Monday, February 2, 2015

Saluni za Urembo na Urimbo

(SALUNI ZA UREMBO NA URIMBO)
  
Mwisho wa siku…sanaa ya umma…inahusu sanaa na umma. Na hilo litaendelea kuwa hivyo pale ambapo huo umma siyo tu kikundi kidogo cha watu wanaojua na kufuatilia sanaa, bali ni mchanganyiko wa taifa lenye matabaka, fursa tofauti, viwango mbalimbali vya kuwa na muda wa kutosha; hivyo basi, sanaa ya umma hakika itakuwa ni ya umma pale tu inapohusu vilivyo vya umma.’(1) 

Mwaka 2008 nilishuhudia uzinduzi wa kile ambacho sasa kimekuwa tamasha maarufu sana la sanaa duniani lijulikanalo kama Infecting The City, yaani ‘Kuliambukiza Jiji’. Hili ni tamasha linaloshirikisha aina nyingi za sanaa na maonyesho katika jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini na hivyo kutoa nafasi na fursa kwa mtu yeyote kuzifikia na kuona kazi mbalimbali za sanaa. Kipindi hicho nilikuwa ndiyo kwanza naanza mwaka wangu wa tatu wa masomo ya Shahada ya kwanza ya Sanaa, hivyo, hata sikujua mwelekeo wangu kitaaluma na kisanii utakuwaje. Lakini nakumbuka jinsi gani wazo la walioanzisha tamasha hilo lilivyonigusa na kunifanya nitamani siku moja na sisi tuazime hata sehemu ndogo tu ya wazo hilo ili kuwe na tamasha kama hilo katika jiji letu la Dar es Salaam, Tanzania. Pia nilitamani niwe mmoja wa waandaaji wa tamasha la aina hiyo jijini Dar es Salaam kwa kadri vionjo, uwezo na muktadha wetu utakavyoruhusu. Hatimaye mwaka huu, ikiwa ni mwaka wa nane toka niupate ule uzoefu ulionigusa kwa mara ya kwanza, nimefanikiwa kuifikia azma hiyo kupitia maonyesho ya Apexart Franchise tuyaitayo “Beauty Salons and the Beast”, yaani, 'Saluni za Urembo na Urimbo.’

Tamasha la Saluni za Urembo na Urimbo ni zao la wasanii wawili – mimi mwenyewe, Rehema Chachage, na Jan van Esch – ambao pia tupo kwenye menejimenti ya taasisi ijulikanayo kama Nafasi Art Space, kituo pekee cha sanaa ya kisasa jijini Dar es Salaam. Wazo la kuwa na tamasha hili liliibuka kufuatia hali tuionayo Tanzania, yaani: kuhudhuria maonyesho ya sanaa kiukweli siyo utamaduni wa Watanzania walio wengi. Hivyo, ukilinganisha na raia wa kigeni, hakuna Watanzania wa kutosha wanaohudhuria maonyesho ya utamaduni pamoja na matukio mengine ya kiutamaduni katika vilinge vya tamaduni jijini. Sisi kama waandaaji wa takribani asilimia 50 ya maonyesho hayo, mara kwa mara tunajikuta tukijiuliza umma wa Watanzania uko wapi na ni kwa namna gani tunaweza kufanya iwezekane kwa umma huo kupata fursa ya kuona sanaa na kuwafikia wasanii.

Baada ya kubunga bongo na kutafakari sana, tukahitimisha kuwa labda njia pekee ya kuweza kuwafikia watu wengi zaidi ni kwa kuazima mbinu ya ‘Kuambukiza Jiji’ na kujaribu kufanya maonyesho yanayoibuka ‘papo kwa hapo’ katika maeneo ya umma ili kuvutia mkusanyiko mkubwa wa Watanzania. Tunasema, ‘Kama hawataifuata sanaa, basi tuiachie sanaa iwafuate wao;’ na tupo kwenye mkakati wa kuwafuata (umma wa) watazamaji wa sanaa popote pale walipo. Katika jaribio hili la kwanza la maonyesho ya ‘papo kwa hapo’, tumeamua kutumia saluni kama maeneo ya maonyesho baada ya kuona makala ya Beauty Salons and the Beast (yaani Saluni za urembo na Urimbo) iliyoandikwa na Erick Mchome. Makala hiyo inaonyesha ni kwa kiwango gani saluni zimekuwa ni biashara zinazokuja juu kwa kasi jijini Dar es Salaam ambapo tunaona kundi kubwa la watu wa matabaka ya juu, kati na chini ya kiuchumi/kimaisha nchini Tanzania yakitumia muda wao wa ziada humo, hasa mwisho wa wiki, yaani, wikiendi.(2) Hawa ndiyo aina ya watazamaji ambao maonyesho yetu yanalenga kuwafikia.

Katika jaribio hili la kwanza la maonyesho ya ‘papo kwa hapo’, tumeona ni vyema tujaribu kwanza kutumia saluni zilizoko katika maeneo ya karibu na tulipo, hivyo tumechagua eneo la Msasani ambalo kiutawala ni kata katika Wilaya ya Kinondoni. Msasani pia ipo kati ya Peninsula (yaani maeneo ya Masaki/Oysterbay), ampapo wanaishi wageni wengi pamoja na Watanzania wengi wa daraja/tabaka la kati na la juu kiuchumi/kimaisha, na Kijiji cha Msasani ambacho zamani kilikuwa ni kijiji cha wavuvi na mpaka sasa kina mkusanyiko mkubwa wa watanzania wa tabaka la chini kiuchumi. Hali kadhalika ni rahisi kwa watu wengine kutoka maeneo mengine ya Wilaya ya Kinondoni (wengi wao wakiwa ni mchanganyiko wa tabaka la chini na la kati kimaisha/kiuchumi) kupafikia Msasani maana biashara nyingi zinazowahudumia ziko hapo. Hivyo mazingira hayo yanatupa fursa ya kuwafikia Watanzania wengi na wa aina nyingi ambao kwa kawaida hatuwaoni kwenye maonyesho ya wazi ya usiku tuyafanyao katika kituo chetu cha Nafasi Art Space.

Kama walivyo wasanii wengi wanaongezeka leo, wasanii waliochaguliwa kwa ajili ya maonyesho ya Saluni za Urembo na Urimbo wanapendelea sanaa ya umma na kuhoji nafasi zao katika jamii kwa kutumia sanaa kuwasiliana na jamii husika kuhusu masuala muhimu ya kijamii. Wanatumia maonyesho haya kama mbinu ya kuitoa sanaa kwenye kuta nne za kituo cha sanaa walichokizoea na kuzipeleka nje kwa watu ambao siyo kawaida yao kuja kwenye vituo vya sanaa. Kwa kuwafikia watu hao, wasanii hawa pia wanapata fursa ya kusikiliza maoni mbadala kuhusu ujumbe wao wa kisanii na hivyo kuwawezesha kukuza maono na usikivu wa vionjo na tafsiri za Kitanzania kuhusu sanaa ya kisasa. Kupitia kitendo hiki, wasanii wanataka kuwapa changamoto watazamaji na wao wazingatie na watazame kwa undani zaidi mazingira waliyopo – yaani, muktadha ambao sanaa yao inapokelewa nao na mitazamo inayoibuka humo ni masuala muhimu katika maonyesho haya. Kwa namna fulani, wasanii hawa wanachukua nafasi ya watetezi (kupitia sanaa) wa mitazamo mbadala inayohoji tafsiri, imani na misimamo ya jamii.

Kuna njia nyingi za kutafsiri mitazamo na maana ya mchango wa kila msanii. Sisi kama wasimamizi wa maonyesho haya ya Saluni za Urembo na Urimbo, tumetoa fursa kwa mtazamo na tafsiri yoyote ile ambayo wasanii wataiongezea kwenye wazo letu la kuwa na maonyesho haya. Japokuwa kila mada ya msanii katika nafasi yake imejikita kwenye taaluma au mfumo fulani wa sanaa, mnyanganyiko wa uzoefu wa  ndani na wa nje wa wasanii wote, kwa pamoja, ni mpana na unaakisi uzoefu wa nchi yetu na siasa zake katika mapana yake.

Maonyesho yaliyojumuishwa katika Saluni za Urembo na Urimbo ni yale ambayo yanagusa fikra zetu na kugusia kipindi hiki na mazingira yetu ya sasa nchini. Mengi yanagusia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 na kurejea miaka 5+ ya Uhuru na miaka 20+ ya mfumo wa demokrasia ya kiliberali pamoja na mikanganyiko yake, mmojawapo ukiwa ni namna ya kuzuia rushwa/ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Kwa kuzingatia upigaji kura, wasanii kwa pamoja walikubaliana tuanze na mfumo wa maswali ya kuchagua kama mbinu ya kwanza na mada mtambuka – kama namna ya kutathmini ambapo watu wanaulizwa wachagua jibu au majibu kutoka kwenye orodha ya majibu, mtu hugudua kuwa mara nyingi jibu linakuwa ni majibu yote, yaani kuna mengi ya kuchagua.

Jan van Esch na Aika Kirei, kwa mfano, wanatumia ‘mbinu ya kutathmini kwa kutumia maswali ya kuchagua’ kuuliza maswali kuhusu namna ambavyo wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati wanavyopata au kukosa fursa. Na, kama ilivyokuwa kwa baba yake aliyekuwa Profesa wa Sosholojia na Mchambuzi wa masuala ya Kijamii  na ambaye anasemekana kuwa mtu wa kwanza kuyachezesha kikejeli maneno ya kaulimbiu ya chama tawala ya uchaguzi wa mwaka 2005, Rehema Chachage naye anayachezea kisanii maneno hayo ya ARI, NGUVU, KASI ambayo kiuhalisia yamekuwa kinyume chake na kuwa A, -NGU, -KA (ANGUKA) kutokana na chama hicho kushindwa kutekeleza mambo mengi waliyoahidi. Vivyo hivyo, japo kwa mbinu tofauti, Gadi Ramadhani anatumia mwendelezo wa maonyesho yake ya Blindfolded (Kufungwa Macho) kuonyesha, kwa mtazamo wa kisanii, ni jinsi gani leo sisi kama jamii tumefungwa kitambaa machoni hivyo ni kama vile tunatembea bila kujua/kuona jinsi ambavyo mfumo tawala (wanasiasa, vyombo vya habari n.k.) unatuhadaa.

Kwenye suala la maamuzi na kuchagua, Delphine Buysse  anatumia madoli 50 yanayoning’inia kichwa chini miguu juu na ambayo yamepakwa rangi ya kijivu kwa asilimia 50, kuonyesha na kuchambua mtanziko wa maisha na ugumu utokanao na kuamua/kuchagua. Eneida Sanches naye analitazama suala hilo hilo ila kwa namna tofauti. Kwa kutumia michoro ya wanaume ambao hawapo (tena) katika maisha yake, sanaa yake inaonyesha mikanganyiko na tafakuri kuhusu wanaume hao na uchaguzi/uamuzi wao wa kumwacha… swali lake kuu likiwa ni; wako wapi na nini kiliwafanya waondoke/wamwache?

Cloud Chatanda anakuja na mtazamo chanya zaidi kwenye mada hii kwa kutumia mchanganyiko tete wa uchoraji na uchongaji kuonyesha jinsi viumbe vya zamani visivyojulikana ambavyo kwa muda mrefu vimegana kwenye Mlima Kilimanjaro vinaamka na kukuta Tanzania iliyo katika hali tata na kuamua kupambana na matatizo ili kulirudisha Taifa kwenye hali yake ya asili. Hali kadhalika Amani Abeid naye anakuja na mtazamo chanya kwa kuonyesha shujaa anaejitokeza (kutoka Tanzania) kuikoa dunia kutoka kwenye majanga baada ya mashujaa maarufu na wapendwao wa nchi za magharibu kushindwa kufanya hivyo.

Onyesho la Vita Maluli, ambalo limejikita zaidi kwenye kejeli, linatumia ‘kango moko’, yaani kipande kimoja cha kanga chenye vijimaneno au vijembe, ambapo tunaona kanga ikiwa imepata uhuru zaidi hivi karibuni baada ya kuacha utamaduni wa kuwa tu vazi la kuvaliwa nyumbani kwa matumizi ya ndani na kuwa pia vazi linaloonekana mitaani, likiwa limevaliwa na wanawake mchana kweupe.

Kila msanii anajaribu, kwa namna yake ya pekee, kupaza sauti yake kuelezea yale yanayomgusa. Kama Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Afrika, Tanner Methvin anavyosema, “propaganda ni kusema hatuna mamlaka ya kujieleza kwa Uhuru. Eti sauti zetu zinahitaji ruhusa kutoka kwa mtu au kitu fulani chenye mamlaka hayo. Kuwa walimu wetu, wakuu wa taasis za elimu, mabosi wetu, na maofisa wa Serikali ndiyo wanaturuhusu kucheza muziki, kuimba, kuchora, kupiga picha, kuandika, au hata kuongea tu. Wanatuambia lini tumechaguliwa au tumeteuliwa na hapo ndipo tu tunaposimama…Hili kwa hakika ni hekaya lakini ambayo tunashiriki kuitunga na kuikuza kila mara tunapojibana wenyewe na kuzikimbia fursa za kuelezea visa vyetu wenyewe.”(3)   

1. Jay Pather, Curator’s Note in Infecting the City: Public Arts Festival, March 10-15, 2014, Cape Town City Centre, exhibition catalog, p. 3.
2. Eric Mchome, “Beauty Salons and the Beast,” Mail & Guardian, Dec. 12, 2011: http://mg.co.za/article/2011-12-12-beauty-salons-and-the-beast.
3. Tanner Methvin, Introductory Note in Infecting the City: Public Arts Festival, March 10-15, 2014, Cape Town City Centre, exhibition catalog, p. 2.

© Rehema Chachage (Msimamizi wa maonyesho, Beauty Salons and The BeastSaluni za Urembo na Urimbo)

TAARIFA KWA WANA HABARI: UZINDUZI WA MAONYESHO YA BEAUTY SALONS AND THE BEAST (SALUNI ZA UREMBO NA URIMBO)

FOR IMMEDIATE RELEASE.

Uzinduzi wa Beauty Salons and the Beast (Saluni za Urembo na Urimbo); maonyesho ya sanaa yaliyopangwa kufanyika katika saluni za kiume na za kike maeneo ya Msasani (Mtaa wa Makangira, karibu na Edo Chips), Dar es Salaam, Tanzania. Maonyesho haya yatahusisha kazi za sanaa zilizotayarishwa na wasanii wafuatao:

Amani Abeid (Tanzania)
Delphine Buysse (Tanzania/Ubelgiji)
Rehema Chachage (Tanzania)
Cloud Chatanda (Tanzania)
Eneida Sanches (Brazil)
Jan Van Esch (Tanzania/ Uholanzi)
Aika Kirei (Tanzania)
Vita Malulu (Tanzania)
Gadi Ramadhani (Tanzania)
  
Muhtasari:
Maonyesho ya “Beauty Salons and the Beast” yaani, “Saluni za Urembo na Urimbo” yamelenga kuwatambulisha Watanzania kwenye sanaa iliyo mpya, ya kisasa na ya majaribio. Lengo kuu ni kuchochea mwamko, na mazungumzo zaidi juu ya umuhimu wa sanaa nchini Tanzania. Maonyesho haya yatagusia mada ya ‘uwezo wa kuchagua’, iwe ni rafiki, mpenzi, mke, raisi, ajira, makazi, n.k. na yataonyesha kazi za sanaa kutoka kwa wasanii wa Kitanzania na wa Kimataifa. Kwa kutumia kazi zao, wasanii hawa wataangalia maswala mbalimbali ya kijamii na kuhoji sehemu ya msanii na sanaa yake katika jamii. Wasanii watatumia mbinu mbalimbali za kutengeneza sanaa zao ili kuhakikisha kwamba jamii nayo inapata nafasi katika ukamilishaji wa kazi zao za sanaa.

Watayarishaji wamebuni maonyesho haya kutoka kwenye msemo huu; ‘kama hawatofuata sanaa, basi acha sanaa iwafuate wao’; hii ni baada ya kugundua upungufu wa jamii ya kitanzania (ukilinganisha na jamii ya wageni wanaoishi Tanzania) katika maonyesho na matukio mbali mbali ya kisanii nchini, hivyo, watayarishaji wa maonyesho haya wameamua kuwapelekea wananchi sanaa kwani imeshindikana kwa wananchi kuifuata sanaa wenyewe. Watatumia njia ya “kuliambukiza” jiji na matukio mbalimbali ya kisanii kama vile maonyesho na majadiliano ya umma kuhusu sanaa na kuhamasisha jamii kujihusisha na kujua zaidi kuhusu sanaa kwa ujumla.

Uzinduzi huu utafanyika siku ya tarehe 7 Februari 2015 kuanzia saa 8.00 mchana. Kutakuwa na kazi za sanaa  zikionyeshwa ndani ya saluni nne (4) za kike na za kiume katika mtaa wa Makangira (Pia hujulikana kama mtaa wa Msasani, karibia na Edo Chips) Dar es Salaam Salaam. Uzinduzi utakuwa na vitumbuizo tofauti vya burudani, pamoja na hotuba fupi kutoka kwa waandalizi wa maonyesh, wasanii, na wafadhili wa mradi; taasisi iitwayo apexart kutoka New York, USA.

Maonyesho yameandaliwa na Rehema Chachage na Jan van Esch.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP