Thursday, January 1, 2015

Wezi Wakuu Watatu?

“Katika shilingi bilioni 306 zilizokuwa na zilizopaswa kuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow kuna fedha za Umma. Serikali inasema hazikuwa 306 bilioni bali 202 bilioni! Hii sio hoja ya msingi. Hoja ya msingi ni kwamba hata zingekuwa bilioni moja, bado ndani yake kuna fedha za umma na ilipaswa utekelezaji wa hukumu ya kupunguza kiwango cha tozo ya uwekezaji kufanyika ili kujua kiasi cha fedha za umma. Tapeli Harbinder Singh Seth alilipwa hizo zilizokuwemo katika akaunti na akaendelea kulipwa bakaa na TANESCO kiasi kwamba shirika hili linalofilisika linamlipa kila siku bwana huyu shilingi milioni 400. Kila siku inayokwenda kwa mungu tunamlipa mtu ambaye hajawekeza hata senti tano nchini mwetu. Alikuja na briefcase tu. Kule Kigoma kuna neno jipya siku hizi, linaitwa umazwazwa. Ni kama ujuha hivi. Huu ni umazwazwa ambao wananchi hawapaswi kuukubali. Watu watatu tu ambao ni raia wa kigeni walichora wizi huu kwa miaka mitatu. Mtu mmoja anaitwa Bwana Baharuddin kutoka Malaysia, Bwana Issa Ruwaih kutoka Oman na Bwana Singh kutoka Kenya na anaishi Afrika Kusini. Walidanganya nyaraka za kuuziana makampuni, bwana Baharuddin akauza hisa za IPTL kutoka Mechmar kwenda kwa Bwana Issa wa kampuni ya PiperLink na Bwana Issa naye akauza hisa hizo zikiwa zimezuiwa na Mahakama kwa Bwana Seth wa kampuni PAP.  Mabwana hawa wanajua Watanzania ni mazwazwa na hawafanyi uchunguzi wa kina, yaani ‘due diligence’ kwani hata kwenye EPA fedha ziliibiwa kwa kutofanya due diligence na kwa kutumia kitu kinaitwa ‘deed of assignment’. Mabwana hawa wanajua kuwa Watanzania wenye ofisi za umma wana njaa na watawahonga kidogo tu na kupitisha kila kitu. Ndivyo ilivyofanyika. Kama viongozi wetu wangefanya ‘due diligence’ kwenye manunuzi ya makampuni haya kama Sheria ya Kodi ya Mapato inavyowataka, tusingekuwa na skandali ya Tegeta Escrow. Mfumo uliganzishwa kwa rushwa. Ukitazama miamala ya malipo kutoka akaunti ya Bwana Seth katika akaunti ya StanBic utaona fedha zimekwenda benki za UAE na baadaye Oman na Malaysia. Fedha hizo zilikwenda kuwalipa mabwana Baharuddin na Issa. Serikali lazima ichukue hatua mara moja kuhakikisha fedha zilizokuwamo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zinarudi, uamuzi wa mahakama ya kimataifa unatekelezwa na fedha za umma zinarejeshwa TANESCO na zile za binafsi zinalipwa kwa wamiliki halali. Tanzania haiwezi kuwa nchi ya kubariki utapeli wa kimataifa na kuchafua sura ya nchi yetu mbele ya jamii ya kimataifa. Baraza la Taifa yaani Bunge, kupitia wawakilishi wa wananchi, tayari wameamua na kupitisha maazimio. Kilichobakia ni maazimio hayo kutekelezwa na Serikali. Hakuna mjadala katika maazimio ya Bunge, maana katika maazimio hayo Serikali nayo imo; ilishiriki kikamilifu katika kuyandaa na hatimaye kupitishwa na Bunge. Hakuna namna ya kukwepa kutekeleza maazimio ya Bunge kwa ukamilifu wake; nasema hakuna, ni utekelezaji tu” - http://zittokabwe.wordpress.com/2014/12/31/speech-by-zitto-kabwe-mtwara-31-12-14/ 

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP