka sana kujifunza kuhusu masuala ya uchumi kwa kusoma na kuongea na manguli wa uchumi, ili kuweza kumsaidia Rais kuwasiliana na wadau mbali mbali kuhusu malengo yake kwa uchumi wa nchi. Kwa hiyo uelewa wangu kwenye masuala ya uchumi na maendeleo kwa ujumla umepanuka kutokana na mazingira ya kazi ile. Na huo ni mfano wa uchumi tu, nimejifunza mambo mengi ya kisera na kimkakati kwenye sekta mbali mbali kama kilimo, afya, miundombinu, na mambo ya ulinzi na usalama” (Uk. 66).“Kwa upande wa wahadhiri na wakufunzi wa vyuo vikuu, nako nina marafiki wengi ambao pamoja na kujadiliana nao kuhusu mustakabali wa taifa letu, tumekuwa pia tunazungumzia changamoto zinazowakabili katika kazi zao….” (Uk. 102)

Uitikadi
January anatuambia hivi: “Katika kipindi chote ambacho nimekuwa kiongozi, nimekuwa naamini kwamba elimu haina itikadi, inagusa maslahi ya kaya moja moja na maslahi ya taifa” (Uk. 6). Kisha anasema: “Katika awamu zijazo, elimu itakuwa ndio siasa” (Uk. 7).

Lakini hakuna siasa ambayo haina itikadi. Itikadi yako ikiwa ni ya mrengo wa kushoto, kulia au wa katikati basi elimu unayotoa kwa kiasi kikubwa itafuata mrengo husika. Ni dhahiri kuwa itikadi ya January ni mchanyato – kama siyo mkanganyiko – wa pande mbali mbali. Pengine huo ndiyo wajihi wa viongozi wengi wa kizazi kipya na zama mpya ambazo Mzee Mwinyi amesema dibajini nazo zina “mitume wake” (Uk. viiii).

Huyu January anayetuambia “Serikali inao wajibu wa kuona fahari ya kutengeneza mabilionea wa Wakitanzania ambao watawekeza fedha zao hapa, watatengeneza ajira, kulipa kodi, kuendeleza nchi yao” (Uk. 87)” ndiye huyo huyo anasema hivi: “Mimi ni muumini wa falsafa za Mwalimu Nyerere na kama kiongozi kijana najitahidi niwezavyo niige mfano wake, mfano wa maisha yake, mfano wa msimamo wake, mfano wa uadilifu na uchapakazi wake” (Uk. 186).

Pia ndiye January anayesema hivi bila kutuelezea huo urasimishaji unatofautianaje na tulioletewa na Hernando de Sotokupitia MKURABITA ili eti tuhuishe mitaji yetu mingi japo ni mfu na kutuwezesha na sisi tuwe na Ubepari wenye tija kwa wamiliki wa rasilimali na biashara: “Juhudi za kurasimisha sekta isiyo rasmi lazima zifanyike kwa kasi mpya na maarifa mapya” (Uk. 10).

Ukigeuka kidogo tena unamkuta January anayesema tuendelee tu na haya ambayo kwa kiasi kikubwa ni ya Kinyerere: “Vilevile, kuendelea na harakati za kuwezesha kuwepo mfumo wa uchumi na biashara duniani wa haki na usiokandamiza nchi changa; kuendelea na harakati za kujenga msingi wa nchi maskini kushirikiana zaidi ikiwemo kufanya biashara zaidi baina yetu; lazima tuendelee na harakati za kurekebisha taasisi za utawala wa siasa za kimataifa zizingatie matakwa na maslahi ya mataifa mengi zaidi; lazima kuendelea kupambana na ukoloni-mamboleo ambao kila kukicha unachukua sura mpya ikiwemo kuhusisha misaada kwa nchi yetu na maslahi ya kibiashara ya mashirika ya nchi zinatoa misaada hiyo, kupewa masharti ya kupata misaada isiyo na msingi, na mashinikizo ya kufuata sera na kuchukua misimamo isiyo na manufaa kwa nchi yetu” (Uk. 92).

Tena anasisitiza kwamba “Rais ajaye lazima athamini mchango [wa misaada kwa “mataifa tajiri na makubwa duniani”] lakini pia ajue kwamba nchi wahisani sio wajomba zetu na lazima aongoze mkakati madhubuti wa taifa letu kujitegemea kibajeti na kubadili mahusiano yetu na nchi kubwa kutoka kwenye ufadhili kwenda kwenye ushirika wa kibiashara na uwekezaji” (Uk. 11).

Ila malengo yake ya Urais/Uongozi wa kizazi kipya yanalenga kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo “Bila kufuta mipango mizuri iliyopo sasa….” (Uk. 74) na moja ya mipango hiyo anaielezea hivi:  “Jitihada nyingi zimefanyika tangu uhuru katika kilimo, lakini kutokana na ukubwa wa sekta hii, matokeo bado ni finyu. Serikali ya Rais Kikwete imeweka kipaumbele kwenye kilimo kupitia sera kubwa kuliko zote toka uhuru wa nchi yetu ya Kilimo Kwanza inayojumuisha miradi mikubwa kama vile mradi wa kisasa kabisa SAGCOT. Sera hii ya Kilimo Kwanza imeundwa kutatua matatizo yote katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi na kuongeza tija ya shughuli za kilimo kwa wakulima na uchumi wa taifa letu kwa ujumla” (Uk. 74).

SAGCOT hiyo hiyo ambayo wanaharakati wa HakiArdhi na wengineo tunaidadisi kuhusu ‘uporaji wa ardhi’ (land grab) kubwa sana ya wananchi na kuwapa wawekezaji/wabia wakubwa hawa kutoka nje wakiwamo ambao wanatiliwa mashaka katika nchi mbali mbali: “Diageo,DuPont, General Mills, Monsanto, SAB, Syngenta, Norfund, Unilever, USAID, YaraInternational, the Irish Embassy, AGRA and FAO”. Lakini January yeye ana jibu la haraka tayari – eti anasema: “Ardhi ambayo haijapimwa ndio chanzo kikubwa cha migogoro. Tumejaribu kupima maeneo mengi nchini lakini kasi ni ndogo na bajeti haitoshelezi. Napendekeza matumizi ya teknolojia ya satellite katika kupima na kupanga matumizi ya ardhi nchini. Kila kipande cha ardhi katika nchi yetu kiwe kimepimwa, kina hati na matumizi yake yanajulikana” (Uk. 75).

Ndiyo maana siyo jambo la kushangaza kuona kuwa miongoni mwa wajumbe wa bodi ya Kampuni/Shirika la Maendeleo la Bumbuli aliowataja mtandaoni na kuelezea nyadhifa zao mbalimbali katika taasisi kadhaa yupo Profesa Andrew Temu ambaye pia ametambulishwa kama mjumbe wa bodi ya SAGCOT. Yupo Betram Eyakuze ambaye ametambulishwa kama mmoja wa wamiliki wa Serengeti Advisers Limited ambaye pia anashiriki katika mradi mkubwa wa kilimo cha kibiashara. Tunamwona pia Dakta Paul Armington ambaye tunaambiwa amewahi kuwa mchumi wa IMF na Benki ya Dunia. Kinara  wa – au kichwa cha – sera za uchumi wa soko na mtetezi mkuu mmojawapo wa sekta binafsi nchini Tanzania, Balozi Juma V. Mwapachu naye yupo ‘bodini’. Hali kadhalika Edward V.K. Jaycox ambaye tunajulishwa kuwa aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia katika ukanda wa Afrika ‘ya Kusini mwa Jangwa la Sahara’. Wanabodi wengine waliotajwa ni Dakta Najim Msenga, Askofu Dakta Stephen Munga, Bi. Grace C. Rubambey na January Makamba mwenyewe. Ukiiweka kwenye mizani ya itikadi ya Nyerere, bodi hii inaangukia kulia badala ya katikati achilia mbali kushoto.
                                                                                   
Utu
Wahenga wetu walinena kuwa “mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni”. Na sisi wachambuzi/wadadisi tunahojiwa pale tunapojikita tu kwenye kuibua mabaya na kufukia mazuri. Hivyo, maadam simjui January kwa undani kama mtu binafsi, ni dhahiri kuwa kwenye kitabu chake ameelezea vitu ambavyo vinakidhi kigezo kikuu kimojawapo cha dhana ya Udadisi wa Viongozi Wenye U Tatu. Kiukweli sijui kama hayo anayosema (w)aliyafanya ni kwa ajili ya maslahi ya kisiasa au la lakini kimaandishi – yaani kwenye karatasi – walau yanaonesha utu. Jukumu la kupima utu, kama dhana ya U Tatu inavyoeleza, ni la wananchi wanaomjua fika ambao hasa hasa ni wale walioko jimboni na mtaani kwake.

Nukuu mmojawapo yenye mguso wa utu ni hii: “Kwa kuzingatia mazingira magumu ya hali ya hewa ya baridi kali, Shirika hili limeanzisha programu ya kugawa viatu vya shule kwa wanafunzi wote wa Shule za Msingi katika Jimbo la Bumbuli kila mwaka. Tumeanza mwaka huu kwa kugawa pea 45,000 na tutaendelea kufanya hivyo kila mwaka. Pia tumeanzisha programu za kuwaandaa wanafunzi wa kidato cha nne kufanya vyema katika mitihani yao ya taifa” (Uk. 32).

Tuhitimishe hili la utu kwa kusisitiza kuwa watu wanaowasiliana na January mara kwa mara na kwa undani ndiyo wenye nafasi kubwa zaidi ya kuthibitisha utu wake kuliko siye wengine tunaomjua kupitia vitabu, magazeti na mtandao. Hao – wakiwamo anaojadiliana/anaobishana nao kwenye mitandao ya twitter n.k. – ndiyo wanaweza, mathalan, kuthibitisha hili alilolisema kitabuni kuhusu mahusiano yake na watu ambao ndiyo msingi hasa wa utu: “Kama ni kukomaa kwa maana ya busara, hekima na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, jibu pia ni ndio, nimekomaa. Sina rekodi ya kuropoka, kutukana, kuhamaki, kushambuliana na watu na kufanya maamuzi ya papara. Najua uzito wa dhamana ya uongozi” (Uk. 29 ).

Ujasiri
Kwenye jalada la kitabu husika, Mzee Yusuf Rajab Makamba, Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu, anamuelezea hivi mwanaye: “Nimemfahamu January katika kipindi chote cha uhai wake kama mtu mwenye msimamo na pia kama kijana mwenye hekima na busara inayozidi umri wake. Lakini sikuwa nafahamu kwamba ana uelewa na ufahamu wa mambo mengi na kwa kina hadi niliposoma kitabu hiki”.  Naye January anamuelezea hivi babaye: “Lakini pia kuna mambo mengi mazuri ambayo nimejifunza kutoka kwake ikiwemo haja ya kuwa na msimamo usioyumba katika unayoyaamini na haja ya kutokumuogopa mtu yoyote” (Uk. 18).

Hivyo, siyo jambo la kushangaza kuona January anatuelezea visa viwili vinavyojaribu kutudhihirishia kuwa ana ujasiri na kutuambia kuwa kuna vingine vingi tu. Kisa cha kwanza ni hiki kuhusu kubaini “wizi mkubwa wa chakula cha wakimbizi”: “Sasa siku moja, tukiwa katikati ya kugawa, kambi nzima ikiwa imesimama kwenye foleni nikabaini kitendo cha wizi. Nilikasirika sana. Nikalazimika kufanya uamuzi wa aidha kuendelea tu kugawa chakula ili tumalize huku nikijua kuna watu wanaiba au kusimamisha zoezi ambako kuna gharama na usumbufu mkubwa. Nilichofanya nilienda kituo cha polisi kambini, nikatoa shitaka la wizi na nikaomba askari waje kwenye eneo na wakaja na gari lao pale kwenye uwanja wa kugawa chakula. Nikawatangazia wakimbizi kwamba tunasimamisha zoezi kwa muda kwa jambo lenye manufaa kwao na kwamba watulie. Nikawaambia askari kwamba naomba wafanyakazi wangu wote wakamatwe na kupelekwa ndani kwa tuhuma za wizi. Walijua ni mzaha. Na nikawaambia kwamba wana nusu saa wataje wezi miongoni mwao la sivyo kila mmoja anafukuzwa kazi papo hapo. Wakati huo huo nilikuwa natafuta vibarua wengine wa muda wa kuendelea kugawa. Chini ya nusu saa wakatajana. Waliohusika wakabaki polisi. Wasiohusika wakaja kuendelea kugawa chakula. Tangu siku hiyo tukakomesha wizi wa chakula cha wakimbizi. Hiyo ilikuwa mwaka 1997 na nilikuwa na miaka 23 tu. Nilijifunza tangu zamani, tangu nikiwa kiongozi mdogo, kwamba, kuna baadhi ya mambo ya msingi, kama wizi au dhuluma, ambayo hakupaswi kuwa na suluhu. Wengine wanaweza kusema huu ni uamuzi mgumu lakini mimi naamini ni katika kutekeleza wajibu (Uk.114).

Kisa cha pili ni kuzuia uchakachuaji wa mafuta uliowahi kushamiri nchini na January anatuambia kwamba: “Matokeo yake, na kama ukiwa unasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze ukihesabu idadi ya vituo vya mafuta aidha vilivyofungwa au vilivyoishia katikati kwenye ujenzi, utaona ni vingi mno kwa sababu vilikufa kutokana na shughuli ya uchakachuaji kukoma. Tulipendekeza na kusimamia uamuzi ambao haukuwa maarufu wakati ule lakini majuzi nimesikia watu ambao hawakuunga mkono suala hili wanapongezana kwa kumaliza tatizo la uchakachuaji” (Uk. 114).

Pia tunaonyeshwa picha yenye maneno haya: “January Makamba akiongoza mkutano aliouitisha kwa ajili ya kutafuta utatuzi wa matatizo katika Kampuni ya Simu ya TTCL. Mkutano huo ulipelekea kusimamishwa kazi kwa baadhi ya maofisa wakuu wa kampuni hiyo. Mafanikio ya mageuzi katika TTCL yameanza kuonekana” (Uk. 171).

Lakini kuna haya maneno yake humo kitabuni yanayotufanya tuutilie mashaka ujasiri wake: “Kuna tatizo kubwa la usimamizi wa miradi ya Serikali. Hapa tunapoteza fedha nyingi sana kwa wajanja wachache. Kwa mfano, daraja ambalo linapaswa kujengwa kwa shilingi milioni 100, linatengenezewa BOQ, yaani mahitaji, ya shilingi milioni 300 na hatimaye linajengwa kwa shilingi milioni 30 na linavunjika baada ya miaka miwili na zinatafutwa fedha nyingine za ujenzi. Au kwenye mradi wa maji, panapostahili bomba la inchi 6 linawekwa bomba la inchi 2 na baada ya muda linapasuka na maji hayatoki tena. Haya nimeyashuhudia kama Mbunge ambapo niliwahimiza watu wa Bumbuli kukataa kupokea mradi uliojengwa chini ya kiwango. Cha ajabu kulikuwa na presha kubwa sana kutoka kila pahala kwamba tuupokee. Cha ajabu zaidi hakukuwa na adhabu yoyote kwa waliohusika. Cha ajabu zaidi mkandarasi huyo huyo akaendelea kupewa kazi nyingine zaidi za ujenzi. Haya yanatokea kila siku, kila mahali kwenye maeneo yetu” (Uk. 182).

Kabla sijakisoma kitabu cha majibu ya January Mtandao wa Wazi wa Wanazuoni ulifanya mjadala mkali mtandaoni wenye kichwa cha habari Kisa Cha Vitabu Viwili Vya Urais? ambacho ulichochewa na picha za kulinganisha kitabu cha Jakaya Mrisho Kikwete: Tumaini Lililorejea kilichoandikwa mwaka 2006 na Prince Bagenda na hiki kinachohusu mazungumzo ya January na Padre Karugendo. Niliwauliza wanazuoni haya: Kwenye mjadala wa Escrow tumeona IPTL ilianza lini na hatua gani zilichukuliwa, umeona ‘uzoefu’ gani? (Kumbuka Rais Mtarajiwa aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, je, alizuia ufisadi sekta-ni (rejea hii Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu Gesi(Ripoti ya Pan African Energy) au baada ya kuwa Naibu Waziri wa Wizara nyingine hakuweza kuendelea na harakati zilizotajwa humo ripoti-ni? Au aliendelea tu ila nyuma ya pazia?)

Baada ya kupata majibu kadhaa kutoka kwa Wanazuoni nikauliza maswali haya ya nyongeza:  “Na ndiyo maana kabla mgombea hajaulizwa ‘utafanya nini?’ inabidi aulizwe ‘ulifanya/umefanya nini?’ Kwenye ule ‘uzoefu’ dhidi ya ufisadi maswali yanakuwa ni marahisi tu, natumai Prof. Kitila Mkumbo et al. watawauliza maswali kama haya kwenye hiyo midahalo ya ITV na UDASA: Ulifanya/Ulisema nini EPA ilipotokea? Ulifanya/Ulisema nini RICHMOND ilipotokea? Ulifanya/Ulisema nini ESCROW ilipotokea? Utaishughulikiaje ESCROW ukiingia IKULU?

Hivyo, nilipata shauku kubwa nilipoona swali nambari 21 la Padre Karugendo kwa January likiuliza hivi: “Wananchi wanalalamikia sana ufisadi. Mikakati ya sasa inaelekea haijafanikiwa kiasi cha kuridhisha wananchi. Je, wewe una mbinu zozote mpya za kupambana na tatizo hili? Je, unaongeleaje ufisadi wa Richmond, EPA na IPTL” (Uk. 108).

Lakini majibu ya moja kwa moja ya January kwa swali hilo hayakuonyesha uzoefu na mchango wake katika masakata hayo. Tunachokiona ni maneno kama haya yafuatayo ya kikaulimbiu yanayovut(i)a hisia: “Rushwa ni kansa mbaya sana ambayo inaweza kuitafuna jamii. Moja ya dhambi kubwa unayoweza kufanya kama kiongozi ni kutumia dhamana uliyopewa na wananchi kujinufaisha mwenyewe na ndugu, jamaa na marafiki zako. Ni zaidi ya ujambazi” (Uk. 108); “Tatizo limekuwa kubwa sasa na watu wanakula mali ya umma waziwazi, bila woga – wanavimbiwa na kujitapikia kwenye viatu vyao. Na wadogo wanawaiga wakubwa” (Uk. 108).

Pia yapo majibu kama haya ambayo hayaonyeshi uchukuaji wowote wa hatua za kijasiri: “Umeuliza pia kuhusu masuala ya Richmond, EPA na IPTL. Hizi skendo zimetudhihirishia kwamba bado tunayo safari ndefu na kazi kubwa ya kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Zimetuonesha kwamba miongoni mwetu wapo ambao kwa tamaa binafsi wapo tayari kuhujumu uchumi wa taifa letu. Lakini vilevile zimetufundisha kuhusu haja ya kuimarisha mifumo ya uwajibikaji kwa watendaji na viongozi wa umma. Inashangaza kwamba kiongozi amebainika kuhusika na ubadhirifu lakini bado anasubiri msukumo wa bunge au jamii kuwajibika. Lazima tujenge utamaduni wa uwajibikaji lakini vilevile kwa viongozi waliobainika kutumia madaraka vibaya au kujihushisha na ubadhirifu, kujiuzulu au kuondolewa kwenye nafasi zao hakutoshi. Lazima jamii ishuhudie wakipewa adhabu kali ili kuzuia matukio ya namna hii kujirudia. Ushauri wangu ni kwamba maswala ya uwajibikaji yasichanganywe na siasa. Kwamba pale kunapotokea wizi na ubadhirifu, wahusika ni watu binafsi, sio vyama na kwamba wabunge na viongozi wa vyama vyote wanapaswa kuungana kulaani na kuchukua hatua bila kuingiza siasa za vyama. Skendo za EPA, IPTL na Richmond zimeandikwa sana kwenye magazeti lakini kila siku kuna wizi mkubwa zaidi unaoendelea katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambao hausikiki” (Uk. 110).

Lakini alishatumbukusha kuwa “Kulizungumzia na kulipigia kelele suala la rushwa pekee hakutoshi” na kutuambia “Ziko namna mbili za kukabiliana na hili tatizo” (Uk. 110). Lakini January hatuambii uzoefu wake katika kutumia hizo njia mbili kuukabili ufisadi wa RICHMOND, EPA na IPTL. Hilo linatufanya tuhoji ujasiri wa kukabiliana na ufisadi. Pia hatuambii moja kwa moja atafanya nini kukabiliana na ESCROW (kama) akiwa Rais.

Ila ndiye aliyetoa msisitizo huu: “Katika kutafakari, nimebaini kwamba Rais ajaye ana mtihani mkubwa wa kurejesha imani haswa ya wananchi wengi masikini kuwa anaguswa na hali yao, na kuwa anachukua jitihada za kuwakwamua kutoka katika hali yao. Hayo yatadhihirika si tu kwa maneno bali hatua atakazochukua dhidi ya viongozi wabadhirifu, wala rushwa na matumizi ya serikali yake. Hapaswi kuhisiwa wala kutuhumiwa kwamba yeye ni miongoni mwa hao” (Uk. 5).

Uchaguzi
Tanzania ina changamoto kubwa. Wale maadui wakuu watatu wa awali – maradhi, ujinga na umaskini – bado wapo na Mwalimu Nyerere alituambia ameongezeka wa nne, yaani, rushwa. Lakini adui rushwa sasa amekubuhu na kuwa ufisadi, yaani, ‘rushwa (m)kubwa’.

Hivyo, nakubaliana na maneno haya ya January: “Katika tafakuri yangu nimejiridhisha kwamba lazima Rais wa Awamu ya Tano awe ni mtu mwenye kuzitambua changamoto hizo na kuwa na mkakati wa kuzitatua. Changamoto hizi ni za kiuongozi na utatuzi wake utategemea tu kiongozi mwenyewe, hulka yake, mtazamo wake na usahihi wa maamuzi yake. Na yote hii inategemea wajihi, yaani character, wa kiongozi mwenyewe. Hivyo, wajihi wa mgombea unapaswa kujibu maswali yanayoletwa na changamoto hizi” (Uk. 3). Ila kuchagua ni kuamua. Na kama January anavyosema: “Cha msingi ni kwamba wenye kuamua kiongozi awe nani ni Watanzania wenyewe – kwa msaada wa Mungu” (Uk. 30).

Mungu na atusaidie tufanye uchaguzi/uamuzi sahihi ili, kama vijana wa kizazi kipya wanavyosema, tusije tena ‘tukapigwa changa la macho’ na ‘kuuziwa mbuzi kwenye gunia’.

Nimeamua kumchagua mtu mwenye uthubutu, ujasiri na uzoefu wa utu, uadilifu na utaalamu. 

Wewe je?

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP